Now we go,,,
A G A N O J E U S I .1
Miaka sasa imesonga, nimekua mtu mzima.
Lakini najuta maana naukumbuka utoto wangu ambapo hatma yangu ya siku ilikuwa kwenye mikono ya Wazazi.
Yaani nikihisi njaa basi nitalia weee! ili nitimiziwe hitaji langu. Tofauti na leo hii ambapo mimi ndiye mwenye jukumu hilo kwa wanangu wawili.
Naachaje kujuta sasa wakati kila kitu sina, kazi sina, elimu sina, biashara sina, mnyororo wa ukoo wangu wote mimi ndiye jicho la matumaini kwao maana niko mjini wao wako vijijini……. Imani yao?,,<<< Mjini tunachezea pesa>>>.
Wanaweza kuwa sawa, maana ukiwatazama sana hawa vitukuu vya Eva wanavyovaa ni kama wanakutahadharisha kuwa, kumiliki pesa yataka moyo wa bastola na pesa haikai kwa mjinga...
Namkumbuka mama yangu kipindi kile nikiwa mdogo ananiambia, “Mwanangu usiwekeze ujana wako kwenye starehe na zinaa. Maana huko kuna mitego ya kila namna. Najua tu watakupenda kutokana na kwamba una juhudi, hivyo juhudi zako zinashawishi kuwa mbeleni watapata mtelemko kwako, usikubali kuwa punda wa hao wanawake kwani watakuigizia kuwa wanakupenda kwenye nyakati za mkate na asali.
Lakini ukweli ni kinyume chake,we jitahidi tu kuwajali wanao na mkeo na wao pia usijitoe kwao kupitiliza maana hawatakulipa bali utafanya kama jukumu lako.”
“Sawa mama nimekuelewa na nitajitahidi sana nizingatie haya unayoniambia” Nilikuwa nikijibu.
“Nashukuru mwanangu kama umenielewa. Jitahidi sana kupambana ili ukae mbali na maisha ya dhiki si unamuona baba yako alivyo?
Kuna siku mlishawahi kulala njaa labda?”
Mimi: Hapana.
Mama: Basi na wewe nataka uwe kama baba yako ili uje kuiepuka laana ya kutelekeza watoto.
Mimi: Sawa mama nimekuelewa.
Ni kumbu kumbu tu maana leo hii wazazi wako kijijini huko nguvu zao zimepungua kifupi wanakula kile walichohifadhi wakati wa utafutaji wao. Si vyema kwangu kuanza kutaka sehemu ya fao lao hilo.
Maana hata wakinipa haliwezi kunifikisha sehemu mimi na familia yangu, hivyo kila mmoja abebe mzigo wake kwa nguvu zake mwenyewe.
Nikiwa nimekaa napokea simu kutoka kwa rafiki yangu Hamadi, huyu ni rafiki yangu wa tangu shuleni japo niliishia kidato cha pili. Kutokana na changamoto za kifedha.
Hamadi ananiambia kuwa kuna mchongo sehemu, anahisi unaweza ukanifaa kwa pesa za matumizi. Hivyo niwahi mpaka maeneo ya kawe Ukwamani ambapo nitamkuta hapo ili tuongozane pamoja.
Mimi naishi Temeke mitaa ya nyuma ya Giraffe Hotel, mtaa maarufu kwa jina la Ngeta.
Basi kwa kuwa ni mida ya saa sita na kama ulijuavyo jiji la Dar mida hii, kwa nyumba zetu za uswahilini ni kwamba panatokota haswa.
Hivyo nachota maji kidogo kwenye jaba na kuingia maliwatoni kujimwagia, baada ya dakika ishirini niko pale kituo cha basi cha Hospitali nadandia daladala la kwenda mwenge maana za kawe ni kama leo hazitaki kuja.
Nikiwa kwenye gari mara nasikia majamaa wawili wakisema “Yaani yule fara ana pesa mwanangu halafu bado mdogo sana ukimuona, daah watu wengine sijui hata walizaliwaje?”
Maneno haya yananivuruga sana akili maana ukizingatia mimi ndio kwanza naitafuta miaka thelasini na tano lakini sijajipata.
Ukaja ule msemo wa <<<<Ukitaka kufanya mambo yako usiyazingatie ya watu>>>.
Ni kweli maana hatukutoka huko kwetu mbwinde kuja kujua nani anatumia pesa zake vibaya, ama nani amepata pesa zake kwa njia haramu. Zaidi ni kwamba tumewaacha wazazi wetu wakiomba dua njema ili tufanikiwe.
Nikiwa kwenye lindi la mawazo nilishituliwa na mlio wa simu, kucheki alikuwa ni Hamadi, nikapokea.
“Oya mwanangu Mswati, mbona hufiki tu kwani umepanda baiskeli?
Mimi: Nisubiri kidogo Mswati nafika muda sio mrefu,
Hili ni jina maarufu baina yetu maana tunaitana hivyo kutokana na namna tulivyokuwa tukimkubali yule mwamba wa Swaziland kwa kuoa wanawake wazuri kila mwaka.
Simu ikakatwa, baada ya muda wa kama lisaa na dakika kumi tulifika mwenge kipindi hicho stendi haijahamishiwa makumbusho.
Fujo zilikuwa ni nyingi na hapa kila mwanamke unaemuona basi ni kama kajiumba mwenyewe, yaani ile kwamba alikuwa anaona tako la huku limepwaya anajiongezea tu.
Kifupi huchoki kuwaangalia vile wanavyojizungusha hapo stendi wakijifanya wanatafuta nguo huku wakiwa wapo mingo.
<<<Unaambiwa jichanganye uishe>>>.
Muhuni nikashuka kutoka kwenye gari ile, konda kazungukwa na watu kibao akiwa anadai nauli miksa kurudisha chenji. Nikazuga kama najisachi, nikazunguka nyuma ya gari fasta nikavuka barabara hadi upande wa pili nikadandia hiAce ya kwenda kawe.
Hii mia nane itanisaidia kununua dagaa-mchele pale mitaa ya Sudani Temeke nikirudi nyumbani baadae.
Kufika kawe, namkuta Hamadi yuko bize kwenye simu, tunapeana tano tu za mikono ama gwara kisha ananyanyuka tunaanza mwendo wa kuelekea Kawe, Maringo.
Tulivyofika Tanganyika pekaz tunachanizia humo uwanjani maana Hamadi ananiambia mchongo upo Kawe ya chini barabara ya Mwai Kibaki.
Naona safi maana kunyoosha na lami na jua hili sio poa .
Tumeyafikia magofu ya mle Tanganyika pekaz nawaona wahuni wanapiga mazoezi huku wengine wakipuliza, tunawapa salamu kiaina kisha wananitembezea kijiti kama pafu tatu hivi nakaa sawa mawazo yote na uoga vinaondoka kisha namkusanya Hamadi tunasebenza misele yetu.
