Alfu lela ulela, kitabu cha nne

Alfu lela ulela, kitabu cha nne

Mhindi akajibu, ‘Seyid yangu, sisemi kwa umbo lake la nje ila kwa manufaa yake ninayoyapata. Kazi yangu ni kumpanda tu na kama nataka kwenda mahali fulani, hata kama ni mbali, kwa dakika chache tu hujiona nimefika. Basi Seyid yangu, haya ndiyo yanayomfanya farasi huyu kuwa wa ajabu kabisa, na kama kwa enzi yako utaniruhusu kumpanda, utaweza kusadikisha mwenyewe.’

Huyu Mfalme wa Ajemi aliyekuwa akipendezwa na kila jambo la ajabu, wala naye hakupata kuona farasi wa namna ile, akamwambia Mhindi ampande farasi, ili apate kuonyesha manufaa yake, Mara akampanda na kumwuliza mtafme wapi anakotaka kumtuma. Mfalme akamwambia, ‘Wauona mlima ule-e?’ Akaonyesha kilele cha mlima mkubwa mno uliopanda juu mawinguni, yapata mwendo wa saa kasorobo kutoka pale Shirazi mpaka kufika huko. ‘Nenda kaniletee tawi la mikindu inayoota chini yake.’

Mfalme alipotamka maneno haya yule Mhindi akaizungusha sukurubu iliyowekwa juu ya shingo ya farasi karibu na tandiko, mara akapaa hewani kama umeme asionekane tena. Muda wa robo saa Mhindi akaonekana anarudi, amechukua tawi la mkindu mkononi mwake, akimteremsha chini farasi wake karibu na kiti cha enzi, akashuka na kuliweka lile tawi mbele ya mfalme.

Sasa mfalme akasadikisha ule mwendo wa ajabu wa yule farasi na akatamani awe naye yeye, na hivyo ndivyo ilivyokuwa, maana yule Mhindi alikuwa tayari kumwuza, na mfalme naye alikuwa akimtazamatazama farasi kama aleyekwisha kumnunua.

Mwisho akamwambia Mhindi, ‘Kwa umbo lake la nje tu, sikumdhania kuwa ni mnyama wa manufaa jinsi hii, nami nimefurahi sana kwa kunionyesha kosa langu, na ikiwa utaniuzia sema bei yako. ‘

Mhindi akajibu, ‘Seyid yangu, sina shaka kuwa mfalme mwenye hekima kama wewe atanifanyia haki kwa farasi wangu baada ya kuona uhodari wake kwa mara ya kwanza, na mimi sikwenda mbali sana kwa kufikiri kuwa labda utampenda awe wako. Basi ni afadhali nimtoe zawadi, na hivyo nitakupa wewe bwana wangu kwa sharti moja. Farasi huyu sikumfanya mimi ila nilipewa na mtu aliyembuni, kwa kubadilishana na binti yangu, tena kwa kuniapisha kiapo kuwa sitotengana naye vivi hivi tu, ila kwa kitu cha thamani sawasawa.’

Mfalme akamwambia, ‘Taja cho chote utakacho. Milki yangu ni kubwa yenye miji mikubwa mikubwa mizuri. Chagua uupendao, uutawale mpaka mwisho wa maisha yako.’

Mhindi hakuona ukarimu huo unatosha kama vile alivyoona mfalme. Akajibu, ‘Seyid yangu, ninakushukuru sana sana kwa kunipa utawala, ila nakusihi usinikasirikie, ikiwa nasema kuwa naweza kukutolea farasi wangu kwa kubadilishana na binti yako.’

Wafuasi wa mfalme waliposikia maneno haya wakaangua vicheko wakacheka, na Feroz Shah mwana wa mfalme, ambaye, ndiye mrithi wake, akakasirika sana kwa ufedhuli kama ule. Lakini mfalme alifikiri kuwa haitamwia thamani kubwa kutokana na binti yake kwa kupata mchezo mzuri kama ule. Basi wakati mfalme alipokuwa akisitasita kujibu, mwanawe akaingilia kati akasema, ‘Seyid yangu, afadhali usifanye haraka kumjibu bazazi huyu fidhuli. Fikiri jinsi damu ya babu zako itakavochanganyika na kuwa duni.’

Mfalme akajibu, ‘Mwanangu, najua wasema ndivyo, lakini naona huitambui thamani ya farasi, na kama nikiyakataa kweli mashauri ya Mhindi, ataondoka aende akamwambie mfalme mwingine maneno haya haya, nami hivyo nitaona kushindwa nikimfikiri mtu ye yote mwingine kuipata hii Ajabu ya Saba ya Dunia.

Kwa hakika sisemi kuwa nitayakubali masharti yake, lakini naye pengine huenda akatoa sharti ingine, basi kwa kitambo hiki tulicho hapa ningependa umwangalie farasi huyu, na kwa ruhusa ya mwenyewe, umjaribu mwendo wake.’

Yule Mhindi aliyekuwa akisikia maneno haya ya mfalme akaona iko dalili ya kupata vile alivyokusudia, akafurahi na kuridhia kwa yale aliyotaka mfalme. Akaja kumsaidia mwana wa mfalme apate kupanda farasi na kumwonyesha namna ya kumwendesha, Lakini kabla hajamaliza kumwonyesha yule kijana akaizungusha Sukurubu, na mara ile ile farasi akapaa hewani akawa haonekani tena.

Watu wote waliokuwapo kuangalia wakakaa kungojea kwa muda, wakitaraji kuwa pengine huenda mara wakamwona kwa mbali akirudi, hata mwisho yule Mhindi mwenyewe akawa na hofu. Ndipo akaenda akajiangusha kifudifudi mbele ya kiti cha enzi, na kumwambia mfalme, ‘Seyid yangu, bila shaka umeona kuwa mwanao hakufanya subira, hakunidirikisha kumwambia yote yaliyokuwa haja kumwambia ili aweze kurudi mahali alipoondokea. Basi nakusihi usiniadhibishe; kwani hilo si kosa langu, wala usinipatilize kwa mashaka yo yote yátakayompata.’

Kwa hofu kuu aliyokuwa nayo mfalme akasema kwa hasira ‘Lakini kwa nini hukumwita arudi wakati ulipomwona anatokomea?’

Mhindi akajibu, ‘Mwendo wake wa kasi ulinitia bumbuazi hata kama ningalimwita hangalisikia. Lakini natutumai kuwa atafahamu kuizungusha sukurubu ya pili, ambayo itamfanya farasi kushuka chini.’

Mfalme akasema, ‘Ehe! Kama akifanya hivyo, kitu gani kitakachomzuia farasi hata asishukie baharini, au kumwangusha majabalini na kuvunjika kenyekenye?’

Mhindi akajibu, ‘Usiwe na hofu, bwana wangu, maana yule farasi ana akili ya kuvuka bahari, na kumpeleka mpandaji wake popote atakapo kwenda.’

Mfalme akamjibu, ‘Vema basi, lakini fahamu kuwa asiporudi tena kwa muda wa miezi mitatu, wala haniletei habari yo yote kuwa ni salama, maisha yako yatapotea.’ Kuisha kusema hivi akaamuru askari wake kumkamata Mhindi wamtie gerezani.

Kwa kitambo hiki chote, yule Feroz Shah mwana wa mfalme alikuwa amepaa hewani kwa furaha, na kwa muda wa saa nzima alizidı kupaa juu hata ile milima mikubwa mikubwa ilionekana sawasawa na tambarare. Kisha halafu akawaza kuwa sasa nai wakati wa kushuka chini, na kufanya hivyo ilimlazimu azungushe sukurubu kuelekeza njia, lakini kwa bumbuazi na hofu aliyokuwa nayo hakuthubutu hata kidogo. Ndipo alipokumbuka kuwa hakufanya subira kuambiwa namna ya kushuka chini tena, mradi akajiona hatari imemsimamia. Kwa bahati akili zake hazikumpotea, ndipo akaanza kuitazama shingo ya farasi kwa makini sana, hata mwisho kwa furaha yake kuu akagundua kigingi kidogo, kidogo sana kuliko kile kingine, karibu na sikio la upande wa kulia. Hata alipokizungusha, mara akajiona anashuka chini pole pole kuliko vile alivyopanda.

Wakati huo ulikuwa giza, na kwa vile ambavyo mwana wa mfalme hakuweza kuona kitu, alimwachilia farasi ajiongoze mwenyewe. Ilikuwa usiku wa manane Feroz Shah mwana wa mfalme alapogusa chini, amechoka, hasa kwa vile alivyokua hajala kitu tangu asubuhi.

Basi aliposhuka juu ya farasi, jambo la kwanza alilofanya ni kupatambua mahali alipo, lakini kwa ajili ya lile giza kuu hakuweza kutambua kitu ila alijiona yuko juu sakafuni kwenye jumba kubwa mno, lenye kuzungushwa viguzo vya vya nawe ya marmar. Katika pembe ya sakafu hiyo kulikuwa na kilango kinachofungulia vidaraja vya ngazi inayoendea chini ndani ya nyumba.
 
1645457414709.png
 
Watu wengine kabla hawajapeleleza sana huona woga, lakini mwana mfalme sivyo alivyo. Akasema, ‘Mimi sidhuru kitu na ye yote aliye mwenyewe akiniona sina silaha hatanidhuru vivyo, mradi akashuka chini pole pole bila ya vIshindo. Alipofika akaona mlango u wazi na sebuleni pana taa inayosinzia.

Basi kabla hajaingia ndani, mwana wa mfalme akasimama kusikiliza, lakini hakusikia kitu ila mikoromo ya watu. Na kwa mwangaza wa taa iliyotundikwa, akaona safu za askari wamelala kila mmoja ana upanga wazi karibu yake, na kisha alijua kwamba ukumbi ni lazima uwe na chumba cha mwanzo kabla ya kufikilia chumba cha malkia au cha binti mfalme.

Feroz Shah akasimama kimya kutazama tazama, mpaka macho yake yakamfunuka na kuzoea giza, ndipo akaona kwa pembeni paziani mwanga wa taa ukimulika ndani. Basi akaenda taratibu kuelekea pazia, na akalifunua upande mmoja na kuingia ndani ya chumba kikubwa kilichojaa wanawake waliolala, na wote walikuwa wamelalia vitanda vidogo ila mmoja ndiye aliyekuwa juu ya kitanda kikubwa; na huyo alimjua kuwa lazima awe binti mfalme. Akaenda pole pole kwa kunyembelea mpaka akafika kando ya kitanda chake, akamwangalia na kumwona ni mwanamke mzuri sana, zaida ya mwingine ye yote aliyepata kumwona. Walakini, japokuwa na yeye pia alikuwa mzuri, alijua sana hatari ya nafsi yake. Maana kama mmoja wao angestuka na kupiga yowe askari wangeamka, nao wangalimkamata wakamwua.

Basi akapiga magoti pole pole, na kushika mkono wa binti mfalme kuuvutia kwake taratibu. Binti mfalme alipofumbua macho yake akaona mtu mzuri aliyejipamba amempigia magoti mbele yake, akawa hana la kusema kwa kustaajabu.

Mwana wa mfalme akainamisha kichwa chini hali amepiga magoti, akasema, ‘Angalia bibi, mimi ni mwana wa Mfalme wa Ajemi, niliye na dhiki kwa masahibu yaliyonipata, na hata kama nitakuhadithia hutasadiki, na sasa najiona nimefika hapa, kuomba hifadhi yako. Lakini jana nilikuwa katika uwanja wa baba yangu, nikishughulika kwa kuitukuza siku kuu yetu kubwa; leo, niko katika nchi nisiyoijua, kisha ni katika hatari ya maisha yangu!’

Sasa huyu binti mfalme aliyeombwa rehema na Feroz Shah mwana wa mfalme, alikuwa ni binti mkubwa wa Mfalme wa Bengali, aliyestarehe ndani ya jumba jipya alilojengewa na baba yake, ambalo lilikuwa mbali kidogo na mji anaokaa mfalme. Akamsikiliza maneno yake mpaka mwisho, kisha naye akamjibu, ‘Sadiki maneno yangu, huko kuifadhiwa unakokutaka utahifadhiwa na wote,’ Kuambiwa hivi, mwana mfalme akataka kumshukuru kwa wema wake, lakini mara binti mfalme akasema, ‘Nitapenda kujua njia uliyosafiria hata ukafika upesi hivi, kisha nakuona umedhoofu kwa jaa, basi nitawaamuru watumishi wangu wakupeleke katika chumba changu kimojawapo ambamo utaandaliwa chakula, ule ulale.’

Wakati ule watumishi wote wa binti mfalme walikuwa wameamka wanasikiliza maongezi. Bibi yao alipowaita wakaondoka na kuvalia upesi upesi, na kuchukua jamii ya mishumaa iliyokuwa ikiwaka chumbani. Wakampeleka Feroz Shah katika chumba fahari, na watumishi wawili katika wale wakawa wanamtengenezea malazi na hao waliobakia wakaenda jikoni, mara wakarudi wamechukua masinia ya vyakula vya kila namna. Halafu wakamwonyesha kabati la nguo na shuka za kitandani, wakatoka.

Wakati ule watumishi walipokuwa hawako, binti Mfalme wa Bengali aliyestushwa sana kwa uzuri wa mwana wa mfalme, alijaribu kulala tena lakini usingizi ulimpaa kabisa. Hata watumishi waliporudi tena chumbani, akawauliza kama mwana wa mfalme amepata vyote alivyotaka, na kisha je walimwonaje?

Watumishi wakajibu, ‘Bibi, kwa hakika hatuwezi kukuambia nia ya kijana huyo jinsi ilivyo juu yako, ama kwa sisi twaona itauwa heri kama mfalme, baba yako, atatoa idhini ya kuolewa na mtu ye yote anayependeza. Hasa katika milki hii ya Bengali hakuna hata mmoja wa kufanana naye.’

Maneno haya ya kusifu mno hayakumpendeza binti mfalme, na kwa vile ambavyo hakupenda kudhihirisha aonavyo mwenyewe akawaambia, ‘Ninyi nyote ni kátika hao wanaopayuka, nendeni mkalale, nami nilale.’

Asubuhi alipokuwa akivalia, watumishi wake wakaona kuwa tabia yake ya desturi imebadilika kabisa, siku ile binti mfalme alikuwa na hadhari sana katika kuvaa nguo zake, na akushurutisha kwamba nywele zake zisukwe mara mbili au tatu na zaidi. Kwani, akasema katika nafsi yake, ‘Ikiwa umbo langu halikumpendeza mwana wa mfalme wakati aliponiona mara ya kwanza kwa hali niliyokuwa, sasa lazima nafsi yake itastuka akiniona nimejipamba vyombo vyangu vyote.

Akatwaa tovu la alması kubwa inayong’aa sana akalibandika nyweleni mwake, kisha akajipamba kwa mikufu ya lulu shingoni na vinagiri vya dhahabu mikononi na mshipi wa Johari kiunoni. Na watumishi wake wakamvika joho zuri la hariri safi lililotarizwa kwa nyuzi za zari, ambalo katika Bara ya Hindi yote halivaliwi na mtu ye yote, ila hao walio na asili ya ukoo wa kifalme.

Hata alipokwisha kuvalia barabara kama alivyopenda, akatuma mtu kutaka kujua kama mwana wa Mfalme wa Ajemi ameamka au kama yu tayari kumkaribisha, maana ndivyo alivyopenda kujitokeza mbele yake.

Mjumbe wa binti mfalme alipoingia chumbani mwa Feroz Shah mwana wa mfalme, akamkuta yu katika kutoka kwenda kutaka ruhusa ya kumwamkia bibi yake kwa heshima, lakini mara alipoambiwa anayotaka binti mfalme, akakubali. Akasema, ‘Hukumu yake ni halali kwangu, nami niko hapa kutii amri zake.’

Basi baada ya dakika chache binti mfalme mwenyewe akatokea, na baada ya kuamkiana kwa desturi, binti mfalme akakaa juu ya kitanda, akaanza kumhadithia mwana wa mfalme sababu zilizozuia hata asimkaribishe chumbani kwake. Akasema, ‘Kama ningalifanya hivyo, tungalikatizwa mazungumzo yetu na mkuu wa matoashi, ambaye ana haki ya kuingia chumbani kwangu kwa wakati wo wote apendao; na hivyo sivyo. Na sasa siwezi kuvumilia tena ila nataka kujua hicho kisa cha ajabu kilichokufikisha huku! Na hiyo ndiyo sababu iliyonileta hapa chumbani pako, ambapo hapana mtu awezaye kutuingilia kwa jeuri. Basi tafadhali, anza kuniambia, usikawie.’

Mradi mwana wa mfalme akaanza kumhadithia toka mwanzo, habari zote za siku kuu ya Nedroz inayofanyika katika milki ya Ajemi mwaka hata mwaka, na jinsi kulivyopambwa vizuri kwa kuienzi siku hiyo. Hata alipofika katika Farasi wa Uchawi, binti mfalme akasema, ‘SIwezi kufananisha kitu kinachostaajabishaKama hicho na kitu cho chote kingine.’

Mwana wa mfalme akaendelea kusema, ‘Mara moja waweza kutambua jinsi mfalme, baba yangu, alivyo na moyo wa matamanio kwa vitu vyote vilivyo vya ajabu, akatamani sana kumpata farasi huyo; mradi akamwuliza Mhindi kuwa atamwuza kwa bei gani.

