*ANGA LA WASHENZI II --- 69*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
“Niliwaambia msimwingize ndani!” bwana Kulanga akafoka. “Ndani tumevamiwa, narudia ndani tumevamiwa!”
Ilikuwa ‘too late’ wanasema wazungu. Raisi alikuwa ameshazama eneoni. Kitendo tu cha bwana Kulanga kumaliza kuongea, umeme ukakatika! Eneo lote likawa giza kana kwamba ni chini ya handaki.
Hapa sasa wale wavamizi wakawa mithili ya majini!
ENDELEA
Basi katika hali hiyo ya giza na purukushani, maafisa usalama wakawa wanawasiliana na jitihada zao kubwa zikiwa ni kwenye kurejesha kwanza umeme ndani ya eneo. Nuru ilikuwa muhimu sana kwa wakati kama huo.
Lakini papo hapo wawe pia wanawasiliana kwa ajili ya kumdhibiti adui. Ila shida inakuja wapi? Utamdhibitije mtu usiyemwona? Mtu usiyejua yupo wapi?
Kurunzi kubwa zikawashwa na kumulika huku na kule, ila Ikulu ina eneo kubwa, bado haikutosha kutoa kile kinachohitajika haswa. Kwahiyo basi kwasababu hapa mlengwa mkubwa alikuwa ni Raisi, basi afisa wa usalama wakamzingira kumhakikishia usalama.
Wakati huo wengine wakiwa wanachakarika, aidha kwa kumtafuta adui ama kutafuta mwanga, wao wakawa wanahakikisha mkuu huyo wa nchi yupo kwenye mazingira swalama kabisa.
Ukapita muda kidogo. Bado purukushani zilikuwa zinaendelea, zavuma, hapa na pale. Katikati ya purukushaniyo, mara sauti ikasikika kwenye vitega sauti vya maafisa wa usalama ikionya,
“Hakuna kupokea amri kutoka kwa mwingine yoyote isipokuwa kwa mkuu peke yake …. Narudia amri, maagizo hutoka kwa Kulanga pekee … Kulanga pekee!”
Sauti hiyo ikakata. Zikapita kama dakika nne, mara sauti ya Kulanga ikavuma, “Mwingizeni Raisi kwenye chumba cha dharura. Haraka, chumba cha dharura!”
Basi baada ya amri hiyo, maafisa usalama nane wakiwa wanamziba Raisi wakaongozana naye mpaka chumba cha tatu ndani ya jengo Ikulu ambapo walimfungia Raisi humo na wakabaki maafisa watatu ndani yake, na watano kwa nje.
“Raisi yupo ndani? Raisi yupo ndani?” sauti ikauliza kwenye vitega sauti.
“Ndio, mkuu. Raisi yupo ndani. Narudia tena, Raisi yupo ndani.”
“Vizuri!”
Sauti ikakata na kisha kuwa kimya kwa wale maafisa waliokuwa beneti na Raisi, na hata wale ambao wamekaa nje mlangoni.
Lakini huko upande wa pili, mambo hayakuwa mambo. Watu walikuwa wanauawa kwa bunduki zenye viwamba vya kumezea sauti. Damu zilikuwa zinamwagwa kana kwamba jinamizi lenye nguvu pagani limeshuka kwenye uso wa dunia. Maiti zilikuwa mahali kadha wa kadha na ubaya ni kwamba hakuna mtu aliyekuwa anafahamu wauaji wapo upande upi wa dunia!
Walikuwa si watu wa kutuama. Walitumia paa, walitumia silaha ndogo ndogo zisizo na madhara ya sauti. Walitumia maarifa na ujuzi wao kwa hali iliyotukuka kabisa. Ilikuwa inashangaza kwa namna ambavyo watu wachache walivyokuwa wanasumbua wale walio wengi.
Mpaka ‘backup’ iliyoombwa kuja kutoa msaada iwasili, basi uharibifu mkubwa utakuwa umetokea hapa.
“Afisa afisa …. afisa afisa…” bwana mmoja alibweka. “Taa zimezimwa zote, imebaki moja tu! Zimezimwa zote imebaki moja tu!” Taarifa ikatolewa na kusambazwa. Kurunzi zote zilikuwa zimezimwa kwa kupasuliwa na watu ambao hawakuwa wanaonekana.
Sasa ilikuwa imebaki kurunzi moja tu iliyo kubwa! Zingine zilikuwa zimegeuzwa kuwa ‘skrepa’ kwa kutobolewa na vifaa vidogo vya vyuma vyenye ncha kali mduara.
Hakuna aliyewaona watu waliotupa vifaa hivyo. Na kwa namna hiyohiyo ndivyo ambavyo watu walikuwa wanauawa. Wengi wao walikuwa wanakutwa wakiwa wametobolewa vifua, shingo au vichwa vyao kwa vifaa vyenye sumu kali iliyokausha miili ya wahusika kwa haraka mno.
“Afisa … Afisa!” sauti ikaita. “Afisa Kulanga amekutwa ameuawa na kupoa … narudia, amekutwa akiwa ameuawa na kupoa!”
Habari hizi zikazidi kuwachanganya maafisa. Lakini zaidi kuwatia hofu!
Mara ya mwisho Kulanga anaonekana ilikuwa ni ndani ya chumba cha kuangazia taswira za CCTV. Huko alikuwa na wataalamu wanne wakiwa wana ‘monitor’ mipango ya kuhakikisha jengo zima linakuwa linaangazwa.