Kufika Kaw echini kule tunasimama nje ya geti moja jeusi. Umaridadi tu wa geti hili unaonyesha ndani yake kuna bangaloe la kwenda,, nabaki tu kumwambia Hamadi “Oya Mswati kuna watu wanaishi aisee cheki huu mgeti yaani bajeti yake mi si nanunua kiwanja huko mkuranga na kuezeka kabisa?”
Hamadi anacheka tu kisha ananiambia, “Ndio tupambane sasa, nyeupe nyeusi ili tuishi mwanangu ujue sisi hapa duniani hatuishi bali tunadumu, hawa ndio wanaishi sasa”
“Laivu kabisa mwanangu hivi fikiria mtu una mtoto mchanga wewe na mkeo mnalalaje kitanda cha tano kwa sita si mnakuwa mmenyooka badala ya kulala? Maana mmoja akisema ajitanue tu atakakalalia kachanga hivyo inabidi mjinyooshe tu” Nilisema. Hamadi akacheka huku akibinya kitufe cha kengele.
Haukupita muda geti dogo likafunguliwa, Sura ni ya kijana makamo yetu. Akatukaribisha ndani akionekana kuegemeza stori zake zaidi kwa Hamadi maana ndie wanafahamiana nae.
Tuliingia na kukaa varandani ambapo kulikuwa kumesheheni hadi sio poa, yaani pa kibabe sana.
Hamadi: Oya Mswati huyu anaitwa Denis baba yake ni Injinia wa wizara ya ujenzi. Oya Denis huyu ni mwanangu sana anaitwa Boyo.
Denis: Ndio yule uliyekuwa unaniambiaga kuwa una mwanao mmoja mmeshibana sana kama Chanda na pete?
Hamadi: Yap Denis na usimuone kakaa kinyonge hapo ni mwamba sana hata zile mishe yaani anapasua anga tu bila tabu.
Denis: Mi mwenyewe namwona, haihitaji maelezo muonekano wake tu ni maelezo tosha.
Nikabaki najiuliza ni michongo gani hiyo ambayo inahitaji mtu uwe mwamba kiasi hicho? Nikabaki na tashwishwi tu.
Mara Denis akazama mfukoni na kutoa kimfuko kidogo cha nailoni nyeupe, ndani yake kulikuwa na unga mweupe utadhani ni glucose.
Akampatia Hamadi, kisha Hamadi akanisogezea karibu na macho. Akaniuliza mswati unafahamu hii kitu?
Mimi: Hapana, ni glucose ama?
Denisi na Hamadi wakacheka kidogo kisha Hamadi akaniuliza unaisikiaga Player au maradona?
Mimi: Hapana.
Hamadi: Mswati hii ni cocaine grade one, mashanta tunaita Player. Kilo moja ya hii kitu inaenda kama milioni mia sasa hivi huwezi amini yaani.
Kitendo cha kuambiwa vile nikahisi kupagawa hivi, yaani mimi na madawa ya kulevya wapi na wapi? Nikamshika mkono Hamadi na kumvuta pembeni kidogo.
“Oya Mswati michongo gani hii sasa tunaleteana, mbona sikusomi mwanangu?” Nilimwambia.
“Mswati, wewe si unataka good life lakini? Sasa wewe maisha mazuri unadhani yatakufuata pale Temeke umekaa tu getto mara mnapiga spana na watoto wadogo wenye umri wa darasa la tatu?” Hamadi alinikata kauli.
Uhakika ni kwamba yale maneno ya Hamadi sio tu kwamba yaniumiza, bali yalipenya ile kisawa sawa na kuingia kwenye mtima wangu.
Ni kweli pale Temeke wengi tunashinda chini ya uvungu wa magari, yaani ni full kupiga spana, muda wote tumetapakaa oil chafu tena ukija mitaa hiyo ya Sudani unakuta madogo kibao wako hapo wanapambana kujifunza spana.
Nahisi kwa Tanzania nzima hakuna sehemu watu wana mzuka na spana kama Temeke sijui kwa sababu tu ya waarabu wengi mitaa ile si unajua tena waarabu hawana ujuzi mwingine nje ya spana na wanaipenda utadhani wameianzia tumboni.
Nikayatafakari maneno ya Hamadi, nikaona mwamba mbona yuko sawa tu sasa kinachonifanya napaniki ni nini?
Kwanza mimi mwenyewe nimepiga ruti kutoka Temeke mpaka huku Kawe nikiwa ninatamani mchongo wa kuingiza pesa, kwani nilitegemea uwe mchongo gani? sikupata jibu.
Nikasikia sauti ndani yangu ikisema Boyo acha ukina, nyaka fasta mchongo huo, sababisha kisha pita hivi, usirembe sana.Wanaume hawajiulizagi mara mbili kwanza huna maajabu mfukoni halafu unachagua cha kufanya?
Nikajikuta namwambia Hamadi “Oya Mswati Fabilillah!! Twende kazi kikubwa unyama uwe wa kutosha isijekuwa tunaleteana mazegere ya kiwaki. Si unanijuaga toka skonga sipoagi nikiwaka?”
“Mswati baaab we amini hii ni kazi tena ya kwenda, Huyo Denis unavyomuona hapo hanaga mba-mba-mba” Aliniambia Hamadi.
Tukarudi tena kwa Denisi kujumuika nae baada ya kuyajenga na mwanangu Hamadi.
“Oya Denis toa fudo mwamba akazie si unajua kule anakotoka yuko kinyonge?” alitanguliza Hamadi.
Denisi akatoka na kuingia ndani kama dakika tano hivi kisha akaja na bonge la hot pot.
Kulifungua hivi namuona kuku mzima na nusu yake, duu!! yuko dry ile mbaya miksa masontojo kama yote, yaani full udambwi dambwi . Akaliweka juu ya meza lile dude.
Denis akaniambia nawa hapo nyuma tu kuna koki. Nikamuambia Hamadi oya twende tukanawe. Akasema yeye yuko njema wala hana mzuka na msosi.
Nikamwambia na Denis nikaona nae ni vile vile tu nikawaza sasa hawa wananiletea mimi peke yangu Kuku na nusu wananitakia nini hawa? kwanza siwezi kummaliza huyo mmoja tu mwenyewe sembuse na nusu yake?
Nikawaza kifaza sana…, nawezaje kula kuku kipande hiki kwa watu halafu kule familia yangu inasokota nguna na wakudunga(dagaa mchele)?
Baada ya kunawa nikamuomba Denis kama kuna kifungashio nimuweke yule kuku mzima kisha nile ile nusu.
Huyu mzima nitawapelekea familia nao wakainjoi, yap ndio maana tupo hai na wao wanaweka matumaini yao kwetu na pale wanaume tunapokuwa tumetoka kwenda kwenye utafutaji basi matarajio ya familia zetu huku nyuma huwa ni kwamba Mshua akirudi mambo yatakuwa gudi sana japo kuna time tunaambulia patupu, basi ni vile tu hatujui jinsi wanavyokuwa Dissappointed yaani.
Baada ya kusema vile Denis alisimama akatabasamu kidogo kisha akaninyooshea kidole cha shada huku akitikisa mkono wake akaniambia maneno yafuatayo, “Nigga, you are a man and a daddy at the same time.What a fucking loving Nigga?”
