*ANGA LA WASHENZI --- 37*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
“Asilimia mia nane, nina uhakika. Inaonekana anamzimia sana huyu malaya wake. Atajileta tu.”
Kukawa kimya kidogo.
“Ila unajua nini Nyokaa, tukimpata tena yule manzi, tujitahidi kumaliza ile ishu mazee. Unajua yule manzi anaweza akawa ametoboa gunia letu la mchele huko kama alivyotoboa la yule boya?”
“Sidhani asee. Namwamini sana yule manzi.”
“Hapo ndipo unapofeli sasa, unamwanijie manzi kiasi hicho Arif?”
ENDELEA
“Najua Miriam ananipenda na yupo radhi kufanya jambo lolote kwa ajili yangu. We unajua ni mangapi yule manzi amefanya kwa ajili yangu?” akauliza Nyokaa. Kabla hajangoja majibu, akaendelea kumwaga sera:
“Amenifanyia mbishe mingi sana asee kabla haya mafyoko hayajatokea hapa kati. Unadhani angekuwa manzi mwingine akithubutu?”
Mwanaume yule mweupe, kwa jina Roba, akatikisa kichwa alafu akashusha pumzi yake akitazama kando. Kuna jambo alikuwa analifikiria, na punde akamshirikisha Nyokaa.
“Unajua mishe zetu, mwanangu. Za hatari kinoma, inabidi tuwe macho sana kuangaza kama kuna snitch, la sivyo tutaharibu kila kitu.”
“Najua,” akajibu Nyokaa kwa ufupi. Na hakutia tena neno lingine kukiwa kimya kwa muda wa kama dakika tatu.
“Umeshandaa kila kitu lakini?” Nyokaa akauliza.
“Kila kitu kipo tayari yani, ni huyo mgeni tu aje.”
Baada ya hapo kimya kikawa kingi.
***
Saa sita mchana.
Chumba SPACE BUTTON
“Naweza nikapata kikombe cha kahawa?” alisema Panky akimtazama Moderator.
“Cha ngapi sasa?” Moderator akauliza kwa lafudhi yake ya kichina.
“Sijui idadi,” akajibu Panky. “Naomba tu uniletee kama hutojali.”
Moderator akasita kwanza na kumtazama Panky. Panky akatabasamu kabla hajageukia tarakilishi yake na kuendelea na kazi aliyokuwa anafanya. Moderator akatoka nje.
Basi haraka Panky akamtazama Marwa. Mwanaume huyo alikuwa yupo mbali naye sana, kitu ambacho kilikuwa kinamkera si kidogo. Alinyanyuka upesi akamfuata na kumsabahi, na pasipo kupoteza muda akamwambia asome jumbe zake ambazo amemtumia kwenye mashine.
Kuepusha kukutwa na Moderator, upesi akarejea kwenye kiti na kuendelea na kazi yake. Na kweli, punde Moderator akatokea akiwa amebebelea chupa kubwa rangi ya bluu. Akaiweka mezani mwa Panky.
“Hiyo hapo, hautasumbua tena sasa!”
Panky akashukuru kwa tabasamu, akajimiminia kinywaji na kunywa akiendelea na kazi. lakini akili yake ikiwa inamuwaza Marwa kama kweli ameelewa kile alichomwambia.
“Kile kichwa kigumu nacho,” alisemea kifuani. Akavizia pale Moderator aliposogea kando, akashusha kazi zake zote chini, alafu akafungua application fulani iliyokuwa na kialama chenye rangi nyekundu, akaandika:
“Unanipata?” alafu akatuma kwenye tarakilishi aliyoitunza kwa jina la M-Spy.
Alipotuma ujumbe huo, akamtazama Marwa kwa wizi, punde naye Marwa akamtazama. Alafu akabofya keyboard.
“Ndio, nakupata. Unataka nini Panky?” Ujumbe ukaingia kwenye tarakilishi ya Panky. Panky akatabasamu kwanza kabla ya kujibu. Alifurahi sasa maana alikuwa amepata ‘chobingo’ ya kuteta na mtu wake. Nafasi adhimu hii.
Panky: sina ishu mpya, ni kuhusu tu ile picha.
M-Spy: Imefanyaje? Kwani hukunielewa?
Panky: Unajua nini Marwa, niliipenda sana ile picha. na nilivyoenda kufanya ile misheni niliyoagizwa, nikajikuta nakumbana nayo. Sidhani kama ni vibaya nikajua maana yake.
