Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Chama cha ACT Wazalendo kimelaani matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu, unyanyasaji wa kijinsia, na ukiukwaji wa mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaodaiwa kufanywa na mamlaka za Serikali ya Tanzania.
Matukio hayo ni pampoja na kuzuiliwa na hatimaye kurejeshwa nchini Kenya kwa wanasheria na wanaharakati waliofika nchini Mei 18 kwa ajili ya kuhudhuria kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam.
Waliorejeshwa ni pamoja na Kiongozi wa Chama cha Ukombozi wa Watu (People’s Liberation Party - PLP) kutoka Kenya, Mwanasheria Martha Karua, pamoja na Jaji wa zamani wa Mahakama ya Juu ya Kenya, Jaji Willy Mutunga.
Mbali na wanasheria hao, baadhi ya wanaharakati wengine kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walikamatwa, kuwekwa kizuizini kwa zaidi ya siku tatu, kuteswa, na kurejeshwa makwao wakiwa na majeraha na maumivu.
Miongoni mwao ni Agatha Atuhaire kutoka Uganda, aliyepatikana karibu na mpaka wa Mtukula, na Boniface Mwangi kutoka Kenya, aliyepatikana eneo la Kaunti ya Kilifi karibu na mpaka wa Tanzania na Kenya baada ya kushikiliwa kwa muda nchini Tanzania. Wanaharakati hawa wametoa ushuhuda kuhusu ukatili walioupitia wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola vya Tanzania.
Kutokana na matukio hayo, chama hicho kimeitaka Serikali na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuunda chombo huru cha uchunguzi kuhusu matukio haya ya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya raia wa Kenya na Uganda waliokuwa nchini Tanzania.
“Matukio haya yanatia doa heshima ya kihistoria ya Tanzania kama taifa lililowahi kuwa kimbilio la wapigania uhuru, na kuchochea umoja wa bara la Afrika kwa kuwasha Mwenge wa Uhuru na kuusimika katika kilele cha Mlima Kilimanjaro Umulike na kuangaza kuleta matumaini palipo na kukata tamaa, Upendo palipo na Uadui na heshima palipo na chuki,” amesema Waziri kivuli wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Janeth Joel Rithe alipozungumza na waandishi wa habari leo Mei 29 Dar es Salaam.
ACT Wazalendo imemtaka Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki atoe maelezo ya kina kuhusu sababu za kukamatwa, kuzuiliwa, kuteswa na kurejeshwa kwa raia hao wa Afrika Mashariki.
Pia ameeleza kusitishwa na kauli zisizo zilizotolewa na baadhi ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambazo zinakiuka Katiba na Kanuni za Kudumu za Bunge.
“Wabunge waliotoa kauli za matusi na dharau dhidi ya wanaharakati hao wafikishwe mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kwa mujibu wa maelekezo ya Spika wa Bunge, ikiwa kweli kauli hizo si msimamo rasmi wa Bunge. Hii ni pamoja na Tauhida Gallos (Mb) na Maryam Omar Said (Mb),” amesema.
Chama hicho pia kimeekeza kusikitishwa na kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa Sera ya Mambo ya Nje (Toleo la 2024), ambapo alielekeza vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje kudhibiti wanaharakati wa Afrika Mashariki kuingia nchini, akiwataja kuwa ni watovu wa adabu.
“Kauli hii ni kinyume na Tamko la Sera ya Mambo ya Nje ibara ya 34 na 35 inayosisitiza ushirikiano wa kikanda na mtangamano.
“Mwenendo huu unavunja kwa dhahiri Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hususan kipengele kinachotoa haki ya raia wa nchi wanachama kusafiri, kuishi na kufanya kazi katika nchi yoyote ya Jumuiya bila ubaguzi,” amesema.