``Mheshimiwa Dk. Mwakyembe ni Mwanasheria, tena Daktari alikuwa anafundisha Chuo Kikuu. Moja ya vitu alivyokuwa anafundisha ni "Natural Justice".
Mheshimiwa Spika, wewe ni Mwanasheria unafahamu suala la Natural Justice. Kwamba Kamati Teule imesikiliza watu wengine wote pamoja na wanaoita minong'ono ya mitaani, wamesafiri mpaka Marekani kutafuta mashahidi, lakini mimi ambaye ni mmoja kati ya watuhumiwa mle hawakunihoji hata siku moja.
Mheshimiwa Spika, nimesimama kueleza masikitiko yangu. Ofisi ya Bunge mpaka ofisini kwangu hata kama wangeniita ningekwenda kwa miguu kama hamna gari na nilikuwa tayari kufanya hivyo.
Hawa ni watu makini sana siwezi kuamini kwamba wanaweza wakafanya oversite kama hiyo. Kulikuwa na shida gani kuja kuniuliza Waziri Mkuu wanasema uliotoa dokezo hili ni sawa sawa kweli?
… Hapa ndipo tunategemea tuwaonyeshe umakini wetu, umahiri wetu katika mambo ya demokrasia. Kwa nhiyo nilichofanyiwa napenda kuweka kumbukumbu sawa kwamba naona si sahihi, nimefadhaika sana, nimedhalilishwa sana, nimeonewa sana katika hili.
Maana zimechukuliwa tuhuma zikaelezwa hapa kwamba hivi ndivyo ilivyo. Mimi sijaulizwa. Kulikuwa na shida gani kuniuliza, kwa nini muamini minong'ono ya mitaani kuliko maelezo yangu. …Hatuwezi, Tume imepewa muda wa kutosha lakini inashindwa kumuona mtu ambaye wanamtuhumu...``