*ANGA LA WASHENZI II -- 29*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
"nimetoka kuongea na BC. Nimemwelezea kuhusu hii chemical. You know what? Amesema si yenyewe ..."
Marwa akahisi baridi la ghafla limempitia. Koo limemkauka. Na joints zote za mwili zimeishiwa nguvu.
Akatoa macho. Ila kabla hajanena, Miranda akamwambia, "ngoja kwanza ..."
ENDELEA
Miranda akanyanyuka akishika kiuno chake. Akang'ata kidole akifikiria. Kisha akamtazama tena Marwa na kumwambia.
"I know it can't be!" Akatikisa kichwa. "It can't be kabisa! Lazima hii iwe yenyewe."
Alikuwa kama mtu aliyewehuka, na Marwa aliogopa kumwongelesha. Akabaki anamtazama aone ataishia wapi. Ila na yeye alikuwa amegawanyika nafsi.
Alikuwa amejihisi mtupu kabisa. Akifikiria shurba alizopita, tundu la sindano, kisha kazi ikawa bure, anachoka kabisa. Alitamani alie, ila hapana. Hata macho yalikuwa makavu.
Miranda akaketi kitini. Akashika kichwa. Akatazama zile seti pale mezani kisha akainamisha tena kichwa chini. Hapa Marwa akatambua mwanamke huyu alikuwa ana roho ngumu.
Haki ingekuwa ni mwanamke mwingine, angeweza kujaza ndoo kwa machozi. Angekuwa tayari ameshanyofoanyofoa nywele zake akisaga meno.
Pengine alikuwa anaugulia kwa ndani, ila kitendo cha kuweza kubakiza gulio hilo kifuani asilitoe, bado kulimfanya Marwa ashangae.
"Sasa tunafanya nini?" Marwa akauliza.
Miranda akashusha pumzi na kukodoa macho. Akaminya lips zake kama apendavyo, alafu akasema kwa sauti ya chini, "tungoje, labda akiziona anaweza kubadili mawazo."
"Una maanisha BC?" Marwa akauliza. Miranda akatikisa kichwa na kujibu kifupi, "yah!"
Kukawa kimya kidogo. Punde Miranda akamuita dada wa kazi na kumuagiza amletee maji ya kunywa. Haraka dada huyo akatii agizo, akamletea Miranda jagi kubwa la kioo na glasi kwa pembeni.
Miranda akafakamia glasi mbili kwa mpigo kana kwamba kilevi, wakati huo Marwa akiwa anamtazama. Angalau akahisi ahueni kifuani mwake.
Marwa akasafisha koo na kumwambia, "pole. I know how you feel."
Miranda akatanua lips zake kama mtu anayetabasamu, hakusema kitu.
"Natumai ile kazi uliyoifanya haitakuwa bure. Naomba Mungu iwe hivyo. Unastahili pongezi sana, ila si bahati kuna muda dunia huwa katili ... si kila saa ipo fair. Na tukio lile linaweza kupita ila kwangu litaacha nyayo maishani mwangu yote. Sitalisahau.
Si tu kwamba niliona ulivyo mkufunzi kwenye sanaa za mapambano, bali namna ulivyokuwa unahangaika kumrudishia uhai mtu aliye hoi kitandani. It was remarkable!"
Miranda akaguguma na kusema, "ingekuwa remarkable kama ningefanikiwa. All of that was useless!"
Kisha akanyanyuka na kwenda zake chumbani. Marwa akabaki peke yake. Akatazama yale maji kwenye jagi kwa sekunde kadhaa kisha akayavuta upande wake.
Ikapita kama dakika tano. Mara akasikia vishindo vya miguu koridoni. Kutazama akamwona Miranda akiwa amevalia taulo kifuani. Uso wake ulikuwa 'fixed'.
Akaita, "Marwa." Kisha akaongezea akinena kwa sauti ya chini, "Thanks kwa compliments. Nisamehe kwa maneno yangu."
Kwa namna moja ama nyingine Miranda alikuwa amejiskia vibaya kumsemesha Marwa vile. Roho ilimsuta.
Marwa akajibu kwa tabasamu lile nesi ampalo mgonjwa. Miranda akaenda zake na ndani ya muda mfupi Marwa akasikia mtu akijimwagia maji kwa 'shower', naye akaamua kumwagia maji ndani ya mwili wake.
Akakaa hapo sebuleni kwa muda mpaka akaanza kusinzia. Kwa mujibu wa saa ya ukutani, ilikuwa ni saa tisa usiku.
Hakujua alikurupushwa na nini, akaamka na kuangaza kisha akajikokota kwenda chumbani alipolazwa Jona, akajimwaga kwa pembeni ya mgonjwa huyo na kuanza kujiongelesha mwenyewe.
"I am sorry, Jona ... I am so sorry ... bado hatujafanikisha ... hatujafanikiwa."
Hakunena tena jingine usingizi mzito ukambeba pasi na huruma. Akakoroma kwa uchovu.
