Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

Nyie wadada nyie acheni mambo yenu mmeanza sasa mara Jona nampenda mara nini sijui kwanini msimseme kinoo mzee wa six pack acheni zenu nyie (Chief kama kawaida yangu nakukubali sana kwa kuwasha moto salute) leo ngoja tuone (Natabiri zitakuwa 3)
 
*ANGA LA WASHENZI II -- 33*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Ni wazi mazingira yalikuwa magumu kujikomboa hapa.

Alipotoka fikirani, akastaajabu kuona tayari wameshafika getini. Gari linasimama.

"Bila shaka ni hapa bibie?" Akasema dereva.

ENDELEA

Miranda akakosa la kunena. Pasipo kungoja wale wanaume wakashuka toka kwenye gari, dereva akitaka kuwa mtu wa mwisho, abaki garini ili afunge na kuweka kila kitu sawa.

Kabla Miranda hajashuka akamgusa kidogo Marwa, mara mbili mguuni mwake katika namna ambayo hakuonekana, kisha akasimama kandokando ya mlango akitazama wanaume wale ambao tayari wameshajongea getini, ni yeye tu ndiye anangojewa awafungulie wazame ndani.

Akakohoa mara mbili, kisha akaanza kujongea. Na kabla hajafika mbali, yule dereva akauliza, "vipi huyu mtu wako?"

Akimaanisha Marwa. Miranda akabinua mdomo kisha akasema, "nadhani twende tukamtoe kwanza huyo mnayemhitaji kisha tukirejea tutamtoa huyo. Au mwaonaje?"

Yule dereva akagutuka na jambo. Akiwa bado garini akauliza, "kwanini tusimtoe tukaenda naye kabisa ndani?"

Miranda akapandisha mabega kupendekeza kwamba lolote ni kheri tu. Kisha akakohoa tena mara tatu na kupigapiga kifua chake kama mtu asikiaye maumivu.

Wale wajamaa waliokuwa wameshuka, wakajiteua wawili wauendee mwili wa Marwa. Miranda akasimama akitazama kwa makini. Na kwa macho ya wizi, akamtazama mwanaume mmoja aliyekuwa amesimama kando yake.

Basi katika namna ya ajabu, haraka ya radi, milio miwili risasi ikavuma. Mara wale wajamaa walioenda kumbeba Marwa wakajikuta chini. Na ni ajabu kama walibakiwa na uhai maana walitulia tuli ya maji mtungini!

Na katika namna hiyo hiyo, yani haraka ya kustaajabisha, Miranda akamsulubu yule jamaa aliyekuwa amesimama naye kwa teke barabara, akajikuta kama mkungu wa ndizi uliochoropoka mgombani! Tih!

Na mara, "tulia hivyohivyo!"

Ilikuwa ni sauti ya Marwa. Sura yake ameijaza ndita na akikodoa kutishia amani. Mdomo wa bunduki ameuelekezea kichwani mwa dereva.

Akampa sisitizo, "ukitingisha hata nywele, basi uhai wako mali yangu!"

Dereva akaweka mikono juu akiwa amefura. Miranda akarejea ndani ya gari na kisha akachukua bunduki aliyokuwa ameishikilia Marwa. Akambonda dereva na kitako chake, akazirai.

"Umefanya kazi nzuri sana, Marwa!" Miranda akampongeza. "Umekuwa mwanafunzi mwepesi sana kushika mambo. Najivunia kuwa nawe."

Basi wasipoteze muda, wakawafungasha wanaume wale ndani ya gari kisha Miranda akamtaka Marwa azame ndani na yeye akamalizane na maadui hao.

Kazi haikuwa ya kulala! Hawana mahali pa kuhifadhi maiti hizo, na huenda ikaleta kesi. Bila shaka majirani watakuwa wamesikia vishindo vya risasi. Amelenga kuwapeleka mahali salama na kisha ampatie ujumbe murua bwana Sheng.

"Basi twende wote!" Marwa akabweka. "Ya nini uje kuniacha kwenye tisa na kumi i-karibu?"

Wasizoze na jamvi, wakakwea na Miranda akatimua chombo mpaka maeneo yapatikanayo makao ya Sheng. Huko akaliweka gari kwenye maegesho yasiyo rasmi, alafu akashuka na kwenda ... baada ya dakika kama tano akarejea na kumwambia Marwa kila kitu kipo sawa japo hakusema alienda kufanya nini.

Na kabla hawajaliacha gari hilo, mwanamke huyo akaandika baadhi ya maneno kwa 'marker pen' nyekundu kiooni.

Kisha wakayoyoma eneo hilo.

**

Zikapita kama dakika kumi na tano, na jamaa mmoja mrefu mwembamba mwenye asili ya kichina akakatiza eneoni akiwa anavuta sigara kwa hisia.

Pengine alikuwa anasikia baridi. Sigara yamsaidia kuiondoa. Ila ambacho alikiona sekunde chache mbele yake, nadhani kilimsaidia zaidi kupasha mwili joto.

