Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

‍♂️‍♂️‍♂️‍♂️‍♂️‍♂️‍♂️‍♂️[emoji134]‍♂️[emoji134]‍♂️[emoji134]‍♂️[emoji134]‍♂️[emoji135]‍♂️[emoji135]‍♂️[emoji135]‍♂️[emoji135]‍♂️
 
*ANGA LA WASHENZI -- 62*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

'The woman will spoil the food. She has already known all of our moves' (Mwanamke atatuharibia chakula. Ameshajua nyendo zetu zote) Miranda aliutuma ujumbe kwa BC.

'What woman? His wife?' (Mwanamke gani? Mkewe?) Ujumbe wa BC ukauliza.

'Yes, it's her.' (Ndio, ni yeye) Miranda akajibu.

'Then take care of her immediately!' (Basi mzingatie mara moja!)

'Thanks' (Ahsante) Miranda akatuma ujumbe huo akitabasamu.

ENDELEA

Saa mbili asubuhi kwa ofisi ya Kamanda wa polisi mkoa ..

"Umeambiwa uingie," alisema mwanamke mmoja polisi aliyetoka ndani ya ofisi ya Kamanda. Mwanamke huyu alikuwa amevalia suti ya kike rangi ya kahawia na alikuwa anamwongelesha Jona.

Jona akamshukuru na kisha akanyanyuka kuzama ndani, akamkuta Kamanda akiwa anasoma gazeti lake kama ilivyo ada nyakati hizi za asubuhi. Akampa heshima yake na kuketi.

"Nimekuja mkuu."

"Karibu," akajibu Kamanda na kama vile hakuwa anajua kama kuna mtu hapo, akaendelea kusoma gazeti lake. Akamkalisha Jona kwa muda wa dakika sita kukiwa kimya.

"Aaannh!" Akafunga gazeti akizinduka. "Ndo umefika enh?" Akauliza kipuuzi. Jona hakusema jambo. Kamanda akatazama saa yake ya mkononi na kisha simu yake.

Alikuwa anamngoja Alphonce. Mpaka muda huo mwanaume huyo hakuwa ameripoti eneoni. Sasa atamruhusuje Jona akaendelee na kazi wakati mwanaume huyo wa kumfuatilia hajawasili?

"Em ngoja kidogo."

Akanyanyua simu yake kupiga. Simu ikaita na kuita pasipo kupokelewa. Akasonya akitikisa kichwa.

_Ananijaribu huyu_ akasema kifuani mwake. Ina maana hakunielewa nilichomwambia? Sasa dharau inavuka mipaka.

Hakuwa na namna akamruhusu Jona aende zake akimuagiza amuitie afande Holombe mara moja pindi atakapotoka nje. Jona akatimiza agizo. Mwanaume mrefu mweusi akaingia ndani ya ofisi ya Kamanda na kusimama kwa ukakamavu.

Kamanda akamuagiza akamfuatilie Jona popote pale atakapokwenda. Jicho lake lisibanduke kumuacha abadani.

"Ukishindwa, usirudi hapa," Kamanda akatoa kitisho. Holombe akaenda zake kutimiza agizo. Akatoka nje ya ofisi hiyo akiangaza kumtafuta Jona, mara akasikia kiganja begani kugeuka akakutana na mlengwa wake.

"Bila shaka unanitafuta mimi," Jona akajinasibu. Holombe akatabasamu. Akajaribu kukanusha lakini uso wake ukimsaliti.

"Usijali, najua umepewa agizo na kamanda. Ila tu kiukweli, hutaweza kunifuatilia Holombe."

"Umejuaje jina langu?"

"Nadhani ungejiuliza kwanza nimejuaje kama umetumwa unifuatilie ... anyway, naitwa inspekta Jona. Nisingependa kukuchosha, tutakuwa pamoja, lakini itakapofikia mahali nitakuacha."

"Lakini mkuu ka--" kabla Holombe hajamalizia, Jona alikuwa tayari yupo mbele hatua nne. Hakuongea tena.
--
Saa nne kasoro robo, Aga khan hospital...

"Karibu," daktari alimwambia Jona huku akitazama tarakilishi yake. Jona pasipo kupoteza muda akamtaka ampashe maendeleo ya mgonjwa wake, Nade, na kama kuna uwezekano wa kuonana naye.

Hapa sasa daktari akamtazama Jona akiacha kila shughuli yake. Akamwambia Nade amefariki. Jona akashangazwa. Hakutegemea kabisa kupokea habari hizo kwani alimwona Nade akiwa tayari amesharudi kwenye hali yake.

Vipi sasa kufa huku ghafla?

Daktari asimpe Jona maelezo ya kutosha, akasisitizia tu amefariki na mwili wake umeshahifadhiwa mochwari.

"Inaonekana alikuwa ana internal damage iliyokawia kupona na hatimaye kuathiri organ zingine za mwili." Daktari akapandisha mabega yake na kumalizia: "Kifo ni kwa kila mmoja."

