*ANGA LA WASHENZI -- 65*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Kichwa chake kilikuwa kimeelemewa mawazo. Na hasira kwa pamoja. Akaenda ofisini kwake na kujilaza kwenye kiti chake. Akaendelea kuwaza akizunguka na kiti kila upande.
Mwishowe akaamua kumpigia simu Jona na kumtaka aje ofisini kwake mara moja. Jona akapokea wito. Akamwahidi ndani ya muda mfupi atakuwa hapo.
ENDELEA
Kamanda akatoa bunduki yake kwenye droo na kuikoki, kwa lolote litakalotokea, kisha akairudisha na kuliacha droo wazi iwe rahisi kuifikia silaha hiyo punde atakapoihitaji.
Akangoja kidogo kabla ya Jona kufika ofisini akiwa amevalia tisheti nyeupe plain na suruali ya kadeti rangi nyeusi. Mgongoni alikuwa amevalia begi. Wakasilimiana, Kamanda akaenda kwenye lengo la wito wake pasipo kupoteza muda. Akamsomea Jona mashtaka ya kumtendea ndivyo sivyo Alphonce akiwa kazini kutimiza maagizo yake.
Kinyume na Alphonce alivyotaka, Kamanda akampatia Jona nafasi ya kujieleza. Na wakati huo Kamanda akiwa anajaribu kwa kiasi kikubwa kutunza mihemko yake asimwonyeshe Jona.
Na kwa wakati huo huo mkono wake ukiwa karibu drooni kwa lolote litakalotokea.
"Mkuu, sikumshambulia Alphonce kwasababu ya kumzuia kutimiza majukumu yake bali yeye kutimiza yaliyo yangu."
"Yapi hayo?" Kamanda akamkatisha. "Hujui ile kesi ipo mikononi mwa Faridi?"
"Nafahamu. Si kwamba nimeamua kuibeba kesi hiyo, la hasha. Nafanya haya Faridi akiwa ana ufahamu na kinachoendelea. Nafanya haya kwakuwa nilihusishwa kwenye jaribio la mauaji na marehemu Eliakimu. Sidhani kama ni vibaya kufuatilia sababu iliyomfanya mheshimiwa akajaribu kuniua. Haswa baada ya kutimiza kazi yake aliyonipatia kwa uweledi mkubwa," Jona akajieleza.
"Kazi gani hiyo? Na ulikuwa mna mahusiano gani na Mheshimiwa?" Kamanda akauliza.
"Hapo nyuma Eliakimu alikuwa akintafuta nimsaidie baadhi ya kazi zake akiamini historia yangu ya kazi na utendaji wangu. Ikumbukwe sikuwa jeshini kwa muda huo. Na malengo yake ya kuntafuta hayakuwa mengine bali mawili akiahidi kunilipa pesa nzuri. Moja, kumtafuta mkewe, nikalifanikisha. Na pili, kumtafuta mfanyakazi wake aliyetekwa, nalo nikalifanikisha.
Lakini nikiwa nafanya kazi hizi, nikagundua Eliakimu hakuwa mtu safi. Alikuwa anajihusisha na biashara kadhaa za magendo zilizopelekea mkewe na hata mfanyakazi wake kutekwa.
Nikiwa nataka kufahamu hayo, siku nampeleka mfanyakazi wake kwake ajabu barabarani nikashambuliwa kwa risasi na vijana kadhaa waliokuwa ndani ya prado nyeusi. Tukafanikiwa kutoka hai isipokuwa dereva.
Nilipowasili kwa Eliakimu nikahitaji kusikia maelezo yake juu ya shutuma zangu. Lakini sikupata maelezo hayo, badala yake akanipiga risasi na kwenda kunitupa porini pamoja na maiti ya dereva yule aliyefia njiani," Jona akaweka kituo kisha akaendelea:
"Na hilo ndiyo likawa sumbuko langu tangu hapo. Kwanini Eliakimu aliniua ilhali nilitenda kazi zake? Nini anaficha?
Ni kheri nikasikia mfanyakazi wake, aitwaye Nade, alinusurika kifo katika jaribio la kuuawa yeye na bosi wake, Eliakimu, ambayo najua wazi wahusika watakuwa ni wale waliomteka mfanyakazi huyo. Nikaona ni busara kwenda kumtembelea kwani atanipatia majibu ya maswali yangu..."
Baada ya hapo Jona akamweleza Kamanda namna gani Alphonce alivyohusika kwenye mauaji ya mfanyakazi huyo na hata baadae kutaka kumpokonya nyaraka alizozipata kwenye nyumba ya Eliakimu.
Alipofikia hapo Jona akatoa nyaraka hizo begini na kuziweka mezani. Alafu akaendelea na maongezi yake huku Kamanda akiwa anapitiapitia nyaraka hizo kwa macho ya wepesi apate kuzimaliza amsikilize Jona vema.
"Sikukubali kumpatia nyaraka hizo kwani sikuona kama ni sahihi. Nilitaka kumkabidhi Faridi anayehusika na kesi hii lakini hakuwa radhi, sikufahamu kwanini lakini baadae nikaja kugundua kumbe naye alikuwa anahusika na madili batili pamoja na bwana Eliakimu na zile zilikuwa ni juhudi za kuhakikisha jambo hilo linabaki kuwa siri.
