Hali ya usalama imezua wasiwasi katika eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa, baada ya kundi la watu wanaoshukiwa kuwa wahalifu kuwashambulia maafisa waliokuwa kazini katika kituo cha ukusanyaji ushuru wa kaunti, na kusababisha kifo cha afisa mmoja na wengine watatu kujeruhiwa.
Tukio hilo lilitokea takriban saa 9:40 alfajiri Jumatatu, Oktoba 26, 2026, katika eneo la Barabara ya Mchanga, Likoni, ambapo maafisa wawili wa Polisi wa Utawala na wawili wa idara ya utekelezaji wa sheria za Kaunti ya Mombasa walikuwa wakilinda kituo hicho.
Kwa mujibu wa taarifa za polisi, washambuliaji waliwakabili maafisa hao kabla ya makabiliano makali kuzuka. Katika vurugu hizo, washukiwa walifanikiwa kumpokonya afisa mmoja wa polisi bunduki aina ya AK-47 iliyokuwa na risasi 30.
Afisa wa kaunti aliyetambuliwa kama Omari Mzerera alipigwa risasi mgongoni, huku risasi hiyo ikitokea kifuani, na kufariki kutokana na majeraha yake.
Maafisa wengine watatu walijeruhiwa, wakiwemo polisi mmoja na maafisa wawili wa kaunti. Walikimbizwa hospitalini kwa matibabu, huku mwili wa Mzerera ukihamishiwa katika mochari ya Hospitali ya Coast General.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Mombasa, Stella Cherono, alisema uchunguzi umeanzishwa ili kubaini waliohusika na sababu ya shambulizi hilo. Idadi kamili ya washambuliaji pia haijathibitishwa, ingawa makadirio ya awali yalionyesha huenda walikuwa takriban watano.
Polisi wanaendelea na juhudi za kuwakamata washukiwa na kurejesha bunduki pamoja na risasi zilizoibwa. Kufikia wakati wa kuripotiwa kwa habari hiyo, hakukuwa na taarifa ya kukamatwa kwa washukiwa.
Sababu ya shambulizi hilo bado haijabainika, huku polisi wakitoa wito kwa wananchi wenye taarifa zitakazosaidia uchunguzi kujitokeza.
Je, unadhani hatua gani zinapaswa kuchukuliwa kuimarisha usalama wa maafisa wa kaunti na wananchi katika eneo la Likoni? Shiriki maoni yako.