Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI -- 60*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Huwa anawakumbuka, lakini leo hii ilikuwa ni kana kwamba ametoka kushuhudia jengo lake likiwa linateketea. Alphonce alimkumbusha kwa kina. Alikitifua kidonda kilichojenga gamba.

Akashindwa hata kupekua mafaili yale, akabaki anakunywa tu. Baada ya kuongeza mafundo matatu tu ya Bacardi, kichwa kikashindwa kuendeleza kazi, fahamu zikakata, akajimwagia kochini!

Jinamizi lililokuwa linamtesa, leo likarudi kwa nguvu zote.

ENDELEA

Saa tatu asubuhi, SPACE BUTTON.

Kulikuwa bize kama ilivyo ada. Watu walikuwa wanatazama vioo vya tarakilishi zao huku vidole vikitwangatwanga 'keyboard'. Watu hawa kwa idadi walikuwa nane, hakukuwa na mwanamke hata mmoja.

Mazingira yalikuwa tulivu ukiachana na sauti za keyboard. Hakukuonekana kama kuna shida yoyote, wala kama inaweza kubashiriwa kwa hapo mbeleni.

Hali ya hewa ilikuwa baridi, viyoyozi vilikuwa moto. Kuna baadhi yao wakawa wanavuta vikamasi na huku pua zao zikiwa nyekundu kwa kuzifikichafikicha mara kwa mara.

Pengine baridi lilikuwa kali kuliko siku zingine. Mmoja akapaza sauti kumuita Moderator na kumtaka apunguze kasi ya viyoyozi hivyo la sivyo watakufa.

Kidogo zogo likatokea hapa watu wakiunga mkono hoja hiyo. Ni kama vile walikuwa wanamngojea 'shujaa' ajitokeze kusemea hilo jambo wapate kum 'mback-up'. Kinyume kabisa na taratibu ndani ya chumba cha SPACE BUTTON watu wakaruruma na kuzoza. Haikuwa inaruhusiwa kufanya hivi.

Moderator alitii haja yao akapunguza kasi ya viyoyozi, kazi zikaendelea tena kwa ukimya. Lakini miongoni mwa watu hao waliopaza sauti zao kuhusu ukali wa viyoyozi, si Marwa wala Panky aliyekuwapo.

Wao walikuwa kimya. Wao walikuwa wakiendelea na kazi zao kana kwamba hakuna kilichojiri, hakuna walichosikia.

Zikapita dakika tano watu wakiendelea na kazi. Kama ilivyo ada ndani ya SPACE BUTTON ni keyboard tu ndiyo zikawa zinasikika. Ilipohitimu dakika ya sita, mara taratibu viyoyozi vikaanza kurudi kwa kasi.

Baridi likawa jingi, watu wakaanza kupata shida. Ni kana kwamba walipelekwa kwenye kilele cha mlima mrefu mno.

Wakaanza kulalamika tena, mada hii Moderator alikuwa ametoka kidogo. Wakazoza na kuzoza, Moderator aliporudi akastaajabishwa na hali hiyo ya 'soko'. Kabla hajafoka kukemea na kutoa vitisho, akatambua baridi lilikuwa limeongezeka maradufu.

Haraka akatazama tarakilishi yake. Akabofya keyboard mara kadhaa. Akapiga ngumi mezani kisha akatoka ndani. Bila shaka alikuwa anaenda kuangazia mitambo kama ina hitilafu.

Kiwizi, Marwa akamtazama Panky, akatabasamu, alafu akarudisha uso wake kwenye tarakilishi.

"Nimefanikisha!" Ujumbe ukaingia kwenye tarakilishi ya Panky kwa kutumia jina la M-spy.

Panky akatabasamu. Akamtazama Marwa kiwizi, alafu akachapa haraka kumjibu.

PANKY: Sure? (Hakika?)
M-SPY: Yah sure. (Ndio hakika).
PANKY: How did you do that man? (Umewezaje jamaa?)
M-SPY: Aaanh! Maswali gani hayo? Nataka nitazame kama naweza pata chochote kwenye mashine yake. Nipe muda kidogo.

Marwa akaanza kuitembelea tarakilishi ya Moderator kwa kutumia ya kwake. Alikuwa anafanya hayo kwa wepesi kwani hakuwa na muda wa kutosha, na usalama ulikuwa finyu mno.

Alijua endapo Moderator angepata muda wa kutulia kwenye mashine yake, angezijua njama zake. Kwahiyo alitakiwa kutumia fursa hiyo upesi kabla mwanaume huyo hajarejea kitini.

