SoC02 Agizo lolote linapotelewa, muongozo wa mbadala wake utolewe, ili kuepusha kukiukwa kwa agizo hilo

SoC02 Agizo lolote linapotelewa, muongozo wa mbadala wake utolewe, ili kuepusha kukiukwa kwa agizo hilo

Stories of Change - 2022 Competition
Joined
Aug 25, 2022
Posts
42
Reaction score
71
Tunaishi katika ulimwengu ambao kila mahali utakapofika au utakapodhuru kuna utaratibu maalum uliowekwa na wahusika wa eneo hilo ili kuepusha sintofahamu yoyote inayoweza kujitokeza, inayoweza kumgharimu mhusika au mgeni yoyote kwa namna moja au nyingine.

Hii inaanzia katika ngazi ya mtu binafsi; sote tunafahamu kuwa wanadamu tunatofautiana kulingana na hulka zetu, kuna watu ambao ni wacheshi, si wepesi wa hasira, wapenda masihara na utani wa kila namna ambao wana uwezo mkubwa wa kutengeneza urafiki na watu tofauti tofauti ndani ya muda mfupi sana kutokana na hulka yao; hawa kitaalam tunawaita "sanguine".

Wengine ni wakimya mno, sio wacheshi, sio wachangamfu, si wazungumzaji, wepesi wa hasira na kubwa zaidi ni watu wanaoweza kufanya jambo lolote hatarishi ndani ya muda mfupi sana endapo mtu atakiuka mipaka yao katika kushirikiana nao, hawa kitaalam tunawaita "choleric". Yapo makundi mengine ya watu kama vile "phlegmatic" na "melancholic" ambao nao wana hulka zao, lakini nisingependa kujikita sana kuzungumzia zaidi hulka za makundi haya. Nilichotaka kumaanisha ni kuwa, kila mwanadamu ana hulka yake ambayo ndio asili yake kisaikolojia.

Huwezi kujaribu kushirikiana kirahisi na mtu ambaye ni "choleric" kama unavoshirikiana na "sanguine" ambaye yeye ni mwepesi kuingilika kulingana na asili yake. Unapovuka mipaka, ni rahisi sana kutokea mtafaruko baina yako na mtu "choleric", tofauti na "sanguine" ambaye mnaweza kukaa chini na kufanya mambo yazungumzike ndani ya muda mfupi.

Hii haishii kwenye ngazi ya mtu binafsi tu, inaendelea kwenye ngazi ya familia, kwani kila familia ina utaratibu wake wa kuishi na mtu yeyote anayedhuru mahali hapo, yampasa kutii maagizo ya wenyeji na kufuata utaratibu uliowekwa mahali hapo.

Hii inazidi kwenda katika ngazi ya jamii, ndio maana unaweza fika katika eneo la jamii fulani, ukashangaa kwanini utaratibu huu ni wa kushangaza kwa upande wako, lakini kwao ni jambo la kawaida. Mfano wenzetu wa Hadzabe na wa Tindiga, kuanzia lugha yao wanayozungumza ni ya kipekee mno, mavazi wanayovaa, vyakula wanavyokula pamoja na utamaduni wao wakuishi maeneo yaliyojitenga na jamii za kawaida. Ndio maana, ukijaribu kudhuru maeneo yao, yakupasa kutii maagizo na utaratibu waliojiwekea katika himaya yao ili uweze kushirikiana nao kwa amani.

Hii itazidi tupeleka mbali zaidi katika ngazi ya mitaa, kata, wilaya hadi mikoa. Ndio maana kuna mikoa mingine nchini kwetu imejiwekea utaratibu ambao ni wa kipekee jinsi ya kupambana na changamoto tofauti tofauti. Mfano, mkoa wa Kilimanjaro nchini Tanzania, una utaratibu maalum na unaotekelezeka kikamilifu kwa miaka mingi sasa wa kupambana na uchavuaji wa mazingira kwa kutoza faini au kuswekwa ndani kutumikia adhabu ya kosa alilolitenda mtuhumiwa. Tofauti na mikoa mingine ambapo sheria au mabango ya amri yakitoa agizo fulani, hatuoni yakipewa msisitizo wa kutosha katika utekelezaji wake.