Jibu lake lilikuwa la upuzi kabisa. Hakutaka kitu cho chote ila kumwoa binti mfalme, dada yangu lakini, ingawa wote waliokuwako walimcheka na kumfanyia dhihaka, mimi nilighadhibika. Nikaona kuwa baba yangu hawezi kukaza nia yake kutoa adabu kwa ufidhuli ule kama ilivyostahili. Nikajaribu kumwonya, lakini haikufaa kitu ila akanitaka nimjaribie farasi, kusudi (kama nilivyojua) anifanye kusadikisha zaidi thamani yake.

Kwa kumridhia baba yangu nikampanda farasi, na bila ya kungojea maagizo ya Mhindi, nikakizungusha kigingi kwa namna nilivyomwona akifanya mwenyewe. Na mara pale pale nikapaa juu hewani kwa upesi sana kuliko kuruka kwa mshale, nami nikaiiona kama nikaribiaye mbingu na kama itakayonigonga kichwa changu! Nikitazama chini sioni kitu, ndipo nikawa na wasiwasi mkubwa hata sikujua ni upande gani niendao. Mwisho, kulipokuwa kwaingia giza nikaona sukurubu ingine; hata nilipoizungusha, yule farasi akaanza kuteremka chini pole pole. Sasa ikanilazimu kutumainia bahati maana ilikuwa usiku wa manane; mara nikajiona niko juu ya dari ya jumba hili. Nikashuka chini ya ngazi ndogo, nikaja pole pole kwa kuelekea mwanga mdogo wa taa niliouona ukimulika kwenye mlango uliokuwa wazi, nikachungulia ndani nikaona matoashi wamelala. Kusema kweli, nilijua sana hatari iliyonikabili lakini kwa kuwa haja yangu ilikuwa kubwa sikuwajali kitu, mradi nikanyatianyatia pole pole nikawapita askari wako salama, mpaka nikalifikia pazia lililoziba mlango wa chumbani kwako.

Binti mfalme, sasa hayo yaliyobakia unayajua wewe, ila langu mimi ni kukuambia ahsante kwa wema wako ulionifanyia. Kwa sheria ya mataifa, mimi nimekwisha kuwa mtumwa wako, sina kitu tena ila moyo wangu tu, huo ndio ulio wangu mwenyewe kukupa. Lakini nasemaje hivi! Moyo wangu mwenyewe? Aa! Bibi, nao vile vile ni wako tokea dakika ile ya kwanza nilipokuona.’

Binti mfalme alijijua uzuri wake na kujipamba alikojipamba, na zile haya zilizomshika zilizidisha uzuri wake.

Huku kafadhaika alijibu, ‘Ewe, mwana wa sultani, umenitia furaha kuu, nami nimesikia masaibu yote yaliyokupata. Nasikitika kwa hatari zilizokupata huko juu hewani. Bahati iliyoje iliyokuleta humu nyumbani mwangu. Kwa wewe kuwa mtumwa, ama kwa hakika huo ni upuzi tu, na kukupokea kwangu nilivyokupokea hapana budi kumekusadikisha kuwa una uhuru hapa kama ulionao nyumbani kwa babaako.’ Akaendelea kusema kwa sauti ya kufariji, Na kwa huo moyo wako, nina yakini kuwa tangu zamani umekwisha elekea kwa huyo binti mfalme anayeustahili, wala mimi sidhani kuwa naweza kuwa ndio sababu ya wewe kumhadaa.’

Feroz Shah mwana wa mfalme alikuwa karibu kutaka kukataa kusema kwamba zamani hakuwa na bibi mwenye haki yeyote kwake, lakini akanyamaza kwa kuingia kwa mtumishi nmoja wa binti mfalme aliyesema kuwa chakula ki tayari. Chakula hicho kiliandaliwa ndani ya chumba fahari, na mezani kulikua na kila aina ya matunda mazuri. Wakati walipokuwa wakila vikatokea vitoto vya kike vilivyojipamba vizuri, vikaimba pole pole uzuri kufuatisha gambusi iliyokuwa ikipigwa. Hata walipokwisha kula binti mfalme na mwana wa mfalme wakaondoka wakaenda kupita chumba kidogo kilichopambwa dhahabu, wakatokea bustanini kulikokuwa na maua na miti ya matunda, iliyokuwa tofauti sana na ile ya Ajemi
 
Kwa haya aliyoyaona mwana wa mfalme, akasema, ‘Hapo kwanza nilifikiri kuwa milki ya Ajemi, siku zote yaweza kujisifu kuwa ina mahali kuzuri, na bustani zinazopendeza zaidi ya milki ingineyo yo yote katika dunia. Lakini sasa macho yangu yamefunuka, nami naanza kuona kuwa po pote palipo na mfalme mkuu hujengwa majumba yaliyo na thamani.’

Binti mfalme wa Bengali akajibu, ‘Mwana wa sultani, maadam silijui jumba la Mfalme wa Ajemi lilivyo, siwezi kulilinganisha na langu, wala sipendi kulikashifu jumba langu mwenyewe. Ila naweza kukusadikisha kuwa juumba langu si bora sana kushinda lile la mfalme baba yangu, kama utakavyoliona hapo utakapokwenda kumwamkia, ambayo natumai itakuwa karibu.’

Sasa binti mfalme akatumai kwamba katika kumkutanisha Feroz Shah na baba yake, lazima lile umbo na tabia nzuri za kijana mwanamume huyo zitamwingia moyoni mfalme, amwoze binti yake. Lakini jibu la mwana wa mfalme halikuwa sawa na vile alivyotumainia. Akasema, ‘Bibi, kwenda kumwamkia Mfalme wa Bengali nimekubali, si kwa ajili ya ugeni wangu tu, ila pia kwa heshima ninayomheshimu. Lakini nikitazama sana, naona hata wewe waona kama hivi nionavyo mimi, kuwa siwezi kabisa kujitokeza mbele ya mfalme mkuu bila kuwa na wafuasi kadiri ya cheo changu, maana kama si hivyo atanidhania ni mpitaji njia tu.’

Binti mfalme akajibu, ‘Ikiwa ni hayo tu, waweza kupata wafuasi wengi hapa kwa kiasi utakacho, maana wako wafanyaji biashara wengi wa Kiajemi. Na ikiwa ni fedha, hazina yangu i wazi kwako, chukua utakazo.’

Feroz Shah mwana wa mfalme akaona binti mfalne anazidi kumwogezea wema, na akawa hana kisingizio tena, lakini hamu ya kwao iliyokuwa ikiongezeka kila dakika haikumsahaulisha nia wake. Basi akajibu bila kusitasita, ‘Binti mfalme, sijui namna ya kukushukuru kwa fadlila zako unazonifanyia, na kama nisingeyakumbuka mashaka mfalme baba yangu anayoyapata kwa ajili yangu, ningekubali mara moja kujitokeza mbele ya Mfalme wa Bengali.

Lakini kama nisiporudi kwetu upesi, nitakuwa kama mtu nisiyestahili mapenzi yake. Maana wakati nifurahiwapo mimi pamoja na mabinti sultani wanaopendeza sana, najua kwamba yeye yumo katika lindi la huzuni, kwa kukata tamaa ya kuniona tena. Nina yakini kuwa utaifahamu hali yangu, kisha utaona kuwa nikiwa mbali naye zaidi ya dakika moja bila ya haja, nitahesabiwa kuwa sina shukrani tena, hata asi labda.’

Mwana wa mfalme akaendelea kusema, ‘Basi kwa sasa ni mwenye kufuata fikra zangu, mpaka hapo utakapopenda kunipa ruhusa yako nijitokeze mbele ya Mfalme wa Bengali, asinione kama mpitaji njia ye yote tu ila kama mwana wa mfalme, kisha nimsihi anioze. Na daima baba yangu ananiambia kwamba nikiisha kuoa ataniachilia huru kabisa, na mimi nikifika kwetu lazima nieleze ukarimu wako, na itataka uwe wangu niwe wako.’

Binti Mfalme wa Bengali akaona kuwa maneno aliyosema Feroz Shah ni kwli, lakini juu ya hivyo aliudhika sana kwa vile mwana Wa mfalme alivyotaka kuondoka upesi, maana aliogopa kuwa akiondoka ile nia aliyonayo juu yake itamwondokea. Mradı akafanya bidii zaidi ya kumzuia, na baada ya kumsadikishia kuwa yeye anakubali kuwa ana wasiwasi sana wa kuonana na baba yake, akamsihi akae siku moja au mbili zaidi pamoja naye.

Mwana wa mfalme hakuweza kumkatalia haja hii, na binti mfalme akawa ni kumletea kila namna ya mazungummzo, hata miezi miwili ikapita bila fahamu, kwa kwenda ngomani, na michezoni, na mawindoni. Hata siku moja mwana wa mfalme akasema hawezi kukaa sharti aende safari yake, mradi akamsihi binti mfalme asimzuie tena lakini akamwahidi kuwa ataruudi upesi. Kisha akasema, ‘Binti mfalme, huenda labda moyo wako utanidhania mimi kuwa sawa na wale wapenzi wa uwongo. Basi ikiwa ni hivyo, wakosa, kwani ningependa sana katika maisha yangu kuwa pamoja nawe, na kama singeogopa kukuudhi, ningependa sana tufuatane. Na makaribisho utakayokaribishwa katika jumba la Mtalme wa Ajemi, yatakuwa mema kama unavyostahili kwa fadhila zako, na anavyostahili Mfalme wa Bengal.’

Binti mfalme akanyamaza kwa kutokuwa na maneno ya kubishana na mwana wa mfalme wa Ajemi, lakini macho yake yalijaa huzuni akanena kuwa hakatai kuandamana naye katika safari yake. Ila shaka yake aliyokua nayo ni kuwa Feroz Shah hatoweza kumwendesha farasi, naye aliogopa wasije wakapatikana na masahibu kama yale ya kwanza. Lakini mwana wa mfalme aliweza kumtuliza hofu yake hata akawa hana wazo lingine ila kutengeneza safari yao kwa siri sana, kusudi asitokee mtu ye yote wa mle nyumbani kushuku.

Basi binti mfalme alipokwisha tengeneza kila kitu tayari akaondoka alfajiri maperma sana hali watu wa nyumba nzima wangalikua wamelala, akanyatia akapanda juu ya paa kulikokuwako na mwana wa mfalme akimngojea, pamoja na farasi wake aliyelekea upande wa Ajemi. Feroz Shah mwana wa mfalme akapanda kwanza kisha akampandisha na binti mfalme nyuma yake, hata alipokwisha kukaa vema na kumshika ukanda wake barabara ndipo mwana wa mfalme akaizungusha sukurubu na farasi akaanza kupaa upesi.

Farasi akapaa kwa mruko wake aliouzoea, na Feroz Shah mwana wa mfalme akamwelekeza barabara, hata kupata muda wa saa mbili unusu akaona jiji la Ajemi limejitandaza chini yake.

Sasa Feroz Shah akawa anajishauri, ashukie katika ule uwanja mkubwa wa mahali pale alipoondokea au katika uwanja wa jumba la mfalme, lakini mwisho akaona afadhali kushukia katika uwanja wa jumba moja la shamba lililo mbali kidogo na mji. Huko ndiko alikomwonyesha binti mfalme jamii ya vyumba vizuri, na kumsihi apumzike, na yeye mwenyewwe aende akamwambie baba yake kuwa wamefika, ili kusudi raia wapashwe habari wapate kujitengeneza tayari kumpokea binti mfalme kwa kadiri ya cheo chake. Ndipo kisha akaamuru farasi atandikwe, apate kutoka.

Humo njiani na mabarabarani, alipokewa kwa shangwe za watu waliokuwa wameondoa kabisa matumaini ya kumwona tena. Alipofika nyumbani kwa mfalme akamkuta mfalme amezungukwa na mawaziri wake, hali wote wamejivika msiba mkuu. Basi katika kule kubisha kwake tu, baba yake moyo ulimpasuka akawa kama mtu aliyezimia kwa kustaajabu na furaha ya kusikia sauti ya mwanawe. Hata alipopata fahamu kidogo, akamsihi mwanawe amhadithie mambo yote yaliyompata.

Kwa hivi mwana wa mfalme akaona amepata njia; naye akahadithia habari ya mambo yote aliyotendewa na Binti Mfalme wa Bengali, wala hakuogopa kusema kweli yake kuwa anampenda sana binti mfalme huyo. Mwana wa mfalme akamaliza kusema akinena, ‘Seyid yangu, nimempa ahadi ya ufalme kwamba hutokataa kuridhia ndoa yetu Nami nimemshawishi kuja nami huku juu ya farasi wa Mhindi. Hivi sasa nimemweka ndani ya jumba lako juu mojawapo la shamba, anangojea kwa wasiwasi kusadikishwa kuwa sikumwahidi bure.’

Alipokuwa akisema hivi mwana wa mfalme alikuwa karibu kutaka kujitupa miguuni pa mfalme, lakini baba yake akamzuia na kumkumbatia tena, akisema, ‘Mwanangu, nafurahi kwa kukuridhia harusi yako wewe na Binti Mfalme wa Bengali na nitafanya haraka niende nikamwamkie, na kumshukuru mimi mwenyewe kwa fadhila zake alizokufanyia. Kisha nije naye mwenyewe mpaka hapa, nipate kutengeneza matengenezo yote ya harusi ifanyike leo.

Basi kisha sultani akatoa amri kwamba mavazi ya msiba yaliyovaliwa na watu yavuliwe yatupwe, tena zipigwe ngoma mji mzima kwa matarumbeta na mabaragumu, na yule Mhindi pia afunguliwe, apelekwe mbele yake.

Kule kutamka tu yote yakatimizwa na yule Mhindi akapelekwa mbele yake, hali amezungukwa na askari. Sultani akamwambia, ‘Nilikufunga kusudi, ili kama mwanangu akipotea, maisha yako yalipize kisasi. Sasa mwanangu amerudi; basi chukua farasi wako, uende zako kabisa wala nisikuone tena.

Mhindi kuambiwa vile akaondoka haraka mbele ya mfalme, hata alipofika nje akamwuliza yule mtu aliyemfungua kifungoni mahali alikokuwako mwana wa mfalme kwa siku zile zote, na jambo gani alilokuwa akifanya huko. Akamwambia habari zote na jinsi Binti Mfalme wa Bengali alivyowekwa katika jumba la shamba kungojea idhini ya mfalme, na mara pale pale yule Mhindi kamjia nia ya kujilipiza kisasi kwa kitendo alichotendewa. Ndipo akaenda moja kwa moja mpaka kule kwenye jumba na kumwambia mlinda mlango aliyeachwa kule ya kuwa ametumwa na Sultani na mwana wa Sultani wa Ajemi, kumchukua binti sultani juu ya farasi wa uchawi, ampeleke nyumbani kwa mfalme.

Mlinda mlango alimjua sana yule Mhindi kwa sura, tena kwa hakika kuwa yakaribia miezi mitatu tangu afungwe na sultani, na katika kule kuona amefunguliwa, yule mtu akasadikisha kuwa asema kweli, wala hakufanya usiri kumpeleka mbele ya binti Mfalme wa Bengali. Alipokuwa amesimama kando yake, akamsikia akisema kuwa ametumwa na mwana wa mfalme, na yule bibi akaridhia kwa furaha kufanya kila aliloambiwa.

Mhindi akafurahi sana kwa kufanikiwa vile na mara akapanda farasi wake. Hata alipokwisha kumpandisha binti sultani nyuma yake akakizungusha kigingi na wakati ule ule kumbe alikua mwana wa mfalme kutoka nyumbani kwao Shirazi kwenda kule shamba amefuatana na sultani pamoja na washauri wake wote. Yule Mhindi kujua hivi, akamwelekeza farasi wake juu sawasawa na mji ili kwamba kisasi chake cha kufungwa bure kiwachome moyo watu.

Sultani wa Ajemi alipomwona farasi na waliompanda akasimama kwa hofu na kustaajabu, akaanza kuapa na kuapiza mapizo ambayo yule Mhindi aliyasikia barabara, naye alijijua kuwa yu salama kabisa wala haandamiki. Lakini uchungu na gadhabu alizokua nazo sultani hazikushinda zile alizokua nazo Feroz Shak mwenyewe, alipomwona mchumba wake akichukuliwa kwa kasi juu hewani. Basi wakati alipokuwa kushangaa hana la kusema kwa huzuni na majuto kwa kutomtunza vema mchumba wake, kutazama juu akawa hamwoni tena, amekwisha pita. Sasa atafanyaje! Alimfuata baba yake mpaka kule katika jumba la shamba, wala hakukata tamaa ya kumuona tena, maana ushujaa wake na mapenzi yake yalimzuia.

Basi katika kule kutokea kwa mwana wa sultani kule shamba, yule bawabu aliyajua makosa yake aliyokosa akajitupa kifudifudi miguuni pa bwana wake, akimsihi amsamehe. Mwana wa mfalme akamwambia, ‘Inuka kwani asili ya taabu hii si wewe, ila ni mimi mwenyewe. Sasa nenda kanitafutie vazi la ki walii lakini angalia! Usimwambie mtu kuwa ni langu.’

