PostGE2025 Anatomia ya Usaliti: Mwaka Mmoja wa Uchaguzi wa Mchongo, Samjo Samjo za Ikulu na Falsafa ya Watawala wasio na dhamiri

PostGE2025 Anatomia ya Usaliti: Mwaka Mmoja wa Uchaguzi wa Mchongo, Samjo Samjo za Ikulu na Falsafa ya Watawala wasio na dhamiri

Conversations and stories after Tanzania's 2025 General Elections

Kijana wa Ifoza

JF-Expert Member
Joined
Oct 31, 2025
Posts
1,180
Reaction score
2,302
download.jpg
Picha : Mwanga wa kumbukumbu katikati ya giza kuu: Mwaka mmoja tangu mioyo ya watanzania ilipojeruhiwa na dhihaka ya demokrasia.

Leo imetumia rasmi mwaka mmoja tangu Taifa hili lishuhudie kile kinachobaki kuwa kovu kubwa la kisiasa katika kizazi chetu—Uchaguzi wa Mchongo wa Oktoba 29, 2025. Haikuwa tu dhihaka kwa demokrasia, ulikuwa ni usaliti wa makusudi dhidi ya mamlaka ya wananchi.

Lakini ukali wa donda hili hautokani tu na vurugu, damu, na machozi yaliyomwagika; unatokana na ukweli wa kifalsafa kwamba watawala wetu wamechagua kuishi katika ombwe la kimaadili, wakionyesha utepetevu na ukosefu vya chembe ya majuto au kuwajibika.

Kuhalalisha Unyama: Falsafa ya Ushindi kwa Gharama Yoyote
Kifalsafa, uongozi uliotukuka unapaswa kuwa kioo cha utu na kimbilio la wanyonge wakati wa majonzi. Hata hivyo, utawala huu umethibitisha nadharia ya Machiavelli—kwamba mbinu zozote chafu na za unyama zinasafishwa na matokeo ya kubaki madarakani.

Katika kipindi chote cha mwaka mmoja uliopita, hatujashuhudia Rais au viongozi wenzake wakuu wakisimama kuomba radhi au kufanya ukarabati wa kijamii kwa familia zilizopoteza ndugu zao [DW Election Violence]. Badala yake, ukweli wa kimkakati unaonyesha namna dola inavyopuuza maumivu haya [Human Rights Watch].

Ripoti ya Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman ilithibitisha vifo vya angalau watu 518 kutokana na sababu zisizo za kawaida. Lakini badala ya kuwataja na kuwawajibisha makamanda na askari waliofyatua risasi hizo, ripoti hiyo ilibaki kuwa koti la kuzuia mvua ya lawama za kimataifa, huku kukiwa hakuna mtuhumiwa hata mmoja aliyekamatwa.

download (1).jpg

​
Picha : Mfumo uliopoteza mwelekeo: Ripoti rasmi inakiri mamia ya vifo vya raia, lakini hakuna mkono wa sheria uliogusa watekeleza maovu.

Wakati kura zikidaiwa kuhesabiwa na Rais kutangazwa mshindi kwa asilimia tisini na nane ya kura, nchi ilikuwa chini ya mtandao uliokatwa na amri ya kutotoka nje. Kusherehekea ushindi wa kishindo uliopatikana kwa kuwazuia wapinzani wakuu kama Tundu Lissu kisheria ni uthibitisho kuwa utu ulishindwa mbele ya tamaa ya madaraka. Hata tunapoadhimisha mwaka mmoja leo, badala ya serikali kuonyesha unyenyekevu, tunashuhudia wimbi jipya la ukandamizaji.

Kukamatwa na kufunguliwa kwa kesi mpya za uhaini dhidi ya viongozi wa upinzani kama John Pambalu mwezi huu wa Oktoba 2026 ni salamu tosha kuwa dola haina majuto, bali ina nia ya kuendeleza vitisho.