**
"Marwa!" Sauti iliita. Haikuwa sauti ya kike bali ya kiume. Kabla hajaitika, akajaribu kuifikiria ni sauti ya nani, akakosa jibu.
Ikajirudia tena, "Marwa, amka! ... Marwa!"
Mara hii alipofikiria kuhusu hii sauti, akagutuka baada ya kupata majibu. Ilikuwa ni sauti ya Jona! ... hapana! ... akakataa ... akatega sikio asikie tena kuhakiki.
"Marwa!" Sauti ikaita tena. "Marwa!" Ikarudia kuita. Na hapa Marwa akapata kweli uhakika wa kile alichokiwaza. Kweli ilikuwa ni ya Jona.
Basi kichwa chake kilikuwa kizito sana. Alikuwa bado ana usingizi pomoni kichwani. Ila akapambana kukinyanyua na kufungua macho aone amwitaye.
Hakuona mtu! Kutazama kando, Jona alikuwa yupo vilevile kama alivyomuacha. Amelala. Dirisha lilikuwa jeupe kuashiria pamekucha.
Sasa nani alikuwa akiniita? Akawaza. Punde akapata jibu.
"Marwaa!" Sauti iliita mlangoni. Na sauti hii akaitambua kuwa ni ya Miranda, na si Jona kama alivyokuwa anasikia! Akasonya na kujibandua kitandani. Akaendea mlango.
"He! Ulikuwa umelala au umekufa?" Miranda akauliza akistaajabu. Alikuwa amevalia gauni refu jeusi lililobana kifua na kumwaga chini. Nywele zake alikuwa amezifichama ndani ya mfuko fulani wa nailoni.
"Sorry, yani nlikuwa usingizini kweli," Marwa akajitetea.
"Na mbona ukalala huko kwa mgonjwa badala ya chumba chako?"
"Aaahm! Unajua nilizidiwa na usingizi, hata huko chumbani nikaona mbali kufika."
Miranda akaguna, kisha akamwambia ajiandae kwani BC amefika. Itakuwa vema wakiwa wote. Basi Marwa akaenda kuoga na kuosha uso kisha akajivuta sebuleni. Ila usingizi bado ulikuwa unamsumbua. Macho yalikuwa mekundu. Na kichwa kizito sana.
Alipotazama saa ya ukutani, akaona ni saa nne kasoro asubuhi. Akastaajabu. Si bure Miranda alimuuliza kama amelala ama amekufa.
Sebuleni alikuwa ameketi BC ndani ya suti ya kijivu na kando yake aliketi Miranda. Mwanamke huyo hakuonyesha dalili ya kuwa na hata lepe la usingizi, hali hii ilimshangaza kidogo Marwa ukizingatia muda waliolala. Ila hakuwa na muda wa kujiuliza sana.
Mezani kulikuwa kuna seti ya zile test tube Miranda alizozikwapua toka maabara ya Sheng, kwa hivyo ilikuwa rahisi kubashiri mada mezani ilikuwa ni hizo kemikali.
"They are not the one," (sio zenyewe,) BC alinena akimtazama Marwa. Ilionekana alishateta tayari na Miranda hapo kabla.
"It seems Sheng did not want to risk. And perhaps, the antidote is not there at all, or it wasnt brought as we thought. But ..." (inaonekana Sheng hakutaka kujiweka hatari. Na pengine, antidote haipo kule kabisa, au haikuletwa kama tulivyowaza. Lakini ...)
Bwana huyu mzungu akaweka kituo, kisha akakunja nne na kuumwaga mgongo wake kwenye ukuta wa kiti.
"... In one way or the other, this may be our starting point." (... kwa namna moja ama nyingine, hili linaweza kuwa kianzio chetu.)
Japo Marwa alikuwa na usingizi kichwani, hakupepesa macho hata kidogo. Alisimamisha masikio yake na kujaribu kukaza macho. Pengine kumsikiliza mzungu akiongea kunahitaji juhudi za ziada kusikia kila analolitamka kwasababu ya ung'ataji wao wa maneno.
"Though this is not the antidote we want, it can act as a great ingredient we need to make one ... the real one." (Japo hii si antidote tunayoihitaji, inaweza kutumika kama kiungo kikubwa tunachokihitaji kutengeneza yenyewe. Ile ya ukweli.)
Hapa Marwa akajikuta anatabasamu. Hatimaye ile kazi haikuwa bure, akawaza. Ila kama kuna kitu hakuwa anakijua ni kuwa ndiyo kwanza kazi ilikuwa inaanza! Maana walitakiwa kupata viungo vingine viwili kutimiza antidote inayohitajika kumtibu Jona.
"So you mean we have to go there again?" (Kwahiyo unamaanisha inabidi turudi tena kule?) Marwa akauliza akiwa na uso wa hofu.
BC akatikisa kichwa na kusema, "No! Maybe it's somewhere more dangerous than there." (Hapana! Labda ni mahali hatari zaidi kuliko kule.)
Marwa akamaliza mate.
"Where is it?" (Ni wapi huko?) Akauliza.
BC akatazamana na Miranda.
***