Katika ngazi ya taifa ndiyo eneo ambalo ningependa kujikita zaidi kupitia andiko hili. Sote ni mashahidi, tunashuhudia sheria, amri na maagizo mbalimbali yakiwekwa na halmashauri zetu, wilaya zetu, mikoa yetu na hata taifa letu kiujumla lakini yamekuwa hayatolewi ufafanuzi zaidi au kutoa mbadala wake katika namna ya kuziishi au kutii maagizo hayo ili kuepusha wananchi kujiingiza kwenye mikono ya sheria; mbali na hapo pia amri nyinginezo zinawekwa lakini hazifanyiwi utekelezaji wowote katika kuwawajibisha wakiukwaji wa amri hizo.

Amri zinazowekwa mahali fulani zina umuhimu mkubwa mno baina ya pande zote mbili yaani mtoa amri na mtii amri. Utaratibu huu unasaidia kupunguza matukio ambayo hayana staha au tabia zisizo njema kuendelea kutendeka katika jamii ya watu fulani, pia husaidia kutoa muongozo ili haki itendeke muda wowote endapo tukio linaweza kutokea na mwisho kuifanya jamii iwe katika mikono salama yenye amani.

Sheria, taratibu na amri mbalimbali ziko kila mahali nchini mwetu, kuanzia kwenye vyombo vya sheria, mitandao, vituo vya habari, maofisini, barabarani, mahospitalini, jeshini, sokoni, mashuleni, makanisani, misikitini, michezoni, vyuoni, mahotelini, kwenye mashirika na asasi mbali mbali sizizo za kiserikali. Kama nilivozungumza awali, hii inasaidia kuwepo kwa ustaarabu na usalama kati ya raia na watoa huduma katika maeneo hayo husika.

Mfano mzuri ambapo amri au utaratibu huwa ni rahisi kueleweka kutokana na utolewaji wa mbadala wake ni maeneo kama vile barabarani. Unakuta labda njia ya upande mmoja imefungwa kutoka na ukarabati unaofanyika na wakandarasi. Katika tukio kama hili, wengi ambao ni wazoefu barabarani wanaelewa kuwa muongozo hutolewa papo hapo kwa njia ya maandishi au alama inayoelewa ya kumuongoza dereva labda apite kushoto au kulia, ageuze au azunguke, asimame kusubiri au aendelee na safari n.k. Hii inasaidia kuondoa sintofahamu yoyote na kufanya utaratibu ufwatwe kirahisi bila kutumia nguvu nyingi na kuondoa watu katika zengwe la kuingia kwenye uvunjifu wa agizo au sheria fulani.

1662976352306.jpeg

Chanzo: iStockphoto.com

Mfano picha ya hapo juu inaonesha dhahiri kwamba kuna ukarabati unaendelea hapo mbele, hivyo yampasa dereva apite kushoto na kuendelea na safari yake kwa usalama zaidi. Hii inaonesha jinsi gani inavyokuwa rahisi kuchanganua mambo endapo tunatoa na muongozo mbadala wa nini kifanyike kuliko kumuacha mdau ajaribu kujiongeza mwenyewe, kitendo kinachoweza kumpelekea avunje sheria au utaratibu fulani pasipo kujua.

Sehemu nyingine ambapo muongozo na mbadala wake hutolewa kikamilifu ni kama maeneo ya vyuo vikuu kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu Ardhi na vyuo vinginevyo nchini. Mavazi yametolewa ufafanuzi kabisa kwamba vazi la aina fulani haliruhusiwi huku wakionesha vazi la aina fulani ndilo stahiki mahali hapa. Hii inasaidia hata mwanafunzi anapokamatwa kwa uvunjifu wa sheria na taratibu zilizowekwa asionekane anaonewa kwani alionyeshwa dhahiri nini kilipaswa kifanyike ili asijiingize matatizoni.
1662976396114.jpeg

