Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, akiwa kwenye kitanda cha wagonjwa wakati akipelekwa wodi ya Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI).
Sakata la ajali iliyompata mbunge wa jimbo la Kyela, Dokta Harrison Mwakyembe, umeingia katika hatua mpya baada ya baadhi ya watu kudai kuwa ajali hiyo ilipangwa na lengo lake lilikuwa kummaliza.
Baadhi ya watu waliozungumza na Alasiri wamesema uwepo wa taarifa tofauti zinazohusiana na chanzo cha ajali hiyo, unaonyesha wazi kwamba `si bure.
Mmoja wa watu waliodai kuwa ajali hiyo ina mkono wa mtu ni Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila ambaye amesema maelezo ya Dk. Mwakyembe na dereva wake ndiyo yanapaswa kuwa ya kweli kwa vile wao ndio walikuwa kwenye eneo la ajali.
"Polisi walifika baada ya ajali, lakini Dk. Mwakyembe na dereva wake wameishuhudia ajali, hivyo maelezo yao ndiyo yako sahihi," akasema Mchungaji Mtikila.
Akasema kitendo cha Polisi kutoa maelezo tofauti na wao ndicho kinachozidi kuleta mashaka.
``Hapa kuna jambo. Walioshuhudia ajali wanatoa maeleo yao na wasioshuhudia nao wanaleta yao
hili ndilo linaleta utata, akasisitiza Mchungaji Mtikila.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama cha TLP,Bw. Augustine Mrema amesema licha ya kuwa Polisi wana maelezo tofauti, kinachopaswa kufanywa hivi sasa ni kuwaachia wachunguze ukweli wa chanzo cha ajali hiyo na kutoa ripoti yao.
Amemshauri Dk. Mwakyembe kutoendelea kulizungumzia suala hilo na badala yake aachie dola ifanye kazi yake.
Kabla ya kutoa rai hiyo, Bw. Mrema alimpa pole Dk. Mwakyembe kwa kupata ajali hiyo, huku akimtaka aendelee kujiweka mikononi mwa Mungu.
Maelezo ya Polisi kuhusiana na ajali hiyo yanadai kuwa gari la Mheshimiwa Mwakyembe wakati likijaribu kulipita lori, lilivaa shimo lililokuwa katikati ya barabara, tairi likachomoka na hivyo gari likapoteza mwelekeo na kuingia porini ambako lilipinduka mara nne.
Hata hivyo dereva wa gari la Dk. Mwakyembe alisema lori lilimpa saiti ya kupita na alipofanya hivyo, likamzibia tena njia, kitendo kilichosabisha ajali.
Dk. Mwakyembe alipata ajali mbaya juzi katika eneo la Ihemi, mkoani Iringa wakati akitokea jimboni mwake kuja Jijini Dar es Salaam.
Baada ya ajali hiyo, Dk. Mwakyembe alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa kabla ya kusafirishwa kwa ndege ya kukodi kuletwa Dar es Salaam na kulazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili, MOI.
Hata hivyo jana jioni Dk. Mwakyembe aliruhusiwa kutoka hospitalini baada ya madaktari kuwa afya yake imeimarika.