ACT: SMZ Isimamie Sheria ya Ukatili na Unyanyasaji (Gender Based Violence) ili kuondosha matukio ya udhalilishaji na Ukatili wa Kijinsia

ACT: SMZ Isimamie Sheria ya Ukatili na Unyanyasaji (Gender Based Violence) ili kuondosha matukio ya udhalilishaji na Ukatili wa Kijinsia

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760
SMZ IHAKIKISHE INASIMAMIA SHERIA YA UKATILI NA UNYANYASAJI (GENDER BASED VIOLENCE)
Ndugu wanahabari, awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru, Mwenyezi Mungu, kwa kutujaalia hali ya uzima wa afya, lakini pia niwashukuru nyinyi wanahabari, kwa kuitikia wito wetu wakuja katika mkutano huu leo hii hapa katika Ofisi za Makao Makuu ya Chama chetu cha ACT Wazalendo Zanzibar, nyinyi ni watu muhimu katika kupeleka habari na matukio mbali mbali kwa jamii, ni Imani yangu kwamba leo hii mutatufikishia taarifa zetu, hizi kwa umma.

Ndugu wanahabari, mutakumbuka kwamba tarehe 06 Septemba 2024, kwa niaba ya Kiongozi wa ACT Wazalendo, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, Mh. Othman Masoud Othman aliteua Wasemaji wa Kisekta kwa upande wa Zanzibar (BARAZA KIVULI). Jukumu kubwa la Baraza la Wasemaji wa Kisekta ni kufuatilia utendaji wa Serikali kisera, kisheria na kuona jinsi gani sera, sheria, utendaji, maamuzi na usimamizi wa shughuli za Serikali unaathiri maendeleo na mustakbali wa nchi na wananchi, uchumi, ustawi wa jamii, usalama wa raia, utengamano wa kijamii, haki, amani na utulivu wa nchi. Aidha Baraza hilo litafuatilia mambo hayo kwa kuzingatia maslahi ya wananchi hasa katika matumizi ya madaraka, rasilimali na fursa za nchi ili kuona kwamba MALENGO MUHIMU yaliyoelezwa na Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Chama cha ACT-Wazalendo yanatimizwa kwa ukamilifu.

Ndugu wanahabari, Kama munavyojua Jana tarehe 10/12/2024 ndio siku ya kilele cha Maadhimisho ya Siku 16 za Kampeni ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia!, hivyo basi tumewaita ili kuzungumza na nyinyi juu ya vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia vinavyofanyika hapa Zanzibar, tunaamini kupitia nyinyi mutatufikishia taarifa hii kwa wananchi.

Hivyo basi taarifa yetu hii itagusia maeneo Makuu matatu ambayo ni pamoja na matatizo wanayokumbana nayo wanawake, Ukatili na Unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na Watoto na Matatizo wanayakobiliana nayo Wazee wa Zanzibar.

Ndugu wanahabari, Wanawake wa Zanzibar wanakutana na matatizo mengi ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Licha ya jamii na makundi ya utetezi wa wanawake kama vile TAMWA, ZAFELA, JUWAUZA NA PEGAO kuchukua juhudi kubwa za kuboresha Haki za Wanawake na ustawi wao, bado wanawake wanakutana na changamoto nyingi zinazohusiana na ubaguzi wa kijinsia, unyanyasaji, na ukosefu wa fursa sawa katika maeneo mbalimbali ya maisha yao kama ifuatavyo:-

Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia.

Ndugu Wanahabari, Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia ni kitendo chochote au mwenendo wowote, ambao husababisha moja kwa moja kwa mtu, kama mateso ya kimwili, ya kimapenzi au ya kiakili kupitia vitisho, kulazimisha au njia nyengine; kwa lengo la kutisha, kuadhibu, kuwadhalilisha, kudhoofisha usalama au kujiheshimu; kutosheleza hamu ya ngono; au kudhoofisha uwezo wa mwili au kiakili wa mtu kwa sababu ya jinsi yake. Kwa mfano, unyanyasaji wa kijinsia, kumpiga mke, unyanyasaji wa kijinsia wa wasichana na wavulana, mwanamke kuua watoto wachanga, Biashara haramu ya usafirishaji wa wanawake na watoto wa kike na ponografia (uenezaji wa ngono haramu).