Alisita, akatazama. Akapekua na kugundua ile ilikuwa gari ya makaoni. Mbona ipo huku? Akajongea kutazama. Akaangalia na mule ndani. Haki alichokiona kikamfanya aachame, sigara ikadondoka chini.

**

"Mkuu, kunaa ... kuna ..." alimwemweta bwana mweusi akijawa na puzo la hofu usoni. Mbele yake alikuwa amesimama bwana Shao, yule jamaa wa karibu na Sheng. Yule jamaa aliyemshawishi Sheng kurusha ndoano kwenye zoezi lingine badala ya kuwamaliza wafanyakazi kwa kuwaua.

Japo ilikuwa ni usiku mkali, bwana huyu hakuwa amelala. Macho yake yalikuwa meupe na uso wake upo moto.

Alikuwa ameketi sebuleni. Usiku huu mzima alikuwa anakaa na kungoja kuja kupewa mrejesho wa zoezi aliloliasisi. Akiwa anategemea mambo yataenda bambam.

Ila kwa namna mtumishi huyu aliyemtoa ndani alivyokuwa anaongea, akaanza kupata shaka. Hata moyo wake ukaanza kuchanganyia kasi.

Haiwezekani akafeli! Haki Sheng hataelewa.

"Kuna nini?" Shao akauliza kwa lafudhi yake ya kimandarin. Macho yake madogo alikuwa ameyakodoa.

Basi mtumishi yule akajikaza na kusema,

"Kuna ujumbe wako ... kule!"

Ikachukua dakika tano tu, Shao akawa ameshajua yale yote ya habari za watu walioagizwa. Ya kwamba wameuawa, na wengine wakazimishwa fahamu.

Na ujumbe akaandikiwa kiooni, "Nenda kaukute ujumbe wako ndani ya kibanda cha mlinzi!"

Akavuta mafundo mawili ya hewa, na tayari ujumbe huo alioambiwa upo kibandani mwa mlinzi ukawa umewasili mkononi mwake. Kuna mtumishi alikuwa tayari anao mkononi.

Ulikuwa ni ujumbe wa maneno machache tu ukiwa umeandikwa kwenye kikaratasi kidogo, ukisema, "Tumepata antidote. Mmepata kifo!"

Shao akaghadhabika haswa. Dharau ya aina gani hii? Ina maana mtu alileta gari hapo, mosi, pili, akazama ndani ya uzio wao na kwenda kwa mlinzi, akaweka karatasi ndani ya droo!

Alafu ... alafu akatoka salama!

Shao akajihisi amevuliwa nguo. Na kwa bayana akatambua jambo hili likimfikia Sheng, hakuna atakayekuwa upande salama hata punje! Sheng hana moyo wa kubeba kejeli kiasi hiki! Ni mwepesi wa maamuzi. Ni mwepesi wa kushika hasira.

Basi bwana Shao akawaita watumishi kumi, akawaagiza wawazike wale watu upesi. Na wale ambao walikuwa amezirai, akawamalizia kwa kuwadunga risasi za kichwa akitumia bunduki yenye kiwamba cha kumeza sauti.

Akasihi jambo hilo liwe la siri mno. Na akatishia endapo likisikika basi ata-deal na hao watumishi kumi aliowapa kazi. Wahakikishe Sheng hajui lolote lile, na yeye anajua cha kufanya!

Wakatii agizo.

Makaburi yakachimbwa, watu wakazikwa kupumzishwa.

**

Asubuhi ya saa mbili ...

"Marwaa!" Sauti nyembamba iliita mlangoni baada ya hodi ya kistaarabu. "Dada anakuita!"

Marwa akafungua jicho moja na kuangaza. Bado alikuwa ana usingizi pomoni. Kwanini jua linawahi kuchomoza kiasi hiki? Alilalama.

Hapa karibuni amekuwa akilala robo usiku. Anachoka. Hii haikuwahi kuwa mfumo wa maisha yake hapo kabla. Yeye ni mtu wa kulala mapema, aghalabu huchelewa sana endapo akibanwa na kazi za hapa na pale, tena haizidi saa sita usiku.

Miranda anawezaje?

Akajikusanya na kuamka. Akajianda kwa muda mfupi na kisha kwenda sebuleni. Huko akamkuta Bwana BC na Miranda. Sebule nzima ilikuwa imejawa na moshi wa sigara za BC.

"Pole, naona bado umechoka!" Miranda alimpokea kwa tabasamu. Akashukuru. Akiwa anaketi, naye BC akampongeza kwa kazi aliyoifanya usiku wa kuamkia siku hiyo. Akashukuru tena.

Basi BC akamwambia kazi imeshakwisha. Ndani ya siku tatu tu, Jona atarejea kwenye hali ya kutia matumaini. Na pasipo kuzidi mwezi, atakuwa amesharejea kuwa Jona kamili.

Habari hizi zikamfurahisha sana Marwa. Akatabasamu mpaka gegoni. Ila BC akamwonya. Akamkumbusha yale makubaliano ya awali waliyoyaweka.

Atampatia Jona antidote, ila wataandikishiana makubaliano. Na atakuwa akitoa kidogo kidogo akitazama kama makubaliano yake yataheshimiwa.

**
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…