Mwendo wa hatua chache kutoka kwenye lile jumba, kulikua na nyumba za mawalii, na mkubwa wao alikua Sheikh, ambaye alikua Rafiki yake bawabu. Basi katika mazungumzo ya uwongo aliyoyazungumza bawabu ghafla, ikawa rahisi kwake kupata vazi la ki walii ambalo alimpelekea mwana wa mfalme nayeye alilivaa mara moja, badala ya nguo zake. Mradi akajibadilisha kama hivyo, na kukifutika kijaluba cha lulu na almasi alichokusudia kumpa zawadi binti sultani hata magharibi ilipoingia akatoka wala hajui aendako, mradi akaikaza nia yake na kusema kuwa hatarudi tena kwao bila kumpata binti sultani.
 
Na wakati huo yule Mhindi alikua amegeuza farasi wake kuelekea ndani ya mwitu, karibu na jiji la Kashmir. Akawa ana njaa sana na vile vile aliona kuwa yule binti sultani naye pia anataka chakula, ndipo akamteremsha farasi wake chini, na kumweka binti sultani kivulini katika kingo za kijito cha maji safi naye akaenda mjini kutafuta chakula.

Sasa yule binti sultani alipojiona yu pekee ikamjia nia ya kutaka kukimbia ajifiche. Walakini kwa vile ambavyo hakula kitu tangu atoke kwao Bengali, akajiona hana nguvu za kubahatisha kukimbia mradi akakaa kuvumilia.

Hata Mhindi aliporudi amejisheheneza vyakula vya kila namna binti sultani akaanza kula kwa pupa, hata aliposhiba barabara akawa haogopi tena kumjibu kwa ukali maneno yake ya ufidhuli. Ikamfanya Mhindi kumsukuma kwa uchungu ili kumtisha na vule bibi akaruka kusimama kando akipiga kelele kuita msaada: kwa bahati kilio chake kikasikilizana na kikosi cha wapandaji farasi, ambao walikwenda kuuliza yaliyotukia.

Na kumbe vile katika hawa wapandaji farasi mkubwa wao alikuwa ni Sultani wa Kashmiri anarudi kutoka kuwinda. Basi mara akamgeukia yule Mhindi kumwuliza yeye ni nani, na yule aliyenaye ni nani. Mhindi akajbu kwa jeuri akinena kuwa yule ni mkewe, wala haimhuzii mtu ye yote kumwingilia kati.

Huyu binti mfalme, ambaye kwa hakika hakujua cheo cha yule mwokozi wake, akayakanusha kabisa yale maneno ya Mhindi, akasema, ‘Bwana wangu, usimsadiki laghai huyu. Ni mchawi mbaya mno ambaye hivi leo amenitoa kwa mchumba wangu mwana wa Mfalme wa Ajemi, akanileta hapa juu ya farasi huyu wa uchawi. Angeendelea kusema zaidi, lakini kule kulia kwake kwa uchungu kulimzuia, na yule Sultani wa Kashmiri, kuutazama uzuri wake na umbo lake jinsi lilivyo akasadikisha maneno yake, ndipo akawaamuru wafuasi wake kukikata kichwa cha Mhindi, na mara kikakatwa.

Lakini ingawa binti mfalme aliokolewa katika hatari moja, alionekana kama aliyeangukia katika hatari ingine, maana yule Sultani aliamuru apandishwe juu ya farasi apelekwe nyumbani kwake, ambamo alimweka ndani ya chumba kizuri na kumchagulia watumishi wa kumtumikia na towashi mmoja wa kumlinda. Tena bila kumwachilia nafasi ya kumshukuru kwa wema wake wote aliomtendea, akamwambia alale kwa raha mustarehe, na masalibu yake yote yaliyompata atamhadithia kesho asubuhi.

Binti sultani akalala akitumainia kuwa anatakiwa kuhadithia habari zake tu, ili ahurumiwe na kurudishwa kwa mwana wa mfalme bila kukawia. Lakini kwa zile saa kidogo alizokaa kule alitanabahi makusudio ya sultani.

Sultani wa Kashmiri alipoondoka mbele yake akanuia kesho kumwoa binti mfalme. Hata kulipopambazuka ikapigwa mbiu mji mzima, kwa magoma kuvuma na matarumbeta na mabaragumu kulia, mradi kila aina ya ngoma ilipigwa ili kufurahisha moyo. Siku ile yule binti Sultani wa Bengall aliamka mapema kwa kelele na vishindo vilivyokuwako, lakini hakutanabahi kuwa ni za kumfanyia nderemo yeye mpaka alipofika sultani. Hata bibi alipokwisha kuvalia mavazi yake, sultani akamwuliza kaamka aje, kisha akamwambia kwamba huko kualika kwa matarumbeta anayoyasiki ni sehemu ya matengenezo ya harusi na kwa hivyo alimsihi ajitengeneze.

Taarifa hii ambayo hakuitarajia kamwe, ilimtisha mno binti sultani hata akaanguka chini akazimia.

Wale watumishi waliokuwa wakimtumikia wakamkimbilia kumwinua, na sultani mwenyewe akamfanyia bidii yote awezayo ili arudie fahamu, lakini wapi! Mwisho wake baada ya kitambo kikubwa, akili zake zikaanza kumrudia kidogo kidogo; ndipo akakusudia kujifanya ana wazimnu kuliko kuvunja ahadi yake na Feroz Shah mwana wa mfalme. Basi akaanza kusema maneno ya ovyo ovyo na kufanya vioja vya kila namna, na sultani hali amesimama kumwangalia kwa huzuni na kustaajabu. Na kwa kuwa ule ugonjwa uliomshika haukuonyesha dalili ya kupungua, sultani akamwachia watumishi wake na kuwaagiza wamtunze sana. Kutwa ikawa namna hiyo, na ugonjwa ukaonekana kuzidi, na usiku ndiyo kabisa!

Siku nyingi zikapita katika hali ile, hata mwisho Sultani wa Kashmiri akawaita waganga wake wote ili washauriane juu ya ugonjwa wa binti sultani. Nao wakajību kuwa wazimu kuna namna nyingi wala hawawezi kuutolea shauri lo lote bila kumwona binti sultani mwemyewe, ndipo sultani alipotoa amri kwamba wale waganga wapelekwe chumbani kwake mmoja mmoja, kila mtu kwa daraja yake.

Yule binti sultani aliyajua mbele mambo haya kuwa yatatokea, naye aliona kuwa akiwaachilia waganga kumgusa basi hata yule ambaye ni mjinga sana atamambua kuwa ni mzima kamili, basi kwa hivi akajizidisha wazimu wake, ikawa kila amkaribiaye hufanya ukali na vishindo vikubwa, wala hapana hata mmoja aliyethubutu kumgusa. Lla waganga wachache waliojifanya hodari kupita wengine, waliosema kwamba wao wanaweza kutambua watu wagonjwa kwa kuwaona tu ndio walioandika kuwa kuwa sehemu fulani za mwili wake hazina dhara.

Sultani wa Kashmiri alipoona waganga wake wote hawakuweza kumpoza binti sultani, akawaita wale wa mjini ambao nao pi hawakuweza kufanya lo lote. Halafu akajaribu waganga wengi wenye sifa wanaokaa katika miji mingine mikubwa, lakini wakaona kuwa kazi ile imepita maarifa yao. Mwisho akatuma wajumbe katika milki zingne zilizo karibu, wenye kuchukua hati ya sultani iliyoandikwa habari zote za ugonjwa wa binti sultani, na yenye kuahidi kulipa gharana za mganga ye yote atakaye kwenda kumwangalia, na kuwa yule atakayempoza atapewa bakshishi kubwa. Basi kwa tangazo hili ikawa walimu wengi wakubwa wakubwa kukutanikia Kashmiri, lakini nao vile vile hawakufaulu kitu kama wale wengine, maana kule kupona hakukufungamana na wao, wala na ubingwa wao, ila na binti sultani mwenyewe tu.

Wakati huu ikawa yule Feroz Shah mwana wa mfalme anazungukazunguka kwa huzuni bila matumaini kutoka mji huu hata mji huu, mwisho akafika mji mkubwa wa Bara Hindi, akasikia watu wakisema sema sana habari za Binti Sultani wa Bengali aliyefanya wazimu kwa siku ile ile aliyotaka kuolewa na Sultani wa Kashmiri. Habari hizi zilimfanya kushika njia kwenda Kashmiri kuuliza habari zaidi, na alipofika katika mgahawa wa kwanza wa mle mjini akapata habari safi, naye alipojua kuwa mwisho amempata binti sultani aliyempotea kitambo, akakaa kufanya shauri ya kwenda kumwokoa.

Jambo la kwanza alilofanya alitafuta joho la kiganga akavaa, na kuvua ile sharafa ya ndevu ndefu alizoziachilia kukua wakati alipokuwa akisafiri akaona kuwa kwa ile hali yake aweza kufikiriwa kuwa ni mganga bila shaka. Mradi hakukawia tena ila alifululiza moja kwa moja mpaka katika jumba la mfalme, hata alipofika akaomba kuonana na bawabu mkuu. Basi kuona kuwa anaweza kumponya binti sultani hali wengine wengi hawakuweza, akasema, ‘Nina siri ya dawa inayopoza kweli, wala hiyo haikosei kupoza kabisa.

Yule bawabu aliposikia hivi akamhakikishia kuwa amekaribishwa kwa wema, na sultani naye atampokea kwa sherehe; na hasa aendapo akafaulu kumpoza kweli, atapata bakshishi ya fahari.

Basi huyu mwana wa mfalme wa Ajemi aliyejigeuza mganga alichukuliwa kupelekwa mbele ya mfalme, wala yule mfalme hakuzungumza naye sana maana ilikuwa yule binti sultani akisha nwona mganga tu, hufanya matata na ghadhabu. Ikawa sasa yule mwana wa mfalme kupelekwa juu darini kulikokuwa sultani, kusudi apate kumchungulia bila ya yeye mwenyewe yule mwana mfalme kupelekwa juu darini kulikokuwa na tundu pana lililo wazi lililokaa sawasawa na chumba cha binti sultani, kusudi apate kumchungulia bila yay eye mwenyewe kuonekana.

Mwana wa mfalme akachungulia ndani akamwona binti sultani amejinyosha kitandani analia, huku akiimba polepole akiomboleza kwa hali yake ya msiba iliyomwondolea kupendwa kwa dhati kwa milele labda. Kusikia hivi, moyo wa kijana mwanamume ukamwemda mbio, maana hakuhitajia tena ushindi mwingine ila aliona kuwa wazimu wake ni wa kujitia mwenyewe makukusudi, na kumpenda yeye ndiko kulikomfanya kutumia hila hivo. Basi mwana wa mfalme akaondoka taratibu pale mahali alipofichwa akarudi kwa sultani, na kumwambia, ‘Kwa dalili kadha wa kadha nilizoziona, nina yakini kuwa ugonjwa wa binti sultani hauponeki ila sharti nimwone niseme naye peke yake.’ Sultani akakubali, na pale pale akaamrisha kuwa yule mganga apelekwe chumbani kwa binti sultani. Yule bibi alipomwona amevaa joho lake la kiganga, akamrukia kwa ghadhabu na matusi. Lakini mwana wa mtalme hakuona neno, ila alimjongelea karibu kusudi yale maneno yake atakayomwambia yasisikiwe na mtu mwingine ila yeye tu, ndipo akasema kwa kunong’ona, ‘Niangalie binti sultani, nawe utanitambua kuwa si mganga, ila ni mwana wa Mtalme wa Ajemi, aliyekuja kukufungua.’

Kwa mnong’ono ule, mara ghafla Binti Mfalme wa Bengali akatulia, na alama za furaha zilienea usoni mwake, kama vile itukiavyo wakati tunapokitaka kitu sana, na mwisho wake kutujia kwa ghafla. Na hivyo ndiyvo ilivyokuwa kwake.

Binti mfalme akawa hasemi kapigwa na bumbuwazi, lakini kwa kule kunyamaza kwake, Feroz Shah mwana wa nmfalme akapata nafasi ya kumweleza yote yalivyokuwa. Hata alipokwisha kumweleza yote, akamsihi binti sultani naye amwambie jinsi alivyofika kule, ili apate kubuni shauri lililo jema la kumwokoa na udhalimu wa sultani.

Na hivyo ilimhitajia binti sultani amweleze habari kidogo ili apate kufahamikiwa na mambo yote, na jinsi alivyolazimika kujifanya mwanamke mwenye wazimu kusudi aepukane na kuolewa na sultani, ambaye hakuwa na heshima ya kutosha. Yule bibi akaongeza kusema kwamba hata kama ingalikuwa sharti kuolewa, angalihiari kufa kuliko kuvunja ahadi yake na Feroz Shah, mwana wa mfalme, aliyempenda.

Halafu mwana wa mfalme akamwuliza yule bibi kama alijua jambo gani lilompata yule faras wa uchawi baada va kifo cha Mhindi. Binti Sultani akajibu kuwa hakusikia habari yo yote yake; walaa naye hadhani kuwa farasi alisahauliwa na sultani, maana baada ya yote alimzungumzia manufaa yake.

Kwa hivi mwana wa mfalme akaridhika, ndipo wakafanya shauri pamoja kutafuta njia itakayowawezesha kutoroka na kurudi Ajemi na jambo la kwanza alilofanya yule bibi, alivalia vizuri, na asubuhi yake sultani alipokwenda kumwangalia akampokea kwa furaha. Sultani alipoona kuwa uganga umefaa, akafurahi na akamsifu mganga na kumtukuza. Hata siku ya pili yake binti sultani akamwendea sultani kumshawashi kuzinguliwa kwake kusikawilishwe sana. Sultani alijaa furaha kuona afya yake inamrudia tena, naye akamwonya azidi kushika miko ya mganga na kumtegemea kabisa bila wasiwasi. Baada ya haya binti sultani akaondoka.

Wakati ule ule mwana wa Mfalme wa Ajemi akatoka chumbani, akaenda mbele ya mfalme kuomba kwa unyenyekevu kama ataruhusiwa kuuliza namna ya Binti Mfalme wa Bengali alivyoflka kule Kashmiri ambako ni mbali muno na ufalme wa baba yake, na jinsi ilivyokuwa hata akapata kukaa vile pekee. Sultani akaona swali hili kuwa la desturi, naye akaanza kumwambia habari ile ile aliyoambiwa na Binti Mfalme wa Bengali, zaidi ya hivyo aliongeza kumwambia kuwa hata huyo farasi wa uchawi aliamrishwa awekwe katika hazina yake kama tunu, ingawa hakujua namna ya kumtumia.

Mganga akajibu, Seyid yangu, Fahari Yako imenipa dalili nilizozitaka kwa kumpozea binti sultani kabisa. Wakati wa safarı yake kuja hapa juu ya farasi wa uchawi, naona sceemu ya uchawi wake lazima ulinuiziwa na nafsi yake, nao huwezekana kuchomolewa kwa mafusho (mavumba) ya siri niliyonayo. Basi kama fahari yako itakubali kuwafanyia raia zako na jamii ya masheikh wako mchezo mmojawapo wa michezo ya ajabu sana ambayo hawajapata kuiona, agiza huyo farasi aletwe hapa katika uwanja mkubwa wa jumba lako, na hayo yatakayobakia niachie mimi. Nami naahidi kwamba muda wa dakika chache, na jamii ya watu wataokusanyika utamwona binti sultani ana afya ya moyo na mwili kuliko hivyo alivyokuwa katika uzima wake. Na katika kuufanya mchezo huo uwe wa kustaajabisha sana, ningependa ajipambe sana, na kichwani avalie taji la lulu na alması.

Sultani akakubali yote aliyosema mganga, na asubuhi yake akataka farasi wa uchawi atolewe katika hazina, aletwe katika uwanja mkubwa wa jumba lake.

Ilipoanza kutangazwa mjini kuwa kutafanyika jambo kuu la ajabu umati wa watu ukaanza kukusanyika na askari waliitwa kuja kuzuia fujo, na kufanya nafasi kwa farasi wa uchawi.

Haya yote yalipokua tayari sultani atatoka, akakaa mbele katika kiti chake cha enzi huku amezungukwa na masheikh na majemadari wake. Walipokuwa wote wamekaa tayari, binti Mfalme wa Bengali akaonekana akitoka kwenye jumba amefuatana na watumishi wake aliopewa na sultani, akienda taratibu mpaka akamkaribia farasi wa uchawi, na wale watumishi wakasaidiana kumpandisha juu ya farasi. Mara pale akajiona amekalia tandiko, na miguu yake i katika vikuku vya kupandia farasi na hatamu mikononi mwake. Yule mganga naye akatwaa vyetezo vikubwa vikubwa vilivyojaa makaa yanayowaka akaviweka chini kumzunguka farasi, na katika kila chetezo akatia mafusho ya kila aina va manukato mazuri. Kisha akafunga mikono kifuani na macho yake akiyainanisha, na kumzunguka farasi mara tatu huku akinuizia kwa kitambo maneno kadha wa kadha. Mara moshi mwingi sana ulipanda juu kutoka vyetezomi, ukamziba farasi na binti sultani na hivi ndivyo alivyokuwa akingojea yule mwana wa mfalme. Akamrukia farasi na kukaa nyuma ya yule bibi, kisha akainamia mbele kuzungusha kigingi, na mara pale pale farasi akaanza kupaa.