Ndugu Wanahabari, Hapa Zanzibar hivi karibuni, tumeona na kushuhudia matukio kadhaa ya Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia kwa Watoto na Wanawake, matukio haya hayooneshi, hadhi na heshima ya watoto na mwanamke wa Kizanzibari, na ni kinyume na mila, utamaduni na silka za Kizanzibari, matukio haya yameshamiri na kuengezeka kila uchao, takwimu za matukio haya zinazotolewa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zinaonesha ni kwa kiasi gani matukio haya yanaogezeka kila siku kwa mfano, Ripoti iliyotolewa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar hivi karibuni inaonesha jumla ya matukio 165 ya ukatili wa kijinsia yaliripotiwa kwa mwezi Julai 2024, ambapo waathirika wengi walikuwa ni watoto. Ripoti inaonesha idadi ya watoto ni 142 sawa na asilimia 86.1 ya waathirika wote, ambapo wasichana walikuwa 115 sawa na asilimia 81.0 na wavulana 27 sawa na asilimia 19.0. Hali hii inasikitisha na inahitaji kudhibitiwa na wadau wote wakiwemo Serikali, taasisi za jamii, viongozi wa dini, walimu pamoja na wazazi, vile vile na watoto wenyewe wapatiwe elimu ya kujilinda na kujikinga dhidi ya watu waovu.

Ndugu Wanahabari, Tumepokea taarifa za kusikitisha kabisa kwa baadhi ya wanawake walioajiriwa kwenye kampuni za Miradi mbali mbali inayoendelea hapa nchi, hasa kampuni za ujenzi kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji, vitendo vya kinyama na ambavyo vinapaswa kulaaniwa na kukemewa na kila mmoja wetu, kwa watoto wa kike kudhalilishwa kingono, na badala yake fedha inatumika kama fidia ya udhalilishaji huo, huku Jeshi la Polisi na Wizara ya kazi Uwezeshaji Wananchi, Kiuchumi kupitia Kamisheni ya Kazi, wakivifumbia macho vitendo hivyo, eti kwa kisingizio cha makubaliano ya pande mbili, bila ya kujali na kulinda heshima na hadhi ya mwanamke.

Ndugu Wanahabari, Tarehe 13/11/2024 tumesikia na kushuhudia tukio la kubakwa na kuuwawa kwa mtoto wa miaka 6 huko Mwera kichaka mabundi, ambae ni mwanafunzi wa Skuli ya Umrat Islamic KG 2, jambo hili lilizua taharuki kwa familia ya mtoto huyo na jamii kwa ujumla, kitendo hichi kinakwenda kinyume na haki za mtoto pamoja na haki za binaadamu.
Upungufu wa Fursa za Kiuchumi

Ndugu Wanahabari, Wanawake wengi Zanzibar wanakumbana na changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira na wengi wao wanategemea shughuli za kilimo na biashara ndogo ndogo au kazi za majumbani ambazo hazina malipo mazuri. Hii inachangia kuwa na kiwango kidogo cha kipato, na inawafanya kuwa na utegemezi mkubwa kwa familia.


Ubaguzi katika, Utoaji wa Mikopo na Uwezeshaji wa Kifedha

Ndugu Wanahabari, Wanawake wanaotaka kuanzisha biashara wanakutana na changamoto kubwa ya upatikanaji wa mikopo au msaada wa kifedha kwa sababu ya ubaguzi unaofanywa na serikali kutokana na itikadi za Kisiasa.

Ndugu Wanahabari, kila mwaka Serikali hutenga fungu la fedha, kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, na program maalum ya kuwawezesha Wanawake, kwa bahati mbaya fedha hizo za serikali hutumika vibaya baada ya kuwapatia, mikopo watu wote wenye uhitaji wa kupata mikopo hiyo, serikali wameamua kuzigawa fedha hizo kwa UWT bila ya kujali maslahi ya wazanzibar, hivi karibuni tarehe 31/10/2024, tumemshuhudia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ndugu Hemed Suleiman Abdulla akiwa Katika Wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba, akiwakabidhi Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) hundi yenye thamani ya Shilingi Milioni 75, iliyotolewa na Serikali ya Mapinduzi, ikiwa ni sehemu ya fedha za program ya mikopo kwa Makundi Maalum, Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu, jambo hili halikubaliki, haiwezekani fedha za Umma kutumika kwa misingi ya kisiasa, ni lazima fedha za umma zitumike bila ya ubaguzi. Kuna vikundi vingi sana vya Vijana, Wanawake na vikundi vya watu wenye ulemavu, ambavyo vimetimiza vigezo vya kupata mikopo hiyo, lakini wakienda hawapewi fedha hizo na badala yake wanapigwa danadana.
Matatizo ya Afya ya Uzazi na Huduma za Kujifungua.

Ndugu Wanahabari, licha ya Serikali kujenga hospitali za Wilaya, lakini bado kuna changamoto kubwa katika huduma za afya ya uzazi, kama vile huduma za kujifungua, upasuaji wa dharura. Upungufu wa wataalamu na vifaa katika hospitali nyingi, hii inapelekea wanawake kuwa katika hatari ya vifo wakati wa kujifungua. Tatizo hili linaendelea kuwa kubwa zaidi baada ya Hospitali ya Mnazimmoja kuhamisha huduma za uzazi katika Hospitali ya Lumumba, ni wazi kwamba Hospitali hiyo imezidiwa.

