ACT Wazalendo: Mjadala wa Kitaifa Kuhusu Mwelekeo na Khatima ya Nchi yetu

ACT Wazalendo: Mjadala wa Kitaifa Kuhusu Mwelekeo na Khatima ya Nchi yetu

Elias Msuya

Platinum Member
Joined
Dec 23, 2011
Posts
267
Reaction score
1,014
Leo Mei 16, Chama cha ACT Wazalendo inafanya mjadala wa Mjadala wa kitaifa kuhusu mwelekeo na khatima ya Tanzania, uliokusanya makada na viongozi wa chama hicho, wasomi, wanadiplomasia na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.


Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud, amesema Tanzania ipo katika mkwamo wa kiuongozi na tusipoangalia tunawea kuingia kwenye mkwamo mkubwa zaidi.


HOTUBA YA MWENYEKITI WA TAIFA WA CHAMA CHA ACT WAZALENDO NDUGU OTHMAN MASOUD OTHMAN KWENYE MKUTANO WA CHAMA NA WADAU WA DEMOKRASIA NCHINI ULIOFANYIKA TAREHE 16 MEI 2026 KATIKA UKUMBI WA SERENA, DAR ES SALAAM.

Ndugu viongozi wa Chama na wadau wa demokrasia mlioshiriki Mkutano wetu wa leo, naomba awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha tukiwa wazima. Nikiwa Mwenyekiti wa Chama, nikiri kwamba hii ni mara ya kwanza kwa Chama chetu kuandaa majadiliano ya kitaifa ambayo yanaendeshwa na kutawaliwa na washiriki ambao zaidi ya asilimia 70 ni watu wa nje ya Chama.

Hatua hii imechukuliwa ili Chama kipate fursa ya kujipima na kuwajibika kwa wadau wa nje ya Chama katika mazingira ambayo yatakuwa huru zaidi. Naomba kutoa ahadi kuwa Chama chetu kitauendeleza utamaduni wa makongamano huru ya namna hii kila tutapokuwa na jambo kubwa lenye maslahi mapana kwa Taifa.

NCHI IPO NJIA PANDA, INAHITAJI UONGOZI

ACT Wazalendo tumeitisha kongamano hili la leo kwa sababu, kwa uchambuzi wetu, tumehitimisha kuwa nchi yetu ipo njia panda na inahitaji uongozi mathubuti kuchagua mwelekeo sahihi. Kama alivyowahi kusema Mwanaharakati wa kupigania usawa duniani Martin Luther King ‘Kipimo halisi cha kiongozi si pale anaposimama wakati wa faraja na urahisi, bali pale anaposimama wakati wa changamoto na mikanganyiko’.

Bila uongozi madhubuti kututoa kwenye mkwamo tulionao, upo uwezekano usio na shaka kuwa nchi yetu inaweza kuingia kwenye mkwamo mkubwa zaidi wa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Ninasimama mbele yenu kueleza, kwa muhtasari, fikra za ACT Wazalendo juu ya mkwamo tulionao kwa kuangazia kiini chake, wasababishaji na namna ya kujinusuru kama Taifa.

Licha ya maneno ya kujifariji ya watawala kuwa nchi inasonga mbele, ukweli ni kwamba Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 umeacha majeraha makubwa sana kwa Taifa kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar, majeraha ambayo yameathiri sana mustakabali wetu wa ndani na heshima ya nchi yetu kimataifa.

Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 umelitumbukiza Taifa kwenye mgogoro mkubwa wa kijamii ambao matokeo yake, zisipochukuliwa hatua sahihi za upesi, unaweza kuligawa na kuliangamiza Taifa letu. Hatupaswi kufika huko! Mifano ya wazi inayoonesha bayana kama Taifa tupo kwenye mkwamo ni kama ifuatavyo;

1. Nchi kuongozwa na viongozi ambao wamepoteza kabisa uhalali kwa sababu hawakuchaguliwa na wananchi. Watawala wa ngazi zote ambao walipaswa kupatikana kwa kuchaguliwa na wananchi, wamepoteza uhalali wa kisiasa kwa sababu kila mmoja nchini hivi 2 sasa anajua matokeo yaliyowaweka madarakani hayatokani na kura za wananchi bali ni matokeo ya kutungwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

2. ⁠ Uchaguzi umeacha simanzi kutokana na mauji ya mamia ya Watanzania na hakuna jitihada za kuleta uwajibikaji kwa wale waliosababisha mauaji haya. Tume ya Jaji Chande ambayo iliundwa kwa ajili ya kuchunguza yaliyojitokeza kwenye Uchaguzi Mkuu 2025 badala ya kuzifuta machozi familia zilizopoteza wapendwa wao kutokana na mauaji ya mwaka 2025, imetia pilipili kwenye kidonda kwa kuja na hitimisho kuwa waliouawa walilipwa kwa ajili ya kuandamana na kwamba wale waliopotea ni kwa sababu zao binafsi.