M-Spy: Panky, acha ujinga.
Panky: Kivipi? Nataka kuuondoa huo ujinga kwa kujua.
M-Spy: Nikukumbushe mara ngapi kwamba hatutakiwi kushirikiana kwa vyovyote tukiwa kazini mpaka pale Mode atakapokuwa anajua?
Panky: Marwa, acha kujifanya bingwa wa kufuata sheria. Ni mara ngapi huwa nakusaidia mambo yako? Huwa unamuita Mode?
Kimya.
Panky akatazama upande aliopo Marwa, akamwona Moderator akiwa amesimama kandokando ya mwanaume huyo. Moyo ukamlipuka kwa kudhani huenda pamebumburuka. Lakini alivyotazama vema akagundua, Marwa alikuwa tayari ameshatoa yale maongezi yao na yupo bize kufanya kazi.
Basi naye kwa muda akazama kazini mpaka baada ya dakika kama tano alipopata ujumbe toka kwa Marwa.
M-Spy: Tukutane wakati wa chakula!
Panky: Poa.
Kazi zikadumu mpaka majira ya saa nane, watu wakafunga kila kitu kwa ajili ya kwenda kutia kitu tumboni. Huko Marwa na Panky wakakutana na kuteta mambo kadhaa kuhusu ile picha. Cha kushangaza ni kwamba, hata Marwa mwenyewe hakuwa anajua nini kimo pichani!
Lakini data alizokuwa amepewa kuzitumia kufuma ile picha zilikuwa ni za kushangaza na zenye kuhitaji mafikira kung’amua.
“Nashukuru sana, Marwa. Nadhani ingekuwa vema kama ungelinitumia picha hiyo kwenye tarakilishi yangu,” alisema Panky akijua wazi pale hawana muda mrefu wa kujadili.
Marwa akatabasamu.
“Unajua hilo jambo haliwezekani, Panky.”
“Inawezekana.” Panky akamkatiza. “Nimetengeneza code ya kuniwezesha kuwasiliana na kila tarakilishi mule ndani. Nina application za kuniwezesha kutengua security na kupokea ama kutuma faili kwa yeyote ndani ya chumba.”
Marwa akastaajabu.
“Umewezaje kufanya hivyo?”
Panky akatabasamu.
“Huu si muda wa kujadiliana, Marwa. Unajua muda wetu hapa.”
“Sawa, ila unajua tarakilishi yangu haina uwezo huo kama wako. Sasa natumaje?”
“Ngoja n’takuonyesha. Wewe kuwa karibu na messenger tu, sawa?”
Wakamaliza kula na kuondoka. Wakafanya kama vile walivyoelekezana, na Panky akafanikiwa kupata picha na maelekezo yote ambayo Marwa aliyatumia kufuma picha hiyo. Basi tabasamu likajaa usoni.
Ila muda si mrefu, akashikwa bega na Moderator, akatazamwa na uso mgumu na kisha akaamriwa:
“Simama!”
Utumbo ukamtetemeka na kichwa kikaanza kumgonga! Watu wote ndani ya chumba wakamtazama. Ila Marwa akiwa anatamazama kwa woga zaidi!
Bila shaka alijua sasa kila kitu kimeanikwa wazi! Mwisho wao ulikuwa umewasili, kifo kinawaita. Marwa akajuta kwanini alifanya ujinga ule.
Moderator akakaa kwenye kiti cha Panky na kuanza kupekua tarakilishi hiyo. akachukua muda wa dakika tano kabla hajanyanyuka na kumtaka Panky aketi chini. Hakuna alichokigundua!
“Unaweza ukaendelea na kazi yako!” akasema Moderator.
Panky akaketi akiwa haamini.
Lakini baadae akajiona ‘jembe’ kwa namna alivyotengeneza mfumo wake madhubuti kiasi cha kumfanya mtaalamu asipate chochote ndani ya mashine yake.
Akajikuta anatabasamu akipekua pekua tena tarakilishi yake. Kila jambo lilikuwapo kama alivyoyaweka.
----
Saa kumi jioni:
Panky anachomoa simu yake mfukoni na kumtafuta Jona. Simu ikaita mara tatu pasipo majibu. Akasonya na kujiuliza atakuwa wapi.
