*ANGA LA WASHENZI II -- 22*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Sheng akawaamuru wamwachilie.
Kamanda akampatia Sheng mkono. Akasema, "nimekuwapo hapa kwa muda."
Lakini uso wake ulionyesha shaka.
ENDELEA
"Lakini sikuwa nafahamu kuwa si silaha tu umeleta. Umeleta pia na watu na chemicals!" Kamanda akakunja uso akitoa macho. Sheng akasimama na kumtazama.
"Kamanda," Sheng akaita, "kwani kuna shida nikiongezea kidogo mzigo wangu?"
Kamanda akabanwa kwanza na kigugumizi. Akatafuta neno la kuongea, akasema, "Hapana bwana Sheng. Lakini nilipaswa kuwa na taarifa rasmi. Namma hii inaweza kututia hatiani!"
Sheng hakumjibu Kamanda. Akaendelea kutembea akiwa anawaza mambo yake kichwani. Alipofika getini, akasimama na kumtazama Kamanda. Akasema, "ni hatia gani hiyo waizungumzia? Kwani nakulipa kwa kazi gani?"
Kamanda akataka kujibu, ila Sheng akasimamisha kidole chake kama ishara ya kumtaka asimuingilie. Alafu akaendelea kunena, "fanya kazi yako, Kamanda."
Kisha akazama getini na ndani ya muda mfupi yakatoka magari mawili makubwa yaliyobebelea kontena rangi za kijani. Zilipotokomea eneoni, Sheng akaonana na Kamanda na kumpatia mkono wa kheri, anataka kwenda zake.
"Samahani," Kamanda akasafisha koo na kuuliza; "Mmefikia wapi kwenye swala la Jona?" Sheng akamtazama kwa sekunde mbili kisha akamwekea mkono begani.
"Kamanda, kati yangu nawe, nani wa kumuuliza mwenzake hilo swali?"
"Aahm pengine unaweza ukawa umepata jambo. Si mbaya kunishirikisha."
"Sijapata kitu. Na nilidhani hata hilo jambo wewe ndiye utakuwa wa kwanza kuling'amua maana limeshusha hadhi ya jeshi lenu."
Sheng aliposema hayo, akamwacha Kamanda pasipo kumuaga. Akatembea hatua tano, ila mara akageuka na kumtazama Kamanda. Akasema, "fom today, hilo swala la Jona, niachie mimi, sawa?"
Kabla Kamanda hajasema jambo, Sheng akageuka na kwenda zake. Kamanda akabaki akimtazama mwanaume huyo anayoyoma.
Akalaani sana. Aliona amedharaulika. Thamani yake imeshuka. Juzi tu, alikuwa akinywa na Sheng kwa furaha, leo anaongea naye kana kwamba kakijana ka mtaani!
Akang'ata meno. Punde akajikuta ndani ya gari lake, akatekenya shina la usukani na kutimka eneoni baada ya kuhakikisha kila jambo limeenda sawa.
Alijua wazi kesho yake vyombo vyote vya habari vitakuwa hapo bandarini. Na hata yeye atakuwapo hapo akiwakilisha jeshi la polisi. Ila akiwa kama mtu asiyejua kinachoendelea hapo. Akiwa ni miongoni mwa wageni rasmi!
**
Saa nane usiku ...
"Kila kitu tayari, unaweza kwenda kupumzika, boss," alisema mwanaume mrefu mweusi, kijakazi wa Sheng. Alikuwa amevalia 'ovaroli' la bluu na kichwani akiwa amejiveka kofia ngumu na usoni amevalia miwani kubwa ya kumkinga macho na mikononi ana glovu ngumu rangi ya njano.
Sheng na Shao walikuwa wamesimama pamoja wakiwa wametia mikono mifukoni. Macho yao yalikuwa yanatazama magari yale mawili makubwa yaliyotoka bandarini, na watu kadhaa wakiwa wanashughulika hapa na pale kwenye upakuaji.
Baada ya kijakazi huyo kusema hayo, wanaume hao wa kichina wakaongozana kwenda kutazama kama kila kitu kipo sawa. Wakakuta kontena limebakia tupu, na ndani ya maabara kulikuwa kumesheheni vitu kadha wa kadha.
Wakatazama maabara ile kwa kitambo kidogo, kisha Sheng akamuuliza Shao, "unadhani vitasaidia?"
Ni nadra kwao kutumia lugha ya kiswahili katika maongezi yao. Ila Sheng aliamua kufanya hivi maana alitaka kumpa Shao mazoezi zaidi ya kutumia lugha hii. Imekuwa ikimsumbua, na kwakuwa yupo ndani ya nchi itumiayo kiswahili katika maongezi ya kila siku, hakuwa na budi kukifahamu.
"Nadhani vitasaidia sana," Shao akajibu kwa sauti ya puani. Kama ungelikuwa unamsikia usingelimwelewa kabisa kwa namna anavyoongea. Ila kwa mwenzake Sheng ilikuwa haina shida maana wanashea lugha.
"Lakini, Shao," Sheng akasema akimtazama mwenzake. "Naona kuna haja ya kuagiza vijana toka China kuja kufanya kazi huku. Hawa vijana wa hapa siwaamini kabisa, haswa ukizingatia Lee sijui alipo.