3. ⁠ Siasa za ushindani wa kidemokrasia zimetoweka na mamlaka ya wananchi kuchagua viongozi imetekwa nyara na watu wachache waliojipa majukumu hayo. Vyama vya Siasa, ikiwemo CCM, haviendeshi tena siasa ya nchi badala yake, siasa imeachwa mikononi mwa kikundi hicho cha watu wachache

4. ⁠ Mshikamano wa kijamii umeyumba. Ishara ya wazi ni kitendo cha watu kufurahia mitandaoni misiba ya watu wenye itikadi na mirengo tofauti na wao 5. ⁠ Kuporomoka kwa heshima ya Tanzania kwenye majukwaa ya kimataifa. Tanzania sasa inajadiliwa kwenye majukwaa ya kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa (UN), Jumuiya ya Ulaya (EU) na Jumuiya ya Madola (The Commonwealth) kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kupunguza ushawishi wetu wa kimataifa.



TUMEFIKAJE HAPA?

Ni bahati mbaya sana, na ni vyema Watanzania kuliepuka hili, kwamba wengi wamefikishwa pahala kuamini kuwa mkwamo uliopo sasa umetokana na Uchaguzi Mkuu wa 2025. Ukweli ni kuwa yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 ni mripuko wa janga lilotengenezwa kwa muda mrefu.

Mkwamo wa kisiasa uliopo nchini ni janga ambalo limetengenezwa hatua kwa hatua katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita. Hivyo basi, si sawa kulitazama suala hili kwa kurejea tukio fulani mahsusi bila kuangalia mahusiano yake na matukio mengine tangu kurejeshwa tena kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Kilichojidhihirisha hivi sasa ni ukweli kwamba CCM ilikubali mfumo wa vyama vingi kwa shingo upande. Hivyo basi, badala ya kuiendeleza mifumo na taasisi huru za kidemokrasia, kwa miaka mingi CCM, kupitia Serikali zote mbili, imetumia dola kulinda maslahi yake dhidi ya maslahi ya Watanzania na vyama vyengine vya siasa ambavyo vilipaswa na vinapaswa kuwa na haki sawa kwenye uwanja ulio sawa wa siasa.

Tanzania hivi sasa imehama kutoka mfumo wa ushindani wa vyama vingi, kwenda katika mfumo wa siasa unaodhibitiwa na dola kupitia vyombo vya ulinzi na usalama (securocracy). Hivi sasa, ni vyombo hivyo ndivyo vinavyoamua nani awe kiongozi wa serikali za mitaa, diwani, mbunge, mwakilishi, Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano! Hali hii haikubaliki kwa sababu inapora mamlaka ya kikatiba ya wananchi ya kuchagua viongozi wao.

(TUZINUKUU IBARA YA 8 YA KATIBA YA MUUNGANO NA IBARA YA 9 YA KATIBA YA ZANZIBAR - ZINAZOSEMA MAMLAKA YA NCHI NI YA WANANCHI NA KWAMBA VYOTE VYA MADARAKA KATIKA NCHI VITAPATA MAMLAKA YAO KUTOKA KWA WANANCHI).

Kama tulivyotanabaisha, hali ya sasa ya demokrasia inayodhibitiwa na vyombo vya ulinzi na usalama (securocracy) haikuzuka tu siku moja. Hatua kwa hatua za ujenzi wa mfumo huo katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita ni kama ifuatavyo;

  • Kupuuzwa kwa mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali ya mageuzi makubwa ya mfumo wa kisiasa nchini kwa kuandika katiba mpya, kufutwa au kufanyiwa marekebisho makubwa kwa Sheria Kandamizi 40 na kufanyiwa mageuzi makubwa taasisi zote za kidola vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama. Hatua hii ilifuatiwa na kupuuzwa na kuvurugwa kwa mapendekezo kama hayo yaliyotolewa na Kamati ya Jaji Kisanga na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Warioba.
  • Hatua zote hizi zinathibitisha kukosekana kwa UTASHI kutoka Chama cha Mapinduzi na Serikali zake katika kuweka misingi madhubuti ya demokrasia na utawala wa sheria na haki.
2. ⁠ Kuzimwa kwa sauti ya umma (will of the people) kwenye chaguzi zote nchini kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2025. Kilichojitokeza mwaka 2025 kilikuwa kilele cha mwenendo wa CCM kupora haki ya umma kuchagua viongozi wake. Utofauti pekee baina ya wizi wa uchaguzi kabla ya mwaka 2020 na ule wa baada ya hapo ni kwamba wizi wa baada ya 2020 ulihusisha kuporwa kwa mchakato mzima wa uchaguzi hali inayopelekea kukosekana kwa uchaguzi wenyewe na badala yake kuwepo kwa UTEUZI!