Alikuwa ameshatoka kazini na akiwa tayari amebebelea flashi ambayo ina faili nyeti la ile picha.
Alikuwa ameketi nyumbani kwake, sebuleni, akitafakari. Mkewe akaja akitokea dukani.
"Vipi mbona una mawazo hivyo?" Akauliza mwanamke huyu mweupe mwembamba aliyevalia kofia ya kuziba nywele pamoja na dera la njano lenye maua mekundu mekundu.
Panky akamlaghai mkewe kwamba yupo sawa na angependa apate muda kidogo wa kutafakari peke yake.
"Unataka nikuache, sio?" Mke akauliza kwa shari. "Yani hapa nyuma uliniacha peke yangu, sikujua wapi ulipo na unafanya nini, leo upo hapa nakaa na wewe unataka nikuache?!"
"Si hivyo mpenzi!"
"Ni vipi? - haya kaa basi mwenyewe!" Mwanamke akanyanyuka na kwenda zake. Panky akabakia kumtazama.
Ila mara na simu ikaita, kutazama alikuwa ni Jona.
"Nimekutafuta sana mzee vipi? ... ishu gani hiyo? ... serious? ... pole sana kaka, sasa inakuaje? ... yah! Nimepata ile kitu sasa ndo nikawa nataka tukutane uione kama vipi ... poa, basi utanshtua au sio? ... haya baadae!"
Simu ikakata. Panky akachomoa flash mfukoni mwake na kuitazama. Akanyanyuka na kwendaze chumbani.
***
Saa moja jioni.
Ngo! Ngo! Ngo!
"Naona ameshafika, acha nikachonge naye!" Glady aliwaambia wenzake wawili aliokuwa nao chumbani kabla hajanyanyuka na kwenda mlangoni.
Alikuwa amevalia gauni fupi la njano lililoacha miguu yake uchi. Nywele zake alikuwa amezikusanyia ndani ya kiremba cheusi cha kulalia.
Alitoka nje akamkuta Mustapha. Alikuwa amevalia shati la buluu, suruali ya kaki na raba nyeupe. Mwanaume huyo akamtaka wakaongelee ndani.
"Kuna watu, tuongelee tu hapa hapa!" Glady akasisitiza. Mustapha akatazama kushoto na kulia kwake kama kuna usalama. Uso wake ulikuwa una mashaka.
"Mustapha, kuna nini?" Glady akauliza. Alihisi kuna mambo hayapo sawia.
"Naomba niingie ndani!" Akasisitiza Mustapha. "Tafadhali!"
Kabla hata Glady hajajibu, Mustapha akazama ndani na akaurudishia mlango yeye mwenyewe. Akashika kiuno na kushusha pumzi. Glady akamtazama na kumuuliza nini shida mbona anamtia woga!
Mustapha akamwambia hayupo salama, kuna mtu anataka kummaliza!
"Nani huyo?" Glady akawahi kuuliza. "Yule mchina?"
Mustapha akatikisa kichwa. Akasema muuaji huyu hamjui, amemkosa kosa na risasi akijaribu kujiepusha kwa kupitia mlango wa nyuma!
"Mustapha, upo serious?"
"Kabisa! Na hapa ninavyoongea na wewe, Bilali ameuawa tayari!"
Glady akatoa macho ya mshangao. Na hapo akawa amevaa hofu nyeusi kiasi kwamba akamshangaa Mustapha kuja hapo ilhali ana songombingo la kumwaga damu!
Vipi kama akiwaambukiza tatizo?
"Sikuwa na kwengine pa kwenda, Glady. Naomba unisaidie hifadhi," alisema Mustapha kwa huruma. Haraka Glady akaenda dirishani na kutazama huko nje.
Akateta na wenzake wakiwa katika hali ya taharuki.
"Mustapha, utakuwa umefanya nini saa hii?"
"Sijafanya kitu, ila nahisi atakuwa ni yule mchina tuliyempelekea ile nyaraka atutafsrie. Anatuzunguka, anataka kuichukua!" Alisema Mustapha. Jasho lilikuwa linamtiririka.
Akamweleza Glady kinaga ubaga walivyoenda kuomba msaada kwa yule mchina ambaye aliwapa lifti kuwarejesha nyumbani.
Wakiwa taharukini, wanasikia mlango unagongwa! Glady anamtazama Mustapha, kisha anawatazama wenzake waliokuwa kitandani.
****
Ati ni nani?