Kisha aliingia ndani na kutoka na aluminium foil pamoja na mfuko mkubwa wa kutosha kuweka na mazaga mengine ikiwa ningekuwa na pesa ya kuhemea vitu vingine.
Denis alimwambia hamadi kuwa “Una kila sababu ya kuwa bampa to bampa na huyu mwamba. He is such a loyal nigga.”
“Haha haha haaa!!! Denis mbona huo ni mwanzo tu ukimwelewa mbona utampenda tu bure, yaani muonekano wake ni tofauti na roho yake huwezi amini”
“Ujue ile first sight niliwaza kidogo nikahisi huyu jamaa anaweza kuja kutugeuka yaani. But I was wrong!” Alisema Denis.
Niliwasikiliza tu huku nikimfunga vyema yule kuku kwenye foil na kumuweka kwenye mfuko kisha nikaanza kula Ile nusu na chombeza(chipsi kidogo) zilizokuwepo mle kwenye hotpot.
Nikawaza ina maana hiki kitendo kidogo tu kimeweza kunijengea Imani kubwa kwa huyu Denis, kumbe watu hudifainiwa kwa vile vitu vidogo ambavyo wao pengine hawakuwa serious navyo kabisa.Duuh!!
Baada ya kumaliza kula maongezi ya kazi yalianza.
Denis alileta ramani ya kazi mezani, kiasi ilikuwa inatisha ila sio kwa mimi maana mazingira niliyokulia hata watoto wenzangu walikuwa wakinihanya na mbaya zaidi hata wazazi wao walikuwa wakiwazuia watoto wao wasinikaribie.
Laiti wangejua kuwa mimi mwenyewe ni introvat sitakagi junction kwenye maisha yangu wasingehangaika kutumia nguvu kubwa kiasi kile.
Nilianza kwa kufundishwa kwanza vituo ambavyo ningekuwa natembelea na kushinda muda mwingi. Na majina yake ya kishanta yaani code maalum ambazo tungetembea nazo vichwani mwetu.
Baada ya kuyacheki maeneo yote nikagundua kuwa hakuna eneo la kizembe hata moja, yaani mbona kote ni kwa mashefa?
Nikaona mbona kazi kama inaanza kunitoa hata kabla sijaanza kuifanya?
Baada ya hapo nilipewa jina sasa rasmi la kinyoka, Nikaitwa Noriega.
Si nikakumbuka ule wimbo wa Rick Ross BMF maana nasikia sana hili jina likitajwa mle kwenye huo wimbo.
Ndio nikajua kuwa kumbe wale jamaa huimba vitu halisi kutokana maisha yao.
Basi Noriega nishakuwa nyoka tayari kinachofuata, nikapewa unga kidogo kwenye mfuko Denis akaniambia kuwa mimi niko safe zone sitaweza kutest wala nini maana mashefa wote wanatumia so wanatest wenyewe mimi nijitahidi tu nisijetumia maana nitawalisha hasara na hapatakalika tena.
Nikamwambia kuhusu hilo asiwaze kikubwa tumalizane kuhusu malipo ili niwe huru kupiga kazi.
Denis akacheka kidogo kisha akaniambia unadhani naweza kukupa mzigo wa mamilioni halafu nikuletee mboyoyo kwenye malipo hapo una mzigo wa kama milioni ishirini na tano.
Malipo tunaanza nayo sasa kwanza chukua hii, akazama mfukoni akatoa noti saba za dola mia mia.
Kwa time zile chenji ilikuwa inasimamia kwenye elfu mbili mia mbili so nikazidisha fasta nikaona inakuja milioni moja na ushee yaani chenji ya juu yake inatosha kuweka banka(mahemezi ya mahitaji muhimu) ndani ya mwezi mzima
Si unajua tena sisi watu wa hali ya chini mahitaji yetu huwa sio mengi ukishaweka mchele kilo hamsini, unga dona kilo mia, sukari kilo ishirini na tano, mafuta kindoo lita kumi na mtungi mdogo wa gesi umejaa vyema na gunia la mkaa kwetu sisi hiyo inatosha hatuna mambo ya kuweka sijui nyama kwenye friji kwanza uswahilini kwetu unaweza hisi tumeazimwa transfoma,,, maana sio kwa kukatika umeme huku. Utawekaje vitu kwenye friji sasa hata ukiwa nalo ujue mgogoro wa umeme wewe ndiye victim muda wote.
Kama feni tu watu wanagombana itakuwa hilo friji si watasema unamiliki mtambo kabisa ujue asili ya uswahilini kwetu ni kwamba watu wanayajua mambo na mienendo yako kuliko hata wanavyoyajua maendeleo ya watoto na ndugu zao so ukiishi huku kwetu ujipange, yaani uwe unaamka saa kumi na moja alfajiri na kurudi saa tano za usiku.
Na ole wako wasijue unapojishughulishia!! Utabambikiwa kila jina baya linaloendana na wizi.Hasa ukiwa mkimya na kaksi kama nilivyo yaani wewe utapata tabu.
Ratiba ilitakiwa ikifika saa mbili za usiku ndipo nisogee kwenye kituo changu cha kwanza kwa siku hiyo.
Basi tuliagana pale lakini Denis aliniambia neno moja ambalo liliniingia na nikalizingatia sana “Nigga, I see you far!! Yaani ukiwa muaminifu, hili jiji utaliweka kiganjani mwako haijalishi una elimu ama huna elimu man.” Kisha alinipatia kiasi cha laki moja nje ya malipo yangu akaniambia This is for our hommies, you have that, we have this.
Akimaanisha kuwa ile pesa ni kwaajili ya familia yangu ambayo nayo anaizingatia kama familia yetu wote kwamba mimi nina yule kuku, ila wao wana kile kiasi cha pesa alichonipa.
Denis hupenda sana kuchanganya lugha nafikiri ni kutokana na kwamba pengine amekaa sana Ulaya huko akiwa anasoma ama kwasababu ya mishe mishe zake hizi maana mara nyingi huwa anasafiri sana kwenda nje.
Basi mimi na Hamadi tulimuaga pale Denis kisha tukashika njia tuliyokuja nayo.
Hamadi alishauri tufanye vile ili kuweza kuitawala pesa badala ya kuruhusu pesa itutawale yaani isiwe ile nimepata tu vipesa kidogo nianze matumizi yasiyokuwa ya msingi kama kuchukua bajaji kutoka kawe hadi Temeke ambapo ingenigharimu elfu ishirini na tano. Alinishauri niwe mtulivu sana maana issue nazozifanya natakiwa kuishi kama mtu ordinary ili nisivute attention za watu kuanza kujiuliza juu ya kazi zangu maana watu wanapenda waone mnafanana na haubadiliki.
Hivyo ikitokea mabadiliko kidogo wanaanza kusaka chanzo cha yale mabadiliko wakikijua tu oya!!! Umeisha man.