3. Kukithiri kwa vitendo vya vyombo vya dola kuingilia uchaguzi na siasa kwa ujumla wake kwa manufaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

4. ⁠ Kuongezeka kwa mbinyo wa uwanja wa kisiasa na kiraia (shrinking of political and civic space) ikiwemo ukandamizwaji mkubwa wa haki za kiraia kama vile uhuru wa habari, haki ya kuabudu, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kuchangamana n.k. 5

5. ⁠ Kukithiri kwa vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo kukithiri kwa vitendo vya utekaji na mauwaji ya raia. Vitendo vyote hivi vilitekelezwa hatua kwa hatua na kujenga msingi wa hali ya kisiasa ambayo tunayo leo. Katika kukabiliana na hali hiyo, ni lazima tuelewe mahusiano ya matukio yote haya kwa ujumla wake.

Maswali mawili nitayaacha wazi kwa mjadala;

Nani anaongoza na kudhibiti mambo haya (who is in control?) b. Nani ananufaika na hali hii? Swali hili ni muhimu kwa sababu kwa maoni yetu, ingawa kwa nje, CCM kinaonekana kuwa mnufaia mkuu, lakini uhalisia wa mambo ni kwamba hata CCM chenyewe kimeshikwa mateka na kinaathirika na hali hii.

Ni vizuri tutafakari na kujua ni nani hasa ananufaika na hali hii.

KIINI CHA VURUGU. UCHAGUZI KUVURUGWA: UZOEFU WA ACT WAZALENDO KATIKA UCHAGUZI

ACT Wazalendo ndio Chama pekee cha upinzani kilichoshiriki Uchaguzi Mkuu 2025, kusimamisha wagombea nchi nzima na kufanya kampeni za kishindo Tanzania Bara na Zanzibar. Hivyo basi, ni sahihi kusema kwamba ACT Wazalendo kina uzoefu mkubwa zaidi juu ya yaliyotokea katika uchaguzi huo. Ninaomba, kwa niaba ya Chama kutoa uzoefu wetu kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.

UZOEFU WA BARA

Mwaka 2025, kwa Tanzania Bara kama ilivyokuwa kwa Zanzibar hakukuwa na uchaguzi bali upangaji matokeo. Vyombo vya dola kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi (INEC) na Chama Cha Mapinduzi viliamua nani atangazwe mshindi, nani asitangazwe 6 kuwa mshindi. Hivyo basi, msimamo wetu ACT Wazalendo ni kuwa mwaka 2025 hakukuwa na uchaguzi ambao unaweza kuitwa kuwa wa huru, haki na kuaminika. Hoja zetu juu ya hili ni kama ifuatavyo;

1. Kuenguliwa kwa Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano, Ndugu Luhaga Joelson Mpina na wagombea Ubunge 54 wa ACT Wazalendo

2. ⁠ Uchaguzi kutofanyika katika sehemu kubwa ya majimbo kama vile Ubungo, Kibamba, Kinondoni, Kawe, Ilemela, Nyamagana n.k lakini matokeo ya mwisho yakatangazwa.

3. ⁠ Mauaji ya mamia ya wananchi walioandamana siku ya uchaguzi na siku zilizofuata.

4. ⁠ Vyombo vya dola kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi kuendeleza mwenendo wa kuwabughudhi na kuwanyima haki zao mawakala wa wagombea wa vyama vya upinzani.

5. ⁠ Maofisa wa Tume ya Uchaguzi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na makada wa CCM kushiriki katika upigaji wa kura kwa idadi waipendayo kwa ajili ya wagombea wa CCM

6. ⁠ Majumuisho ya kura kutofanyika kwa asilimia kubwa ya majimbo 7

7. ⁠ Wasimamizi wa uchaguzi kutangaza matokeo wanayoamua wao wenyewe kinyume na matokeo kutoka vituoni. Kwa hayo tuliyoyaeleza na yale ambayo hatujayaeleza kutokana na ufinyu wa muda, ACT Wazalendo tunahitimisha kuwa Mwaka 2025 hakukuwa na uchaguzi nchini bali upangaji wa matokeo.

B. UZOEFU WA ZANZIBAR

Tokea kurudishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992, uendeshaji wa chaguzi umekuwa ukigubikwa na vitendo vya ukiukuwaji mkubwa wa taratibu za chaguzi huru, haki na uwazi. Jambo hili limejenga mizizi ya chuki kwa wananchi kwa kuona kuwa matakwa yao hayasikilizwi kupitia sanduku la kura.

Kwa masikitiko makubwa, kila uchaguzi mmoja unapomalizika, na vyama vya upinzani na wadau wa demokrasia wanapolalamikia juu ya ukiukwaji wa taratibu, badala ya kujipanga kurekebisha kasoro zilizojitokeza ndipo mamlaka husika zinapojipanga kwa ukiukwaji mkubwa zaidi wa taratibu kwa chaguzi zinazofuata.

