Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI --- 35*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

“Jona,” Mheshimiwa akaita. “Achana na yote yaliyopita. Najua kuna mambo ambayo yalitokea hapa kati, nisingependa kuyaongelea kwa sasa maana si muda muafaka. Nimekuja hapa maana nina shida na ninahitaji tena msaada wako.”

Jona alikuwa kimya akimtazama. Mheshimiwa akameza kwanza mate, alafu akasema:

“Nade ametekwa, naomba unisaidie kumuokoa.”

ENDELEA

Ni kama vile Jona alikuwa anategemea kauli hiyo kwani hakushangazwa hata kidogo. Alikunywa fundo moja la mvinyo ndani ya glasi alafu akaendelea kumpatia atensheni mgeni wake.

“Utahitaji kiasi gani?” mheshimiwa akauliza akichojoa pochi yake mfukoni.

“Sitahitaji pesa yoyote toka kwako,” akasema Jona. Na kisha akaongezea: “Ninachohitaji toka kwako ni taarifa tu ya yale unayonificha.”

“Yapi hayo?”

“Kwanza kwanini unataka kuniua?” Jona akauliza akimkazia macho Mh. Eliakimu. Swali hilo likamshtua muulizwaji, akajitahidi kulimudu akiwa tayari amechelewa kwani Jona alimshasoma.

Kama haitoshi, Jona akataka kujua kwanini Nade alikuwa anamfuatilia na kwasababu gani haswa alikuwa anamtafuta mkewe. Maswali hayo yakamfanya mheshimiwa akose cha kunena.

Hakuwa amejiandaa nayo, na kutafuta ahueni akamwambia Jona kwamba watatafuta siku waongee vizuri kila kitu. Kauli ambayo kwa Jona haikuwa na uzito, ila akaridhia kwa kuona hamna haja ya kulumbana. Mheshimiwa alikuwa ni ndege wake, ahitaji kumshikia manati.

“Sawa, hamna shida,” Jona akajibu. “Nitafanya.” Ndani ya moyo wake alikuwa ana nia ya kumsaidia Nade, lakini pasipo kumsahau na Miriam kwa wakati huo huo.

“Na vipi kuhusu Miriam?” akauliza. Mheshimiwa akamjibu kuwa watu waliomteka Nade wanamtaka Miriam kubadilishana na Nade. Jona akataka kujua zaidi juu ya hao watu, ila Mheshimiwa hakuwa na majibu ya kumpa. Yeye mwenyewe hakuwa anajua lolote kuwahusu.

Kwahiyo Jona akawa amepata kibarua kingine, kuwachambua na kuwajua hao watu. Kutopoteza muda zaidi, akakubali kufanya kazi na kumtaka mheshimiwa akapumzike.

“Una hakika auhitaji chochote toka kwangu?” Mheshimiwa akauliza tena. Hakuwa anajua ni namna gani Jona atawapata hao watu ukizingatia hajamuuliza chochote, wala kutilia shaka lolote.

Na akasita kuuliza. Kifuani akizoza kwani yeye shida yake nini wakati ameambiwa kazi itafanywa? Akajikusanya na kuondoka zake akitingwa kichwani. Akajiweka kwenye gari na kuondoka toka eneo hilo.

“Ni lazima nimpate huyu jamaa,” akajisemea peke yake kifuani. “Endapo nikiwa naye hakika mambo yangu yataenda vema.”

Safari nzima akawa anawazia kwa namna gani angekuwa na Jona, jinsi mambo yake yangemalizika kwa wepesi na kwa uhakika. Vipi kama akiwa na Nade na Jona kwa wakati mmoja? Hatakuwa na haja ya kumiliki jeshi. Maadui zake wataona cha mtemakuni.

Basi akajikuta anatabasamu kwa taswira yake hiyo ambayo alitamani iwe uhalisia.


***


Saa mbili asubuhi…


Bodaboda ilisimama nyuma kidogo ya fremu, akashuka Jona na kuvua kofia ngumu na kumpatia dereva kisha akamlipa. Akaenda zake ofisini na kumkuta Jumanne akamsalimu na kumwambia hayupo hapo kwa muda mrefu, amepita maana ameona ana haja ya kumpasha habari.

“Sitakuwepo hapa kazini kwa muda, kuna ishu fulani nafuatilia. Sawa?” Jona alisema. Jumanne akastaajabu kidogo, haikuwa kawaida. Akauliza nini shida.

Jona akasisitizia tu kwamba kuna ishu anafanya ila haitakuwa milele. Atarejea.

"Hakikisha kila kitu kinakuwa sawa. Tutakuwa tunawasiliana. Sawa?"