Kweli tulitembea mpaka Kawe ukwamani, ambapo tulikaa tukapiga stori moja mbili tatu huku nikiwa nasubiri gari la Temeke.
Nakumbuka katika zile stori Hamadi aliniambia kitu ambacho kiliniacha mdomo wazi kwanza aliniuliza, “Mswati unadhani mimi sina pesa? Pesa ninazo yaani kwenye akaunti imo zaidi ya milioni hamsini. Lakini ona bado naishi uswahilini, lakini huko nyumbani kwetu Geita nimewajengea wazazi nyumba ya zaidi ya milioni ishirini. We nione hivi tu”
Kwanza nilishangaa sana maana muda mwingi ambao tulikuwa tunakutana mimi na hamadi ni kweli bili za misosi kwenye migahawa ya kati hii isiyo mikubwa sana wala midogo sana alikuwa analipia yeye na muda mwingine ananipa hata elfu hamsini kwaajili ya kurekebisha mambo ya mezani pale nyumbani kwangu, lakini sikuwahi kuwaza kama huyu mshikaji ni milionea tena amekaa kimya tu.
Hapo ndio nikajisemea ama kweli usiseme una rafiki we sema una mshikaji ambae mnashea kile kinachowafanya muwe pamoja kwa muda huo maana urafiki ni gharama sana
Asikwambie mtu, yaani kuwa na mtu ambae utamshirikisha michongo ya namna unavyopata riziki wakati huo yeye hana mbele wala nyuma halafu akakuacha salama!! Basi ujue hapo unae rafiki na bado haitoshi maana anaweza kuja kukusaliti hata kwa mkeo sehemu ambayo hukuamini kama ataanguka, kumbe ikawa ndio udhaifu wake.
Baada ya kuniambia vile alizama mfukoni nae akatoa laki mbili na kunipa akidai kuwa zile ni Baraka ni kawaida kumbariki mtu anapokuwa anaanza kazi.
Basi nilipokea huku nikijiona kama nimekuwa mpokea michango kila mtu sasa ananichangia lakini hii ni baada ya kuungana na familia yao mpya.
Hatukukaa sana, gari la Temeke likaja DCM moja watu wakaanza kuingia kwa fujo mimi nikamuaga Hamadi na kujitoma ndani ya gari nikikaa siti ya dirishani na kumpungia mkono Hamadi. Nae akanipungia, haukupita muda gari ikaanza mwendo Nilifika mtaa wa Ngeta mida ya saa kumi na moja kasoro ambapo nilipofika kwanza nilanzia kwa mangi upande wa kulia kuna watu wa ukoo wa Mtei jina kwa Paschal, ana duka lake hapo nyumbani so mahemezi yangu nilipenda kuyafanyia hapo kutokana tuna muunganiko Fulani na hao watu kiaina.
Baada ya kununua unga na baadhi ya vitu nilipeleka nyumbani ambapo niliikuta familia imejikusanya kwenye kideo ni sauti ya Juma Khan Chikongwe imetawala sebule nzima.
Unashangaa nini sasa? Sisi huku uswahilini kwetu huyo ndiye mwamba anaefagiliwa mno. Yaani wanamhusudu kama vile Sharuh Khan huko India.
Pisi nyingi za huku kwetu hazijui mara burger mara pizza zenyewe ziambie mihogo ya kukaanga na chachandu pale kwa mama Faridu basi utazikonga nyoyo. Na ukitaka kuwang’oa wewe waambie mvua zimekaribia kuanza utakuwa unawabeba mgongoni unawavusha maji wakitaka kurudi ama kutoka nyumbani basi hapo ni wewe tu ila hakikisha mvua zikianza kunyesha uwe umehama huo mtaa maana utawabeba hadi wake za watu hapo ndio utajua kwanini wahuni hutembea na mafuta nyuma ya sikio.
Uswahilini kwetu mwenyekiti ana nguvu kuliko greda linalochimba mitaro na barabara, maana kesi nyingi za pale mtaani anakalisha, zinaisha bila kwenda mahakamani.
Halafu kila mwenyekiti ni aliwatani, maana madili mengi ya pale mtaani lazima ashirikishwe ili likitokea soo analizima. Yaani hiyo ndio torati ya sehemu kibao kuanzia pande majumba sita, kiwalani, vingunguti kwa pera pera, kushuka tabata liwiti mpaka kule mitaa ya Ghana buguruni shuka hadi marapa kwa mwamba Chidi benz hapo mwendo ni huo huo. ukizingua night watu wanakusaka na vitofa. Kifupi watu hawapendi mambo ya kupelekana polisi wanapenda sana street justice.
Uswahilini watu wanazijua sheria sana lakini ni zile za kuchonga mdomo tu wakisikia kuna mwenzao kaenda hata selo tu polisi hawaendi hata kumpelekea msosi wote wanaogopa, sasa unaanza kushangaa si ni hawa waliokuwa wanachonga mdomo kuwa hata polisi na mahakama hawaziogopi?
Ingia mkenge sasa, utiwe lupango uone, hautamuona mtu hata mmoja kutoka pale mtaani kwenu uswahilini akiileta sura yake pale kituoni ulipo zaidi ya ndugu zako. Ambao nao watakuja ile tu kuondoa lawama huku wakikusema ile vibaya maana umewaharibia hesabu zao za hela ile mbaya.
Na kama huna ndugu mjini Daslam, umekuja kama gunia la mkaa utaishia segerea baada ya miezi sita au mwaka ukitoka unawakuta wahuni wameshikilia pole nyingi hakuna cha maana.
Ukiwauliza mbona hamkuja kuniona? utasikia mara walikusanya michango wakampa sijui nani nani akatokomea nazo wanamwangushia jumba bovu msela ambae wanajua alishahama kitaa chenu.
Basi baada ya kuingia ndani ilikuwa ni full shangwe kwa familia maana nina makid wawili tu na mke wangu. Makid ni wa kike na wa kiume wana fujo hao na wote wanasoma shule iliyopo hapo jirani tu yaani pale uwanjani tunapopigia mazoezi jioni ni uwanja wa shule yao.
Basi kwakuwa tayari ni uelekeo wa jioni mke wangu huyu ambaye ni mzuri yaani sometimes nikitafakari alinipendea nini nakosa majibu maana pesa sina uhakika wa maisha ya kesho pia sina zaidi ya ahadi za kujiamini tu za mdomoni kuhusu fyucha yetu.
Ujue wanawake nao wana maamuzi yao ambayo yanabaki kuwa siri yao pengine huwa wanatuonea Imani tu ama huwa wanapenda kitu ambacho wewe mkulungwa hukijui kama ndicho kinamzuzua yaani yote heri tu.
Kikubwa tuendelee kuwa pamoja sisi wanaume na wanawake maana tunafaana sana achana na hizi swaga za kifala mara eti haki sawa mara vijana hawataki tena ndoa wanataka kuwa wanachapa na kusepa Jiulize je wewe baba yako angechapa kwa mazaako na kusepa ungeinjoi vipi mapenzi ya baba na mama ama ndio ungekuzwa na mama yako peke yake ili uwe na tabia za kike kike zile za wote mna mitondoo ndani ya kukojolea usiku hakuna wa kumsindikiza mwenzake nje kukojoa?.