Kilele cha uvurugaji wa Chaguzi kilishuhudiwa mwaka 2015 ambapo kwa upande wa Zanzibar uchaguzi ulifutwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar, Ndugu Jecha Salim Jecha kwa maamuzi yake binafsi wakati Tume ikiwa imeshatangaza matokeo ya Urais kwa majimbo 31 kati ya majimbo 50.

Aidha Matokeo ya Uwakilishi na Udiwani kwa majimbo yote 50 yalikwishatangazwa na washindi kukabidhiwa shahada za kuthibitisha kuchaguliwa kwao na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, mwenye mamlaka ya kutengua matokeo hayo yakishatangazwa ni Mahakama pekee lakini Zanzibar imewezekana kufuta Uchaguzi mzima kinyume cha Katiba na Sheria na hakuna aliyethubutu kukemea.

Pamoja na kwamba lawama zote alishushiwa Ndugu Jecha [Marehemu] lakini wengi tunafahamu kwamba Ndugu Jecha alilazimishwa na vyombo vya Dola kutangaza matokeo baada ya Vikosi vya Serikali “kuteka” Kituo Kikuu cha kutangaza matokeo Bwawani Hotel.

Aidha, vikosi hivyo vilimchukua Makamu Mwenyekiti wa Tume Jaji Abdulhakim Ameir Issa ili kumzuia asiendelee na zoezi la kutangaza matokeo kwa mujibu wa Sheria. Haya yote yalifanyika mchana kweupe na hakuna aliyehoji au kupaza sauti.

Uchaguzi wa mwaka 2020 ndio ulivunja rikodi kabisa kwani huu haukusubiri kura kuhesabiwa na kubadilisha matokeo kama ilivyozoeleka katika chaguzi za nyuma. Kulishuhudiwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu kuanzia kuenguliwa kwa wagombea 16 wa Uwakilishi na 12 wa Ubunge, uingizaji wa karatasi za kura kwenye masanduku, karatasi za kura kuzagaa mitaani, mawakala kutolewa vituoni na baadhi ya wagombea kuwekwa kizuizini na kupigwa na kuumizwa vibaya huku kukiwa na vitisho vikubwa kutoka kwa vyombo vya ulinzi na usalama. Kuhusu matokeo ya Uchaguzi, kura hazikuhesabiwa wala kufanyiwa majumuisho.

Hata kura za Urais wa Zanzibar hazikuhesabiwa wala kufanyiwa majumuisho. CCM iliamua kuchukua viti takriban vyote vya Uwakilishi na Ubunge [ikibakisha viti vine tu vya Ubunge na Vinne vya Uwakilishi] na asilimia 80 ya kura za Urais wa Zanzibar.

Kibaya zaidi, watu 21 waliuliwa na vyombo vya dola, takriban wote wakiwa majumbani mwao. Watu 18 walijeruhiwa na kuachwa na ulemavu wa kudumu. Watu 48 waliachwa na majeraha makubwa, wanawake kadhaa walibakwa baadhi yao mbele ya familia zao.

Watu zaidi ya 1000 walipata madhara ya namna mbali mbali. Watanzania walifahamu maafa haya lakini wachache sana waliopaza sauti. Pamoja na maafa hayo, ACT Wazalendo ilikubali kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya makubaliano kuwa mambo 9 kadhaa yatafanyiwa marekebisho ili yaliyotokea katika Uchaguzi wa 2020 yasijirudie tena. Kwa bahati mbaya, mamlaka hazikutaka kuchukua hatua yoyote ile kurekebisha hali hiyo.

ACT ilitumia muda wote wa kuwemo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ikiwa ni pamoja na kuonana na Viongozi wakuu Bara na Zanzibar, kuwaandikia na kushiriki kwenye kamati zote zilizoundwa pamoja na vikosi kazi bila mafanikio yoyote.

Kutokana na hali hiyo, tukaingia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 katika mazingira mabaya zaidi, na kwa hiyo haishangazi kuona katika uchaguzi wa mwaka 2025, uvurugwaji wa uchaguzi ulikuwa ni mkubwa zaidi ukishindana na ule wa mwaka 2020 lakini ukiwa na sifa zile zile.

Miongoni mwa uvurugaji uliofanywa ni kama vile watu wenye sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura zaidi ya 21,000 kunyimwa haki hiyo kwa makusudi, kuwapa haki watu zaidi ya 65,000 wasio na sifa ya kuandikishwa kuwa wapiga kura, upigaji wa kura wa zaidi ya mara moja, kujaza karatasi za kura katika masanduku ya kura, karatasi za kura kuzagaa mitaani, mawakala kuzuiliwa na kutolewa katika vituo vya kupigia kura, kura kutokuhesabiwa, na kutangazwa matokeo yaliyopikwa kinyume na matokeo sahihi kwa yale maeneo ambapo kura zilizesabiwa.



