Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
Prof. Omar Fakih Hamad, Mnadhimu wa ACT Wazalendo, Baraza la Wawakilishi Zanzibar
Ndugu Wanahabari! Hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, aliyetujaalia uhai na uzima na kutuwezesha leo hii tukajumuika pamoja hapa katika ukumbi wetu wa Chama kwa ajili ya kuzungumza nanyi masuala yaihusuyo nchi yetu na watu wake. Sala na Salamu kwa Mtume Muhammad (S.A.W).
Kwa niaba ya Wawakilisho wa ACT Wazalendo katika Baraza la Wawakilishi, tunawashukuru sana nyinyi ambao tumewaalika katika muda mfupi tu na hamukusita kuitikia wito wetu. Kwa hakika, hii ni heshima na thamani kubwa sana munayotupatia katika Chama chetu, na tunaamini kwamba wema huu wa sisi kufanya kazi na nyinyi utaendelea. Tunakuombeni mutufikishie salamu zetu kwa wananchi na wapenda haki wote juu ya ambayo tunawahabarisha hapa siku hii ya leo.
Ndugu Wanahabari! Sisi Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, tunaotokana na Chama cha ACT Wazalendo, tumeshitushwa na kushangazwa na kauli za kubabaisha za Serikali kuhusu, ukweli na usahihi wa gharama za ujenzi wa miundombinu ya AFCON 2027 hapa Zanzibar. Tunaitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutowababaisha wananchi na kutoa taarifa sahihi na kamilifu kwa umma na kuweka wazi juu ya tofauti zilizojitokeza katika taarifa za gharama za ujenzi wa miundombinu ihusianayo na maandalizi ya Kombe la AFCON 2027, hapa Zanzibar.
Ndugu Wanahabari! Kama inavyoeleweka, hivi karibuni kumezuka mjadala mkubwa unaohusu usahihi wa gharama halisi za Ujenzi wa Miundombinu ya AFCON hapa Zanzibar. Mjadala huu umezuka baada ya Mwenyekiti wa Chama chetu cha ACT Wazalendo Taifa, Ndugu Othman Masoud Othman, wakati akifanya Mahojiano na Mtangaazaji wa Wasafi TV, Ndugu Charles William, alipoeleza mtazamo wake na kuainisha uchambuzi wake juu ya baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza hasa kuhusiana na ukubwa usiowiana kiuchumi wa gharama za miundombinu hiyo ya AFCON kwa Zanzibar, akieleza wasiwasi wake juu ya uwezekano wa kurudi kwa gharama hizo kubwa za TZS 1.6 Trilioni zilizotajwa kutengwa kwa mpango huo wa AFCON 2027, hasa ukizingatia ukweli kwamba, Zanzibar sio muandaaji wa mashindano hayo wala mwanachama wa CAF.
Ndugu Wanahabari! Siku chache baadae, wakati akifungua Kituo cha mabasi ya Umeme, Rais wa Zanzibar aliipinga kauli kuhusu gharama halisi za uwekezaji wa miundombinu ya AFCON, kama zilivyofafanuliwa na kuhojiwa na Mwenyekiti wetu, na Rais kueleza kwamba, gharama sahihi za miundombinu yote ya AFCON Zanzibar ni wastani wa TZS 300 bilioni tu.
Ndugu Wanahabari! Tunasimama leo hii kuukumbusha umma kwamba wakati wa kusomwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa Fedha 2026/2027. Waziri wa Fedha na Mipango, alilieleza Baraza la Wawakilishi kwamba “Kufuatia fursa ya Uwepo wa Mashindano ya Kombe la AFCON ya mwaka 2027, Serikali imetenga kiasi cha shilingi 1.69 trilioni ili kuwekeza katika kuimarisha maandalizi ya kitaifa katika mindombinu ya michezo, usafiri, utalii na huduma za kijamii, kwa lengo la kutumia mashindano hayo kama kichocheo cha ukuaji wa Uchumi, ajira na kulitangaaza taifa kimataifa”
Ndugu Wanahabari! Kwetu sisi Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, tunaotokana na Chama Cha ACT Wazalendo, tumepata wasi wasi mkubwa wa utafauti wa taarifa sahihi zilizotolewa na Serikali moja - taarifa ya kwanza iliyotolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Ndugu Juma Maliki Akili katika Baraza la Wawakilishi wakati akiomba kupitishiwa Bajeti Kuu ya Serikali na taarifa ya pili, ni ile iliyotolewa na Rais, Mkuu wa nchi, wakati akifungua kituo cha Mabasi ya Umeme pale Malindi, na taarifa ya tatu iliyotolewa tena na Waziri wa Fedha na Mipango wakati akifanya Mahojiano na waandishi wa Habari, Baya zaidi ni kwamba, taarifa hii ya tatu ilikuwa inapingana sana na ile taarifa yake ya kwanza aliyoitoa katika Baraza la Wawakilishi wakati akiwasilisha na kuomba kuidhinishiwa Bajeti Kuu ya Serikali.