Wakati mke wangu anapambana na vyombo na majiko mimi nilikuwa nikicheki time kwenye simu yangu muda wote nisije nikazingua siku ya kwanza.
Maana nakumbuka niliambiwa mida ya saa mbili na madakika yake niwe kituo namba tatu yaani ilikuwa ndio jina la siri la eneo husika.
Basi saa kumi na mbili na dakika kumi niliaga huku nikichukua koti langu kwaajili ya kujihami na baridi la usiku.
Mke wangu aliuliza tu kwa hamaki kuwa naenda wapi maana hajazoea mimi kutoka mida hiyo ya jioni labda kama kuna mechi za Ulaya ambapo napo mimi sio mpenzi sana kihivyo.
Nilimuaga kuwa natoka japo naweza kuchelewa kurudi maana kuna watu natakiwa kuonana nao niseti mipango ya kazi. Basi baada ya wife kusikia kuhusu mipango ya kazi akawa kichwa juu juu Enhee kazi gani baba?
Nikamwambia taratibu sasa mchele wenyewe hata haujaoshwa uanze kutengeneza kachumbari kweli?.
Wife ni muelewa ikabidi anyuti huku akinitakia mafanikio mema huko niendako.
Basi raundi hii sikwenda pale stendi ya hospitali bali nilipitia njia ya nyuma nikapandia stendi ya Girraffe hotel.
Huyo!!!! saa moja ikanikuta ndani ya Mwenge. Niliamua kukaa na kupoteza muda pale mwenge kutokana na kwamba kuna vile vitu vyetu yaani sisi ambao hatujajipata basi huwa tunapenda kukaa sehemu ambayo wanapita akina dada wengi hususani mitaa ile wanayopita masista duu wengi hii huwa ni kwaajili ya kuburudisha macho na kusuuza roho kwa kuangalia maumbo yao hawa wadada huku mara moja moja tukivaa mabomu na kuwatongoza kujaribu bahati yetu wanasema usipoamini ndipo linatokea jambo halafu pale ambapo unaamini sana ndio hakitokei kitu eeeeh!! Maana si hatuna Kamba za kuwavutia?
Sasa mwanaume nikijiangalia mfukoni sina maajabu, nyumba sina, gari sina kazi ya kunikutanisha nao muda wote wawe wanaililia saini yangu sina nitawashikia wapi wadada wanaoingia salooni na kuacha karibia laki mbili na nusu kwa mara moja?
Halafu unajifariji eti mapenzi hayaangalii? Sio kwa hawa wauza ngono. Na wengi wa wauza ngono ndio hutuvutia kingono maana wanajibrand kingono ngono ili wawaingize wanaume kwenye kumi na nane halafu natokea mimi mnuka jasho mwenye sugu mikononi nataka nipendwe na huyu muuza ngono daaah nitasubiri sana.
Basi nikiwa pale Mwenge mara nikamuona mwanamke mmoja namfahamu kindaki ndaki anaitwa Vero, huyu tulisoma wote shule ya Ally hassan Mwinyi pale Magomeni makuti, barabara ya Magomeni- Sinza,, yuko na Nadia.
Huyu Nadia ni mtoto shombe shombe nae pia tunafahamiana vizuri japo yeye alikuwa anasoma shule ya Benjamin mkapa nayo iko mazingira hayo hayo kiasi kwamba ukiwa hauko sawa unaweza usijue kama kuna shule tatu tofauti lakini Benjamini mkapa na Ally Hassan Mwinyi ndizo zinaonekana kama shule moja zaidi huku shule ya Turiani ikiwa pembeni kidogo tena hii ni ya sekondari.
Umaarufu wa Nadia ni kwasababu huyu mtoto wa kike ni mzuri kuanzia sura mpaka umbo sema ana mwili Fulani hivi wa kivivu sana lakini ni mtu ambae muda mwingi anapenda kucheka sana hususani akiwa amekuzoea na hakawii kumzoea mtu.
Sasa huyu Vero baada ya kumaliza shule ya msingi alienda jangwani pale ambapo tulikuwa tukikutana mtaani kipindi cha likizo tu ndio nikaja kurusha ndoano lakini niliulizwa swali moja tu kuwa kwetu tuna nini mpaka nimshawishi awe na mimi?
Kiukweli alinikata maini kipindi hicho niko form two ilikuwa ni mwezi wa sita ambapo miezi miwili baadae niliachana na masuala ya shule na kutokomea mtaani mazima.
Baada ya kumuona nilipata mshawasha tu wa kumsalimia ambapo nilimuita Vero akageuka lakini aliponiona ni mimi akanywea yaani dizaini ile ya mtu ambae hakutaka kabisa akute ni mimi naemuita.
Lakini Nadia alipogeuka na kuniona alijawa na furaha ya ghafla sijui tu ni kwanini akamvuta mkono Vero waje kunisalimia lakini Vero aligoma, ndipo akamuacha na kuja peke yake akanikumbatia huku akinishikilia mikono yangu miwili kwa muda mrefu.
Sasa kutokana na kwamba watu ni wengi, hata sehemu za kupita kuna muda inakuwa ni shida na sisi bila kutambua kuwa tumeingia njiani kidogo tu nilishituka nikisukumwa na jamaa mmoja aliekuwa anajifanya yuko kasi na haraka hata sielewi alichokuwa anakiwahi ni nini, huku akifoka “Mnakaa kaa njiani kama ni mahaba si mwende bongo muvi mkatuonyeshee kwenye tivii?
Sasa kile kitendo cha kusukumwa na ikumbukwe alinisukuma mgongoni kwenda mbele kwakuwa sikuwa nimetarajia,, nilikosa balansi na kujikuta namkomba Nadia tukaangukia kwenye meza ya dada mmoja alikuwa anauza nguo za ndani.
Fasta nikajizoa zoa toka kwenye mwili wa Nadia maana nilimwangukia kwa juu , kichwa changu kikajam sana.
Lakini Nadia yeye alinipa pole huku akitabasamu tu kama vile hakuna kilichotokea. Huku akijitahidi kunitengeneza shati pale lilipokaa vibaya.
Yule dada mwenye meza ni mtu na nusu maana baada ya kuinuka na kusimama alitabasamu tu na kutuambia haya jamani wapendanao mniungishe sasa kila mmoja amnunulie mwenzake maana hapa kuna boxer za kiume na chupi za kike aina zote na tight pia.
Nadia bila kupoteza muda alianza kukagua Boxer pale, nikabaki najiuma uma sijui hata nifanye nini.
Lakini mara alifika Vero na kumvuta mkono Nadia kwa nguvu huku akimwambia “We Nadia umechanganyikiwa? Unataka kumnunulia huyu nguo za ndani? We Nadia wewe haumuheshimu Hassan eti?” Basi alimvuta mkono ile wangu wangu lakini nadia aligeuka na kunipungia mkono, lakini Vero aliachia msonyo mrefu huo sijapata kuona.