Sasa akasema kwa sauti kubwa ili kusudi maneno yake yapate kusikiwa na wote waliokuwapo: EWE SULTANI WA KASHMIRI, UKITAKA KUOA MABINTI SULTANI WALIOTAKA HIFADHI YAKO, KWANZA JIFUNZE KUTAFUTA IDHINI YAO.

Hivi ndivyo Mwana wa Mfalme wa Ajemi alivyomwokoa Binti Mfalme wa Bengali akarudi naye Ajemi. Safari hii walishukia mbele ya jumba la mfalme mwenyewe. Lakini harusi ilikawilishwa sana ili kusudi wazidi kutengeneza ada za harusi, ipate kuwa ya fahari zaidi. Hata sherehe na karamu zote zilipokwisha, akapelekwa mjumbe kwa Mfalme wa Bengali kumwambia yote yaliyopita na kumtaka idhini yake kwa harusi, naye akaitoa kwa moyo wake.
 
KISA CHA NDUGU WAWILI WANAWAKE WALIOMWONEA KIJICHO DADA YAO MDOGO



Hapo kale paliondokea sultani mmoja aliyetawala nchi ya Ajemi, jina lake Kosrushah, ambaye tangu utoto wake alikuwa akipenda sana kujigeuza mavazi ili apate kupeleleza mambo yapitayo katika mji, naye alikuwa akifuatana na mmoja wa mawaziri wake aliyekuwa akijigeuza kama yeye. Hata siku moja usiku akatoka na waziri wake hali wote wamevalia nguo za kiraia wakipita katika njia za siri.

Wakaenda mpaka wakatokea katika barabara moja kulikokuwa na nyumba ya pekee. Walipofika hapo sultani akasikia sauti za wanawake wakizungumza. Moyo wake usimpe kupita na kushika nja yake ikawa anachungulia ndani katika ufa wa mlango, akaona ndugu watatu wamekaa katika kitanda kilichokuwa ukumbini wakizungumza vizuri kwa heshima. Na katika yale maneno machache aliyoyasikia akafahamu kwamba kila mmoja alikuwa akieleza namna ya mume anayemtaka amwoe.

Mkubwa wao akasema, ‘Ama kwa nafsi yangu mimi, sitaki mume ila mwokaji mikate wa mfalme ndiye nimtakaye kuwa mume wangu, akifikiri kuwa ataweza kula sana kama apendavyo, hasa mkate ule ule mtamu anaookewa mfalme tu! Haya basi natusikie utakavyo wewe.’

Wa pili akasema, ‘Mimi, nitakuwa radhi kabisa kama nikimpata mpishi mkubwa wa mfalme kuwa mume wangu. Ukoje utamu wa rojorojo ya viazi kwa nyama nitakayokula! Na maadam nimesikia kwamba mikate ya mfalme huliwa nyumba nzima, nitaipata mingi niiuze nipate faida. Je! Dada, waonaje fikira yangu, si bora kuliko yako?

Sasa ikawa zamu ya yule dada yao mdogo ambaye alikuwa mzuri kuliko wale wawili, na juu ya hivyo alikuwa na akili, akasema, ‘Ikiwa twajichagulia waume, mimi sitaki mume ila sultani mwenyewe ndiye atakayenifaa.’
 
Sultani akapendezewa sana kwa mazungumzo haya alayoyasikia, naye akakusudia kumjalia kila mtu kwa kadiri alivyotaka, ndipo akamgeukia waziri wake mkuu akamwambia aitunze sana nyumba ile, na asubuhi yake aende akawalete wanawake wale mbele yake.

Kulipokucha waziri akaenda kufanya kama alivyoagizwa na kwa jinsi alivyowahimiza haraka wamfuate nyumbani kwa mfalme: hata ile nafasi ya kubadili nguo zao walipata kwa shida.

Walipofika wakapelekwa mmoja mmoja mbele ya sultani hata walipokwisha kumwinamia, mfalme akawauliza ghafla, ‘Je, mwakumbuka mliyoyataka jana usiku, wakati mlipokuwa mkijifurahisha? Msiogope, ila niambieni kweli.’

Maneno haya ambayo hawakuyatarajia kuulizwa yaliwatia wasiwasi sana na kutahayari, na zile haya alizokuwa nazo mdogo wao hazikuacha kupenya moyoni mwa sultani. Wote watatu wakanyamaza kimya, na sultani akazidi kuwahimiza akiwaambia ‘Msiogope, kwani sikusudi kuwaadhibu hata kidogo. Basi sasa sikilizeni niwaambie, maana najua kupenda kwa kila mmoia wenu jinsi alivyojitamania. Akamgeukia mdogo wao akamwambia, ‘Wewe, uliyependa mimi niwe mumeo, haja yako itaridhiwa hivi leo.’ Kisha akawageukia na wale wengine wawili akawaambia, ‘Na ninyi, mtaolewa hii hii leo pia, mmoja ataolewa na mwokaji mikate wangu na wa pili ataolewa na mpishi wangu mkuu.’

Sultani alipokwisha kusema hivi, wale ndugu watatu wakajitupa miguuni pake, na mdogo wao akasema kwa kubabaika, ‘Aa! Seyid yangu, umeyajua maneno yangu ya kipumbavu, nakuomba sadiki mana yalikuwa ya ubishi tu. Na hiyo heshima ukusudiayo kunifanyia si fani yangu, naomba unisamehe.’ Na wale dada zake nao pia walijaribu kumtaka radhi, 1akini wapi sultani hakuwasikiliza.

Akasema, ‘La, la, maadam moyo wangu umependa, haja zenu zitatimizwa’

Mradi harusi tatu zikafanywa siku ile ile, lakini kwa tofauti kubwa Maana ile ya mdogo wao ilifana mno kama ilivyokuwa desturi ya harusi ya Mfalme wa Ajemi, na furaha zilizofanyika katika harusi ya mwokaji mikate wa mfalme na ya mpishi wake mkuu, zilikuwa za kadiri ya kutosha hali zao.

Na ijapokuwa hii ndiyo kawaida ya hali za watu, wale dada zake hawakupendezewa kabisa, wakawa na wivu ambao mwisho wake uliletea watu wengi taabu na mashaka. Baada ya kupita siku nyingi, ikawa siku moja wale dada zake wawili walikutana ziwani siku walikokwenda kuoga, wakapata nafasi kubwa ya kusemezana wala hawakujaribu kuigeuza nia waliyokuwa nayo.
 
Mmoja akamwambia mwenziwe, ‘Waweza kufahamu ni uzuri gani alionao yule kipaka sultani akawa hajijui hajitambui?’

Mke wa yule mpishi mkuu akajibu, ‘Labda ameonekana kijana zaidi yetu sisi. Ingekuwa vizuri zaidi kama wewe ungekua mke wa sultani.’

Mkubwa akajibu, ‘Aa, mimi sisemi kitu, na hata kama sultani angekuchagua wewe yote yangekuwa mema pia; lakini ah ama yanihuzunisha sana kwa sultani kuchagua kidude baa kama kile walakini haidhuru, na kwa kadiri itakavyokuwa lazima nimtie adabu, nami nakuomba unisaidie katika shauri hii, tena uniambie jambo gani unalofikiri laweza kumtia aibu.’

Kwa kutaka kuitimiza nia yao mbaya, hawa ndugu wawili walikutana mara kwa mara kuzungumza juu ya mashauri yao ingawa wote walijifanya wema mbele ya ndugu yao mke wa sultani, ambaye naye kwa upande wake, hakubadilika katika kuwatendea mema. Baada ya kupita siku nyingi bila kutokea jambo lo lote la kuwaonyesha hawa madada wawili kuwa shauri yao itafanikiwa, mwisho wake tazamio la kuzaliwa mtoto likawapa nafasi waliyokuwa wakiitumainia. Sultani alikuwa kawapa ruhusa ya kukaa nyumbani mwake muda wa juma mbili tatu, wamtunze ndugu yao mchana na usiku.

Mwishowe mtoto mwanamume, mzuri, ang’aa kama jua, akazaliwa. Nao mara wakakilaza katika kitanda chake kidogo na kukichukua kwenye mto uliochimbwa kupitia chini ya jumba la sultani, na hapo mtoni ndipo walipokiachilia kitoto kichukuliwe na maji.

Kisha wakarudi kumwambia mfalme kuwa mkewe badala ya kuzaa mtoto amezaa mbwa. Sultani kusikia hivi akafanya hasira na uchungu sana, hata yasemwa kwamba ilikuwa ni vigumu kwa waziri mkuu kuweza kumwombea sultana katika ghadhabu zake.

Na wakati ule kile kitanda kilikuwa kinaelea kwa amani kikifuata mto mpaka nje ya mipaka ya mashamba ya mfalme, mara kwa ghafla kikaonekana na msimamizi ambaye ni mmoja wa watu wema anayehishimiwa sana katika ufalme.

Akamwambia nokoa aliyekuwa akitumika karibu yake. ‘Nenda kaniopolee kitanda kile.’ Nokoa akaenda kufanya kama alivyoambiwa na mara ile ile akamletea kitanda mikononi mwake.

Yule msimamizi wa serikali akastaajabu sana kuona alichokidhania kuwa kitupu kumbe kina kitoto kichanga kizuri, vile veye mwenyewe hakupata kuzaa mtoto tangu kuoa kwake, akakusudia kukichukua kitoto akilee kama chake mwenyewe. Basi akamwambia yule mtu kukichukua kitanda na mtoto pamoja, afuatane naye mpaka nyumbani kwake.

Kufika tu akaita, Mke wangu! Japokuwa Mungu katunyima watoto, lakini huyu hapa mmoja aliyeletwa kuwa badili yao, Basi fanya ukamwite yaya, na mimi nitafanya yote niwezayo ili ijulikane waziwazi kuwa ni mwanangu.’

Mkewe akakipokea kitoto kwa furaha, na ijapokuwa yule msimamizi alijua sana kule kinakotoka, lakini aliona kuwa si kazi yake kutafutatafuta na kuulizauliza mambo ya siri.

Mwaka wa pili mtoto mwingine wa mfalme akazaliwa, na huyu naye akapotezwa vile vile, lakini ikawa kwa bahati siku hiyo yule mwenye bustani alikuwa akitembeatembea kando ya ule mto, akakiona na kukichukua kwake kama kwanza.

Safari hii ya pili sultani akakasirika sana kuliko mara ya kwanza, lakini kioja kile kile kilipotendeka tena mwaka wa tatu, hakuweza kustahimili tena akaamuru kwamba mkewe auawe, na hivyo ikawa furaha kuu kwa wale nduguze waliomwonea kijicho. Lakini yule bibi masikini alipendwa sana na jamii ya watu wa baraza ya mfalme, na ile hofu ya kusema kuwa akijiingiza katika mambo hayo na yeye pia atakuwamo katika ushirika wa mauti yake haikuweza kumzuia waziri mkuu na masheikh wakubwa wakubwa kujitupa miguuni pa mfalme wakimsihi asipendelee kumtia adhabu ya ukatili kwa jambo ambalo si amri yake.

Waziri mkuu akazidi kusihi, ‘Mwachilie aishi, ila katika hizo siku za maisha yake yaliyosalia, mfukuze atoke mbele yako. Kwani hilo nalo latosha kuwa adhabu yake.’

Hasira za sultani zilipokwisha poa moto, akasema, ‘Maadam ninyi mmelisimamia sana jambo hili, namwachilia aishi. Lakini maisha yake ataomba kufa asipate. Haya! Muundieni sanduku lenye kilango cha kutokezea kichwa na shingo yake mumtie, mwende mkamweke katika lango la msikiti mkuu akakae huko siku zote, hali amevaa magunia, ili kila Mwislamu apitaye kuingia msikitini amtemee mate usoni. Na ye yote akataaye kufanya hivyo ataadhibiwa adhabu hiyo hiyo. Na wewe waziri utakuwa ukiangalia kama amri yangu yashikwa.

Waziri mkuu akaona kusema zaidi ni kazi bure, na wale nduguze walifurahiwa sana ikawa wanasimama kuangalia sanduku ikiundwa, na huku wakisikiliza masimango ya watu juu ya bibi sultani asiye na mtu wa kumwombea asiwekwe ndani ya sanduku. Lakini yule bibi masikini heshima yake na upole wake ulimsaidia kwa watu wala haikupata muda mwingi mara akasikitikiwa na watu wote waliokusanyika ambao walikuwa wema kwake.

Sasa na tuangalie majaliwa ya mtoto wa tatu; safari hii alizaliwa mwanamke, ikawa naye kutupwa vile vile na kuokotwa na nduguze na msimamizi yule yule wa bustani, naye pamoja na mkewe wakawalea vizuri sana na kuwahurumia wote watatu.

Basi watoto walipokuwa wakubwa uzuri wao wa umbo na sura ukazidi kusifiwa, na tabia zao zikawa za upole na heshima. Baba yao wa kuwalea akawapa majina wale watoto wanaume wa sultani, mmoja akaitwa Bahman na wa pili Perviz, haya yalikuwa ni majina ya wafalme wawili wa kale wa Kiajemi, na yule binti sultani akaitwa Parizade, maana yake mtoto wa jini.

Yule msimamizi aliwatunza sana katika kuwalea kwao kama vile wanavyostahili kwa cheo chao hasa, na akatafuta mwalimu wa kuwafundisha wale watoto wanaume kusoma na kuandika. Lakini na yule dada yao hakupenda kuachwa nyuma, ikawa anaonyesha dalili ya kutaka sana kujitunza pamoja na nduguze ndipo yule msimamizi akamridhia kusoma pamoja nao, wala haikupata siku nyingi kabla hajajua kusoma na kuandika kama vile walivyojua nduguze.

Mradi mafunzo yao yote yakawa mamoja. Wakapata na walimu hodari wa ramani, wa mashairi, wa hadithi na kadhalika, hata elimu zingine zinazosomwa na wachache, na kila jambo lilikuwa rahisi kwao, hata wale walimu wao walistaajabu sana kuona maendeleo yao.

Binti sultani alikuwa na bidii sana kutaka kujua kupiga kinanda, na mwisho wake aliweza kuimba na kupiga kila namna ya vinanda, na kadhalika alijua kupanda farasi na kumtimua sawasawa kama nduguze, tena alikuwa na shabaha ya kupiga mshale na kutupa mkuki kwa ustadi kama wao, na pengine kuwashinda.

Hata walipokwisha hitimu mafundisho yao, yule msimamizi akaona kuwa haipendezi kwa watoto wake wa kalea kuwa katika zizi jembamba la nyumba ya shamba kama ile aliyokuwa akikaa, katika mradi akaona ni vizuri anunue nyumba moja nje yam ji, iliyozungukwa na shamba la miti mingi mikubwa. Ndani ya shamba hilo, akatia kila aina ya nyama mwitu, ili kusudi watoto wake wawe wakiwinda maridhawa kama wapendavyo.

Basi kila kitu kilipokuwa tayari, yule msimamizi akaenda akajitupa miguuni pa sultani, na baada ya kumhesabia umri wake na siku nyingi alizotumika, akamwomba ruhusa ya kuacha kazi yake sultani akakubali na kumwambia maneno machache yaliyo mazuri kisha akamwuliza ni zawadi gani atakayoipenda kwa utumishi wake wa waminifu. Lakini yule msimamizi akasema kuwa hataki kitu ila anataka yeye sultani azidi kumkubalia ombi lake la kuachishwa kazi, kisha akajiangusha tena kifudifudi miguuni pa sultani, ndipo akatoka akaenda zake.

Baada ya kupita miezi mitano au sita katika furaha na anasa zote alizokuwa nazo kule nje ya mji, akashikwa na mauti ya ghafla hata kule kuidhihirisha siri ya kuzaliwa kwa wale wanawe wa kulea hakuwahi, kwani na yule mkewe pia alikuwa amekufa zamani. Mradi sasa ikawa yaonekana kuwa wale akina bin sultani na binti sultani hawatajua asili ya kuzaliwa kwao.

Ama msiba wao ulikuwa mzito mno kwa kifo cha baba yao, mradi walikaa kwa amani katika nyumba yao mpya bila kutamani kuitok.

Hata siku moja, kama ilivyokuwa desturi yao, wale mabinti sultani wakatoka kwenda kuwinda, lakini dada yao alibakia chumbani mwake pekee. Huku nyuma akatokea wali mzee wa Kislamu na kubisha mlango kutaka ruhusa ya kuingia ndani, maana saa ya kusali ilikuwa imefika. Binti sultani akamwamrisha mtumishi wake kumpeleka yule mwanamke mzee katika chumba cha faragha cha kusalia, na atakapokwisha kusali amchukue na kumwonyesha nyumba na kumtembeza bustanini, halafu ampeleke mbele yake.

Japokuwa yule bi kikongwe alikuwa mcha Mungu sana, lakimi alipendezewa mno na vitu vilivyomzunguka, ambavyo vilimstaajabisha, hata alipokwisha kutazama vyote, watumishi wakampeleka mbele ya binti sultani, aliyekuwa amekaa katika chumba ambacho kilipita vingine vyote kwa ubora.