Ndugu Wanahabari! La kusikitisha na kutia wasi wasi zaidi, ni kwenye taarifa iliyosambaa tarehe 28/07/2026, ya Waziri wa Fedha na Mipango, Ndugu Juma Maliki Akili, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari, alipoonekana akilalamika kwamba taarifa ya 1.69 trilioni aliyoizungumza katika Baraza la Wawakilishi, Siku ya tarehe 11/06/2026, wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali sio sahihi na hivyo, amenukuliwa vibaya au Video inayoonekana katika Mtandao (Link ya YouTube) ya Shirika la Utangaazaji la Serikali Zanzibar (ZBC) imechezewa. Na akaeleza usahihi wa Taarifa ni TZS1.069 trilioni.
Ndugu Wanahabari! Sisi wajumbe wa Baraza la Wawakilishi tunaotokana na Chama Cha ACT Wazalendo, tunaitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, itoe majibu kwa umma na kueleza dhahiri Je, ni nani mkweli kati ya Rais ambae ndie Mkuu wa Nchi, au Waziri wa Fedha na Mipango ambae anafanya kazi kwa niaba ya Rais? Ikiwa kauli ya Rais ndio kauli sahihi, Je, Rais amechukua hatua gani kwa Waziri wake wa Fedha na Mipango ambae ameudanganya Umma wa Wazanzibari na Baraza la Wawakilishi na kulisababisha kujadili na kuidhinisha bajeti ambayo sio sahihi na inayokinzana kwa kiasi kikubwa?
Ndugu Wanahabari! Sisi Wawakilishi tunaotokana na ACT Wazalendo, Suala ambalo tunaliuliza kwa niaba ya wananchi wenzetu ni “Ni ipi hasa taarifa sahihi ya Waziri wa Fedha na Mipango? Je, ni ile aliyoitoa katika Baraza la Wawakilishi wakati wa Bajeti au ni hii ambayo ameitoa wakati wa kuzungumza na waandishi wa Habari nje ya Baraza?” Wananchi wanabaki kujiuliza Je, kati ya Rais ambae amezungumza bayana kwamba Miundombinu hiyo itatumia 300 Bilioni tu na Waziri wa Fedha na Mipango ambae amekuwa na kauli mbili kuhusu bajeti halisi ya miondombinu ya AFCON kwa upande wa Zanzibar, lakini zote ni za gharama ya zaidi ya trilioni moja, aaminiwe nani?
Ndugu Wanahabari! Hoja ya msingi ya wananchi iko kwenye ukubwa wa uwekezaji na uhalisia wa kuweza kurudisha faida ya uwekezaji huo. Asili ya Uwanja wa Fumba na Mji wa Michezo wa AFCON ni miradi ya uwekezaji na sio ya huduma kwa Jamii. Kama ni kwa huduma kwa jamii tu, Uwanja wa Amani, Uwanja wa Mao na Viwanja vya kila Wilaya vinatosha. Kama gharama za ukarabati wa Uwanja wa Amani, takriban TZS 102 bilioni zinahitaji miezi 2,040 sawa na miaka 170 kuweza kurejeshwa, basi uwekezaji katika miundombinu ya AFCON utahitaji miaka mia ngapi? Ni dhahiri kwamba Zanzibar bado haina mvuto wa Utalii wa Michezo kwa sababu hatuna hata timu - iwe vilabu au timu za Taifa - zinazoshiriki na kutoa ushindani Kimataifa. Ushahidi upo wazi kwamba, hata ligi za ndani zenyewe hazina mvuto wala uwekezaji unaolingana.
