Wahenga walisema isipokufa haizai; huenda pia ni kweli Tanzania ya kale isipokufa mpya haiwezi kuzaliwa. Tukubali kuinywa sumu ilimradi inahuisha; anachofanya Magufuli ni sumu kwa wengi, maisha yatatetereka, mazowea yatakoma hata yale tunayoyapenda sana. Bunge litaonekana kama sio lenyewe linaburuzwa, demokrasia itaonekana inahujumiwa, nk. hilo ndilo tanuru la moto; natung'ate meno tupite humo kwa uchungu kwa manufaa ya kesho. Mradi wote tunakubali tumepata jembe, basi tuweke tumaini letu sote hapo. Wote tumuunge mkono, tukae nyuma yake, tuone anatufikisha wapi; hili lisijalishe upinzani wala jumuia za kijamii. Kiongozi wetu jembe anayo maono, si vyema kukwazwa na vibwagizo vya demokrasia za majukwaani au makelele ya kila uchao hata hajapata wasaa wa kusimamisha agenda yake na mizizi kuota. Tena ingefaa siasa za majukwaani zikome kwa mwaka mzima au hata miwili; kama jembe anatufikisha kwa njia ya mkato shida iko wapi? demkrasia ni njia na udikteta ni njia pia, lakini ya mkato. Suala hapa ni kufika na kama hatufiki si itakujaonekana tu? si kila mwananchi atajionea mwenyewe? kuna haja gani kuwalazimisha watu kuvuka daraja ambalo hawajalifikia? Watanzania sio wajinga wa kufanya kujulishwa matatizo yao; wanayajua kama yapo.