MCHANGO WA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA KATIKA KUVURUGA CHAGUZI;

Katika chaguzi zote zilizofanyika nchini tokea kuanzishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, vyombo vya ulinzi na salama vimekuwa na nafasi kubwa sana katika kuvuruga chaguzi badala ya kuhakikisha kuwa chaguzi zinafanyika kwa amani, salama na utulivu.

Kazi ya vyombo hivi imekuwa ni kulinda maslahi ya CCM na kwamba yeyote anayepingana na CCM kwao wao ndio adui wa 10 Taifa. Na kwa sababu hii haishangazi kuviona vyombo vyetu vikichukua hatua kali ikibidi hata kuuwa wale wanaowaita maadui wa nchi hii kwa kuipinga CCM.

Chukulia mfano wa yaliyotokea katika uchaguzi wa mwaka 2015 Kituo cha kujumuisha kura za Urais wa Zanzibar na kutangaza matokeo pale Hoteli ya Bwawani kilivamiwa na JWTZ wakiongozwa na Meja General Said Ali Juma Shamuhuna.

Jeshi hilo lilisitisha zoezi la majumuisho na utangazaji wa matokeo wakati huo huo Jeshi la Polisi lilitumika kumteka kwa nguvu aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jaji Abdulhakim Ameir Issa ili asiendelee na zoezi la kutangaza matokeo kwa majimbo 19 yaliyobakia wakati Mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha, akiwa amedhibitiwa na vyombo vya ulinzi na usalama kabla ya kutangaza kufuta Uchaguzi.

Mfano wa pili ni yale yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, ambapo vyombo vya ulinzi na usalama vilisimamia uvurugaji wa uchaguzi na kusababisha maafa makubwa kuwahi kutokea ikiwa ni pamoja na mauwaji ya wanananchi 21, watu kadhaa kupigwa na kusababishiwa ulemavu wa kudumu, udhalilishaji wa kijinsia na ubakaji, na maelfu kutekwa na kuwekwa vizuizini.

Haya yote yamefanyika ili kukisafishia njia Chama Cha Mapinduzi kubakia madarakani kwa njia ya kupora mamlaka kwa nguvu, kinyume na matakwa ya wananchi na kinyume na Katiba. Uchaguzi wa mwaka 2025 ulikuwa ni muendelezo wa Uchaguzi wa mwaka 2020, chini ya Uongozi wa makamanda wa JWTZ waliokabidhiwa Vikosi vya SMZ chini ya uongozi wa Azana Hassan Msingiri wa KMKM na Said Ali Juma wa Valantia, operesheni ya kubaka demokrasia kwa kuongoza vikosi vya ulinzi ikiwa ni pamoja na kuteka vituo vya kupigia kura, na kuwatoa nje ya vituo mawakala wa vyama vya upinzani.

Aidha uchaguzi huu ulivuka mipaka pale Idara ya Usalama wa Taifa, hasa kupitia kwa baadhi 11 ya Maofisa wa Usalama wa Wilaya (DSO) na hasa kwa kisiwa cha Pemba, kuingia katika biashara ya kuuza ubunge na uwakilishi kwa Wagombea wa CCM waliotoa pesa.

Zipo taarifa za baadhi ya DSO kupokea pesa kuanzia Tsh 10,000,000 na kulazimisha wagombea wa CCM watangazwe kuwa washindi. Kutokana na uharamia huo yapo majimbo Pemba ambapo Wagombea wa CCM waliopata chini ya kura 400 wametangazwa kuwa Washindi kwa msaada wa DSO wakishirikiana na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa.

Kwanini Zanzibar imebaki na utulivu kabla, wakati na baada ya Uchaguzi wa 2025? Pamoja na yote yalioyoelezwa hapo juu, Zanzibar imebaki kuwa na utulivu wa muda na sio amani endelevu kwani watu wake wanaendelea kuishi na machungu moyoni kwa namna wanavyokatishwa tamaa na mfumo wa demokrasia.

Kwa kutambua maandalizi makubwa yaliyofanyika kwa vyombo vya ulinzi na usalama ambapo viashiria vyote vilionyesha uwezekano wa kutokea kwa maafa makubwa zaidi ya yale ya mwaka 2020 kama wananchi wangejaribu kusimama kidete kupigania haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Pamoja na kutoa maonyo kwa viongozi wakuu wa nchi, ikiwa ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kabla ya uchaguzi na kuonana na viongozi kadhaa wa makundi ya kijamii na viongozi wa dini, hakuna hatua yoyote ya kurekebisha hali hiyo iliyochukuliwa.

