Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI II -- 37*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Kwa Lee halikuwa gumu hilo. Akaliafiki. Ila shida kidogo ilikuja pale alipoambiwa mtu wa kwanza wa kummaliza.

Alikuwa ni makamu wa raisi!

ENDELEA

Nieng akamwambia Lee kuwa makamu huyo wa raisi ndiye kikwazo cha kwanza katika mambo yao. Yeye ndiye amekuwa kibaraka wa Li family kinyume kabisa na serikali ilivyo. Amekuwa akichukua taarifa na mipango yao yote na kuifikisha mezani mwa familia ya Li.

Yeye ndiye ambaye amekuwa kiungo kikubwa cha Wu family kudhoofika ndani ya nchi na hata huko ulimwenguni.

Lee alitakiwa kummaliza mwanaume huyo pasi na simile hata kidogo. Ahakikishe habaki na uhai na hata kama kutakuwa na uwezekano basi familia yake nayo itokomee kisibaki kitu.

Hiyo itakuwa salamu mwanana kabisa kwa familia ya Li. Na kwa namna iliyo kubwa itawapa kimuhemuhe na joto miilini.

Ila Nieng akaenda mbele zaidi kwa kumwambia Lee kuwa kazi hiyo haitakuwa nyepesi kabisa maana makami huyo mbali tu na kulindwa na serikali kama afisa mkubwa, pia analindwa na ulinzi binafsi unaopewa nguvu na familia ya Li.

Inabidi awe makini sana. Ahakikishe hakuna kosa lolote linalotokea.

Basi Lee baada ya kupewa maelekezo hayo pamoja pia na anwani ya makazi ya makamu wa raisi akaenda kuonana na watu atakaofanya nao kazi. Walikuwa wengi mno, kadiri kama watu alfu mbili wenye mafunzo.

Ila kwasababu alitaka wanaume waliokomaa kimafunzo ili kazi ikawe rahisi na kwa ufanisi, basi akafanya 'interview' kidogo akisaidiwa na Nieng, wanaume wale wakapewa fursa ya kupambana wenyewe kwa wenyewe, mwishowe Lee akachagua watu watano wa kazi.

Akawataka waonane baadae usiku kwa ajili ya kuyapanga. Yeye akatoka kwenda kukagua makazi yale ya makamu wa raisi ambayo alikuwa amelenga kufanya tukio kesho yake.

Ilikuwa ni umbali uliomgharimu masaa maana kiongozi huyo alikuwa anakaa Beijing na si Hongkong. Alipofika huko akatumia tu macho yake kuchambua eneo, kwa dakika kumi, kisha akayeya.

Baadae usiku kama alivyopanga miadi akakutana na wale watu wake watano wa kazi, akaanza kuwapanga namna ya kuenenda. Ila wakiwa maongezini, shifoo Nieng akaingilia kwa kumhitaji Lee dakika chache.

Akamweleza kuwa mambo yamebadikika. Amepata taarifa kuwa kiongozi huyo hayupo nchini, amesafiri kikazi kwenda Mongolia, nchi jirani na China kwa upande wa kusini. Hivyo basi inabidi aende huko kufanya kazi, na pia itakuwa wepesi zaidi kwa maana ulinzi wake utakuwa hafifu.

Basi kwa maelezo hayo, Lee akaona ni kheri akaenda mwenyewe kutekeleza hiyo kazi. Ila Nieng akamwambia kuwa taarifa juu ya wapi anakaa huko Mongolia, haijapata. Ni jukumu la Lee sasa kuitafuta atakapokuwa huko.

Kumbuka ilikuwa usiku. Lee akiwa peke yake baada ya maongezi hayo alijikuta anaugawa muda wake wa kupumzika kwa kufuatilia mitandaoni ziara ya kiongozi huyo huko Mongolia.

Akagundua alienda kufungua balozi yao huko na pia miradi kadhaa. Kwa makadirio akaona kiongozi huyo atadumu ndani ya nchi hiyo kwa siku zisizozidi mbili. Hivyo basi kesho anatakiwa kumaliza kila kitu.

Atatumia njia za vichochoro kuzama ndani ya Mongolia, mosi kwasababu ya usalama. Anaenda kufanya mauaji huko, hakutaka kubakiza harufu yoyote maana endapo akitumia njia rasmi anaweza akatiliwa shaka na hata atakapotafutwa ikawa rahisi kupatikana.

Pili, hakuwa na nyaraka stahiki.

**

Baada ya Miriam kukaa nje kwa muda mrefu, shangazi yake alimfuata na kumjulia hali. Alikuwa na uso uliopooza na macho yanayohakisi mawazo kichwani.

Shangazi akamuwekea mkono begani na kumuuliza kama ni lile lile ndilo linalomtatiza. Miriam akatikisa kichwa kuafiki. Alikuwa anamuwaza Jona.

Hapa siku za karibuni hakuwa na furaha hata chembe maana hakuonana na mwanaume huyo. Na zile taarifa za kuhusishwa na kumuua Kamanda na pia tena kutoroka jela, zilimtia kimuhemuhe sana.