Binti sultani akanena, ‘Bibi yangu mwema, njoo ukae hapa naribu nami, kwani leo nimefurahi kwa kupata nafasi ya kusema na mtu mcha Mungu kwa dakika chache.’ Yule bibi akajaribu kukataa kufanyiwa heshima nyingi kama vile, lakini binti sultani hakumridhia, ikawa ni kumshurutisha akisema kuwa ni lazima mgeni wake akae mahali pazuri, na kwa vile alivyomwona kuwa amechoka sana akamwagizia chakula ale aburudike.

Wakati bi kikongwe alipokuwa akila, binti sultani akamwuliza maswali mengi ya namna anavyoishi na jitihadi aliyoifanya hata akayazoea maisha yake, kisha akamwuliza na namna alivyoiona ile nyumba wakati alipokuwa akitembezwa kuonyeshwa.

Yule bi kikongwe akajibu. ‘Bi mkubwa, ama kwa hakika ni vigumu kwa mtu kuweza kuitia kasoro yo yote. Kwa uzuri ni nzuri tena yapendeza na imekamilika. Lakini maadam waniuliza sina budi nikuambie kuwa imepungua vitu vitatu kuifanya ikamilike zaidi.’

Binti sultani akauliza, ‘Ni vitu gani hivyo? Niambie tu, nami nitavipata.’

Bi kikongwe akajibu, ‘Bi mkubwa, vitu hivyo vitatu, kwanza Ndege Anenaye, ambaye sauti yake huwavuta karibu ndenge wengine wote wanaoimba, waje kuitikia. Pili ni Mti Uimbao kwani kila palipo na jani ni wimbo usio nyamazika kamwe, Tatu ni Maji ya Dhahabu, ambayo haja kubwa ni kutiwa bakulini tone moja tu, nalo litachipuza chemchemu ya maji yasiyokauka.’

Bi sultani akamwambia, ‘Nikushukuru namna gani kwa kuniambia mali kama hiyo! Lakini nakuomba kwa hisani yako, uzidi kuniambia na mahali pa kwenda kuyapata.’

Yule msafiri akajibu, ‘Bi mkubwa, kama nikikataa kukuambia nitakuwa kama mtu ninayekulipa uovu kwa fadhila zako. Hivyo vitu vitatu nilivyosema, vyote vyapatikana mahali pamoja katika mipaka ya ufalme huu huu, kuelekea Bara Hindi. Na huyo mtumishi wako utakayempeleka afuate njia hii hii ipitayo karibu na nyumba yako, muda wa siku ishirini, na mwisho wa siku hizo endapo akikutana na mtu ye yote njiani amwulize mahali kuliko na Ndege Anenaye, na Mti Uimbao, na Maji ya Dhahabu.’ Kuisha kasema haya akaondoka na kumuaga binti sultani, akaenda zake.

Kuondoka kwake kulikuwa kwa ghaffa sana hata Parizade binti sultani hakummwona alikokwenda, tena ilikuwa ni shida sana kuweza kutafutwa akaonekana. Mradi sasa ikawa yule binti sultani kuzidi kufikiri yale maneno, na pis furaha yake ingelikuwaje kupata tunu kama zile! Hata ndugu zake waliporudi kutoka kuwinda, Bahman akamwuliza, ‘Una nini dada yangu? Mbona una huzuni sana? Waumwa au liko jambo lililotokea?’

Parizade akanyamaza asijibu upesi, lakini mwisho akainua macho na kujibu, ‘Sina neno.’

Bahman akashikilia kusema, ‘Lazima liko neno, kwani hata alai yako imebadilika sana kwa muda huu mfupi tuliokuwa hatuko. Basi n naomba usitufiche, au wataka kuwa kule kutegemeana tulikonako siku zote sasa kumekwisha.’

Binti sultani akasema, ‘Niliposema kuwa sina neno, maana yake linalokuhusuni ninyi, ingawa mimi mwenyewe naona kuwa ni lazima sana kwangu. Maana ni hivi: kuwa ninyi siku zote mlidhani kuwa nyumba hii aliyotujengea baba yetu imekamilika kila kitu, lakini leo nimeambiwa kuwa bado vimepungua vitu vitatu. Vitu hivyo ni Ndege Anenaye, na Mti Uimbao, na Maji ya Dhahabu.’ Baada ya kueleza aina ya kila kimoja peke yake, ya binti sultani akaendelea kusema, ‘Walii ndiye aliyeniambia haya yote, na huko vinakopatikana. Na pengine ninyi, mtaona kuwa uzuri wa nyumba hii watosha kama hivi ulivyo, nasi tutaweza kukaa kwa raha pasipo kuwa navyo; lakini kwa hayo siwezi kuwakubalia, maana nafsi yangu haitakuwa radhı mpaka nivipate. Basi naomba mnishauri, nani wa kumtuma kazi hii.’

Bahman mwana wa mfalme akajibu, ‘Dada yangu mpenzi, ikiwa sisi hatupendezewi na mambo hayo, nawe kumbe mwenyewe wapenda basi vema na sisi pia tutayatia moyoni pamoja nawe. Na maadam mimi ndiye mkubwa nitakuwa wa kwanza kujaribu kuvipata vitu hivyo, iwapo utanielekeza njia ya kwendea na namna ya kufanya.’

Kwanza Perviz nduguye mdogo akamkataza asiende kwa kuwa yeye ndiye mkubwa wa nyumba, wala hakupendelea kwamba nduguye aachiliwe kwenda kujitia hatarini; lakini Bahman hakukubali, na muda ule ule akaanza kutengeneza safari yake.
 
Asubuhi yake Bahman akaamka alfajiri sana, na baada ya kuwaaga nduguze, akapanda farasi wake. Lakini alipokuwa karibu kutaka kumpiga mjeledi wake, akazuilika kwa kilio cha binti sultani dada yake, akinena, ‘Aa! Ndugu yangu, huenda pangine usirudi tena kwani hapana ajuaye ajali gani itakayokupata. Basi tatadiali, nakuomba usiennde, nami nitakuwa radhi mara elfu kumkosa huyo Ndege Anenaye, na Mti Uimbao, na Maji ya Dhahabu, kuliko kukuacha wewe uingie hatarini.’

Mwana wa mfalme akajibu, Dada yangu mpenzi, ajali huwapata watu wasio na bahati, nami natumaini kwamba mimi si mmoja wao. Lakini kwa vile ambavyo kila jambo si kweli, nakuusia utahadhari sana. Twaa kisu hiki, akampa kimoja kilichokuwa ndani ya ala zilizoko kwenye ukanda wake na kumwambia awe akikichomoa mara kwa mara kukitazama.‘Na kwa kadiri unapokiona safi, chang’aa kama hivi kilivyo sasa, utajua kuwa ni hai, lakini kama bapa lake utaliona na madoadoa ya kutu, utajua kuwa nimekufa.’

Kuisha kusema hivyo, Bahman mwana wa mfalme akawaaga tena nduguze ndipo akashika njia akaondoka. Akaenda moja kwa moja muda wa siku ishirini, mpaka akajiona anakaribia mipakani mwa Ajemi. Hata alipogeuka kutazama chini ya mti uliokuwa kando na njia akamwona mzee mmoja anayetisha, mwenye masharubu meupe marefu na ndevu zilizomshuka kifuani na mpaka miguuni. Kucha zake zilikuwa ndefu mno, na kichwani mwake alivaa kofia kubwa mno aliyokuwa akitumia kama mwamvuli.

Bahman mwana wa mfalme akamtambua yule mzee kuwa ni mcha Mungu. Akashuka juu ya farasi wake akaenda akasujudu mbele yake na kumwamkia: ‘Babaangu, siku zako duniani ziwe ndefu na dua zako zisibu.’

Yule walii akajitahidi kujibu lakini masharubu yake yalimzuia kwa wingi hata maneno yake yalikuwa hayafahamiki. Mwana wa mfalme alipoona vile, akatoa mkasi kwenye mfuko wa tandiko la farasi wake na kumtaka ruhusa amkate masharubu yake, kwa sababu alikuwa na neno la haja sana kutaka kumwuliza. Yule walii akamfanyia ishara kuwa afanye apendavyo.

Hata zilipokwisha punguzwa pande zote, mwana wa mfalme akamwambia, ‘Ni shida sana kwa mtu kuweza kukutambua leo, kwa namna uonekanavyo kijana. Kwa maneno haya walii akacheka, na kumshukuru kwa hayo aliyoyafanya.

Kisha naye akamwambia, ‘Ngoja nami nikuonyeshe shukrani zangu kwa ulivyonifaa; hebu niambie unalotaka nikutendee.’

Bahman mwana wa mfalme akasema, ‘Ewe walii mpole, mi natoka mbali kuja kutafuta Ndege Anenaye, na Mti Uimbao, na Maji ya Dhahabu. Nasikia kwamba vitu hivyo vyapatikana pande hizi, lakini mahali penyewe hasa sipajui. Basi tafadhali nakuomba uniambie, kama ukiweza, ili nisije nikapata taabu ya kutafuta bure. Wakati alipokuwa akisema hivyo akaona kuwa uso wa walii umebadilika, tena alikaa kitambo bila kujibu.

Mwisho akasema, ‘Bwana wangu, naijua njia unayouliza, lakini wema wako wanifanya nisite kukuonyesha.’

Mwana wa mfalme akauliza, ‘Kwa nini, kwani huko kuna hatari gani?’

Walii akajibu, ‘Kuna hatari kubwa mno, maana watu wengi waliokuwa mashujaa kama wewe, niliwaona wakipita nija hii hii, na kuniuliza swali hilo hilo. Nami nikafanya nilivyoweza kuwageuza nia zao, lakini haikufaa kitu. Hapana hata mmoja aliyesikiliza maneno yangu, wala hapana hata mmoja niliyemwona akirudi. Basi nakutahadharisha kabla, ni heri urudi, wala usipendelee kwenda mbele.’

Bahman akamwambia, ‘Ninakushukuru sana kwa kunipenda unakonipenda, na kwa shauri uliyonipa, hata ijapokuwa sitaishika. Lakini huko kuna hatari gani ya kustaajabisha ambayo hata kwa ushujaa wangu na upanga mkali siwezi kupigana nayo?’

Walii akajibu, ‘Ehe waonaje, ikiwa hao adui zako hawaonekani je?’

Mwana wa mfalme akajibu, ‘Hapana kitakachonizuia nisiende, na kwa mara ya mwisho nakuuliza tena, niambie wapi niende.’

Walii alipoona kuwa mwana wa mfalme haambiliki akatoa mpira mfukoni mwake, akanena, ‘Nhu! Ikiwa ni sharti iwe hivyo, chukua mpira huu uutupe mbele yako wakati ukimpanda farasi wako, nao utabingiria mpaka ufike chini ya mlima, na ukiuona umesimama nawe simama. Mradi ukishuka chukua hatamu za farasi wako uzitupie shingoni mwake, wala usiogope kuwa atakimbia apotee. Na wakati unapoanza kupanda huo mlima utaona katika kila upande kuna chungu kubwa kubwa za mijiwe nyeusi, tena utasikia na jumla ya sauti zinazotoa ufidhuli, lakini usizisikilize ila panda tu, na zaidi ya yote, tahadhari usigeuke nyuma. Ukigeuka, nawe mara ile ile utageuka jiwe jeusi kama hayo mengineyo. Kwa hakika hayo nayo yalikuwa watu kama wewe waliokuja kutafuta vitu vile vile nao wakashindwa, nami nachelea kuwa hata wewe utashindwa vile vile. Lakini kama ukiweza kujizuia usianguke katika mtego huo, na kufika jun ya mlima, utamwona Ndege Anenaye ndani ya tundu zuri, kisha utaweza kumwuliza yeye huko kuliko na Mti Uimbao na Maji ya Dhahabu. Basi haya ndiyo maneno yangu yote niliyonayo kukuambia. Sasa wajua namna ya kufanya na namna ya kujizuia, lakini kama u mwenye akili ni afadhali urudi utokako.’

Mwana wa mfalme akacheka na kutikisa kichwa kisha akamshukuru tena yule walii, ndipo akamrukia farasi wake na kuutupa mpira mbele yake.

Mpira ukabingiria njiani kwa haraka sana, hata ilikuwa shida sana kwa Bahman mwana wa mfalme kuweza kuutazama vizuri, wala nao haukupunguza kasi zake mpaka ulipofika chini ya mlima ndipo ukasimama kwa ghafla. Mara mwana wa mfalme naye akashuka na kutwaa hatamu akazitupia kwenye shingo ya farasi wake. Kisha akasimama kidogo kimya ili kuangalia jinsi alivyozungukwa na chungu za mijiwe myeusi iliyofunika mlima pande zote, ndipo halafu akaanza kupanda kwa uhodari. Kupata hatua tatu au nne, ingawa hakuona mtu, mara akasikia jumla ya sauti zimemzunguka. Zingine zasema, ‘Nani huyu mwenye kichaa? Mzuieni upesi.’ Zingine zasema, ‘Mwuwemi! Mwuweni ati! Shime! Shime jamani! Wevi! Wevi! Wauaji! Wauaj! Shime Shime jamaa!’ zingine zikimdhihaki zikinene, ‘E! Mwacheni maana huyu ndiye hodari kushinda watu wote, naye ni kijana mzuri basi kwa hivyo twasadiki kuwa yule ndege na lile tundu hapana budi kuwa amewekewa yeye!’

Kwanza mwana wa mfalme hakusikiliza ufidhuli ule ila alifululiza kwenda mbele tu, lakini ah! Masikini, badala ya zile kunyamaza, zikazidi kumtia hofu. Basi baada ya kitambo kidogo akafanya wasiwasi na miguu yake ikaanza kutetema, akajiona yu katika kuanguka, akasahau kabisa wasaa aliopewa na walii. Akageuka nyuma kutaka kukimbia, na mara pale pale akageuka mnara wa jiwe jeusi.

Basi kama vile isemwavyo kuwa wakat ule wote Perviz mwana wa mfalme na dada yake walikuwa katika taharuki kubwa, ikawa mara kwa mara kwenda kuangalia kile kisu cha uganga. Na kila walipokwenda kukitazama waliona bapa lake liking’aa wala halina doa lo lote, lakini katika saa ile ile ambayo Bahman mwana wa mfalme pamoja na farasi wake walipogeuka mawe meusi, kile kisu kikaonekana na madoa makubwa ya kutu. Binti sultani akastuka kwa hofu na kukitupa kisu akalia: ‘Ah! Masikini ndugu yangu mpenzi, sitakuona tena, kwani mi ndiye niliyekuua. Nilikuwa mpumbavu kusikiliza maneno ya yule mwanamke shawishi, ambaye labda alikuwa haniambii kweli. Vina faida gani kwangu vitu hivyo: Ndege Anenaye, na Mti Uimbao, vikilinganishwa na wewe, ijapokuwa navitamani sana niwe navvo!’

Ama msiba wa Perviz mwana wa mfalme ulikuwa mzito mno kwa kifo cha nduguye kuliko ule aliokuwa nao Parizade binti sultani, lakini Perviz hakupoteza wakati wake kwa kulia bure.

Akasema, ‘Dadaangu, kwa nini kumdhania yule bi kikongwe kuwa alikudanganya, na kusudi yake ya kukudanganya hivvo ni nini? Basi la, usiseme hivyo. Kifo cha ndugu yetu ni lazima kimetokana na ajali au kwa kukosa kujitunza mwenyewe, nami kesho nitaondoka niende kuko huko nikapeleleze.’

Binti sultani akaogopa sana na kufikiri kuwa pengine nduguye aliyesalia atapotea vivyo, mradi akamsihi aachilie mbali shauri hiyo, lakini hakusikia. Walakini kabla ya nduguye kuondoka huyu alitwaa tasbihi ya shanga mia za lulu akampa, akimwambia, ‘Nikiondoka, kuwa ukihesabu hizi kila siku na uonapo shanga zimekwama wala haziteremki chini moja moja, jua kwamba yale mauti yaliyompata ndugu yangu yamenishukia na mimi. Ila na tutumainie Mungu.’

Basi akaondoka, hata siku ya ishirini ya safari yake akamfikia yule walii mahali pale pale ambapo Bahman nduguye alikutana naye. Mara akaanza kumwuliza, ‘Mahali gani kunakopatikana Ndege Anenaye, na Mti Uimbao, na Maji ya Dhahabu?’ Walii akajaribu kumkanya kama vile alivyomkanya nduguye, na juu ya hivyo akamwambia, ‘Juzi juzi kulipita kijana mmoja nja hii hii, na sura zake kama wewe, lakini sikumwona kurudi tena.’

Perviz mwana wa mtalme akajibu, ‘Ewe walii mtakatifu, huyo alikuwa ni kaka yangu ambaye sasa amekufa, na namna alivyokufa sijui.’

Walii akamwambia, ‘Amegeuka mnara wa jiwe jeusi, kama hao wengine waliokwenda kwa haja hizo hizo, ma wewe kama usipoangalia sana na kushika maonyo yangu, utakuwa nmoja wao.’ Basi kwa vile alivyompendelea mema akaanza kumweleza, akimwambia kuwa hizo sauti za ufidhuli zitakazomwandama juu ya mlima asishughulike nazo, ndipo halafu akatoa mpira mfukoni mwake akampa, ili kusudi upate kumwongoza njia.