Kifupi niliuona wivu ndani ya Vero tena ule wa wazi.
Basi saa moja na nusu nilichukua bajaji pale mpaka Masaki hapa ndio ilikuwa kituo namba tatu. Nilisogea mpaka kwenye Lounge moja upande wa kushoto ambapo bajaji ilifika na kupaki nje maana mule ndani hawakuruhusu piki piki na bajaji kuingia maana mlinzi kazi yake ni kuminya rimoti kisha geti kubwa linafunguka hapo ujue linaingia ndinga la kifahari.
Baada ya kumlipa dereva ujira wake nilishuka na kuingia kupitia geti dogo yaani hata mlinzi hakuamini kuwa kwa muonekano ule naweza kuwa nimedhamiria kuingia mle ndani.
Ambapo alinifuata upesi na kuniuliza “We jamaa unaenda wapi?”
Nikamwambia naenda mle ndani kwani kuna tatizo?
“Kuna mtu unamjua mle labda?”
Nikaona huyu mlinzi anataka kunizoea vibaya yeye kazi yake ni kulinda hapo getini huku akifanya kazi ya kufungua na kufunga sasa hivi anajikuta kanipata mnyonge wake anataka anioshee aisee haiwezi kuwa kweli.
Nikaweka koo la mamlaka kisha nikamuuliza “Ndio kazi iliyokuweka hapo si ndio? Acha upumbavu fanya kazi yako ilyokuweka hapo” Baada ya kutamka vile sikutaka kumpa nafasi ya kujiweka sawa maana nilimuona kaingiwa na kiwewe na mie kupitia upenyo huo huo nikautumia kusogea mpaka kwenye meza moja ambayo ilionekana amekaa mtu mmoja tu.
Baada ya kukaa tu, Mhudumu wa kiume alikuja na kunipa menu ambapo niliangalia haraka haraka sana nisijue niagize nini maana vingi vya vyakula pale sikuwa nikivijua hata vinafananaje japo niliona burger na pizza sikutaka kuagiza.
Baada ya kutuliza macho vizuri ndipo nikaona grilled meat kwenye mabano nikaona goat bei yake elfu sabini.
Nikamuonyeshea muhudumu ambapo aliondoka chap baada ya kuonekana kama nimemchelewesha kuchagua msosi kwa muda mrefu nikashangaa hajataka kusubiri nimwambie labda alete na ugali au ndizi ama wali. Yeye tayari keshaondoka.
Angejua angenisamehe tu bure kwa kuchukua muda mrefu kuagiza maana sisi tushazoea migahawa yetu ya huko uswazi ambapo kwanza ukiwa unanawa unakuwa unatoa maelekezo kwa muhudumu tena kwa sauti kubwa.
“Nipakulie wali nyama na maharage weka ya kutosha, jitahidi nyama iwe nzuri isiwe na mifupa sana” Hizo ndio oda zetu sehemu za chakula uswahilini kwetu.
Nikiwa nashangaa shangaa mazingira ya mle ndani mara muhudumu huyu hapa kafika na bonge la sinia juu yake kuna sahani na vibakuli kama vyote yaani nikawaza kwani kabeba oda double?
Mara akashusha vyote pale mezani kwangu, mi nipo macho kodo tu baada ya kumaliza kushusha akanikaribisha “Broo karibu sana” Akaninawisha mikono na kuondoka.
Ile fujo ya vyakula iliyokuwa pale mezani ndio niliamini kwanini bei ni elfu sabini. Kwanza kulikuwa na supu ya mboga mboga, supu ya utumbo wa mbuzi ikiwa imewekwa vikorombwezo kama vyote hiyo nyama ya mbuzi iliyochomwa ilikuwa nyingi sana na kulikuwa na pan-cakes mikavu Fulani iliookwa ndani yake kukiwa na mayai ya kuku wa kienyeji.
Mwanaume nikaanza kula pale huku nikitazama mazingira ya pale. Aisee ndio maana watu wanaopata pesa wakishazijua hizi starehe ni vigumu sana kuacha mpaka pale wanapohakikisha kuwa wamefilisika kabisa mpaka kukosa hata pesa ya kuagizia andazi humu.
Maana wanawake unaowaona kwenye masaloon makubwa makubwa yale wakiwa wanaonekana kama malaika wote huishia maeneo kama haya maana huku huuza miili kwa watu wenye pesa.
Niliona wanawake wazuri wa ajabu mpaka nikajiuliza hivi sisi watu wa kawaida tukifa tukaulizwa kama tumewafaidi hawa viumbe tutakuwa na uwezo wa kujibu ndio kweli?
Nilianza kuhisi kuwa hawa sio wanawake wa kawaida aisee ila nikiri tu kwamba Kuna wanawake wazuri yaani ukisikia mtu anasemwa kuwa alikuwa yuko vizuri kiuchumi halafu akafilisiwa na Malaya Usije ukampinga mtu huyo kwa niliyoyashuhudia ni kweli wanawake hawa wana uwezo wa kumfilisi Mwanaume yeyote yule ikiwa atawakenulia meno tu hata awe na ukwasi kiasi gani.
Maana kwanza bia zinazouzwa humu ni zile za kutoka nje ambapo Windhoek moja ambayo mtaani tunauziana elfu tano tena hapo unakuta muhuni nabana manzi asinywe zaidi ya nne huku moja tu inauzwa elfu ishirini. Na watu wanawaagizia hawa wanawake mpaka mwanamke analewa yaani.
Savanah nazo ni vivyo hivyo. Nikiwa ndio nimemaliza kupata msosi wa nguvu mara alinisogelea mdada mmoja na kuulizia kampani yangu, nikamwambia aniache kwanza kuna mambo nayatafakari then muda ukifika kama atakuwa available basi tutaungana wote.
Mara nikasikia sauti kwa nyuma yangu “Noriega” Nikashituka na kukaa sawa kumcheki ni namba moja ya kilatino imeweka nywele mtindo wa bambucha ina vipuli masikioni vinang’aa sana vya silva.
Likavuta tu kiti likakaa na kuongea Kiswahili cha kuunga unga ambapo lilinitajia namba tatu, nikalionyesha karatasi moja alinipa Denisi imechorwa vidoti vitatu tu.
Baada ya kumuonyesha ile karatasi, akanishika mkono na mimi nikanyanyuka akaniachia akinielekeza kuwa nimfuate tukaingia kwenye ukumbi baada ya kusukuma mlango upande wa kulia.
Humo nilikutana na mimoshi tu watu wapo bize kusmoke yaani ni fujo tu huyu ana shisha yule ana Ciga mara huyu kitu cha Jamaica basi Yule mwamba akaniuliza nasmoke nini?
Nikamwambia nasmoke marijuana zikaletwa puli mbili zikawashwa nikataka kusmoke mara simu ikaita kucheki namba ni ngeni nikapokea na kuweka sikioni sauti nasikia ni ya Denis huwa sisahau sauti hata kama mtu nimekutana nae mara moja.