Tuna haja ya kutuma maombi nyumbani watukabidhi baadhi ya vijana waliowapika huko kwa mafunzo magumu, waliojawa stadi za mapambano, waje kutusaidia."
Shao akaminya lips zake nyembamba. Akatoa mkono wake mmoja mfukoni na kufikicha pua yake kidogo kama mtu mwenye mafua.
"Sishani kama itawezekana kwa shasha," akasema Shao akitikisa kichwa. "Unajhua shasha hivi kule nyumbani kumekuwa na shiida shana. Li wameamka na kuwa ngufu kuba tofauti na mwashoni. Inasemekana wanafadhiliwa na matafa ya magaribi. Wanapambana shana kuhakksha Wu inakufa na waon ku-rise."
Li ni wakina nani?
Miaka kadhaa huko nyuma koo ya Li ilikuwa ni moja ya koo ya kawaida sana ndani ya nchi ya China. Hakuna mtu aliyekuwa anaizungumzia wala kuipa uzito kwenye maongezi yao. Ilikuwa ni koo iliyoundwa na wakulima na wafanyabiashara wadogowadogo.
Na katika kipindi chao, koo hiyo ikashuhudia koo ama familia ya Wu ikipanda kwa kasi sana mbele ya macho yao haswa baada ya kuonekana kuvutia serikali katika namna ambavyo ilikuwa ikiwasaidia kupata na kulinda mikataba ya China. Vilevile ikihakikisha dola ya China inakua kiuchumi kwa kutumia mkono wowote, aidha wa damu ama kitabu!
Na kwasababu hiyo basi, Wu wakatengewa kitengo maalum ndani ya chemba za serikali. Kitengo ambacho kiliikabidhi koo ya Wu ofisi ya ujasusi wa kiuchumi dunia nzima. Kwa hivyo basi, koo hii ikawa si siri tena ndani ya nchi ya China japo biashara zao zingine zilikuwa haramu kama vile utumwa wa kileo, madawa na utekaji.
Sasa basi kwa kuitambua hili, nchi za magharibi ambazo hazipo tayari kuona dola zao zinawekwa miguuni na China, zikaamua kufanya jambo kujinasua na kuwadhoofu wachina wajao kwa kasi. Na njia bora waliyoichagua ikiwa ni ile ile ya 'kikulacho ki nguoni'. Wakiwa wanafahamu nguvu ya China ni familia koo ya Wu, basi wao wakaungana na koo ya Li kuhakikisha wanamtokomeza na kumdhoofisha Wu!
Na basi kwasababu Li walitaka umaarufu na pesa (Fame n' money), kwao hili hawakuliona gumu. Wakalipokea wakiwa vichwani wamedhamiria kifuta kiburi cha Wu, na kuirejesha koo ya Li kama koo yenye nguvu zaidi kama ilivyokuwa kabla ya mapinduzi ya nchini China ya mnamo mwaka 1945 mpaka 1950.
Na sasa, Li wamekuwa wakiitawala Hongkong. Taratibu wakijipanga kutanuka na kwenda kuikabili Wu popote ilipo.
Je, vipi kuhusu ile nyaraka ya Lee na saga la Chen Zi huko Hongkong??
Tuurudi kwa Sheng na Shao ...
Sheng alitikisa kichwa chake. Alikuwa ameelewa nini Shao amemaanisha. Akalaani. Akalaani tena maana aliona ni uzembe umefanyika mpaka kufikia hali kama hiyo ya sasa. Hakuwa anaamini kama Li ingefikia kipindi kuwa tishio na hata sasa Wu ikashindwa kusambaza wapambanaji wake na basi wakabakizwa hukohuko China.
Akafikiria kidogo na kuona kuna haja ya kwenda huko China. Akakutane na viongozi wake juu na kujadili mambo kadhaa. Lakini Shao akampa tahadhari. Haitakuwa vema kama akienda huko akiwa hajakamilisha kwanza kazi yake ya kumtia Jona mikononi.
Toa boriti kwenye jicho lako ndipo utazame ya wengine. Sheng akakubali shauri hilo. Punde atakapomalizana tu na Jona, atasafiri kwenda China angalau kwa juma moja tu.
Na aliamini hilo la kumshughulikia Jona halitachukua muda maana ameshaleta vifaa vya kazi.
Wakatoka maabara na kwenda kwenye ghala za silaha. Napo wakatazama ingizo jipya na kufurahishwa nalo. Baada ya hapo wakatoka na kwenda kupumzika maana muda ulikuwa umeshaenda sana.
**
Asubuhi Redioni ...
" ... kwa hivyo basi, mimi kama kiongozi mkuu wa mkoa, ningependa kutoa rai kwa wananchi wangu kutumia fursa hii adhimu. Kuanzia majira ya saa mbili asubuhi kesho mpaka majira ya kumi jioni, wafike pale kwenye meli ya kichina ili wapatiwe matibabu na vipimo bure kabisa!
Hili lamaanisha na kuonyesha namna gani serikali yao inavyowajali, na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata afya bora akaijenge nchi kwa kufanya kazi."
Ilikuwa sauti ya mkuu wa mkoa.
**