"Poa." Jumanne akajibu kishingo upande. Alikuwa anawazia ni kwa namna gani atakavyokuwa mpweke. Japokuwa hapa karibuni hakuwa pamoja na Jona ila kitendo cha kupewa taarifa rasmi kuwa hatakuwepo tena kwa muda usiojulikana, Jumanne akafadhaishwa.

Jona asipoteze muda, akayeya! Sasa alikuwa yupo katika hatua nzuri ya kupotea kwenye mazingira yake zoefu. Yote haya kwasababu ya kutengeneza mazingira bandia ya kifo chake.

Lakini pia kujipa muda wa kutenda mambo yake kwa ufanisi zaidi.
Alishatafuta mahali pia pa kuishi tofauti na makazi yake ya kila siku. Kila kitu kilikuwa kinaenda kwa mujibu wa mipango karatasini.

"Karibu," akasema Jumanne akimtazama mgeni wake aliyekuwa amesimama mlangoni. Japokuwa bidhaa zilikuwa zimejaa, nyingi, Jumanne alimwona mwanaume huyu mrefu mweusi.

Alikuwa amevalia suti ya kahawia iliyomzidi ukubwa kidogo. Alimtazama Jumanne na kisha akazama ndani baada ya kuhakikisha yupo mwenyewe.

Mwanaume huyu ni nani? Akatazama bidhaa ya kwanza na ya pili, kisha akatazama tena nje. Akasogea akizama ndani ya duka. Jumanne alikuwa pembeni yake akisubiria kutoa maelezo pale yatakapohitajika.

Lakini mteja huyu hakuuliza kitu! Akaendelea kukagua bidhaa. Alipomalizikia ndani ya duka, akamnyaka Jumanne na kumminyia kwenye mikono yake minene meusi kumkaba!

Jumanne akafurukuta kutetea uhai wake kwa hali na mali, ila hakufua dafu! Mwanaume huyu aliyemkaba alikuwa mkufunzi wa hili tukio haswa!

Alikuwa amejawa na nguvu na sanaa ya mauaji. Jumanne akaishiwa na nguvu na mwisho wa siku akatulia tulii kukubali sheria!

Mwanaume huyo akahakikisha kama amefanikiwa kisha akahepa zake mara moja kupotea eneo hilo. Alijipaki kwenye pikipiki ambayo ni wazi ilikuwa inamngojea yeye.

Wakayeya!


***


Saa kumi jioni...


"So what did yo do?" (Kwahiyo ulifanyaje?) BC aliuliza.

"I did nothing. I asked her to wait," (sikufanya kitu. Nilimwomba angoje,) akajibu Miranda.

"Thats good of you! But dear, we have nothing to do here except accepting it." (Hilo ni jema! Lakini mpenzi, hatuna cha kufanya hapa zaidi ya kukubali.)

"And what about th...." (Na vipi kuhusu ....)

"https://jamii.app/JFUserGuide those excuses! Jus do it." (Acha hizo sababu! We fanya tu.) BC akasema kisha akakamata kinywaji chake, John Walker, na kumiminia kinywani.

"Go do that commercial. I will handle the rest." (We nenda fanya hilo tangazo. Nitashughulikia mengine.) Akasema kwa kujiamini.

Miranda akatikisa kichwa chake alafu akashika simu yake na kuitazama. Swala hilo lilikuwa limeshaisha. Ilibidi afanye ile interview kama ambavyo mke wa Boka atakavyo.
Ilibidi akajianike mbele ya kamera na yote hayo kwasababu tu ya kuhakikisha hiyo dili yake na mke wa Boka inatimia.

Kukawa kimya kidogo. Mazingira ya ufukweni walipokuwepo yalikuwa tulivu. Upepo ulikuwa unapuliza na hakuna kingine chochote kinachosikika.

Ukimya huo ukavunjwa na sauti ya BC punde baada ya kunywa kidogo kinywaji chake glasini.

Alimuuliza Miranda kama amesumbuliwa na Eliakimu hapa karibuni. Miranda akatikisa kichwa chake kukataa. Hakuwa na mawasiliano na mwanaume huyo tangu siku wakutane.

Habari hizo zikamfanya BC awaze kidogo. Eliakimu atakuwa anapanga nini na ukimya wake huu? Akanywa mafundo kadhaa ya Walker akiwa anawaza. Aliona kuna hitaji la kujua Eliakimu ana mpango gani, akamshirikisha Miranda.

"We don't need to bother. Let us wait for his step first," (Hatuhitaji kusumbuka. Ngoja tuone hatua yake kwanza.) Akasema mwanamke huyo.