Dakika mbili tu, Moderator akawasili. Tayari hali ya hewa ilikuwa imetulia. Akatazama wafanyakazi wake akikagua tarakilishi zao kwa macho, kisha akaketi. Akashusha pumzi ndefu.

Akakagua tarakilishi yake akijiuliza nini shida. Akakagua kila kitu, hakuona tabu. Akakagua na tarakilishi za wafanyakazi wake kwa kutumia ya kwake, kote akaona wakifanya kazi zao.

Akajilazimsha kuamini tatizo lile la viyoyozi litakuwa ni la mitambo.

PANKY: Umefanikiwa?
M-SPY: Kiasi chake. Bado nahitaji kuingia tena kwenye mashine yake kuna kitu sijamalizia.
PANKY: Utaingiaje? Amesharejea. Ataongeza uangalifu sasa hivi kuliko mwanzoni.
M-SPY: Najua. Natazamia namna nitakavyofanya jambo hili kwa usalama.
PANKY: Be careful. (Kuwa makini)
Kukawa kimya kidogo kwa dakika nne, Ujumbe wa Marwa uka 'pop-up' kwenye kioo cha tarakilishi ya Panky.
M-SPY: Nimepata wazo.

Akamshirikisha wazo hilo Panky, naye akalikubali. Ikapita dakika moja, mara Panky akadondoka chini akihangaika kuhema kana kwamba koo lake la hewa limesiliba! Mbavu zikamsimama. Mishipa ikamchomoza. Macho akayatoa huku shingo ikishupaa.

Watu wakapigwa na butwaa. Wakaamini Panky atakuwa ameathiriwa na mabadiliko yale ya hewa yaliyokuwa yanatokea ndani ya chumba hicho hapo nyuma.

Haraka wanaume watatu wakafanya kumsaidia wakiwa pamoja na Moderator. Wakampeleka kupata huduma huko nje. Sasa Marwa akatimiza adhma yake upesi.

Baadae wakati wa kupata chakula cha mchana, wakaketi meza moja na Panky kuteta. Walihakikisha hakuna mtu aliyekuwa anawasikia, na wapo salama.

"Panky, kwanini hukuwa muigizaji?" Marwa akatania. "Unajua ulintisha aisee. Nikadhani huenda kweli umepata tatizo! Ilinihitaji roho ngumu kweli kukupuuzia."

Panky akatabasamu.

"Sikujua kama nina kipaji hicho, nitalifanyia mazingatio ... anyway, umefanikisha?" Panky akauliza.

Marwa akameza tonge kwanza. Akatikisa kichwa.

"Ndio, nimefanikiwa. Nadhani nimepata kila tunachokihitaji."

Panky akatabasamu. Lakini mara kiganja kikagusa bega lake, akageuka na kukutana na uso wa Moderator.

"Njoo," Moderator akamwambia kwa lafudhi ya ki Mandarin, kisha akaenda zake. Marwa akamtazama Panky kwa hofu. Moyo wake ulikuwa unakimbia kwa kasi. Alimshika mkono Panky akamwomba awafikishie taarifa familia yake endapo hatofanikiwa kutoka hai.

Kwa haraka pia akamwambia Panky taarifa alizozipata atakazikuta chini ya keyboard karatasini, kisha akaenda zake.

Panky akabaki na mawazo. Vipi kama Marwa amegundilikana? Hakupata hamu ya kula tena. Kifua chake kilikuwa kimejawa hofu. Je, watatambua hata kuumwa kwake kulikuwa ni mpango? Akajiuliza.

Alihisi mwili wake umekuwa wa baridi.

Mara kengele ya kurejea kazini ikalia, wote wakanyanyuka toka kantini na kurejea ndani ya SPACE BUTTON. Marwa hakuwapo kwenye kiti chake. Akamtazama na pale kwa Moderator, hakumwona, si yeye wala Moderator.

Basi haraka akanyanyuka na kwenda sehemu ya Marwa, akavuta droo ya keyboard na kutazama kwa chini, akaona kikaratasi kidogo cheupe. Akakibeba na kurudi sehemu yake upesi.

Hakukitazama kikaratasi hicho, alikiweka mfukoni na kuendelea na kazi yake lakini kila saa akawa anatazama kama atamuona Marwa ama Moderator.

Baada ya kama nusu saa, Moderator akarejea ila Marwa hakuonekana. Hapo sasa Panky akapoteza matumaini. Akahisi kweli pengine Marwa ameuawa.

Hakuweza kufanya kazi vizuri kabisa. Kichwani hakukuwa na maelewano kabisa, alikuwa anamuwaza Marwa. Mpaka unafika muda wa kuondoka kazini, Marwa hakuonekana popote pale!

