HALI HALISI YA SASA
Tunapenda kuujulisha umma kuwa Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Ndugu Dorothy Jonas Semu akiambatana na Naibu Katibu wa Mambo ya Nje Ndugu Nasra Nassor Omar na Katibu wa Haki za Binadamu Pavu Juma Abdalla wamerejea nchini Tanzania takribani saa 9:40 usiku wa tarehe 14 Machi, 2025 baada ya kuzuiwa kuingia nchini Angola.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Ndugu Othman Masoud Othman bado yupo Jijini Luanda nchini Angola kwa ajili ya kukamilisha taratibu za usafiri kurejea nyumbani Tanzania. Chama kitaendelea kutoa taarifa mara kwa mara kwa umma juu ya maendeleo ya suala hili.
UKIMYA WA TANZANIA HAUKUBALIKI
Chama cha ACT Wazalendo kimesikitishwa na ukimya wa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kulikalia kimya suala hili. Ni jambo linaloshangaza na kusikitisha kwa Serikali ya Tanzania kushindwa kutoa kauli yoyote dhidi ya kitendo hiki kinachokiuka taratibu za kidiplomasia, ari ya mshikamano wa Afrika na undugu wa kihistoria baina ya Tanzania na Angola.
Tunaitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itoke hadharani na kufafanua kilichotokea Angola na msimamo wa Serikali juu ya hilo ikizingatiwa kuwa miongoni mwa viongozi waandamizi waliokumbwa na kadhia hiyo yumo pia Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar. Pia, tunarejea rai yetu ya kuitaka Serikali kumuita mara moja Balozi wa Angola nchini Tanzania kujieleza kuhusu kilichotokea kwa viongozi wetu nchini Angola.