Wakuu,
Mwanahabari mkongwe nchini, Absalom Kibanda amesema angekuwa kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), asingefanya makosa kwenye mchakato wa kusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi Mkuu zilizotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi kwa vyama vya siasa.
Amesema kwa kusaini tu, chama kingepata fursa ya kushiriki uchaguzi huo na angeendelea kushikilia msimamo wa kampeni ya No reforms, no election.
Amesema Chadema kabla ya kufikia uamuzi wa kususia, wangerejea kilichotokea mwaka 2013/14 kwenye Bunge la Katiba.
Kibanda amesema chama hicho kilisusia kikitarajia baadhi ya mambo yangefanyika lakini haikuwa hivyo.
Mwandishi huyo aliyebobea kwenye uandishi wa habari na makala za siasa ameyasema hayo leo Jumatano Aprili 16,2025 wakati akichangia mjadala wa Mwananchi X Space wenye mada isemayo: Kanuni za maadili ya uchaguzi 2025 na mustakabali wa siasa za Chadema, ulioandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL).
Aprili 12, 2025 Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), Ramadhan Kailima aliyesema Chadema hakitashiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba na chaguzi ndogo zitakazofuata kwa muda wa miaka mitano baada ya chama hicho, kususia kusaini kanuni, hivyo kukosa sifa ya kushiriki mchakato huo.