Moto mkubwa uliotokea katika makazi ya Wang Fuk Court eneo la Tai Po, Hong Kong, usiku wa kuamkia Novemba 26, 2025 umeua watu 128, akiwemo Afisa mmoja wa Zimamoto, huku zaidi ya watu 200 wakiwa bado hawajulikani walipo.
Zaidi ya watu 79 wamejeruhiwa, na juhudi za uokoaji zinaendelea huku miili zaidi ikiendelea kutolewa kwenye majengo hayo. Taarifa za awali zinaonyesha kuwa mlipuko wa ghafla na kuenea kwa moto kwa kasi ndiyo yaliyowafanya watu wengi kukwama ndani.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa povu la plastiki (styrofoam) lililotumika kufunika madirisha ya lifti na maeneo mengine ya ukarabati ndilo lililosababisha moto kusambaa kwa haraka. Nyenzo hiyo, ambayo ni rahisi kushika moto, ilichochea kuwaka kwa sehemu za ndani kupitia korido za majengo.
Aidha, neti na vifuniko vya nje vilivyotumika wakati wa ukarabati viligundulika kutokidhi viwango vya usalama wa moto, hivyo kuchangia ukubwa wa maafa.
Kutokana na tukio hilo, Serikali ya Hong Kong imeanzisha uchunguzi wa kijinai, huku Waziri Mkuu John Lee Ka-chiu akiagiza ukaguzi wa haraka katika miradi yote ya ukarabati inayoendelea kwenye makazi ya umma.
Wakati huohuo, kikosi cha zimamoto kinaendelea na kazi ya uokoaji. Baadhi ya manusura, akiwemo mwanamke, mzee, na wanyama kadhaa, wameokolewa wakiwa hai kutoka maeneo ya juu ya majengo.
Taasisi ya Kupambana na Rushwa (ICAC) imewakamata Wakurugenzi wawili wa Will Power Architects, kampuni mshauri wa mradi wa ukarabati. Hii imefanya idadi ya waliokamatwa kufikia watano.
Watatu wengine kutoka kampuni ya Prestige Construction & Engineering Co. Ltd, wakiwemo Maafisa Wawili wa juu, wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kuua bila kukusudia baada ya kutumia nyenzo zisizokubalika kisheria ikiwemo styrofoam na neti hatarishi ambazo zimehusishwa moja kwa moja na kusababisha maafa hayo makubwa.