Busara za Viongozi wa ACT Wazalendo ndio pekee zilizoivusha Zanzibar na maafa mengine wakati wengine wakijiandaa kuuwa. Wananchi wanaponasihiwa kutulia na viongozi wao wanaweza kusikiliza kwa wakati fulani, sio lazima watii na kuzingatia muda wote. Wanapochoka ndipo wanapochukua hatua na baadae dola 12 kutumia nguvu kubwa sana za ziada kuwatuliza wananchi. Hilo ndilo lililotokea Oktoba 29 na siku zilizofuata. Dharau na kutokutibu viashiria mapema.



KUDHOOFISHWA KWA MIUNDOMBINU YA DEMOKRASIA NA UTAWALA BORA

Yote yaliyofanyika katika uwanja wa siasa na chaguzi yamewezekana na yanaendelea kwa sababu ya hatua za makusudi za kudhoofisha Taasisi za demokrasia na utawala bora katika Nyanja zote. Kuanzia Mahkama, Bunge na Baraza la Wawakilishi, Vyombo vya Habari, Vyama vya Wafanyakazi, NGOs, Taasisi za Elimu ya Juu ikiwemo Serikali za Wanafunzi, Wasanii, Vyama vya Ushirika na Vikundi vya Wakulima. Nyingi ya taasisi hizo sasa zimejazwa “uchawa”.

Udhibiti wa taasisi hizo umekuwa mkubwa sasa kuliko hata wakati wa Chama kimoja na matokeo yake nyingi ya taasisi hizo sasa ni dhaifu hata kuliko wakati wa Chama kimoja. Vyama vya siasa navyo vingi vimetekwa na kufanya kazi chini ya mfumo na vichache vilivyobaki vimekuwa katika vita ya kudumu dhidi ya hujuma zinazofanywa na taasisi za umma zilizopaswa kuzilinda.

Matokeo ya mfumo huo, hata CCM yenyewe imo katika wakati mgumu, hata wakatae kwa kiapo lakini kila Mtanzania anafahamu yanayoendelea ndani ya CCM, LABDA inaitika ule msemo wa Kiswahili kuwa MCHIMBA KISIMA HUINGIA MWENYEWE!

TUNATOKAJE TULIPO?

Kwa mtu yeyote yule anayejali maslahi mapana ya nchi hii dhidi ya maslahi yake na wenzake, hawezi kufurahia hali ya kisiasa iliyopo nchini. Wanaoweza kuifurahia hali hii ni mafisadi wachache wanaonufaika na mpasuko wa kitaifa unaozalisha kutokuwepo kwa 13 uwajibikaji. Katika kukabiliana na hali tuliyonayo, ACT Wazalendo tunapendekeza maeneo makuu matatu yanayohitaji tafakuri na mazingatio;

  • HAKUNA MARIDHIANO BILA UKWELI, HAKI NA UWAJIBIKAJI
  • Kwa pande zote mbili za Muungano kwa maana ya Tanzania Bara na Zanzibar, Marais wamenyoosha kile kinachoitwa “mkono wa maridhiano”. Hata hivyo, ACT Wazalendo tumetafakari kwa kina na tumejiuliza swali moja muhimu; tunaridhianaje katika hali tuliyo nayo? Maridhiano yanaanzaje katika hali ambayo makumi ya viongozi wa kisiasa na wanaharakati wapo magerezani na mamia hawajulikani walipo?

  • Tunaanzaje maridhiano ikiwa maelfu bado wanaombeleza mauwaji ya ndugu zao waliouawa kwa risasi. Mathalan, tunaielezaje lugha ya maridhiano familia ya Dafrosa, Diwani wetu wa Kata ya Sirari huko Tarime ambaye aliuawa kwa kuvunjwa kichwa, mbavu na viungo vingine vya mwili na dhambi yake pekee ikiwa ni kuwa mgombea wa upinzani?

  • Kwa Wazanzibari, tutawaeleza vipi lugha ya maridhiano bila kwanza kuonesha nia ya dhati ya utekelezaji wa hoja ambazo Wazanzibari wamekuwa wakizidai miaka nenda miaka rudi? Tunaingiaje kwenye maridhiano ikiwa kura ya mapema ama “wizi wa mapema” ukiendelea kuwepo na Serikali ya CCM ikiwa haina nia hata kidogo ya kuiondosha? Maoni ya ACT Wazalendo ni kwamba kinachopaswa kutangulia kabla ya maridhiano ni UKWELI, HAKI NA UWAJIBIKAJI.
  • Hii ni hatua ya kwanza; ni ngumu lakini ya lazima. Bila kuwa wakweli juu ya makosa yaliyotokea Oktoba 2025, kutoa haki kwa wahanga wa uchaguzi huo kwa kufanya uchunguzi huru na kuwawajibisha wale wote waliosababisha mauwaji hayo hasa vyombo vya ulinzi na 14 usalama, hakuna mafanikio ya uhakika yanaweza kupatikana kupitia wito wa maridhiano ya maneno matupu.