Akaniambia “Noriega, no smoking bro. Even though I forgot to tell you”
Duuh ilikuwa kidogo tu nismoke, hata sijui ingetokea nini hebu Mungu nilinde. nikajikuta najisemea.
Ghafla nikajikuta naitupa ile puli chini huku nikimuangalia usoni yule jamaa wa kilatino.
Akaniambia njoo huku, tukafika kwenye meza moja kubwa hapa walikuwepo mashanta wakubwa wamekaa na vikaptura tu matumbo makubwa yakiwa yanachezewa na wadada wakali sana. Ile kufika tu hivi Jamaa mmoja akaniuliza Noriega?
Nikajibu yap yap sikutaka kukaa kizembe nikaamua kuanza kwenda sambamba na hizi code.
Namba tatu nikafungua kikaratasi pale chap nikamuonyesha akapiga vidole viwili cha shada na cha kati kama vile mtu anaomba ulinzi kwake. Baada ya ile ishara tu nikaona wale wanawake wote Malaya wakisambaa, na kuwaacha wale watu peke yao. Kisha akaja mtu mmoja ni baunsa ana kiboksi kidogo akanipatia huku akiniambia zikague uhesabu nikafungua kile kiboksi na kutoa zile noti nikazihesabu zilikuwa ni noti za dola mia zikiwa noti mia na ishirini.
Baada ya kuzihesabu, yule mlatino alitoa katochi kadogo na kunipatia akiniambia hako ni maalum kwaajili ya kukagulia pesa kama feki au zenyewe. Akanipa maelekezo na jinsi ya kukatumia kale katochi. Kisha mimi nikazama sehemu ya maliwatoni na kutoa mzigo wao nikawaletea hapo baada ya wao kuutesti mzigo wao na kujiridhisha kuwa ndiyo mali kusudiwa, chap nikatoka humo smoking room nikaenda zangu hadi nje kabisa ambapo simu yangu iliita,, sauti ni ya Denis, yaani sijui ni kwanini sikutaka kuendelea kubaki kwenye yale mazingira tena sijui ni kwasababu ya ile pesa au ni nini.
Denisi aliniuliza unaona upande wa kulia kwako kuna gari inapiga indicator ifuate haraka ingia humo.
Niilifuata fasta ambapo ile naikaribia tu hivi mlango wa nyuma ushafunguliwa nikaingia na ikapiga moto tukaondoka pale na kunyooka hadi eneo la Msasani club ambapo dereva alisimamisha gari kisha ikaja gari nyingine na kupaki pale pale tulipo sisi nikamuona Denis akishuka na kuingia kwenye hii gari yetu, Alikaa nyuma ambapo tulikuwa wawili mimi na yeye tu nikatoa kile kiboksi nikamkabidhi nae akakipitia kile kiasi cha pesa na kufurahi sana.
Basi dereva alipewa tu maelekezo ambapo aligeuza gari tukarudi tena uelekeo wa kisiwani ambapo tulivuka mataa ya morocco pale na kwenda mpaka pale Biafra wakanishusha pale, Denis akiniambia nichukue taxi inipeleke temeke maana kwenye gari alinipa kiasi cha dola mia nane na laki moja ya usafiri kwa usiku huo.
Kwanza nilianza kuhisi mbona Dunia inanifungukia kwa haraka sana kiasi hiki? Kulikoni au ndio baada ya hizi ruti zote nitaambiwa niende nje ya nchi nikamezeshwe madawa tumboni?
Pia Denis alinishauri kuwa kama nataka niwe accurate kwenye hizi kazi basi sina budi kuhamia mitaa ya karibu yaani kifupi niwe ndani ya wilaya ya Kinondoni.
Akaniambia itakuwa vyema kama nitatafuta chumba maeneo ya Mbezi beach ama Sinza. Nikajibu sawa.
Basi niliwasogelea madereva taxi wa pale Biafra ili tu kumridhisha Denisi lakini uhalisia sikuwa nazungumzia issue ya safari ya kwenda Temeke bali nilimlenga jamaa mmoja nilimuona kavaa jezi ya Simba nikamzuga mimi ni wa Yanga tukaanza kubishana masuala ya mpira pale mpaka ile gari aliyomo Denis ilipoondoka na mimi ndio nikaaga na kuondoka.
Mbele nilimpata boda boda mmoja tukaelewana bei ambapo alianzia elfu ishirini, Nikamwambia nina elfu kumi kwakuwa ilikuwa usiku kuelekea saa nne tukafunga hesabu kwenye elfu kumi na tano
Nikakwea chuma tukatambaa zetu hao nikiwa kwenye pikipiki mara nasikia simu inaita kucheki ni wife, nikapokea Ananiuliza vip mme wangu kwema huko lakini?
Nikamwambia niko kwenye piki piki nakuja kisha nikakata simu dereva akawasha tena tukaendelea na safari maana nilimwambia apaki pembeni kidogo niongee na simu.
Baada ya kufika mtaani kwangu nilishuka na kumpa dereva cha kwake akasepa na mimi nikaingia ndani nikatulizana.
Mwanamke akanivaa na maswali yake Enhee vip baba Fulani mipango yako iliendaje?
Nikamwambia kuwa Mungu anabariki naona kama nitafanikiwa ila nijipe muda tu, Uhhu!!! Afadhali sasa labda tutaweza kubadilisha hata maisha yetu maana yaani kiukweli nimepachoka hapa ni vile hujui tu natamani hata tuhame kesho kama ingekuwa inawezekana.
Nikamwambia hiyo jeuri ya kuhama hapa kwenye gharama ndogo unaitoa wapi wewe mama Fulani?
Kiukweli sio kwamba napapenda hapa kihivyo ni vile tu uwezo wa kipato na uungwana wa mwenye nyumba wetu kwanza haishi hapa yeye anaishi huko Kigogo hata kodi ikiisha anaweza kukaa hata mwezi ukapita ndio anakuja kukudai.
Hata ukimwambia umepungukiwa atakusikiliza tu na kukutia moyo ili kesho uzidi kupambana mambo yaende sawa, kifupi hii ndio sababu inayonifanya niendelee kuishi hapa japo maji ya bomba hamna zaidi ya maji chumvi ya visima tena kuna kisima maarufu tu ukiwa unaenda mashariki kuna nyumba moja ya mzee muarabu ndio hutuuzia maji ndoo shilingi hamsini anasema anauza bei ya chini ili ile nusu iwe kama zaka kwa Allah..
Wapi nitaenda nipate chumba na sebule kwa elfu thelasini niambieni mimi. Kama sio huko msasani lutamba ama tandale kwa mtogore , ukikoswa sana kigogo luanga au Kino shamba.
Unapajua huko kwanza? Huko wanaishi nusu duniani nusu kuzimu na hapo bado mvua hazijanyesha, unashangaa ulienda kwenye utafutaji unarudi jioni hata ile nyumba uliyopangapo chumba huioni ishaenda na maji.