Alikuwa anahofia sana maisha ya Jona. Aliona si mtu anayestahili hayo anayoyapitia kwa namna alivyo mtu wa kujali. Na hata pasipo kusita, kwa moyo wake wote, alikuwa anaamini Jona hakuhusika na mauaji ya Kamanda kwa namna yoyote ile. Japo hakuwa anajua kuna mchezo gani nyuma ya pazia.

Anajiuliza sana Jona yupo wapi. Na ana hofu kama mwanaume huyo atakuwa mzima wa afya kwani kama ingelikuwa yu mzima, anaamini angelikuja kumtembelea na kumjulia hali.

Ila hofu haijengi.

Hofu yanyima kula hata kunywa. Yanyima amani. Na hichi ndicho Shangazi yake alikuwa anamweleza. Kuendelea kuwaza namna ile hakutamfanyia chochote chema zaidi ya kumuumiza.

Akamsihi waende ndani. Na kama chambo kitaungua, basi watasikia tu harufu. Kama Mungu alivyomlinda yeye alipokuwa mikononi mwa wale wadhalimu, basi ndivyo atakavyomlinda na Jona kama vile wanavyomwombea kila uchwao.

Wakaenda ndani.

Basi kama ni kheri hii ilikuwa ya asubuhi. Kwenye majira ya saa mbili asubuhi mlango ukagongwa shangazi akaenda kufungua. Akamkuta Marwa mlangoni.

Akapatwa na hofu. Hakuwa anamtambua mtu huyo. Akiwa amekunja sura akamuuliza Marwa nini anataka, Marwa akamtaka kwanza amwambie kama hapo ni makazi ya Miriam. Alipomjibu akamweleza kuwa ametumwa na Jona kufikisha salamu.

Basi shangazi akamruhusu Marwa kuingia ndani na kumkutanisha na Miriam. Akamweleza kuwa Jona anamsalimu sana. Alikuwa hoi na pindi alipopata ahueni akamuulizia na kumwelekeza aje kumwona.

Miriam akafurahi sana. Akataka kumwona Jona ila Marwa akamwambia haitawezekana kwa sasa. Na ahakikishe hilo jambo linakuwa siri kupita kiasi. Jona atakuja kumtembelea yeye mwenyewe atakapotengemaa.

Marwa hakukaa sana, akaaga aende zake. Ila Miriam akamtaka angoje kwanza. Akaingia ndani na kutoka na karatasi na peni, akaandika ujumbe na kumkabidhi Marwa ampelekee Jona. Akamsisitizia sana ujumbe huo ufike mikononi mwa Jona.

Marwa akamuahidi. Kisha sasa akaenda zake.

**

Saa tatu usiku ...

Jona alitabasamu punde aliposoma ujumbe wa Miriam. Hakika ulimgusa moyo wake na kumpa ahueni sasa ya kuwa mwanamke huyo ni mzima wa afya maana alikuwa anahofia huenda wakina Nyokaa wakawa wamefanya jambo kumdhuru.

Bado hakuwa na afya tenge, ila angalau kwa siku moja ya kutumia antidote, aliweza kutazama, kutambua na hata kunena. Pia kujisogeza huku na pale japo kichovu.

Alifurahi sana kumwona Marwa ni mzima. Kila saa alikuwa anamkumbatia kwa kutoamini. Alimshukuru pia na Miranda kwa kazi waliyofanya. Hata kabla hajaelezwa alikuwa anafahamu ni kazi kubwa imefanyika mpaka yeye kuwa pale.

Ila kutokana na hali yake bado kuwa si nzuri, Miranda na Marwa hawakuona kama ni muda sahihi wa kuanza kumchanganya mwanaume huyo mapema yote hiyo. Bado alikuwa anastahili kupumzika, tena sana.

Ndo maana hata huu ujumbe wake alikuja kuusoma saa hizi japo uliletwa kwa muda mrefu sana maana ndo muda aliofungua macho.

Marwa akamletea chakula na kisha akakaa naye kwa muda kidogo wakiteta. Akamuuliza kuhusu Miriam. Jona akamweleza kwa ufupi.

Marwa hakutaka kumpeleleza sana. Akatoa vyombo na aliporejea akamkuta Jona amekwisha lala. Antidote zilikuwa zinamchosha.

Basi akakaa pembeni yake na kuchukua ile karatasi ya Miriam na kuisoma. Akajikuta anatabasamu. Miriam alikuwa ana hamu sana ya kumwona Jona. Na akiapa siku hiyo itakuwa ya furaha sana kwake.

Marwa akaikunja vema hiyo karatasi, kisha akaiweka chini ya mto wa Jona. Akatoka chumbani.

Ila siku hii bado haikuwa imekwisha. Ndiyo kwanza ilikuwa imeanza. Kabla ya jua la kesho kuchomoza, kuna misheni mbili kubwa zilikuwa zinatakiwa kumalizika.

Mosi, Sarah kutambua kama Jona anaishi kwa Miranda. Na pili, Lee kummaliza makamu wa raisi ndani ya nchi ya Mongolia.

Litakalojiri, si mimi wala wewe anayejua. Ila ni wazi kiti kilikuwa cha moto.


**
 
Back
Top Bottom