Kipindi anataka kunipokonya nyaraka hizo, akawa anasema maneno haya,"
Jona akacheza sauti ya Alphonce aliyoirekodi. Kamanda akiwa ametoa macho akaskiza sauti hiyo huku moyo wake ukimdunda mithili ya trekta linalopambana na ardhi ngumu ya shamba.
Mpaka sauti hiyo inakoma, hakusikia kuhusishwa kwake moja kwa moja. Akashusha pumzi ndefu na akajawa na hasira sana juu ya Alphonce. Hakutegemea kama mwanaume huyo angeenda kuropoka upuuzi wa namna hiyo kwa Jona.
Akatikisa kichwa kwa masikitiko akilaza mgongo wake kitini. Akatazama feni, pangaboi, likizunguka akichambua nini cha kufanya kwa dakika kadhaa. Akaona mwanya wa kumwangushia msala huu bwana Alphonce wakati yeye akijinadi kuwa safi.
Na kwakuwa hakuhusika na bwana Eliakimu kwa namna yoyote ile, hili halikuwa gumu kwake kulitenda.
"Alphonce! Alphonce!" Kamanda akabamiza ngumi nzito mezani. "Sikutarajia kama ungekuwa na wivu wa kijinga kiasi hiki!"
Akaendelea kumshtumu Alphonce hewani akimlaani kwanini wivu wake wa kipuuzi unamuingiza kwenye mauaji yake aliyoyatenda kwa mkono wake mwenyewe.
Akakana kabisa kuhusika na mauaji ya familia ya Jona akisema yeye si 'mkuu' huyo anayetamkwa sautini. Hiyo ilikuwa ni janja tu ya Alphonce kujisafisha na kutakatisha matendo yake ya kidhalimu.
Mwishowe,
"Nakuomba haya mambo ya Alphonce yaishie hapa Jona, niachie mimi nitamshughulikia huyo fisadi wa maadili! ... unaweza kwenda."
Jona akaenda zake akimwacha Kamanda kichwa kinamuuma kwa mawazo.
Alichambua kila alilolisikia na kuambiwa. Kwa akili yake akaona Alphonce sasa ni tishio kwake kuliko Jona. Mwanaume huyo si tu kwamba atafanya ijulikane alitia mkono kwenye mauaji ya familia ya Jona, ambacho ni uhalisia, bali atamfanya aonekane alikuwa anashirikiana naye kwenye biashara zake za kidhalimu azifanyazo kwa kofia ya polisi.
Kitu ambacho si uhalisia!
Kwa kujilinganisha na Alphonce akajiona yeye ni mtu safi. Na kuwa safi zaidi alitakiwa kufanya namna.
Ipi hiyo?
Akaweka simu sikioni na kuongea maneno machache.
"Kericho, fika ofisini kwangu mara moja."
Ndani ya dakika chache akaja hapo mwanaume mrefu mzito maji ya kunde ndani ya kaunda suti.
**
Saa moja asubuhi ...
"Ameshaondoka," mke wa Boka aliongea na simu. Haikupita hata lisaa kamili tangu mumewe amuage kwenda kazini. Mama huyu alikuwa ameketi sebuleni akiwa amevalia khanga kifuani.
"Ndio ebu njoo shoga angu maana hapa sielewi kitu yani! ... yani nahisi kuchanganyikiwa ... njoo bana ... kwani hajatoka? ... mida gani? ... basi nakuja mimi ... sawa nikukute hapo ndani ya robo saa."
Akaacha simu yake na kwenda kujiandaa. Hakupata hata kifungua kinywa. Ndani ya muda mfupi, akawa ameshavalia batiki lake lililomkaa vema. Akajipaki kwenye gari na kuanza safari.
***
Saa nne asubuhi ...
"Samahani, Mheshimiwa," sauti ya kike ilimfanya Boka abandue macho yake kwenye karatasi kadhaa alizokuwa anazipitia. Alikuwa ni sekretari wake, bi Salma, mwanamke mnene aliyevalia shati jeupe, sketi ndefu nyeusi na hijabu ya pinki.
"Kuna barua yako hapa."
"Toka wapi?"
"TFF."
"Ooh niwekee hapo," akaonyeshea mezani kwa kichwa kisha akaendelea na kazi yake. Bila shaka alikuwa ametingwa. Hii ilikuwa ni miongoni mwa siku zake alizo bize.
Alilenga kufanya kazi pasipo kupumzika mpaka majira ya chakula cha mchana amalizie kila kiporo mezani. Lakini hakufanikiwa kwenye hilo. Kwani muda si mrefu akapata taarifa mkewe amefariki kwenye ajali mbaya ya gari iliyotokea maeneo ya Makumbusho.
Akachanganyikiwa!
***
- AJALI HII IMETOKEAJE? NANI ANAHUSIKA? UNADHANI NI MIRANDA, UNA UHAKIKA?
- NINI KAMANDA ATAFANYA KWA ALPHONCE? NAYE JONA JE AMEPANGAJE KICHWANI?