Lakini muda mfupi kabla ya Kulanga kuuawa, kamera zilianza kupoteza mwelekeo. Zilianza kugomagoma na aidha hata kurudia picha. Na kabla tatizo halijafanyiwa kazi, mara kamera zikakaa vema. Kumbe ulikuwa ni mchezo wa mapumbazo.
Ulikuwa ni mchezo wa ulaghai! Na kweli mtegwaji akazama anapotakiwa kuzama.
Ni hivi, wakati video hizo zasumbua, ‘attention’ za watu zilihama. Macho na masikio yao yalikuwa yanaangazia kwenye video na namna ya kukabili tatizo. Kumbe basi mlango unafunguliwa! Hawakujua mlango ulifunguliwaje, kwa kutumia nini, ila wanakuja kutahamaki kuna mtu mlangoni.
Hawajafanya jambo, wakaona vitu vipo hewani, navyo hawakuwa wanajua ni vitu gani, ila wakaja kuvijua baada ya kutua kwenye miili yao. Vilikuwa ni vyuma vyenye ncha na sumu! Japo vyuma hivyo vilitupwa vingi, havikumgusa Kulanga isipokuwa tu kuuchanja mkono wake wa kuume uliobebelea silaha, hivyo akadondosha silaha yake na kuwa mtupu!
Hapo wenzake wote wakiwa tayari wamehamia ulimwengu wa wafu. Walikuwa tayari wamehudumiwa na zile silaha ipasavyo.
“Now we are going to do it by my rules if you want to live, officer,” sauti ya mvamizi ikaruruma. Bwana Kualnga kabla hajataka kuleta ubishi, akatazama mkono wake uliochanjwa. Ulishaanza kubadili rangi kuwa wa zambarau!
***
Afisa usalama wakatazamana. Habari ya kuwa Afisa Kulanga amekutwa mfu iliwatibua akili. Hapa wakapata shaka, mmoja akagonga mlango na kuuliza kama waliomo ndani wako salama. Hawakupata majibu!
Wakagonga zaidi na zaidi, bado kulikuwa kimya. Na kwasababu basi ya kuimarisha usalama, wale maafisa waliokuwemo ndani walikuwa wameufunga vema mlango. Kumbuka hiki kilikuwa ni chumba cha dharura endapo hatari itajiri ndani ya Ikulu hivyo kilikuwa kimesanifiwa katika namna ya ulinzi.
Mlango ulikuwa mzito na makufuli yake yalikuwa kana kwamba vile visanduku vihifadhivyo vitu vya thamani. Si ya kuvunja kwa wepesi hata kidogo.
Basi mabwana hawa, ambao tayari wameshahisi mambo hayako sawa, wakaanza kuhangaikia mlango, na huku wakitoa taarifa juu ya hali waliyomo ili wapate msaada.
***
Ilikuwa ni muda mfupi sasa tangu waone kazi huenda ikawa imekamilika. Basi wakawasiliana na kupanga kutoka ndani ya eneo la Ikulu haraka iwezekanavyo.
Kila mmoja akiwa kwenye ‘angle’ yake wakachoropoka na kukutania upande wa mashariki ya Ikulu. Muda huo sasa vikawa vinaingia vikosi vingine vya wanajeshi na hata maafisa wengine wa usalama.
Wavamizi walipoukaribia ukuta, wakaanza kuchumpa kujikuta nje dhidi ya ukuta mkubwa wa Ikulu walioufanya watakavyo. Wakiwa wamebakia wawili ndani ya eneo la Ikulu, wakaonekana!
Wanajeshi watatu waliokuwa wamebebelea bunduki mikononi, wakawaonyeshea silaha na kuanza kuwafyatulia risasi. Risasi zikaruka kama kumi hivi, na miongonizo zikafanikiwa kumwangusha mmoja wa wavamizi wakati mmoja akifanikiwa kuchumpia nje.
Ila naye alikuwa amejeruhiwa! Alikuwa anakimbia akivuja damu.
Wakaliendea gari lao na kujipaki upesi. Kuwasha gari, halikuwaka! Wakawasha na kuwasha. Bado hakukuwa na amfanikio. Ilikuwa ni hatari mno kubakia hapo kwa usalama wao. Eneo hilo lilikuwa limechafukwa. Lilikuwa ni eneo ambalo lipo ‘busy’ kuliko eneo lolote lile nchini kwa muda huo.
“What’s wrong!” akauliza Denmark, sauti yake ilimtambulisha. Alikuwa anauliza kana kwamba kuna mtu anayejua kinachoendelea hapo ukizingatia yeye ndiye alikuwa dereva.
Alijitahidi sana kuwasha gari pasipo mafanikio. Walipoona wanapoteza tu muda hapo, wakashuka. Kabla hawajaenda popote, wakawa wamezingirwa na watu watatu waliovalia barakoa na kubebelea silaha za moto. Wakapewa na amri ya kunyoosha mikono juu upesi!
Lakini hapahapa, tena ikiwa ni kama sekunde kadhaa tu toka wavamizi wawekwe chini ya ulinzi, vikasikika vishindo vya watu! Mara, “Wale pale!”
Risasi zikaanza kutupwa kwa fujo kuwalenga wavamizi pamoja na wale waliowaweka wavamizi chini ya ulinzi!
***