  • Uzoefu wa Nchi kadhaa umeonesha kuwa wamepitia hatua hii ya kuweka bayana UKWELI kama hatua ya awali ya kuelekea Maridhiano ya kweli. Baada ya hatua hizo, kwa pande zote mbili (Tanzania Bara na Zanzibar) kuundwe Tume za Kudumu za Utengamano, Haki na Maridhiano katika Taifa (National Cohesion, Justice and Reconciliation Commissions), ambazo zinapaswa kuanzishwa kisheria (statutory bodies).

  • Tume hizo ziongozwe na watu huru na wanaoheshimika kwenye jamii na wajumbe wake wote wawe na sifa hizo hizo. Moja ya kazi zake iwe ni kukinga athari mbaya kwa kuchukua hatua za mapema kwa kila kiashiria kinachojitokeza ambacho kikiachwa kinaweza kuliingiza taifa ama jamii katika utengano au ukosefu wa haki.

  • MFUMO MZIMA WA KIUTAWALA, KIUTENDAJI NA KIUSALAMA UNAPASWA KUFUMULIWA

  • Kama tulivyoeleza awali, hali ya sasa ya kisiasa inatokana na janga lililojengwa kwa miongo mitatu na kuathiri mfumo mzima wa uendeshaji wa nchi yetu. Kutibu hali hiyo, hakuna hatua moja inayoweza kufaa. Kwa hali ilivyo, hata baada ya utawala wa sasa, utawala mwingine utakapokuja, kuna uwezekano wa mambo kuwa yale yale! Kurekebisha hali hii tunahitaji kufumua mfumo mzima wa uendeshaji wa nchi yetu.

  • Tunapaswa kuandika KATIBA MPYA kwa mchakato shirikishi; tunapaswa kubadili kabisa uwajibikaji wa vyombo vya ulinzi na usalama na mfumo mzima wa utumishi wa umma ili uwajibike kwa wananchi badala ya kuwajibika kwa Chama Cha Mapinduzi.

  • Katika kuipata KATIBA MPYA, sisi tunaona hatua zifuatazo zinapaswa kuzingatiwa;

  • Suala la Muungano ambalo limekuwa kikwazo linaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kuundwa TUME YA WATAALAMU itayopitia mambo yote ambayo yana migogoro ikiwemo mambo yaliyoainishwa na Serikali zote mbili lakini hayajatekelezwa.
  • Kupitiwa upya na kufanyiwa marekebisho kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Constitutional Review Act 2011) na Sheria ya Kura ya Maoni (Referundum Act 2011) ili kukidhi matakwa ya sasa na kuhuisha mchakato wa Katiba Mpya. Muswada wa sheria ya kurekebisha sheria hizi uwasilishwe na kupitishwa Bungeni katika Mkutano wa Bunge unaoendelea.
  • Uitishwe Mkutano wa Kitaifa (National Sovereign Conference) utaoshirikisha wadau wote nchini ili kupata muafaka wa masuala juu ya Katiba ambayo ni nyeti na hayana muafaka ikiwemo Muundo wa Muungano.
  • Iundwe Timu ya Wataalam Wabobezi (Committee of Experts) ili kuandaa rasimu mpya ya Katiba. iv. Iitishwe kura ya maoni (Referundum) ili wananchi waamue kukubali au kukataa rasimu ya katiba itakayoandaliwa. Mbali ya Katiba Mpya, ACT Wazalendo tunaamini tunapaswa KURUDI KWENYE MISINGI kwa kuyarudia MAPENDEKEZO 16 YOTE YA RIPOTI YA TUME YA JAJI NYALALI ambayo yaliweka mambo yote muhimu yanayopaswa kuwepo katika nchi inayofuata DEMOKRASIA YA VYAMA VINGI.
Miongoni mwao ni:-

a). Kufutwa au kurekebishwa kwa Sheria Kandamizi 40 zilizoorodheshwa kwenye Kitabu cha Tatu cha Ripoti ya Tume ya Nyalali.

b). Ziangaliwe na Sheria nyingine Kandamizi za ziada zilizotungwa baada ya 1992 kama Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015, Sheria ya Takwimu ya 2025, Sheria ya huduma za habari ya 2016, Sheria ya Vyama vya siasa, 1992 (Hasa mabadiliko yake makubwa ya 2019 ambayo yamempa madaraka makubwa Msajili wa vyama vya siasa na Sheria ya Tume huru ya Uchaguzi ya 2024.

c). Kutungwa kwa Sheria mpya ya Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itakuwa HURU KWELI kutoka ngazi ya Taifa hadi ngazi za vituo vya kupigia kura, kuhesabu na kufanya majumuisho. Baada ya Sheria, hatua za uundaji wa TUME HURU zianze mapema kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2029 na Uchaguzi Mkuu wa 2030.

