TITO MAGOTI HAJAKAMATWA, AMETEKWA!
Baada ya shinikizo kubwa kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari la kutaka kuachiwa huru kwa Mwanaharakati na Afisa wa Kitengo cha Elimu kwa Umma wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Ndugu Tito Magoti, hatimaye Jeshi la Polisi lilijitokeza jana jioni na kukiri kuwa linamshikilia.
Kauli ya Jeshi hilo iliyotolewa na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Lazaro Mambosasa imeacha maswali mengi bila ya majibu. Taarifa hiyo imesheheni mapungufu mengi ya kisheria na kimantiki. Kwa mazingira yaliyosemwa na Kamanda Mambosasa, ni dhahiri kuwa Ndugu Tito Magoti ALITEKWA na sio kukamatwa na polisi kama anavyosema Kamanda Mambosasa.
Kukamata watuhumiwa (arrest) kunaendeshwa kwa mujibu wa sheria. Jeshi la Polisi haliwezi kumkamata mtu bila kuzingatia sheria. Kwa kilichofanyika kwa Tito, hakina tofauti na utekaji.
Ili atuaminishe kuwa Tito Magoti alikamatwa na polisi kama anavyodai na sio kutekwa, Kamanda Mambosasa atujibu maswali yafuatayo;
1. Kwa nini kuchukuliwa kwa Tito kulikuwa na taswira ya utekaji? Kwa nini watu waliomchukua walimchukua kimabavu akishuka kwenye bodaboda, kumpiga pingu na kutokomea naye kusikojulikana? Kwa nini hawakufuata utaratibu wa kisheria wa kujitambulisha, kueleza kosa na kuondoka naye kiungwana? Tito alikuwa na tishio gani kustahili kukamatwa kama kuku?
2. Tito Magoti ni mfanyakazi anayefahamika wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu. Kwa nini Jeshi la Polisi halikuwasiliana naye aende polisi kwa mahojiano au kumfuata ofisini kwake?
3. Kwa nini Tito Magoti hakupewa haki ya kuwataarifu ndugu, mwajiri na mwanasheria wake kuhusu kukamatwa kwake?
4. Kwa nini kulikuwa na kupishana kwa taarifa za Jeshi la Polisi? Kwa nini Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni Mussa Taibu alikana kushikiliwa kwa Tito alipoulizwa na waandishi wa habari mapema baada ya Tito Magoti kuchukuliwa?
5. Kwa nini Kamanda Mambosasa amejitokeza baadaye kwa kuchelewa baada ya msukumo mkubwa kushinikiza Tito aachiwe?
6. Kwa nini Kamanda Mambosasa hasemi Tito yupo Kituo gani?
7. Kwa nini Tito hajapewa haki yake ya kuonana na mwanasheria wake? Anahojiwaje bila kupewa haki ya mwanasheria wake kuwepo?
6. Kwa nini Kamanda Mambosasa hajasema kosa analotuhumiwa nalo Tito?
7. Kwa nini Tito Magoti hajafikishwa mahakamani licha ya masaa 24 kupita tangu achukuliwe?
RAI YETU
Kutokana na mazingira haya tata yanayoligubika suala la kuchukuliwa kwa Tito Magoti, tunatoa rai ifuatayo;
1. Tito Magoti aachiwe huru mara moja.
2. Kama kuna makosa anatuhumiwa nayo, Tito Magoti afikishwe mahakamani.
3. Jeshi la Polisi limpe Tito Magoti haki ya kuonana na ndugu, mwajiri na mwanasheria wake.
Ado Shaibu,
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano na Umma,
ACT Wazalendo.
21 Desemba 2019.