Chanzo: quora.com

Changamoto inaanza kuja pale ambapo utaratibu fulani umewekwa katika eneo husika lakini haueleweki au haujitoshelezi na kupelekea kuwaacha wadau njia panda wasielewe nini kinachohitajika kufanyika ili kwenda sambamba na agizo hilo. Ningependa kutolea mfano wa hapa jijini Dar es Salaam kwasababu mimi ni mkazi wa hapa, unakuta amri imewekwa “MARUFUKU KUKOJOA ENEO HILI”. Huku mtu akiangalia huku na kule hamna mtu wa kumuona, mbaya zaidi choo cha karibu kipo kilometa 5 na zaidi kutoka mahali alipo. Sasa mtu huyu umempa amri ya asikojoe hapa, alafu hakuna huduma ya choo karibu naye; Anaweza jikaza mara ya kwanza na ya pili akatafuta huduma hiyo ilipo, lakini kesho na kutwa hatoweza kumudu shida yote hiyo kama labda hapo ndio eneo lake la kazi. Mfano mwingine ni amri ya “MARUFUKU KUTUPA TAKA ENEO HILI”. Unakuta mtu ana uchafu na anahitaji kuutupa; eneo la karibu na ulilompa amri ya asitupe taka, hakuna vihifadhi taka (dustbins), mbaya zaidi eneo hilo hilo kwenye bango la amri ni pachafu; sasa kama mamlaka husika, mdau huyu mnamsaidiaje ili msimweke katika mikono ya sheria. Kwa kawaida kama mwanadamu niliyestaharabika, siwezi kutembea na takataka mkononi, sina budi kuiweka mahala husika ili niendelee kuwa huru na nadhifu.
1662976473682.jpeg

Chanzo: mtaakwamtaa.co.tz
Hata kwenye mitandao ya simu pia, unakuta promosheni mbalimbali zinafanyika, washiriki wa promosheni hizo mnawaambia vigezo na masharti kuzingatiwa, huku wao wenyewe hawavijui vigezo na masharti hayo. Mnaweza mtangaza leo mshindi, alafu kesho mnamwambia amekiuka vigezo na masharti hivyo ushindi wake ni batili, hii inawaumiza sana na inasikitisha kwa kweli. Ukweli ni kwamba haki haitendeki kwa namna hii na huu ni udanganyifu, laiti washiriki hawa wangekuwa na uwezo wa kuchanganua mambo na kujua kudai haki na stahiki zao, promosheni nyingi zingekuwa na kesi za kujibu kutokana na kukithiri kwa vitendo hivi.

Mapendekezo:
  • Popote amri au agizo fulani linapotolewa, kuwepo na suluhu ya kuepuka kukiukwa kwa agizo hilo katika eneo hilo hilo mdau anapokutana na sharti hilo kama baadhi ya mifano hapo juu ilivyojidhirisha. Hii ni kuanzia ngazi ya mtu binafsi jinsi anavyopenda kushirikiana na watu yaani mipaka baina ya mtu kwa mtu, hadi katika ngazi kubwa ya kitaifa na kimataifa.

  • Serikali pamoja na mamlaka husika, zijitahidi zaidi katika kutoa huduma za msingi ambazo zinamgusa mwanadamu. Kama inavyopambana kujenga barabara ili maeneo yafikike, kujenga mahospitali ili watu watibiwe, kuweka miundombinu ya maji ili yawafikie watu, basi vilevile waweke na vyoo vya umma kadhaa katika kila halmashauri hususani maeneo ya mjini. Hata kwenye swala la taka, lihakikishe vyombo vya kuhifadhi taka vipo vya kutosha kwenye kila halmashauri ili kupunguza wigo wa uzagaaji wa taka ovyo kwenye jamii zetu.
  • Mitandao ya simu, iweke wazi maswala ya vigezo na masharti kuzingatiwa ili kuwepo na haki kwa washindi wa promosheni hizo. Ukweli ni kwamba pesa nyingi sana zinakusanywa na mitandao hii na mitandao hii kutokana na washiriki kuwa wengi. Hili sio tatizo kwasababu kupanga ni kuchagua, lakini shida inakuja kwenye ugawaji wa hizo stahiki katika hao wachache wanaobahatika, basi wapewe stahiki zao kuliko kunyonywa na kauli ya VIGEZO NA MASHARTI KUZINGATIWA. Serikali kupitia Wizara ya Michezo naomba iingilie kati kwenye swala hili, ili litafutiwa ufumbuzi na kuwaondoa watu katika sintofahamu hii.

  • Kuwepo na uwazi katika kila sheria au amri pamoja na adhabu zake, ili kupunguza wigo la urasimu au rushwa kwenye kuitafuta ufumbuzi au suluhisho endapo tatizo fulani au kosa fulani linapotendeka.
Hitimisho:
Endapo yote yaliyoelezwa katika andiko hili yatafanyiwa kazi na kutekelezeka kikamilifu, hakika tutakuwa tumezikomboa jamii zetu na wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakijikuta wakiingia kwenye mikono ya sheria pasipo kukusudia, maana wanasema kutokujua sheria au amri fulani hakuwezi kumuondoa mtuhumiwa kwenye hatia.

Nakabidhi,
Andrew Ikingura
 
Upvote 4
Back
Top Bottom