Samjo Samjo na Shughuli Nyinginezo: Kudhihaki Kilio cha Wanyonge
Ukiitazama ratiba ya viongozi wetu leo, utadhani wanaongoza kisiwa cha malaika ambacho hakijawahi kushuhudia dhuluma. Katika hotuba zao za kimataifa na kitaifa, naratibu kuu ni kusifu ustawi wa kidemokrasia na kiuchumi kana kwamba Oktoba 29 ilikuwa tukio la kawaida la kihistoria.

Rais na wasaidizi wake wako bize na samjo samjo za kisiasa—ziara za kukata utepe, teuzi mpya, na shughuli za kawaida za kiofisi zinazoakisi mtindo wa business as usual. Huku ni kukwepa ukweli. Wanajifanya hawaoni kuwa chini ya zulia jekundu la Ikulu kuna mabaki ya kilio cha yatima na wajane wa uchaguzi ule.

download (4).jpg

​
Picha : Nyuma ya pazia la itifaki na samjo samjo za kiutawala: Historia haiwezi kufutwa kwa zulia jekundu wala tabasamu za kisiasa.

Hitimisho : Madaraka Yana Kikomo, Laana ya Historia Haina Mwisho
Watawala lazima wakumbushwe ukweli mmoja wa kihistoria: Machozi ya wanyonge hayana sauti ya kushindana na ving'ora vya misafara yenu, lakini yana uzito wa kimaadili unaoweza kuzamisha himaya yoyote ile. Unaweza kuwa na jeshi, mahakama, na tume ya uchaguzi mfukoni mwako, lakini huwezi kuimiliki dhamiri ya pamoja ya jamii uliyoikwaza.

Kutokuwa na remorse si ishara ya nguvu; ni ishara ya uoga wa kukabiliana na ukweli. Mnaweza kuendelea na samjo samjo zenu na kujifanya hamuoni kilio cha waliojeruhiwa, lakini fahamuni kuwa historia inarekodi kila tabasamu lenu la dhihaka juu ya makaburi ya demokrasia yetu.

Watawala lazima wakumbuke kuwa historia ya mwanadamu ni historia ya mapambano ya kitabaka, na unyonyaji pamoja na ukandamizaji unapovuka mipaka, unajenga mazingira yanayowaunganisha wanyonge kiotomatiki chini ya kauli mbiu isiyo rasmi ya kuwaunganisha waliodhulumiwa.

Katika muktadha huu wa kifalsafa kama alivyowahi kuonya Karl Marx, utawala wowote unaokataa kusikiliza maumivu ya watu wake na kuendekeza dhuluma, unakuwa unajitengenezea wenyewe mazingira yatakayochochea uasi wa lazima; kwa maana hiyo, unakuwa unajizidishia mtego na kujizalishia wenyewe watu watakaokuja kuuzika mfumo huo, ambao mwishowe hawataona cha kupoteza katika kupigania utu wao isipokuwa pingu zilizowafunga.

Raha ya Milele Uwape E Bwana, na mwanga wa milele Uwaangazie wapumzike kwa Amani. Amina
Eternal rest grant unto them, O Lord, and let perpetual light shine upon them. May they rest in peace.

Ee Mwenyezi Mungu, uwasamehe na uwarehemu, uwakubalie siri zao na uwajaalie mapumziko mema katika Pepo ya Firdaws.

اللَّهُمَّ اغْفِرْ لَهُمْ وَارْحَمْهُمْ وَعَافِهِمْ وَاعْفُ عَنْهُمْ، وَأَكْرِمْ نُزُلَهُمْ، وَاجْعَلْ قُبُورَهُمْ رَوْضَةً مِنْ رِيَاضِ الْجَنَّةِ فِي فِرْدَوْسِكَ الأَعْلَى.





Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
 

Attachments

  • 1793273141026.png
    1793273141026.png
    277.7 KB · Views: 2
  • download (2).jpg
    download (2).jpg
    13.5 KB · Views: 2
  • download (3).jpg
    download (3).jpg
    54.5 KB · Views: 2
Back
Top Bottom