Perviz mwana wa mfalme alipofika chini ya mlima, akashuka juu ya farasi wake, na kusimama kimya kidogo ili apate kuyakumbuka maonyo aliyopewa na walii. Halafu akaanza kupanda bila ya woga, lakini kupata hatua tano au sita mara akastushwa na sauti ya mtu iliyokuwa ikinena karibu na sikio lake, ikisema, ‘Simama we! Mpumbavu, nije nikuadhibu kwa ujeuri wako. Ufidhuli huu ulimtoa fahamu kabisa hata akasahau maneno ya walii, mara akavuta upanga wake na kugeuka nyuma kusudi ajilipize kisasi, lakini ah! Masikini, kabla hajatambua kuwa hapana mtu, mara yeye na farasi wake wakageuka mawe mawili meusi.

Na tangu siku zile Perviz alizoondoka kwao hapana hata siku moja iliyopita bure bila Parizade binti sultani kuhesabu shanga zake, na usiku usiku alikuwa akiivaa ile tasbihi shingoni mwake ili kwamba asubuhi akiamka tu upesi ajihakikishe uzima wa nduguye. Naye alikuwa hachoki kuhesabu kwa vidole vyake, hata katika dakika ile ile mwana wa mfalme alipopatikana na masaibu yale kwa kutokuwa na subira, mara moyo ulimfa: alipoona chembe ya kwanza ya ushanga wa lulu imekwama mahali ilipo. Lakini akajikaza kiume ikawa anatafuta njia ya kufanya jambo kama lile; hata asubuhi yake binti sultani akajigeuza, akavaa mavazi akatoka kwenda mlimani.

Na kwa vile alivyokuwa amezoea kupanda farasi tangu utoto wake akawa kila siku kusafiri mwendo mkubwa kama vile valivyo safiri nduguze, hata kupata siku ya ishirini akafika pale pale anapokaa walii. Akamwuliza kwa heshima, ‘Ee walii mwema, je! Utaniruhusu nipumzike hapa kando karibu yako kwa dakika chache? Na labda pengine huenda ukanambia, iwapo umesikia, habari za Ndege Anenaye, na Mti Uimbao, na Maiji Dhahabu yanayopatikana karibu na hapa.’

Walii akajibu, Bibiye, ijapokuwa umevaa mavazi ya kiume lakini sauti yako yakutambulisha, nami nitaona fahari kuu kukutumikia kwa kila njia niwezayo. Lakini nakuuliza, asili ya wewe kuuliza hivyo ni nini?’

Binti sultani akajibu, ‘Ewe walii mwema, nimesikia habari za furaha juu ya vitu hivyo vitatu, nami siwezi kustarehe mpaka nivipate.’

Walii akasema, ‘Bibi, kweli ni vizuri zaidi ya vitu vinginevyo vyote, lakini nakuona huyajui mashaka hayo yaliyo mbele yako, na laiti kama ungaliyajua hungethubutu kujitia katika masaibu hayo. Basi heri uache, nakusihi, urudi kwenu wala usiniombe kukusaidia kukupeleka katika mauti ya ukatili.’

Binti sultani akajibu, ‘Ewe, baba mtakatifu, mimi nimetoka mbali kuja huku, wala siwi radhi kurudi nyuma bila kupata nitakalo. Tena umetaja habari za mashaka: basi tafadhali nakuomba uniambie, ni mashaka yaliyoje! Ili kusudi nipate kuona kama nitayaweza au sitayaweza.’

Basi yule walii akamhadithia habari zote, hasa vitisho vya zile sauti za ufidhuli na vya mawe meusi, ambayo kwanza yalikuwa watu, na taabu za kupanda milima. Kisha akamwambia kuwa njia iliyo bora ya kufanikiwa ni kutotazama nyuma mpaka lile tundu alitie mkononi mwake.

Binti sultani akasema kuwa kadiri alivyoweza kufahamu, jambo la kwanza ni kutosikiliza jamii ya sauti za ufidhuli zitakazo niandama mpaka nifikilie hilo tundu, na tena nisigeuke kutazama nyuma. Kwa hayo, naona nitaweza kujizuia nayo na kutazama mbele yangu sawasawa, na ilivyo pengine huenda ikawezekeana kutishwa na sauti hizo kama vile walivyotishwa hao mashujaa wengine, nitayazima masikio yangu kwa pamba, na wao na wafanye makelele mengi kama wapendavyo, lakini sitasikia.’
 
Walii akasema, ‘Bibiye, katika hao wote waliokuja kuniuliza njia ya mlimani wewe ndiyo wa kwanza uliyetoa fikra kama hiyo ya kuponea hatari, na hivyo humkini ukafanikiwa, ila hatari ndiyo kubwa.’

Binti sultani akajibu, ‘Ewe walii mwema, ama katika nafsi yangu naona nitafanikiwa, na sasa lililobaki kwangu ni kukuuliza njiaya kwendea huko.’

Yule walii kuona kuwa kusema sana haifai, akatoa mpira akampa naye akaupokea na kuutupa mbele yake.

Binti sultani alipofika chini ya mlima, jambo la kwanza alilofanya ni kutwaa pamba akaziba masikio yake, kisha akasimama kidogo kutuliza moyo wake, ndipo akaanza kupanda. Na hata ijapokuwa aligitia pamba hivyo, lakini zile sauti zilimfika masikioni kama miangwi na haikuwa ya kuudhi sana, na kwa hivyo alizidi kupanda.

Binti sultani akacheka na kusema kimoyomoyo, ‘Sitayaacha hata kidogo maneno ya jeuri kunisimamia kati yangu na makusudio yangu,’ basi mradi akawa anapanda tu. Hata mwisho wake akaona tundu la ndege kwa mbali, na sauti ya huyo ndege iliungana na sauti kali za wale wengineo, ikisema, ‘Rudi! Rudi huko utokako, wala usithubutu kunikaribia.’

Binti sultani kumwona huyo ndege, akaenda haraka haraka bila kuchukizwa na zile sauti za ufidhuli, akafululiza moja kwa moja mpaka kwenye tundu, akalishika akisema, ‘Ndege wangu mzuri, sasa nimekupata, nami nitakutunza sana ili usipate kuruka ukaenda zako.’ Alisema hivi huku akitoa zile pamba masikioni mwake, maana hakuwa na haja nazo tena.

Ndege akasema, ‘Ewe bibi hodari, usinilaumu kwa kuwanga sauti wale waliokuwa wakifanya bidii kunilinda nisipatikane. Ingawa kweli nilikuwa nimefungiwa ndani ya tundu, lakini nilikuwa radhi na majaliwa yangu, na ikawa imenilazimu kuwa mtumwa, sitapenda bibi mwingine aliye bora kuliko yule aliyeonyesha uvumilivu, na tangu sasa naapa kukutumikia kwa uaminifu wote nawe siku moja utakuja ushuhudie mwenyewe kuwa nimesema kweli, kwani mimi nakujua vema wewe ni nani, kuliko hivyo unavyojua mwenyewe. Basi sasa niambie utakalo nami nitakutii.

Binti sultani kusikia hivi akajaa furaha ambayo hata yeye mwenyewe ilimstaajabisha akifikiri jinsi ndege alivyo mwangamizia maisha ya nduguze wawili. Akajibu, ‘Ewe ndege niache kwanza nikushukuru kwa habari zako zilizo njema, kisha nikuulize wapi kunakopatikana Maji ya Dhahabu.’

Basi ndege akamweleza mahali yalipo ambapo hapakuwa mbali na pale alipokuwa, na binti sultani akaenda akajaza chupa yake ndogo ya fedha aliyoichukua kwa kusudi hiyo. Halafu akarudi kwenye tundu akanena, Ndege wangu mwema, kuna kitu kimoja bado, nitauona wapi huo Mti Uimbao?’

Ndege akajibu, ‘Tazama nyuma yako ndani ya mwitu, basi binti sultani akawa anazungukazunguka mwituni kuutafuta, mpaka akasikia mlio wa sauti tamu zikimwambia, ‘Umeupata uutafutao.’

Lakini ule mti ulikuwa mkubwa na mretu, tena mgumu, wala haung’oleki. Binti sultani alipoona kuwa hautang’oleka akarudi kwa ndege kutaka shauri, na ndege akamwambia, ‘Usiwe na haja ya kutaka kuung’oa, vunja kitawi tu ukakipande bustanini mwako, nacho kitashika na kuchipua, tena kitakua kiwe mti mkubwa.

Basi Parizade binti sultaní alipovipata vitu vile vitatu vya ajabu alivyoambiwa na yule bi kikongwe, akamwambia ndege, ‘Hivi vyote havinitoshi, maana kama si wewe ndugu zangu hawangaligeuka mawe meusi. Wala mimi siwezi kuyatambua kwa wingi wa haya mengine, ila wewe bila shaka unayajua, basi nakusihi unionyoshe kwani napenda kuyachukua.’

Ndege alipoambiwa hivyo akanyamaza kimya, na binti sultani akamsubiri kidogo. Basi kwa vile ambavyo binti sultani hakujua kuwa ndege hakupendezewa na maneno yale akamtolea ukali, akamwambia, ‘Je! Umesahau kuwa umesema kwamba u mtumwa wangu na utafanya kila nikuambialo, hata maisha yako nayo pia ya katika mamlaka yangu?’

Ndege akajibu, ‘La, sikusahau, ila hayo uniulizayo naona magumu sana, walakini nitafanya kadiri niwezavyo. Ndege akaendelea kusema, ‘Kama ukizunguka kutafutatafuta utaona gudulia lenye maji, basi lichukue ushuke nalo mpaka chini ya mlima, na hayo maji yaliyomo ndani yake, nyunyizia kidogo kidogo juu ya kila jiwe jeusi na hivyo ndivyo utawaona ndugu zako wawili.’

Parizade binti sultani akalichukua gudulia, na tundu, na chupa, na kile kitawi, akashuka navyo mpaka chini ya mlima. Na kwenye kila jiwe jeusi akawa anasimama kulinyunyizia maji; basi ilikuwa kila tone la maji likigusa jiwe tu, mara pale pale hugeuka mtu. Hata alipowaona ndugu zake kwa ghafia, hiyo furaha yake ilikuwa ya ajabu.

Akawauliza, ‘Namna gani! Mnafanya nini hapa’

Wakajibu, Tulikuwa tumelala.’

Binti sultani akasema, ‘Kweli mlikuwa mmelala, lakini kama si mimi nadhani huo usingizi wenu haungewatoka upesi mpaka siku ya kiama. Mmesahau kuwa mlikuja huku kutafuta Ndge Anenaye, na Mti Uimbao, na Maji ya Dhahabu? Na yale mawe meusi yaliyokuwa chungu chungu humu njiani, angalieni kama sasa mtaona hata moja liilobaki! Waungwana hawa wenyewe pamoja na farasi wenu wote waligeuka mawe nami nimewaokoa kwa kuwanyunyizia maji ya gudulia hili. Na ijapokuwa nilipata hivyo vitu nilivyokuwa nikivitamani kwa moyo wangu wote, sikuweza kurudi kwetu bila yenu ninyi, nilipomshurutisha Ndege Anenaye aseme vipi kuzingua uganga.’

Bahman na Perviz waliposikia hivi, wakafahamu yote waliyofanyiwa na dada yao, na wale waungwana waliokuwa wamesimama wakajinadishia utumwa kwake na kuwa tayari kufanya lolote apendalo. Lakini binti sultani alipokwisha kuwashukuru kwa heshima yao waliyomfanyia, akawaambia kuwa yeye hatapendelea yeyote aandamane naye ila nduguze tu, na wengine wote waliosalia wana uhuru kwenda ko kote wapendako.

Kuisha kusema haya binti sultani akapanda farasi wake, na yule Ndege wake Anenaye hakumwachilia ye yote ila mwenyewe kumchukua; ila Bahman alimpa kitawi cha Mti Uimbao, na Perviz nduguye akampa chupa ya Maji ya Dhahabu.

Halafu wote wakapanda wanyama wao wakaondoka na wale waungwana wakaomba ruhusa ya kufuatana nao. Walipokuwa wakirudi, ule umati ulikusudia kupiga kambi pale pale njiani alipokuwa akikaa yule walii ili wapate kumhadithia mambo yaliyowapata, lakini ah! Masikini, walimkuta amekufa, kama ni kwa uzee au ni kwa kuona kuwa kazi yake imekwisha, hapana aliyejua. Mradi wote walisikitika sana.

Basi wakawa wanaendelea katika safari yao, na kila siku jumla yao ikawa inapungua Kidogo Kidogo, maana wale waungwana walikuwa wakienda kwao mmoja mmoja, mwishowe wale nduguze ndipo tu ndio waliobaki.

Walipofika kwao binti sultani akachukua tundu akaenda nalo moja kwa moja mpaka bustanini, na mara ndege akaanza kuimba, yakakusanyika makundi makundi ya ndege waimbao, vizuri, na namna zote za ndege wakachanganyisha sauti zao kuitikia. Na kile kitawi akakipanda karibu na pembe ya myumba yao na baada ya siku chache kilikua mti mkubwa. Yale Maji ya Dhahabu yalimiminwa ndani ya bakuli kubwa la jiwe la marmar lilotengenezwa kwa kusudi hiyo, yakawa yanafurika na kutoa povu na kisha kujivuta juu hewani futi ishirini bila kumwagika.

Sifa za mambo haya ya ajabu zilifika mbali, hata ikawa watu kutoka mbali na karibu kuja kuangalia.

Baada ya siku chache Bahman mwana wa mfalme na Perviz nduguye wakarudia hali yao ile ile, na wakati wao mwingi ulikuwa katika kuwinda. Hata siku hiyo ikatukia Sultani wa Ajemi kwenda kuwinda upande ule ule. Wale vijana waliposikia kelele za wawindaji zawakaribia, wakakata shauri kurudi. Lakini katika kule kurudi kwao kwa bahati wakarudia njia ile ile aliyokuwa akijia sultani. Walipomwona wakashuka juu ya farasi wao na wakapiga magoti na kuinamisha chini nyuso zao, basi kwa vile sultani alivyokuwa akitamani kuona nyuso zao, akawaamuru wainuke.

Vijana wakainuka na kusimama kwa heshima bila wasiwasi, na sultani akawatazama kwa muda wa dakika chache bila kusema nao. Kisha akawauliza, ‘Watoto wa nani ninyi, na huko mnakokaa ni wapi?’

Bahman mwana wa mfalme akajibu, ‘Seyid yangu, sisi ni watoto wa marehemu msimamizi wa mashamba yako, nasi twakaa katika nyumba aliyoijenga hivi karibuni kabla ya kufa kwake, na hivi twakaa kungojea wakati wetu utimie tuje tukutumikie.’

Sultani akawambia, ‘Naona mnapenda sana kuwinda.’

Bahman akajibu, ‘Seyid yangu, haya ndiyo mazoea yetu ya desturi, na yule asiyeweza kuwinda si mtu wa kutumainiwa kushika silaha.’

Sultani akapendezewa sana na maneno haya, na akasenma, ‘Ikiwa ni hivyo, nitafurahi kuangalia uhodari wenu. Basi njooni mchague mnyama yo yote mtakayempenda kuwinda.’

Mara pale pale mabin sultani wakarukia farasi wao na kumfuata sultani nyuma nyuma. Na kabla hawajafika mbali sana mara wakaona kundi la nyama mwitu linakuja, Bahman akaanza kufukuza Simba na Perviz nduguye akafukuza simba marara. Na wao wote wawili walikuwa stadi sana wa kutumia mikuki midogo na walipopata nafasi ya kupiga, simba na simba marara wakapigwa wakaanguka. Sasa Bahman akafuata simba mwingine na Perviz akafukuza Simba marara wa pili, na kwa muda wa dakika chache nao pia wakaanguka wakafa, Basi walipokuwa wakijitayarisha kwa windo la tatu, sultani akawazuia kwa kutuma mmoja wa watumishi wake kwenda kuwaita walipokuja sultani akasema na huku akicheka.

‘Kama nikiwaacha mwendelee kuwinda, naona mara moja wanyama watakwisha. Walakini juu ya hivyo, ushujaa wenu na heshima zenu zimenipendeza sana, wala sitapendelea mjitie katika hatari zaidi. Sasa nimesadikisha kuwa siku moja nitaona manufaa yenu kama hivyo nlivyosema.

Halafu sultani akawataka sana wakakae kwake pamoja lakini wao wakamshukuru sana kwa heshima aliyowafanyia na kuomba awawie radhi, na kuwastahimilia wakae kwao.

Yule sultani ambaye hakuzoea kuona neno lake likikataliwa akauliza sababu yake, na Bahman mwana wa mfalme akaeleza kuwa hawapendi kumwacha dada yao, wala hawakujizoeza kufanya jambo lo lote bila kushauriana pamoja wote watatu.

Sultani akawajibu, ‘Basi nendeni mkamtake shauri, na kesho mje tuwinde pamoja, halafu mnipe na majibu yenu.’
 
Basi wale mabin sultani wawili wakarudi kwao, na kwa kuwa yale mambo yaliyowapata yaliwatia wasiwasi kidogo walisahau kabisa kumwambia dada yao. Hata asubuhi yake walipokwenda kuwinda, wakakutana na sultani kwa mahali pale pale walipoachana jana, naye akawauliza shauri gani waliyoipata kwa dada yao. Vijana wasiwe na la kujibu ila kutazamana wenyewe kwa wenyewe kwa haya. Mwisho Bahman akasema, ‘Seyid yangu tunakuomba utuhurumie kwani si mimi wala si ndugu yangu, hapana mmoja kati yetu aliyekumbuka.’