d). Kutenganishwa kwa nafasi za utawala (administrative set-up and structures) na siasa ili ngazi zote za tawala za mikoa, wilaya, tarafa, hadi kata ziwe huru na zitumikie umma badala ya chama cha siasa kilichopo madarakani.

e). Kufanya mageuzi makubwa ya utumishi wa umma ili kuutenganisha na siasa na kujenga a PROFESSIONAL AND DEPOLITICISED PUBLIC SERVICE.

f). Kutekelezwa kwa hatua za kikatiba, kisheria, kikanuni, kiutawala na kimafunzo za kuviondoa kwenye utii wa kisiasa vyombo vya ulinzi na usalama katika nchi (depoliticisation of defense and security organs). Katika hili, pengine mapendekezo ya Tume ya Rais iliyochunguza Mfumo wa Haki Jinai yanaweza yakasaidia.

g). Vyombo vya Habari vya umma kufanyiwa mageuzi ili vitofautishe matangazo ya shughuli za serikali na za umma na zile za chama kinachotawala, na panapokuja matangazo ya shughuli za vyama vya siasa basi vyama vyote vitendewe haki sawa.

h). Kuweka uwanja wa siasa ulio huru na sawa kwa vyama vyote ikiwemo kutekeleza pendekezo la Tume ya Nyalali lililokitaka Chama Cha Mapinduzi kurudisha mali zote ilizojilimbikizia wakati wa chama kimoja ambazo zilitokana na michango ya wananchi wote au mapato ya Serikali.

i). Kuchukuliwa hatua ya kutoa elimu ya uraia juu ya mfumo mpya wa demokrasia ya kweli ya vyama vingi tunaokusudia kuujenga.

TUREJESHE THAMANI YA KURA

Kwa hali tuliyonayo, thamani ya kura ya Mtanzania imetoweka. Swali tunalopaswa kujiuliza ni kiongozi aliyepatikana kwa rushwa au kupachikwa anawezaje kuwa mwadilifu? Anawezaje kupambana kwa dhati dhidi ya rushwa na ufisadi wakati yeye mwenyewe amepatikana kifisadi? 18 Kwa ajili ya kuliponya Taifa, ni lazima sauti ya wananchi iheshimiwe kupitia sanduku la kura. Hili linawezekana kupitia uchaguzi ambao ni huru na wa haki. Uchaguzi huru na wa haki utapatikana pale tu ambapo tutakuwa na Tume Huru ya Uchaguzi inayosimamia uchaguzi kwa weledi badala ya kulinda maslahi ya CCM kama ilivyo sasa.

HATUA ZOTE nilizozitaja hapa zinahitaji MUAFAKA WA KITAIFA utakaotupeleka mbele kwa pamoja kama TAIFA. Kwa hivyo, tunahitaji kuanzisha jukwaa la majadiliano ya kitaifa litakaloongozwa na misingi tuliyoitaja ya UKWELI, HAKI NA UWAJIBIKAJI ili kukubaliana juu ya namna bora ya kuzifikia hatua hizo.

HITIMISHO

Kama tulivyoeleza kwenye utangulizi wetu, Tanzania ipo njia panda. Tunapaswa kuchagua njia inayofaa kwa nchi yetu baina ya njia ya ukweli, haki na uwajibikaji au njia ya ubabe wa vyombo vya dola. Baada ya yale yaliyotokea Oktoba 2025, kwa maoni yetu, kama nchi hatuna namna isipokuwa kuchagua njia ya ukweli, haki na uawajibikaji.

Ni uamuzi tunaopaswa kuufanya kwa pamoja kama Taifa. Viongozi tuna wajibu wa kuongoza mchakato huu. Kama hatutafanya hivyo kwa kuhofia kupoteza maslahi yetu, umma, kama ilivyokuwa kwa matukio ya Oktoba 2025 utatuongoza kwenye matukio, pengine makubwa zaidi, kuliko yale ya Oktoba 2025. Kwa pamoja,

TUSIKUBALI!

Othman Masoud Othman,

Mwenyekiti wa Taifa ACT Wazalendo

16 Mei, 2026. Dar es Salaam.
 
Leo Mei 16, Chama cha ACT Wazalendo inafanya mjadala wa Mjadala wa kitaifa kuhusu mwelekeo na khatima ya Tanzania, uliokusanya makada na viongozi wa chama hicho, wasomi, wanadiplomasia na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

View: https://www.youtube.com/live/yw9QUyBkdXE?si=_psmu3H58c7p20re

Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud, amesema Tanzania ipo katika mkwamo wa kiuongozi na tusipoangalia tunawea kuingia kwenye mkwamo mkubwa zaidi.

bilshaka yoyote,
patakua na ngonjera, mpipasho na uropkaji tu usio na athari zozote kwa taifa letu

just porojo za kupoteza muda tu 🐒
 
Back
Top Bottom