Niacheni na Ngeta yangu mie, kwanza huku kuna watoto wa kike mashombe shombe wasio na idadi kutokana na wingi wa waarabu halafu wanakula spidi ile mbaya, hiyo ni miguu ya kuku na utumbo wa kuku poa usipime.
Ukiwanunulia chipsi au ndizi mzuzu umewamaliza wanatulia halafu wanazipenda ndoa kama nini yaani ni kama wanashindana kuolewa ila hao waoaji ndio wa kuhesabika hivyo wapo wapo tu majumbani kwao kutwa kupokezana vibao vya mbuzi na mama zao jikoni
. Sasa wataenda wapi unadhani?
Na wengi ni masingo maza mimba kapigwa na msela wa mtaa wa pili hapo msela mwenyewe bado anaishi kwao hana mitikasi yoyote basi mimba inalelewa na mtoto anazaliwa na kulelewa hapo hapo kwa akina binti.
Siwezi sema kuwa sababu ni uchumi hapana pia kutojitambua kwa vijana kunachangia maana sisi wengine tulivuta jiko ndani hatuna hata godoro.
Na mpaka leo hii life tunalisebenza kiaina.
Mida ya saa tano nilitoka bafuni maana lazima nioge kwanza kutokana na mizunguko niliyotoka pili kuupoza mwili ili uende kukabiliana na joto la ndani maana kuna muda ,hata feni inanyoosha mikono juu nayo inaanza kutema joto .
Baada ya kutoka bafuni sikuwa na uhitaji wowote ule wa chakula maana nilikuwa niko full sana kutokana na ile shoo ya kule Masaki.
Tulikaa muda mfupi na wife kitandani huku tukingojea watoto wazame usingizini, ili tuweze kula chakula cha uzima.
Hatimaye mida iliwadia nikaukwea mlima nikiwa na nguvu kama simba kutokana na mawazo juu ya pesa kuwa hayapo tena hata namna moyo wangu ulivyokuwa ukidunda nilihisi mabadiliko makubwa sana. Kifupi nilikuwa comfortable sana yaani.
Hii ni nguvu ya pesa,, kwa sasa halipingiki hilo yaani michongo ya pesa ikivurugika tu hata performance kitandani inapungua kwa mwanaume maana tendo lile hisia zinaanzia kwenye akili jinsi unavyoitafsiri picha ya utupu wa aliyepo mbele yako.
Ni muda gani nilipitiwa na usingizi? Hata sikumbuki, si unajua tena baada ya mshindo ni kiasi tu cha dakika kadhaa usingizi unakuvaa?
Niliamshwa na simu mida ya saa kumi na moja na madakika yake, Namba ni ile ya Denis. Akaniuliza kama bado niko home, nikamjibu yeye ndie kaniamsha maana sikuwa na ratiba ya kudamka.
Akanipa ramani ya kazi ya siku hiyo maana ilitakiwa mapema sana nifike namba saba kuna mtu ana mzigo natakiwa niupokee kisha nisambae nao mpaka napopajua kusubiri maelekezo ya baadae.
Basi nilijiwasha kimoja cha fasta ili kuiweka akili sawa.
Mida hii najiwasha alipita mwanangu mmoja wa hapo kitaa tu ambae huwa tunawasha wote mida ya jioni kwa jina la Hamza.
Akaniambia kuwa ana mzigo mmoja amenunua juzi tu yaani ni mkali ile mbaya hajui hata unalimwa wapi, Akasema kama sio kitu cha Tukuyu Mbeya kile, basi kitakuwa cha Kisimiri Arusha, au Kilibho Tarime.
Nikamwambia kama kitu kinawaka sana akilete chote maana nahitaji mzigo mzuri kwaajili ya matumizi yangu binafsi.
Alikubali ambapo aliondoka na kuchukua kama dakika kumi akawa amerudi tayari. Tukaanza kuvuta kitu chetu.
Ni kweli kitu ni kikali tena sana maana nilivuta puli moja hata sikuimaliza nikawa niko juu sana, nikamuacha Hamza akivuta baada ya kubeba mfuko mzima ambao ulikuwa kama kisado hivi nilimpa kama elfu ishirini hivi, ile kimemba tu. Nikarudi zangu ndani kujiandaa maana ilitakiwa nimuwahi mtu huyo ambae niliambiwa mida ya saa mbili na nusu atakuwa kituo namba saba.
Saa mbili kamili ilinikuta niko mtaa wa Uwazani kwenye mgahawa mmoja maarufu sana kwa mitaa ya magomeni unaitwa Mnaa hoteli.
Nilikaa zangu pale nikaagiza maziwa na maandazi Fulani hivi malaini sana ni mgahawa ambao unasimamiwa na watu kutoka Pemba kuanzia mapishi mpaka wahudumu wa hapo so nafikiri wapemba wengi hujaa sana hapo kutokana na vyakula vya jadi yao kupatikana hapo.
Saa mbili na dakika zake nilikuwa nasogea taratibu kutoka uwazani kwenda mtaa wa dosi ili nifike kituo namba saba.
Ile nimefika kwenye kona ya mkono wa kulia inayoingia New bondeni hotel au maarufu sana kwa jina la Kwa Macheni.
Kuna gari moja nyeusi, imekaa utamu ile mbaya ilikunja kutoka kwenye kona hiyo na kunipiga mkasi kwa mbele, kisha kioo kikashushwa kidogo nikakutanisha macho na Kaburu moja lenye macho ya paka janki Fulani tu hivi miaka kama thelasini hivi.
Likauliza tu “Who?”
Nikajibu “Noriega”
“Stop number?”
Nikajibu “Seven”
Likanirushia kibegi kidogo kama hivi ambavyo wanavipenda hawa watoto wa kiume uzao wa masingo maza.
Nikakidaka na kukivaa kisha gari ikapiga mwendo na kutoweka pale.
Kibegi kilikuwa kizito kwa makadirio ni kama mzigo uliomo unafika kilo tatu.
Basi nikageuka ili niondoke lakini nikahisi kama kuna gari nyuma yangu. Ni kweli nyuma yangu niliona gari ikija kwa kasi sana na hivi ni njia ya vumbi basi vumbi lilikuwa likitimka nyuma yake.
Na baada ya kunifikia dereva alifanya kuzungusha matairi ya nyuma na kutimua vumbi zaidi Akili yangu ilikuwa inawaza ni kitu gani kinataka kutokea hapa ?
Yaani mikago nishaiotea halafu kunataka kuibuka maseke tena? Mungu niepushie dhahma ya aina yoyote ile maana si unajua tena nishaupima mziki kupitia vibunda nikajua kuwa nacheza sebene la bei. Sasa nani yuko tayari kupishana na vile vitita vya dolari? Yaani ile wanji wanji mshindo mmoja unaiona milioni hii hapa, walete.
<<<<<<<<<<<<< ****** ********** >>>>>>>>>>>>>>>>>>>...
Ile gari ina heri ama shari kwa Boyo?
Tutaendelea tena panapo majaaliwa ya aliyetuumba.
Wako katika utunzi Sonko Bibo.
0653532222 Piga masaa 24 itapokelewa..