‘Sultani akajibu, ‘Basi leo hala hala msisahau, na kesho mnirudishie majibu yenu.’

Walakini, jambo lile lile lilipotukia tena mara ya pili, waliogopa kuwa sultani atawakasirikia sana kwa kusahau kwao. Lakini sivyo, ila sultani alitoa mipira mitatu ya dhahabu mfukoni mwake akampa Bahman, akimwambia, ‘Iweke kifuani pako, nawe hutasahau tena, kwani hapo utakapovua mshipi wako usiku, itaanguka, na huo mshindo utakaofanyika hapo utakukumbusha nilivyoagiza.’

Na haya yote yakatokea kweli kama vile alivyotangulia kusema sultani, ndipo wale ndugu wawili wakaingia chumbani mwa dada yao wakati alipokuwa akitaka kulala, nao wakamhadithia habari zile.

Binti sultani Parizade akafanya wasiwasi sana kwa habari zile wala hakuwaficha nduguze namna alivyokuwa akiona, akasema, ‘Kukutana kwenu nà sultani kutakuleteeni heshima na utukufu, nami nafikiri mtapewa kazi za vyeo, lakini ikiwa hivyo mtaniweka mimi katika hali ya wasiwasi sana. Najua ni kwa ajili yangu mimi hata mkashikilia kuupinga haja ya sultani, nami nawashukuru sana kwa hilo. Lakini kumbukeni kwamba wafalme hawapendi kukinzwa neno, na hivyo atawawekea kinyongo kwa siku nyingi na hayo yataniondolea furaha kabisa. Basi nendeni mkamshauri Ndege Anenaye, ambaye ana hekima nyingi na busara, kisha mje mniambie asemavyo.’

Vijana wakatoka kwenda kumleta ndege na kumwelezea habari ile. Ndege akanena, ‘Ama ninyi mabwana haifai kabisa kumkatalia sultani. Kwa hakika lazima mmwalike sultani aje aangalie nyumba yenu.’

Binti sultani akakataa, akasema, ‘Ewe ndege, wajua jinsi sisi tunavyokaa kwa kupendana mno, lakini je, waonaje! Hayo yote hayatatuvunjia udugu wetu?’

Ndege akajibu, ‘La, udugu wenu hautavunjika kamwe, ila mtashikamana zaidi.

Binti sultani akasema, ‘Lakini mwisho wake sultani ataniona.’ Ndege akajibu ‘Naam, imemlazimu akuone, na kila jambo baya litageuka liwe zuri.’

Siku ya tatu yake sultani alipowauliza kama walimwambia dada yao na shauri gani aliyowapa, Bahman mwana wa mfalme akajibu kuwa wanapokea kwa unyenyekevu ualishi wake kwake, na dada yao amestaajabu sana juu ya kusitasita kwao kuupokea ualishi huo, na hivi wanaomba msamaha.

Sultani akakubali msamaha wao, na kuwaambia kwamba na yeye pia alikuwa na yakini kuwa wote watatu watakuwa waaminfu kwake, na kwa mchana ule uliosalia akawataka wawe pamoja naye, na hivyo ikawa waziri mkuu kukirihika na watu wengine wa mfalme kukasirika.

Mradi akafuatana nao taratibu mpaka wakaingia ndani ya mji mkuu wa mfalme, na watu waliokusanyika mabarabarani kumwamkia mfalme waliwakodolea macho wale vijana wawili Wanaume, walioonekana wageni kwa kila mtu. Ikawa ni kunong’onezana wakisema, ‘Aa, masikini, laiti kama sultani angekuwa na watoto kama wale! Tazama jinsi wanavyoonekana watukufu, tena wa makamo mamoja.’

Mara ile sultani akaamuru watengeezewe vyumba viwili vilivyo vizuri na kuwashurutisha wakae mezani kula pamoja naye. Wakati walipokuwa wakila, sultani akawatia katika mazungunmzo ya mambo mengi ya elimu, naya visa na hadithi; na katika kila jambo alilokuwa akiwazungumzia, aliwaona kuwa wale vijana wanamsikiliza kwa makini. Ndipo sultani akasema katika nafsi yake, ‘Kama hawa wangelikuwa wanangu mwenyewe sidhani kama ningeweza kuwaelimisha vema kama hivi ikawa ni kuwasifu sana kwa mafunzo yao na jinsi walivyobobea elimu.

Hata jioni ilipoingia mabin sultani wakajilaza kifudifudi mbele ya kiti cha enzi kuomba ruhusa ya kurudi kwao, na mfalme akawaambia maneno mazuri ya kuwaaga. Bahman mwana wa mfalme akasema, ‘Seyid yangu, tunaomba utufanyie hisani sisi na dada yetu, kuja kupumzika nyumbani mwetu kwa muda mchache wakati wewe na wawindaji wako mkipita njia ile.’

Sultani akajibu kwa furaha, Maadam nina hamu ya kumwona dada yenu ambaye natumai mwenye elimu na maarifa kama ninyi nitarajieni kuja kwenu kesho kutwa.’

Yule binti sultani naye angependa sana kumkirimu sultani, lakini kwa vile ambavyo hakujua desturi za kukaribisha mgeni, akamwendea Ndege Anenaye kumshauri namna ya vyakula vya kuandaa. Ndege akajibu, ‘Ewe bibi yangu mpenzi, wapishi wako ni hodari sana, basi mambo yote waachie wao, ila jambo moja hili: chakula cha kuandaliwa kwanza sharti kiwe kachumba ya matango na lulu.’

Binti sultani akamaka, ‘A! Matango na lulu? Lo, ndege wee kwa nini? Nani aliyepata kusikia chakula kama hicho? Sultani atataraji kuandaliwa chakula anachoweza kula, si kama hicho. Na juu ya hivyo, hata nikitumia lulu zangu zote nilizonazo, hazitatosha hata nusu yake.’

Ndege akajibu, ‘Bibi, fanya kama nikuambiavyo, hapana neno ila mema yatatokea. Na kwa hizo lulu, kama ukiondoka kesho alfajiri na kuchimba chini ya mti wa kwanza katika bustani, upande wa mkono wa kulia, utapata nyingi kadiri utakazo.’

Binti sultani alimwamini sana yule ndege kwa kuwa siku zote alisema kweli; hata asubuhi kulipopambazuka akamchukua nokoa wake kwenda kufanya vile alivyoambiwa. Baada ya kuchimba kidogo wakakiona kisanduku cha shaba kilicho fungwa kwa vibizimu vidogo akavifungua, na kile kisanduku kikakaonekana kimejaa lulu ambazo hazikuwa kubwa kubwa sana ila za kiasi tena zenye rangu nzuri.

Binti sultani akakichukua kisanduku akarudi nyumbani, tena akamwacha nokoa akifukia shimo.

Wakati binti sultani alipokuwa akienda kule bustanini, kumbe wale nduguze wanaume walikuwa wakimwona ikawa wametaharuki mno kwa yeye kuondoka alfajiri kama ile. Mradi nao wakaondoka kuvaa nguo na kumwandama dada yao, mara kwa ghafla wakakutana naye anarudi, amechukua kisanduku mkononi.

Wakamwuliza, ‘Watokapi? Kwani nokoa alikuja kukuambia kuwa ameona mali?’

Binti sultani akawajibu, ‘Mimi ndiye niliyeona mali.’ Mara pale pale akakifungua kile kisanduku kuwaonyesha nduguze lulu zilizokuwamo ndani yake.

Basi walipokuwa wakirudi ndani ya nyumba binti sultani akawahadithia nduguze jinsi alivyomtaka ndege shauri, na namna alivyoambiwa. Sasa ikawa wote watatu kujaribu kubahatisha kutambua maana yake lakini hawakuweza, na mwisho wake wote wakakiri kuwa wameshindwa, mradi wakalazimika kuwa radhi vivyo hivyo.

Binti sultani alipoingia ndani ya nyumba, jambo la kwanza alilofanya alituma aitwe mpishi mkuu, na kumwambia apike karamu ya sultani. Hata alipokwisha kumwambia mara kwa ghafia akanena, ‘Katika vyakula hivyo nilivyokutajia, kuna kimoja ambacho hicho ni lazima ukiandae vizuri kwa ajili ya sultani, wala kisitengenezwe na mtu mwingine ila wewe mwenyewe. Na chakula chenyewe ni kachumba ya matango na lulu.’

Yule mpishi mkuu ambaye katika maarifa yake yote hakupata kusikia chakula kama kile, akarudi nyuma kwa kustaajabu. Na mara hiyo hiyo binti sultani akatambua kuwa yule mpishi ana shaka katika nafsi yake, akamwambia, ‘Naona wanidhania kuwa nina kichaa, lakini najua mwenyewe hivyo nifanyavyo. Nenda kachukue lulu, ukatengeneze kachumba vizuri sana.’

Asubuhi siku ya pili mabin sultani wakaenda porini kuwinda, mara kwa ghafa sultani akawatokea. Sasa kuwinda kukaanza na kuendelea mpaka adhuhuri; hata jua lilipokuwa kali sana wakalazimika kuacha kuwinda. Mradi ikawa kama hivyo ilivyotengezwa; wakageuza vichwa vya farasi wao kwenda kule nyumbani kwa kina Bahman, ambaye akawa pamoja na sultani.

Perviz yeye akatangulia kwenda nyumbani ili kumpasha habari dada yake kuwa sultani anakaribia kufika. Hata mfalme alipofika uwanjani, binti mfalme akaenda kujitupa chini miguuni pake, lakini mfalme akainama kumwinua na akamkodolea macho kwa kitambo jinsi alivyostushwa na uzuri wake na heshima zake, na kwa umbo la kupendeza alilokuwa nalo huyo kijana mwanamke wa shamba. Akasema mwenyewe kwa mwenyewe, ‘Ama kweli hawa wanategemeana sana, wala nami sioni ajabu kama hawa wawili wanayashika sana mashauri yake. Nataka nijue habari zao.’

Wakati ule ule haya alizokuwa nazo binti sultani akaanza kusema maneno ya kumkaribisha, akinena, ‘Seyid yangu, hiki ni kijumba cha shamba tu, kinachowafaa watu kama sisi tunaonakaa pekee yetu. Wala hakiwezi kulingana na majumba makubwa ya mjini, na kwa hakika hakilingani hata na vijumba hivyo vidogo vya sultani.’

Sultani akajibu, ‘Siwezi kukubali kwa hayo usemayo, hata hii ndogo niliyoiona yanishangaza sana, lakini sasa sisemi neno mpaka hapo utakapokwisha kunionyesha mwote.’

Basi binti sultani akamchukua kumtembeza chumba hata chumba kumwonyesha, na sultani akatazama kila kitu barabara. Mwisho wake akamwuliza, ‘Hii ndiyo unayoita nyumba ovyo ya shamba? Kama kila nyumba ya shamba ingalikuwa namna hii, hiyo miji ingalikuwa hali gani? Sasa sistaajabu tena kwa nini hampendi kuiacha. Haya twende bustanini, ambayo nina yakini kuwa ni nzuri kama hivi vyumba.

Kasema vile, mara kilango kidogo cha bustanini kikafunguliwa, na kitu cha kwanza alichokiona sultani kilikuwa Maji ya Dhahabu. Sultani akastaajabu akinena, Yapendeza namna gani rangi ya maji haya! Kiwapi hicho kijito chake, nawe watanyaje hata kikapata kufurika kwenda juu sana kama hivi? Sifikiri kama katika dunia kuna jambo lingine la kupendeza kama hili!’ Akawa anasogea karibu kuzidi kutazama, hata alipotosheka na upekuzi wake, binti sultani akamwongoza kwenye Mti Uimbao.

Walipokuwa wakikaribia, mara sultani akastushwa na mlio wa sauti nzuri za ajabu, lakini hakuweza kuona kitu. Akamwuliza binti sultani, ‘Umewaficha wapi wapiga vinanda wako? Wako juu hewani au chini ya ardhi ama kwa hakika watu wenye sauti nzuri kama hizi, haifai kujificha!’

Binti sultani akajibu, “Seyid yangu, sauti zote zinatoka katika huo mti ulosimama sawasawa mbele yetu, na kama ukijongea hatua chache mbele, utasikia zikitokeza waziwazi.’

Sultani akafanya kama alivyoambiwa, na akasimama kitambo kusudi kusikiliza. Mwisho akasema, ‘Bibi nakusihi uniambie, jinsi mti huu wa ajabu ulivyopata kuingia bustanini mwako. Bila shaka umetoka mbali sana, na hasa mtu kama mimi ninayependa kupata vitu vya tunu, singekosa kusikia mahali ulipo! Waitwaje jina lake?’

Akajibu, ‘Seyid yangu, jina lake ni Mti Uimbao wala nao si mti wa nchi hii. Kisa chake kimechanganyika pamoja na kile cha Maji ya Dhahabu, na Ndege Anenaye, ambaye bado hujamwona. Na kama utaridhika, nitakuwa tayari kukuzungumzia habari zote, hapo utakapokwisha kupumzika.’

Sultani akajibu, ‘Bibi ingawa umenionyesha miujiza mingi, sioni kuchoka. Twende mara moja tena nikayatazame yale Maji ya Dhahabu, kisha natamani kumwona na huyo Ndege Anenaye.’

Yale maji ya dhahabu yalimshangaza mno sultani, hata hakuweza kuvuta miguu kutoka pale yalipo. Akamgeukia binti sultani akanena, ‘Wasema kuwa maji haya hayatoki katika kijito cho chote, wala hayaletwi na mfereji! Basi hivi nifahamuvyo mimi, si maji wala si huo Mti Uimbao, vyote havitoki katika nchi hii.’

Binti sultani akajibu, ‘Seyid yangu, hivyo usemavyo ndivyo, na kama ukiangalia bakulini utaona maji yote yako mahali pamoja wala hayangewezekana kuletwa kwa humo. Ila jambo moja linistaajabishalo sana ni hili: ya mimi kumimina bakulini maji kidogo tu yaliyokuwamo kichupani, nayo yakaongezeka kwa kiasi kama hiki ukionacho.

Sultani akajibu, ‘Vema, lakini leo sitayatazama sana, sasa nipeleke huko kwenye Ndege Anenaye.’

Katika kuikaribia ile nyumba, tahamaki sultani akaona kundi la ndege wengi na sauti zao zilijaa hewani. Sultani akauliza, ‘Kwa nini hapa ndege wakawa wengi zaidi ya kule kwingine?’

Binti sultani akajibu, ‘Seyid yangu, waona tundu lile linaloning’inia dirishani juu ya baraza? Yule ndiye Ndege Anenaye, sauti yake yasikilizana zaidi ya zinginezo zote, hata imeshinda sauti ya yule ndege aimbaye vizuri usiku. Na ndege wengi hukusanyikia hapa ili kujumlisha sauti zao pamoja na yake.’

Sultani akasogea karibu dirishani, lakini yule ndege hakumjali, akawa anaendelea na wimbo wake kama kwanza. Binti Sultani akamwambia ndege, ‘Ewe ndege wangu mzuri, huyu ni Sultani, basi mpe maneno mazuri.’ Mara ile ile ndege akanyamaza kuimba, na ndege wengine wote wakanyamaza pia.

Ndipo ndege akaanza kusema, Sultani amekaribishwa, nami namwombea maisha marefu na kufanikiwa kote.’

Sultani akamjibu, ‘Nakuambia ahsante, ewe ndege mwema, nami nimefurahi sana kukuona wewe uliye sultani na mfalme wa ndege.’

Karamu ilikuwa imeslhaandaliwa. Sultani kuona chakula akependacho, cha kachumba na matango, kuwekwa mbele yake akaanza kula, lakini akastaajabu sana kuona kimepangiliwa lulu. Ama hiki ni kioja, na sifahamu maana yake, kwani hakuna awezaye kula lulu!’

Basi kabla ya mabin sultani au binti sultani kujibu, Ndege akajibu’ Mbona hukustaajabu bali ulisadiki bila shaka yo yote ulipoambiwa kuwa mkeo amekuzalia mbwa, na paka, na kigogo cha mti badala ya watoto?

Sultani akajibu, ‘Kweli nilisadiki, kwa kuwa wakunga ndiyo walioniambia.

Ndege akasema, ‘Seyid yangu, hao wakunga walikuwa nduguze mkeo, nao walimwonea kijicho kwa fahari uliyomfanyia wakati wa harusi, na kwa kujilipiza kisasi chao walibuni shauri hiyo. Hebu nenda kawaulize, nao watakuungamia kosa lao. Hawa ni watoto wako walionusurika na mauti kwa kuokotwa na marehemu msimamizi wa bustani zako, akawalea kama wanawe.’

Sultani kusikia hivi ikawa kama fahamu kumwingia. Akasema, ‘Ndege, moyo wangu waniambia kuwa hayo usemayo ni kweli tupu. Kisha akanena, ‘Wanangu, niacheni nikukumbatieni kisha nanyi mkumbatiane vile vile, si kwa ukaka na udada tu, ila kwa kuwa mna damu ya Mfalme wa Ajemi. ‘

Hata dakika zile za furaha ya kwanza zilipokwisha, sultani akajihimiza kumaliza chakula chake, kisha akawageukia wanawe na kuwaambia, ‘Leo mmejuana na baba yenu, na kesho nitawaletea mama yenu. Basi kaeni tayari kumpokea.’

