Kundi la nchi saba tajiri zaidi duniani G7 hivi karibuni lilitangaza mpango wa kuchangisha dola za kimarekani bilioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika nchi zinazoendelea, ikiwa ni jaribio la kushindana na pendekezo la China la "Ukanda Mmoja, Njia Moja".
Mpango mkubwa wa miundombinu kama huu hakika unakaribishwa katika bara la Afrika ambalo linakabiliwa na pengo kubwa la fedha. Lakini nchi nyingi za Afrika zinatazamiwa kuchukua mtazamo wa “subiri tuone”, kwani kama alivyosema waziri wa zamani wa kazi za umma wa Liberia W. Gyude Moore, "huu si mpango wa kwanza wa miundombinu uliotolewa na nchi za Magharibi, hivyo suala la kuamini litakuja hadi maelezo ya kina juu ya jinsi ya kutekelezwa yatakapotolewa.”
Mpango huo, unaoitwa kama Ushirikiano wa Miundombinu ya Kimataifa (PGII), unaonekana kama mapitio ya mpango wa Kujenga Dunia Bora Zaidi (B3W) uliozinduliwa na G7 nchini Uingereza mwaka jana, ambao tayari umekufa katika Bunge la Marekani. Na katika utawala wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, Marekani pia ilizindua Mpango wa Ustawi wa Afrika (PAI), lakini serikali ya awamu hiyo iliondoka madarakani kabla ya kutekelezwa miradi yoyote mikubwa.
Akielezea mpango wa PGII, rais wa Marekani Joe Biden alisema: "Hii si misaada au hisani, bali ni uwekezaji ambao utawafaidisha wote. Mpango huo unafadhiliwa na fedha za serikali na sekta binafsi." Juu ya hili, Moore, ambaye sasa anafanya kazi katika Kituo cha Maendeleo ya Dunia CGD chenye makao makuu mjini Washington anaona kuwa G7 ilitoa wazo tu kuhusu uwezo wao wa kuchangisha mamia ya mabilioni ya dola kutoka taasisi za sekta binafsi na benki za maendeleo za kimataifa.
Alikumbusha kuwa mwaka 2015, Ajenda ya Hatua ya Umoja wa Mataifa ya Addis Ababa iliyofikiwa kwa ajili ya kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu, ndio ilitumia njia kama hii kwamba jumuiya ya kimataifa ilitumia "mabilioni" ya fedha kuvutia "matrilioni" ya mitaji binafsi, na matokeo yake ni kuwa ajenda hii bado haijazaa matunda yoyote hadi leo. Kwa hivyo, ni vigumu kusema kama PGII iliyopendekezwa na G7 inaweza kuwa na matokeo yoyote tofauti. Isitoshe, kama mpango huo wa G7 utaweza kutekelezwa au hapana, ni sharti kwanza kujadiliana na wadau mbalimbali wa nchi za Magharibi, na kuidhinishwa kwenye mabunge.
Mbali na sintofahamu zinazojitokeza kwenye kuchangisha fedha na vizuizi vya kisiasa, pia ni vigumu kusema kama mpango huo wa PGII utaleta matokeo yatakayowaridhisha Waafrika. Hadi sasa pendekezo la China la "Ukanda Mmoja, Njia Moja" limekita mizizi barani Afrika kwa takriban miaka kumi. Miongoni mwa nchi 53 za Afrika zenye uhusiano wa kibalozi na China, nchi 52 na Kamati ya Umoja wa Afrika zimesaini hati za ushirikiano na China katika ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”. Ikiwa ni pamoja na bandari, reli, barabara kuu na mabwawa, kuna miradi mingi mikubwa isiyohesabika ya ushirikiano kati ya China na Afrika chini ya "Ukanda Mmoja, Njia Moja", na kuifanya China kuwa mwenzi muhimu wa kusaidia kutimiza "Ndoto ya Afrika". Profesa wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya XN Iraki alisema mpango huo wa G7 umechelewa mno, na ushawishi na sifa za "Ukanda Mmoja, Njia Moja" tayari uko juu sana barani Afrika. "Inaweza kuwa chanya ikiwa na masharti rahisi na kugusa masuala ambayo ni muhimu kwa mtu wa kawaida kama vile elimu, afya na ajira. Waafrika sasa wanajua ni upande gani wa mkate wao unaotiwa siagi.”
Waswahili husema “ahadi ni deni”. Iwe ni “kujenga dunia bora zaidi” au “ushirikiano wa miundombinu”, itapongezwa na nchi za Afrika kama itachukuliwa kama ni “nyongeza” ya “Ukanda Mmoja, Njia Moja” na kuleta manufaa halisi kwa maendeleo ya miundombinu ya nchi za Afrika. Lakini sharti ni kuwa lisiwe jina moja baada ya jingine, bali iwe mradi wa utekelezaji unaoweza kuzaa matunda.