Panky akakosa amani.

"Kuna shida?" Moderator akamuuliza Panky aliyekuwa amebaki mwenyewe kitini. Chumba kizima cha SPACE BUTTON kilikuwa cheupe.


***

MARWA YUPO WAPI? ANAFANYA NINI? NINI MODERATOR AMEFANYA? NINI ATAGUNDUA KWA PANKY?
 
*ANGA LA WASHENZI -- 61*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Hakuweza kufanya kazi vizuri kabisa. Kichwani hakukuwa na maelewano kabisa, alikuwa anamuwaza Marwa. Mpaka unafika muda wa kuondoka kazini, Marwa hakuonekana popote pale!

Panky akakosa amani.

"Kuna shida?" Moderator akamuuliza Panky aliyekuwa amebaki mwenyewe kitini. Chumba kizima cha SPACE BUTTON kilikuwa cheupe.

ENDELEA

Panky akashtuka sana. Hakuweza kutazamana macho na Moderator. Alizama fikirani na hata hakuwa anawaza kama mule ndani kaachwa na Moderator pekee.

Akaweweseka,

"Hamna shida! -hamna!"

"Sasa mbona upo hapa mpaka muda huu?"

Akakosa jibu. Akatazama kushoto na kulia kwake, hakukuwa na mtu yeyote. Akazima tarakilishi yake na kusimama.

Pasipo kuaga akaenda zake. Moderator akamtazama mpaka mwisho mwanaume huyo akiishilia.

Alipotoka ndani ya jengo hilo, asiamini, akaongeza kasi mpaka kituo cha mabasi. Akashangaa hakuitwa. Akaketi hapo kituoni akitazama barabara, labda anaweza kumwona Marwa.

Akaketi kwa muda mrefu hapo pasipo matunda. Akaamua kupanda zake gari arudi nyumbani. Sasa akawa anafikiria ni kwa namna gani awataarifu wazazi wake Marwa juu ya mtoto wao.

Kwahiyo kama Marwa akiuawa, wazazi wake wataendelea kupewa antidote? Ama ndiyo wataachwa wajifie maana hawana tena umuhimu?

Alilaza kichwa chake juu ya kioo cha dirisha akiwaza.

Watakuwa wamemuuaje Marwa? Na kama kweli wamegundua alidukua tarakilishi ya Moderator, hawatamdadisi kujua kwanini amefanya hivyo? Je, Marwa atawatoa chambo?

Yalikuwa ni mawazo baada ya mawazo. Shukrani tairi la gari lilizama kwenye kabonde kadogo barabarani gari likayumba, Panky akajigonga na kurudi fahamuni. Akatambua alikuwa anakaribia kupitishwa kituo!

"Shushaa! Shusha hapo!" Aliropoka akisimama. Mfukoni akatoa simu na pesa yake akijongea kwenda mbele kushuka. Mara ujumbe ukaingia.

Haraka akausoma.

'Mbona hujaningoja? Upo wapi?' Ilikuwa ni ujumbe toka kwa Marwa. Akajikuta anapiga yowe la ushindi. Akampatia konda shilingi alfu mbili na wala chenji hakuchukua.

"Oh no keep change, una mawazo mengi itakufariji weekend!" Alisema kisha akiondoka kibingwa.

Alicheka. Alihisi kifua chake kimekuwa chepesi.

Marwa yupo hai!

***
Saa kumi jioni, Jangwani Sea breeze.

Akiwa amevalia gauni fupi jeusi lililombana na chini viatu vyekundu vyenye kisigino kirefu Miranda alitazama huku na kule baada ya kuingia kwenye hoteli hii ya wastani.

Alikuwa kapendeza na anavutia japokuwa usoni hakuwa amejipara. Alibaki kiasili.

Nywele zake ndefu za bandia zilikuwa zinarukia huku na kule akipepesa kichwa. Mara akamwona mke wake Boka akiwa ameketi kwa juu, kwenye ghorofa moja iliyokuwepo hapo. Akapandisha ngazi kuelekea huko juu kumkuta.

"Usiniambie nimechelewa?" Akasema Miranda kwa tabasamu huku akiketi. Mke wa Boka alikuwa ametulia kitini ndani ya vazi la kitenge. Mezani kulikuwa kuna chupa ya soda ya Cocacola.

"Wala hujachelewa, karibu," akasema Mama huyu. Macho yake mekundu yalikuwa yameingia kwa ndani.

Wakasilimiana. Miranda akatazama huku na huko kisha akauliza:

"Hao wazungu wako wapi? Hawajafika bado?"