Ndugu Wanahabari! Kwa wakati wa sasa, kuna kila dalili za mradi huu wa miundombinu ya AFCON 2027 kuwa White Elephant Project! Kwa kutopata faida kamili kama zinavyonadiwa sasa
(to fail to deliver expected benefits) na kutumika kwa uchache wake (underutilized). Serikali iwaeleze wananchi mipango yenye maana na tija kuhusu mji huo baada ya kumalizika kwa mashindano ya AFCON 2027. Ikizingatiwa kuwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutakuwa na Viwanja vipya vyengine vikubwa - Uwanja wa Mkapa na Uwanja wa Uhuru na Uwanja wa Arusha unaojengwa kwa malengo ya AFCON, ukijumlisha na viwanja vinavyotumika sana kama KMC, Azam Chamanzi, na Major General Isamuhyo Stadium, kwa kuvitaja vichache. Serikali iwaeleze wananchi, ni ipi nafasi yetu kibiashara ukizingatia kimataifa nafasi yetu ipo chini ya mikono ya TFF?
Ndugu Wanahabari! Wakati tukiandaa miundombinu kwa ajili ya Mashindano ya AFCON 2027, bado Serikali haijui hadi sasa idadi ya mechi na ukubwa wa timu za Taifa zitakazocheza Zanzibar. Ni kwa vipi tunajihakikishia kwamba AFCON italipa upande wetu wakati hatuna nafasi ya kuamua kuhusu mechi. Maana sisi sio waandaji rasmi.
Ndugu Wanahabari! Ili kuondosha taharuki iliyojitokeza kwa Serikali moja kuwa na taarifa tafauti kwenye jambo moja, tunaitaka Serikali itoke hadharani na kauli moja ya uhakika na yenye kueleweka ni zipi hasa gharama kamili na sahihi za miundombinu ya AFCON kwa Zanzibar.
Ndugu Wanahabari! Kwa kuwa siku zote chama chetu kimekuwa kikijipambanua na kusimamia rasilimali za nchi hasa katika kulinda maslahi ya Umma kama ilivyodhihiri wakati tukiihoji Serikali katika Bajeti na Masuala mbali mbali ndani ya Baraza la Wawakilishi na wakati mwengine kuibua mijadala ya kitaifa, hivyo basi, kwa niaba ya wananchi wenzetu, tunaitaka Serikali ifanye yafuatayo:-
- Serikali iwaambie wananchi ukweli kuhusu jambo hili na pale ilipokosea iwaambie wananchi. Majibu yanayotolewa kwenye jambo hili ni mepesi sana na hayalingani kabisa na uzito wa hoja yenyewe;
- Tunaitaka Serikali iwaeleze wananchi jumla ya fedha, ugawaji wa fedha hizo kimiradi, na vyanzo na masharti ya fedha hizo. Tofauti za nambari (TZS 1.69T, TZS 1.069T, na TZS 300B) kibajeti ni kubwa sana na zinahitaji ufafanuzi wa haraka kutoka kwa Serikali, sambamba na Bajeti iliyoidhinishwa na Baraza la Wawakilishi mwezi Juni 2026;
- Ikiwa kulikuwa na makosa ya kuwasilishwa kwa taarifa, Serikali itoe taarifa sahihi na ufafanuzi wake rasmi unaoeleza chanzo cha kosa na hatua zilizoachwa kuchukuliwa;
- Kwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, ameueleza umma kwamba fedha zilizotarajiwa kutumika kujenga miundombinu hiyo ni fedha za mkopo ambazo bado hazijapatikana, lakini ujenzi unaendelea, Serikali iwaeleleze wananchi, mkopo huo ulitarajiwa kuchukuliwa kutoka wapi, utalipwaje na kwa masharti yapi, na kwa kuwa, mkopo huo bado haujapatikana Serikali iwaeleze wananchi fedha za ujenzi wa Miundombinu hiyo inayoendelea kujengwa zinatoka wapi na katika fungu lipi?
Prof. Omar Fakih Hamad
Mnadhimu wa ACT Wazalendo, Baraza la Wawakilishi Zanzibar