Basi sultani akapanda farasi wake na kurudi mjini kwa haraka sana. Hata alipofika, mara ile ile akatuma kuitwa waziri mkuu, na kumwamuru kuwakamata ndugu za mkewe apate kuwauliza maswala siku ile ile. Hayo yakatimizwa. Wakasimamishwa mmoja mmoja kuulizwa na hatia yao ikathibitika, mradi haikupata saa. Wakauawa.

Lakini sultani mwenyewe hakungojea kuambiwa kuwa hukumu yake imetimizwa, ila aliondoka akaenda kwa miguu hali amefuatwa na watu wake wa baraza nzima mpaka kwenye mlango wa msikiti mkuu, akamtoa mkewe kwa mkono wake mwenyewe mle tunduni alimokuwa kajibana, ambamo alikaa kwa miaka mingi. Akasema huku machozi yakimtoka, ‘Mke wangu nimekuja kukuomba msamaha kwa haya niliyokutendea yasiyo haki na kuyatengeneza kwa kadiri niwezavyo. Na wale waliolizusha kosa hili ovu nimekwisha waadhibu, nami sasa natumai kuwa utanisamehe hapo nitakapo kuonyesha watoto wetu wanaopendeza sana. Na tena katika dunia nzima hapana watoto walio elimika sana na kuhitimu kabisa kama wao. Njoo twende zetu, ukarudie kikao chako na fahari zote zinazokustahilia.’

Maneno haya yalisemwa mbele ya watu hadhara waliokusanyika kutoka pande zote za mji kwa lile shindo la kwanza lililoingia mjini juu ya yale yaliyokuwa yakitendeka, maana habari zilienea upesi kwa muda wa dakika chache tu. Hata siku ya pili yake Sultani na Malkia wakaondoka asubuhi mapema kwenda kule kwa watoto wao, hali wote wamevalia majoho ya kifalme, na masheikh wote kuwafuata. Walipofika, sultani akawakabilisha watoto wake mmoja mmoja kwa mama yao, na kwa kitambo kizima ilikuwa hapana kitu ila makumbatiano na kulizana na maneno ya huruma. Kisha wakaandikiwa chakula kilichotengenezwa kwa ajili yao wakala. Baada ya kuisha kula wote wakaondoka kwenda bustanini ambako sultani alimwonyesha mkewe Maji ya Dhahabu, na Mti Uimba. Na yule Ndege Anenaye, alikuwa amekwisha kujuana naye. Hata jioni ilipoingia wakapanda farasi wao kurudi mjini, mabin sultani wakawa upande wa baba yao, na binti sultani pamoja na mamaake. Kwa mbali kabla hawajalifikia lango la mji, njia yote ilijaa makundi ya watu waliokuja kuwapokea kwa shangwe, tena yasemwa kuwa kelele za furaha ambazo zilichanganyika pamoja na nyimbo za Ndege Anenaye, aliyekuwa ndani ya tundu lake lililopakatwa na binti sultani, na za ndege wengine waliomfuata, ailihanikiza kote kila upande.



Basi hivi ndivyo ilivyokuwa hata wakapata kurudi nyumbani kwa baba yao.



MWISHO
 
KISA CHA BABA-ABDALLA KIPOFU​





“EWE, Jemadari wa Uaminifu, mimi nilizaliwa Baghdadi, nami niliachwa yatima wakati nilipokuwa mtoto mdogo sana, maana wazazi wangu wote wawili walikufa. Basi nikarithi mali kidogo niliyoifanyia biashara kutwa kucha ili nipate kuiongeza, hata mwisho nikajiona nimepata ngamia themanini. Hawa niliwaajirisha kwa wafanyaji biashara waliokuwa wakisafirisafiri, ambao nilikuwa nikiandamana nao katika safari zao nyingi, na kila mara nilikuwa nikirudi na faida kubwa.

Hata siku moja mchana nilipokuwa nikirudi kutoka Basra, nimechukua bidhaa nilizokusudia kupeleka Bara Hindi, nikaja nikatua mahali pa pweke nilipopaona pana malisho mazuri kwa ngamia wangu, nami mwenyewe nikakaa chini ya mti kupumzika. Mara nikitazama nikamwona walii aendaye Basra kwa miguu amekaa kitako karibu yangu anapumzika, nikamwuliza anakotoka na wapi anakokwenda; mara pale tukasuhubiana. Na baada ya kuulizana habari kama desturi, tukatoa chakula tulichokuwa nacho tukala.

Tulipokuwa tukila, yule walii alitukia kutaja mahali palipofichwa mali ambapo hapakuwa mbali sana na pale tulipokaa, akanena, ‘Hata kama ngamia wako themanini wangepakiwa barabara hata wasiweze kuchukua zaidi, ile mali iliyofichwa huko ingeonekana nyingi vile vile kama haikupnguzwa.’

Kusika habari hii nikawa na furaha sana kwa tamaa, nikamtupia mikono yangu shingoni mwake kumkumbatia, nikinena: ‘Ewe walii mwema, nasadikisha kuwa mali ya dunia hii si kitu kwako, na kwa hivyo yakufalia nini kujua mali hiyo ilipo? Kwa wewe pekeo njiani kiasi waweza kuzichukua kiganja tele. Lakini niambie mimi zilipo, niende nikawapakie ngamia wangu themanini, na mmoja wao nitakupa wewe kuwa dalili ya shukrani zangu.’

Ama kwa kweli ile kiasi nilichokisia kumpa hakikuwa kikubwa sana, lakini kwangu mimi niliona kikubwa mno, maana kwa choyo na tamaa iliyoniingia moyoni, nikaona kuwa ngamia sabini na tisa watakaonibakia hawatakuwa sawa kama wakilinganishwa na yule mmoja.

Walii aliyaona waziwazi mawazo yaliyokuwa yakinipitia moyoni

Mwangu, lakini yeye hakunibainishia jinsi nia yangu ilivyo. Ila alijibu taratibu, ‘Ndugu yangu, wajua sana kama nijuavyo mimi, kuwa kufanya hivyo si haki. Maana hapo mahali nilionyeshwa mimi tu kusudi nizuie siri, na hiyo mali iwe yangu mwenyewe. Lakini maadam nimekuambia jinsi ilivyo yaonyesha kuwa nilikuwa na matumaini nawe, na hivyo nataraji kupata shukrani zako daima, kwa kukufanya wewe uwe na malı kama mimi.

Lakini, kabla sijakufunulia siri ya mali hizo, huna budi uape, kuwa baada ya kwisha kuwapakia hao ngamia wako kwa kadiri wanavyoweza kuchukua, na mimi utanipa nusu, kisha kila mmoja ashike njia yake. Nadhani hivi ni vizuri, kwani kama ukinipa ngamia arubaini, na mimi kwa upande wangu nitakuonyesha njia ya kununulia elfu wengine.’

Sikuweza kukanusha maneno yake, maana yale aliyoyasema yule walii ndiyo sawa hasa, lakini pamoja na hayo, lile wazo la kuwa yule walii atakuwa tajiri kama mimi lilikuwa halistahimiliki. Mradi nikaona hapana haja ya kubishana au kuililia hasara ya mali nyingi hiyo mpaka mwisho wa maisha yangu, ndipo nikakubali masharti yake.

Basi nikawakusanya ngamia wangu tukaenda pamoja na walii. Baada ya hatua kidogo, tukafika mahali palipokuwa kama bonde; lakini kijia cha kuingilia hapo kilikuwa chembamba mno hata ngamia wangu hawakuweza kupita wote pamoja ila mmoja mmoja. Lile bonde dogo au pale palipokuwa na nafasi wazi, palizibwa na milima miwili, na kwa kila upande kulikuwa na majabali yaliyosimama sawasawa wala hayapandiki.

Hata tulipokuwa hasa katikati ya milima hiyo, yule walii akasimama. Akaniambia, ‘Wakalishe chini ngamia wako hapa palipo na nafasi, ili tuweze kuwapakia kwa urahisi, kisha wewe na mimi tutakwenda huko kuliko na mali.’

Basi nikafanya kama nilivyoambiwa, na kisha nikamrudia walii, niliyemwona akijaribu kupekecha moto kwa vijiti vikavu.Hata moto ulipowaka, akatwaa konzi tele ya uvumba akatia motoni huku akinuizia maneno ambayo sikuyafahamu, na mara pale pale moshi mnene ukapanda juu hewani, naye akawa anautandua moshi pande mbili, ndipo halafu nikaona jabali lililosimama kama nguzo kati ya milima miwili, likafunguka taratibu, na jumba zuri kama nini likaonekana ndani yake.

Lakini, Ewe Jemadari wa Uaminifu, ile tamaa ya dhahabu ilinishuka sana hata nisiweze kujizuia kutazama mali jinsi ilivyo, ila nikaivamia chungu ya kwanza ya dhahabu iliyokuwa karibu nami, nikitia ndani ya kanda nililokuwa nalo. Na yule walii naye akaingia kazini vile vile, lakini mara nikaona kuwa yeye hakushughulika na dhahabu ila alishughulika kukusanya vito tu, basi na mimi nikaona ni afadhali nimwige afanyavyo. Mwisho wake wale ngamia tuliwapakia sana kadiri walivyoweza kuchukua, sasa ikawa hakuna jambo lililobakia ila kufunga ile hazina, twende zetu.

Lakini kabla hatujaifunga, yule walii akaenda kwenye dawati kubwa la dhahabu lililokuwa limenakshiwa vizuri, akalifungua na kutoa kisanduku kidogo cha mbao akakifutika kibindoni mwake; nilipomwuliza kina nini, akaniambia kuwa kina mafuta ya namna ya pekee. Halafu yake akapekecha tena moto, na kutwaa konzi ya uvumba akatia motoni na huku akinuizia maneno ambayo sikuyafahamu, na mara pale pale jabali likafungika, pakawa kama zamani.

Jambo la pili lilikuwa la kugawanya ngamia pamoja na mali yao, basi tulipokwisha gawanya kila mtu akawa anachunga mwenyewe wanyama wake, tukatoka bondeni. Hata tulipotokea njia kuu kwa mahali palipokuwa na njia panda tukaagana kwa kukumbatiana kwa mapenzi huku nikimpa shukrani zangu kwa ukarimu aliyonifanyia, kwa kunigawia mali nyingi kama ile. Nami nilimuaga kwa wema, kisha tukapeana migongo na kila mmoja akakimbilia ngamia wake, yeye akashika njia yake kuelekea Basra na mimi kuelekea Baghdadi.

Kusema kweli, mimi nilifika kwa shida kwenye ngamia wangu jinsi shetani mbaya alivyonikalia moyoni, hata nikasema binafsi, ‘Mtu aliye walii, mali kama ile aitakia nini? Yeye pekee ndiye aaminiwaye na hazina ile, na siku zote aweza kwenda kuchukua nyingi kwa kadiri aitakayo.’ Basi kuisha kusema hivi, mara nikasimamisha ngamia wangu kando ya njia, nikarudi mbio kumfuatia.

Nilikuwa hodari sana wa kupiga mbio, na hivyo sikukawia kukutana naye. Nilimwita, nikinena, ‘Ndugu yangu, wakati tulipokuwa tukiagana mara nilijiwa na mawazo ambayo labda ni mageni nawe, Na hasa kwa kazi yako, wewe u walii unayeishi maisha ya utulivu, wala hutamani kitu cho chote cha dunia hii ila kufanya mema tu. Na sasa naona umesahau kuwa wajitweka mwenyewe mzigo kwa kujikusanyia mali nyingi kama hiyo, na baada ya hivyo, kwa kusema kweli, hakuna mtu ambaye tangu kuzaliwa kwake hajapata kuzoeana na ngamia, akaweza kuchunga wanyama wakaidi kama hawa. Basi kama u mwenye akili, hutapendelea kujidhili nafsi yako kwa taabu za ngamia zaidi ya thelathini, nawe utaona mwenyewe kuwa taabu na mashaka yatakayokukuta kwa hao thelathini tu, yatosha.

Yule walii, ambaye alinifahamu sana, akajibu kwa upole maana hakupenda tubishane, ‘Hayo usemayo ni kweli, lakini mimi hapo kwanza sikufikiri hayo, na sasa ikiwa ni hivyo, chagua kumi uwapendao uchukue.’

Basi nikachagua ngamia kumi walio wazuri nikaenda nao, ili nikawachanganye pamoja na wale niliowaacha nyuma kule njiani. Sasa nikawa najisifu kimoyomoyo: ‘Nimepata niliyoyataka, lakini yule walii alikuwa rahisi sana kushika maneno. Kwa nini nisimtake kumi zaidi. Mara nikageuka nyuma kumtazama. Kumwona hajafika mbali sana, nikarudi kumfuatia.

Hata nilipoona namkaribia nikamwita, ‘Ndugu yangu -e-e! Mara naye akageuka, akasimama kuningojea. Nikamwambia, ‘Sipendi kuachana nawe kabla sijakuambia jambo moja ambalo naona hulifahamu vema. Kuchunga ngamia kunahitaji maarita makubwa, hasa kwa mtu ye yote anayekusudia kufuga kundi la ngamia thelathini. Na kwa faida yako mwenyewe, nina yakini kuwa utapendezewa mno, iwapo utaniamini na ngamia kumi wengine, maana kwa ustadi wangu nilionao kama nikiwa na ngamia wawili au mia mbili, kwangu mamoja.’

Basi ikawa vile vile kama zamani, yule walii hakufanya matata nami nikachukua ngamia kumi wengine nikaenda nao kwa furaha, nikamwachia ishirini tu, wawe sehemu yake. Sasa nikawa nimepata ngamia sitini, na hivyo mtu ye yote aweza kufikiri kuwa nimeridhika.

Lakini, ewe Jemadari wa Uaminifu, kuna methali inenayo: Zaidi mtu apatavyo, ndivyo zaidi atamanivyo; basi na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwangu. Sikuweza kuridhika kabisa kuona ngamia mmoja akibakia kwa walii, ndipo nikamrudia kuzidi kumwomba na kumshika miguu, na kumwahidi shukrani za milele, mpaka wale ngamia ishirini wa mwisho aliokuwa nao wakaingia mikononi mwangu.

Walii akasema, ‘Ndugu yangu, wachukue wakakufae. Lakiní kumbuka kwamba mara moja mali huweza kuruka; mfano kama vile isemwavyo: Mtaka yote kwa pupa hukosa yote.’

Macho yangu yalifumba nikawa kipofu kwa dhahabu, na masikio yaliniziba nikawa kiziwi hata sikusikiliza kamwe shauri lake la maarifa, ila nikawa nikitazama tazama huku na huku kufikiri nimtake kitu gani kingine.

Mara kwa ghafla nikakikumbuka kile kisanduku kidogo cha mafuta alichokifutika kibindoni mwake, ambacho nilikidhania kuwa kina mali ya thamani zaidi ya ile nyingine yote. Basi nikamshika miguu mara ya mwisho, na kumwuliza, ‘Wenda kifanyaje kile kisanduku kidogo cha mafuta? Ama naona vigumu kukichukua wewe; labda na hicho nacho utapenda kuniachia mimi vile vile. Hasa, kwa kusema kweli, walii aliyeacha mambo ya dunia hana haja na mafuta!’

Aa, laiti kama angenikatalia haja yangu! Nhu, lakini alijua mambo. Ehe kama angalikataa? Ningalikichukua kwa nguvu, maana hivyo ndivyo nilivyokuwa nimeazimia. Lakini hakukataa, pale pale akakitoa akanipa kwa kusema nami kwa wema, akinena, ‘Chukua rafiki yangu, na kama kuna kitu kingine niwezacho kukutendea, lazima uniambie.

Basi kile kisanduku kilipokwisha kuwa mikononi mwangu nikakifunua kifuniko. Kisha nikamwambia, ‘Maadam wewe u mtu mwema namna hii, tafadhali nakuomba uniambie faida ya mafuta haya.

Walii akanena, ‘Ni mafuta ya ajabu sana sana. Kama ukitwaa kidogo na kujipaka katika jicho lako la kushoto, saa ile ile utaona hazina zote zilizofichwa chini ya ardhi. Lakini tahadhari usije ukaligusa na mafuta jicho lako la kulia, au kuona kwako kutapotea milele.

Maneno yake yalinitia tamaa kubwa, nikamwambia, ‘Twaa unijaribie nakusihi, kwani wewe utajua vema zaidi kuliko mimi, namna ya kupaka kwake.’ Ama moyo wangu ulifanya hamu sana kujaribu uzuri wake, na hivyo nikatoa kisanduku cha mafuta nikampa.

Walii alipokwisha kipokea kile kisanduku akaniambia nifumbue jicho langu la kushoto, naye akalipaka mafuta taratibu. Hata nilipolifumbua tena nikaona mali za kila namna zisizo hesabu zimetandazika, kama zilizo mbele yangu. Lakini wakati huo wote lile jicho langu la kulia nilikuwa nimelifumba, nalo sasa lilikuwa limechoka sana kwa kufumbwa. Basi ndipo nilipomsihi huyo walii kulipaka mafuta na jicho lile pia.
 
Back
Top Bottom