Upungufu wa huduma za wazee
Ndugu Wanahabari, Wazee ni watu ambao wanastahiki kupata huduma maalum, kama vile Matibabu na Usafiri, lakini tafauti kwa hapa petu Zanzibar Wazee mara nyingi hawapati huduma maalum za afya wala za usafiri, zinazohitajika kutokana na ukosefu wa vifaa vya kisasa, madaktari waliobobea katika kutunza wazee, na huduma zinazohusiana na matatizo ya umri mkubwa kama vile uangalizi wa muda mrefu (long-term care).

Fedha za Pencheni Jamii kwa Wazee
Ndugu Wanahabari, Zanzibar ni miongoni mwa Nchi chache ambazo zinatoa Pensheni jamii kwa wazee waliofikia umri wa miaka 70, ni jambo jema na zuri, lakini kwa bahati mbaya sana Pencheni hii jamii wanayopewa wazee hawa, imegeuka kuwa adhabu na kutaka kutumika au kutumiwa kisiasa, kila panapofanyika shughuli ya Chama cha Mapinduzi. Jambo hili sio sahihi na wanawakosea wazee hawa heshima yao, na kuwadhalilisha, haiwezekani kwamba Pencheni jamii wanayopewa iwe ndio sababu ya kuwataka kuwatumia wao kisiasa, tuwaache wazee hawa wapunzike na sio kuwadhalilisha kutokana na Penshini hii jamii wanayopewa.

Ndugu Wanahabari, kutokana na Mambo tuliyoyaeleza hapo juu, tunaitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, kufanya mambo yafuatayo:-

1. Kuweka utaratibu maalum wa kinamama kuhudumiwa bila ya usumbufu pale wanapokwenda kujifungua, kwenye hospitali ambazo zimehamishiwa huduma za kujifungua na huduma zote zilizokuweko katika hospitali ya Mnazimmoja.

2. Kufanya Uchunguzi, juu ya matendo ya udhalilishaji yanayofanyika katika kampuni zinazosimamia ujenzi wa miondombinu na kuchukua hatua stahiki kwa wahusika, na kuchukua hatua kali kwa kila alihusika kusimamia makubaliano ya kuchukua fedha kama fidia ya udhalilishaji huo.

3. Ihakiki, kuweka na kusimamia, sera maalum ya idadi ya wataalamu wa afya wanohitajika katika vituo vya afya ambao watahudumia wazee.

4. Ihakikishe inasimamia sheria ya ukatili na unyanyasaji (gender based violence), ili kuondosha matukio ya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia

5. Itilie mkazo kwenye mafunzo ya amali, sayansi na teknolojia, TEKNOHAMA na mafunzo mengine, endelevu ili kumuwezesha mwanawake kujiajiri na kujikomboa kiuchumi.

6. Itayarishe sera itakayowasaidia, wajasiriamali na wafanyabiashara wanawake kupata huduma za ushauri, mafunzo ili kuongeza uzalishaji na kuweza kuingia katika soko la kiushindani.

7. Ihakikishe inatengeneza mpango maalum wa kuwashughulikia na kuwapatia wazee mahitaji yao muhimu, kama vile matibabu na usafiri

8. Serekali kupitia vyombo vya kutunga sheria, waandae mpango wa kuwasaidia wazee kupatiwa bima ya afya bure na huduma ya usafiri

9. Serikali na Chama cha Mapinduzi, kupitia Masheha waache mara moja, tabia ya kuwasumbua wazee wanaopokea fedha za Penseni jamii kwa kuwataka kwa kuwalazimisha, kuwaunga mkono na kuwalazimisha kuhudhuria katika shughuli za Chama cha Mapinduzi, bila ya ridhaa yao

Hitimisho
Ndugu Wanahabari, sisi ACT Wazalendo, daima tutasimama pamoja na kuyasemea matatizo yanayowakabili wananchi wa makundi mbalimbali bila ya kusita, tunawataka wananchi wasikubali kurubuniwa na vijisenti kwa kushawishiwa na maafisa wa serikali kukubali kuchukua fedha ili kufuta kesi za udhalilishaji wanazofanyiwa na badala yake waendelee na mashauri yao bila ya kuchoka na pale ambapo wanaona kuna uvizishwaji wa kuendesha mashauri hayo wasisite, kuja kwetu tupo tayari kuwapa msaada wa kiushauri na kisheria ili haki isimame dhidi yao.

Imetolewa leo, tarehe 11/12/2024 na,
Ndugu Halima Ibrahim Mohammed,
Msemaji wa Sekta ya Maendeleo ya Wanawake, Watoto na Makundi Maalum – Zanzibar.


t.jpg

tt.jpg

ttt.jpg

tttt.jpg

ttttt.jpg
 
Back
Top Bottom