ACT Wazalendo
JF-Expert Member
- May 5, 2014
- 631
- 1,577
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi maalum wa Akaunti ya Pamoja ya Fedha za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni fungamano baina ya nchi mbili huru, Tanganyika na Zanzibar, zilizoungana na kuweka misingi, kanuni na taratibu ili zifuatwe kwa lengo la kukuza na kuimarisha umoja na mshikamano, kwaajili pia ya kuhamasisha maendeleo ya pande hizo kuu.
Yapo mambo muhimu yaliyowekwa na kuendelea kujiri kupitia muungano huo yakipewa baraka za majina mbali mbali, mara "Articles of Union", "Masharti ya Kuungana", Misingi, Kanuni, Ibara, na hatimaye au hata yalivyozoeleka baadhi yao kama "Kero za Muungano" au vinginevyo.
Miongoni mwa hayo ni suala la Akaunti ya Pamoja ya Fedha za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ambavyo Ibara ya 133 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1984 Toleo la 2010 inaelekeza na kwamba hiyo itakuwa sehemu ya Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali, kuhifadhi Fedha za Muungano, kwa madhumuni ya shughuli za Jamhuri ya Muungano, kwa mambo ya Muungano.
Kwa masikitiko makubwa ni kwamba Ibara hiyo imekuwa haitekelezwi tokea utaratibu wa Akaunti ya Pamoja ya Fedha ulipowekwa katika Katiba ya mwaka 1984 au tuseme tangu kuasisiwa kwa Muungano huo mnamo Tarehe 26 April 1964, ambapo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hajawahi kutoa taarifa ya ukaguzi kuhusu mapato na matumizi yanayotokana na au yanayohusu utekelezaji wa Mambo ya Muungano.
La kusikitisha zaidi ni kukosekana kwa uwazi na taarifa sahihi katika eneo hili maalum na muhimu kwa ustawi wa Jamhuri Mbili huru zilizoungana, hali ambayo bila shaka inatishia ile hima, hamasa, shauku na imani ya kweli katika kuulinda Muungano wetu.
Chama cha ACT Wazalendo kinaamini kuwa hili ni eneo ambalo ni kero kubwa katika uendeshaji wa Muungano wetu ambao hauna budi kuimarishwa na kuendelezwa, ingawa kwa kuzingatia sasa nia safi, azma njema na heshima kubwa kati ya Nchi mbili huru zilizoungana.
Tunamuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi maalum wa eneo hili, ili azishauri mamlaka kupitia Tume ya Pamoja ya Fedha kuhusu mfumo wa shughuli za fedha kwa Jamhuri ya Muungano, na pia uhusiano katika mambo ya kifedha kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Pamoja na yote hayo, na kwa kuzingatia ukweli na uelewa wa dhati wa eneo hilo, kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Mheshimiwa, Samia Suluhu Hassan aliwahi kushika wadhifa wa Mwenyekiti wa Kamati ya Pamoja ya Mawaziri wa pande zote katika kujadili na kukabili kero za Muungano; tunatoa wito kwa Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na mwenzake Rais wa Zanzibar na Mwyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dokta Hussein Ali Hasan Mwinyi, walichukulie jambo hili kwa uzito wa pekee kwaajili ya kulinda maslahi ya Zanzibar, na ili pia historia ije kuwakumbuka.
Pamoja na Salamu za Chama Chetu!
ACT-WAZALENDO! TAIFA KWANZA LEO NA KESHO!
MABADILIKO NA UWAZI! CHUKUA HATUA!
Ahsanteni sana,
................................
Salim Bimani,
Kaimu Naibu Katibu Mkuu, ACT Wazalendo, Zanzibar
leo tarehe 17/04/2021