Mke wa Boka akamtazama kwa sekunde tano, alafu akamjibu:

"Hamna mzungu yoyote anayekuja hapa. Hamna wageni wowote toka nje. Nimekuita hapa uje uonane na mimi!'

"Serious?" Miranda akatahamaki.

"Yes, serious," mama akajibu akijitengenezea kitini.

Miranda akaanza kuhisi jambo. Kwa kiasi akawa na hofu moyoni. Aliukagua uso wa mke wa Boka vema, akajua kitumbua kitakuwa kimeingia mchanga.

Akapanga kukana kila jambo hapa endapo ataulizwa kuhusu Boka.

"Miranda, umeanza lini mawasiliano na mume wangu?"

Nilijua tu, Miranda akasemea kifuani. Mawazo yake yalikuwa sahihi. Kitumbua kimeingia mchanga.

"Mawasiliano ya kivipi, mam?" Akauliza kana kwamba hajui kinachoendelea. Mke wa Boka akamjuza anajua kila kitu na hivyo basi asijaribu kumdanganya hata kidogo.

Anajua amekuwa akikutana na mumewe na pia wana mahusiano kati yao hadi kupanga mikakati ya kusafiri pamoja na hata ndoa.

Miranda akabaki amestaajabu. Sasa rangi zake zilikuwa wazi, hakujua kipi cha kusema zaidi ya kuwa kimya na kutazama chini.

"Sikujua kama wewe ni mbweha kiasi hiki!" Mke wa Boka akateta akisaga meno. "Najua humpendi Boka, unataka tu pesa zake ama kumtumia. Unajua nimetoka naye wapi?"

Miranda hakusema kitu.

"Nakuuliza wewe, unajua nimetoka naye wapi?" Mama akasisitizia swali kwa sauti ya kufoka. Bado Miranda alikuwa kimya anatazama chini.

"Nakuuliza wewe malaya una ..." Mama akanyanyua chupa ya soda na kumrushia Miranda kwanguvu. "...jua nimetoka naye wapi?"

Ajabu, Miranda akaidaka chupa hiyo kana kwamba kitenesi kisha akaiweka mezani. Akamtazama mke wa Boka na kumwonyeshea ishara ya kidole kikicheza.

"Usijaribu tena huo ujinga."

Mke wa Boka akastaajabu. Mwanamke wa aina gani huyu? Asiseme kitu, Miranda akanyanyuka na kwenda zake mke wa Boka akimtazama.

Punde kwenye siti ile aliyokuwa amekaa Miranda, akaja kuketi mwanamke mwingine mnene mweupe. Naye alikuwa amevalia kitenge kama kile cha mke wa Boka, sare.

Huyu alikuwa ni rafiki yake mke wa Boka na walikuja naye hapo tukioni lakini wakatengana muda mfupi kabla Miranda hajawasili eneoni.

"Vipi shoga?" Mwanamke huyo akauliza kwa hamu. "Mbona ameondoka anatamba kiasi kile?"

Mke wa Boka akaminya lips zake. Hakutaka kusema kitu. Alisimama na kumwambia shoga yake waende zao.

Wakajipaki kwenye gari na kuanza safari.

"Niambie basi, Adela. Umeniita mwenyewe hapa alafu unaninyamazia, ndo nini?" Shoga akalalama.

"Hamna kitu nilichomfanya," akajibu mke wa Boka kisha akang'ata lips yake karibia kuichana. "Amenionyeshea dharau kubwa sana. Lazima nimfunde adabu!" Akabamiza usukani.

"Lazima nimfunze adabu! Hawezi akanifanyia dharau kiasi kile malaya mbwa yule!"

Macho yake yakaanza kulowana. Hata shoga yake akaogopa kumwongelesha, akaomba tu safari yao iwe salama maana dereva hakuwa sawa hata kidogo.

"Nitaona kama na risasi utaweza kuidaka!" Akasema mke wa Boka kwa ghadhabu.

---

Baada ya robo saa...

Miranda ndani ya gari kwenye foleni la mataa.

'The woman will spoil the food. She has already known all of our moves' (Mwanamke atatuharibia chakula. Ameshajua nyendo zetu zote) Miranda aliutuma ujumbe kwa BC.

'What woman? His wife?' (Mwanamke gani? Mkewe?) Ujumbe wa BC ukauliza.

'Yes, it's her.' (Ndio, ni yeye) Miranda akajibu.

'Then take care of her immediately!' (Basi mzingatie mara moja!)

'Thanks' (Ahsante) Miranda akatuma ujumbe huo akitabasamu.

***

ATAMZINGATIAJE MKE WA BOKA? JE NAYE MKE WA BOKA ATAMFANYAJE MIRANDA?
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…