Lakini vipi kama hatua hiyo ikawa na hatari kwao? Swali lilikuja hapo. Tahadhari ikaonekana kuhitajika. Miranda asirefushe mada, akapendekeza kuwasiliana na Eliakimu kama njia ya kumchokonoa.

Ila swala hilo akapendekeza lifanywe na BC.

BC akakaa kimya kwa muda. Akaendelea kunywa na kunywa akiyapanga kichwani.

Fikra zake zilienda mbali sana akiwazia na mzigo wao wa kemikali ambao upo tayari, unangoja tu amri ili upate kuja. Kukaa kwake bandarini kunazidi kuchojosha pesa, na huku bado hakujaeleweka. Afanye nini?

Akakuna kidevu chake akiendelea kuyapanga. Hamna namna BC, ni kurudi kwa Eliakimu tu! Hapana, sirudi huko kwani gharama zake zinawiana na gharama za mzigo kabisa! Sasa tufanyeje na huku Boka bado hajawekwa kwenye mstari?

Akaendelea kuyapanga akizoza na nafsi yake.

Boka lazima akalishwe. Lazima ajaribiwe kama mkono wake utakuwa mwepesi kuenenda na kutenda. Na udhaifu wake ni Miranda.

Miranda inabidi atumie mwili na akili yake kufyatua bomu hili mara moja! Ila pia na hekima yake ni jambo la msingi hapa.

"Miranda," BC akaita. "Accept the man, Boka, and tell him that I wana see him," (Mkubalie huyo mwanaume, Boka, na umwambie nataka kumwona.)

Mchezo ukapangwa namna ya kwenda. Miranda amwambie Boka kwamba amemkubalia ila 'baba' yake angenda amwone na wajadili mambo kadhaa juu ya mahusiano yao.

Na hapo ndipo BC atakapotumia 'ubaba' wake kumminya na kumkamua Boka kama kweli anamhitaji 'mtoto' wake kama mpenziwe.

Hapo ndipo Boka ataelezwa juu ya shida za 'mkwe' wake na kuzitimiza iwe ndiyo kama mahari. Kama kipimo cha upendo wake kwa mwanamke huyo mrembo, Miranda.

Waliamini tamaa ya kimwili ya Boka, itazima uwezo wake wa akili. Hatafikiria kwa kichwa chake cha juu, bali kile cha chini.

Na hapo, ndipo mcchezo utakapokuwa umeishia.


***


Saa moja jioni...


"Una uhakika ndiyo hapa?" Akauliza Mustapha akinyooshea kidole getini. Alikuwa ameongozana na mwenzake aitwaye Bilali, mwanaume mfupi ambaye uso wake umejawa na majeraha.

Mwanaume huyu alikuwa ni miongoni mwa wale waliopokea vichapo toka kwa Nigaa na Lee. Sasa wote walikuwa wamesimama mbele ya nyumba ndogo iliyozungushiwa uzio, yenye rangi nyeupe na kupendezeshwa na bustani.

"Ndio, ndiyo hapa!" Akasema Bilali akitikisa kichwa. Alafu wakagonga na kutulia hapo. Baada ya muda akafungua mwanaume fulani aliyekuwa amevalia bukta na kaushi ya zambarau. Alikuwa amesokota nywele zake zikisimama kama miba.

Akawauliza wageniwe namna gani angewasaidia.

"Tunahitaji kumwona bosi wako," akasema Bilali.

"Bosi ametoka," wakajibiwa kwa ufupi.

"Ametoka?" Bilali akastaajabu. "Mbona aliniambia atakuwepo mida hii mzee?"

"Sijui, ila hayupo. Ametoka," akasisitizia mwenyeji.

Lakini kabla wakina Mustapha hawajaondoka, ikaja gari hapo, Alphard nyeupe yenye vioo vyeusi. Wakasimama na kutazama. Kioo kikashushwa na akaonekana mchina mmoja mwanaume. Akawasalimu kwa kuwapungia mkono.


"Ndiyo huyo hapo sasa!" Balali akamwambia Mustapha. Wote wakajikuta wanatabasamu.


***
 
Nashukuru sana mkuu kwa kukubali hii kazi. Inanipa hamasa zaidi
Hongera sana mkuu hakika we ni mkali hakika nakuombea kwa maulana akupe kadiri ya kiu yako,endelea na ustaarabu wako wa kutokua na mapozi ya kishamba na kuvimba kichwa km wengine!keep it up young bro!
 
Hongera sana mkuu hakika we ni nkali hakika nakuombea kwa maulana akupe kadiri ya kiu yako,endelea na ustaarabu wako wa kutokua na mapozi ya kishamba na kuvimba kichwa km wengine!keep it up young bro!
Ni wewe ndio umeandika au kuna mtu amekuandikia
 
Back
Top Bottom