Jona akahisi kuna jambo halipo sawa hapa, na hakuwahi kuwa na shaka na akili yake pindi awazapo hivyo. Akamwagiza daktari aongozane naye kwenda kuutazama mwili wa Nade huko mochwari.

"Hapana. Nimeba --"

"Sasa hivi!" Jona akaamuru akimtazama daktari kwa macho ya simba. Daktari akahofu. Akanyanyuka na kutii amri, Jona akapata kukagua mwili wa Nade.

Punde akagundua jambo.

"Ameuawa," akasema kwa kujiamini. Alitomasa tomasa shingo ya marehemu Nade akagundua misuli yake ilikuwa imetapanywa, na koo lake lilikuwa lina ufa.

Akamtazama daktari na kumwambia:

"Ameuawa kwa Manual strangulation. Ulikuwa unajua hilo, sio?"

Manual strangulation ni nini? Tendo hili kwa jina lingine hujilikana kama throttling. Ni kitendo cha kuminya shingo ya mlengwa kwa presha kubwa mpaka kupelekea kupoteza fahamu ama kufa kabisa.

Daktari akashtuka kusikia habari hizo. Akabanwa na kigugumizi.

"Unataka kuniambia ulikuwa hulifahamu hili ama ulikuwa unanificha?" Jona akamuuliza. Hakuwa yule Jona umjuaye, alikuwa sasa anatisha. Endapo mtoto amgemtazama, basi angekunywa bilauri lote la uji kwa kauli moja.

"Nani kamuua?"

"Sijui nani kamuua!"

"Nani alikuwa wa mwisho kuingia ndani ya chumba chake?

Daktari akababaika. Jona akamlamba kofi moja zito. Daktari akapepesuka kama kapitiwa kimbunga.

"Alikuwa ni yule ... alikuwa yule askari mwingine!" Daktari akaropoka akisugua shavu lake lililozabwa.

"Sasa naenda kukutia ndani kwa kushirikiana na muuaji!" Jona akafoka. Akamwamuru daktari aongoze mpaka chumba cha kusimamia CCTV kamera zilizopo hospitali. Walipofika huko Jona akataka kuchukua tape (tepu) inayomuonyesha Alphonce akitoka katika chumba cha Nade.

Ajabu tape hiyo haikuwapo. Wale wasimamizi wakamwambia Alphonce aliwapokonya. Akaishiwa nguvu. Akatoka hospitali na kwenda kantini akiwa ameketi na Holombe. Kwa muda akawa kimya. Hakuagiza hata chakula, isipokuwa Holombe pekee. Mara akachomoa simu yake mfukoni na kupiga, akaibinyia sikioni.

Alikuwa anampigia yule polisi aliyempatia kazi ya kumlinda Miranda. Punde polisi huyo akapokea na kumweleza Jona kuwa alipewa oda toka kwa mkubwa wake aache kazi hiyo mara moja na kureja kituoni. Ni kwa muda sasa hakuwapo hapo.

Na ni kweli, Jona akajilaumu kutotambua jambo hilo mapema. Ilikuwaje akapitiwa na uzembe kama huo.

"Ni nani huyo?" Akauliza.

"Inspekta Alphonce," akajibiwa. Akakata simu na kuiweka mfukoni. Akaagiza maji makubwa akawa anakunywa akiwa anawazua.

Sasa ilikuwa wazi Alphonce alikuwa anajaribu kuficha jambo. Kumuua Nade na kung'ang'ania mafaili aliyoyapata kwa Eliakimu vilithibitisha hayo. Lakini vikathibitisha zaidi kuwa Alphonce hakuwa polisi safi. Kwa namna moja ama nyingine atakuwa anahusika na genge la Sheng, BC au pia wakina Nyokaa.

Kuna haja ya kumfikisha mbele ya dola? Akajiuliza. Akatafakari na kubaini hana haja hiyo. Moja, Alphonce alikuwa tayari ni nusu mfu. Atamwacha afe taratibu tu kuonja ladha ya madhalimu yote aliyoyafanya. Pili, inawezekana kabisa kufanya jambo hilo kukawa ni mbio za sakafuni. Alphonce alishasema hapo awali, anajua kulamba mkono wa wakubwa. Je watamwacha aangamie?

Haikuingia akilini mwa Jona.

Lakini vipi kama kibao kikaja kugeuzwa kwake? Napo akajiuliza. Ila hakuwa na hofu sana kwani alikuwa na ushahidi wa kumfanya awe salama.

Simu yake ilikuwa ina sauti za Alphonce alizozirekodi kipindi mwanaume huyo akiwa anaropoka. Kumbe alipokuwa ameweka mkono wake mfukoni alikuwa akifanya kazi hiyo.

Na kama haitoshi, alikuwa ana nyaraka za Eliakimu mkononi.

Akashusha pumzi ndefu. Mara ujumbe ukaingia simuni.

***
 
*ANGA LA WASHENZI -- 63*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Lakini vipi kama kibao kikaja kugeuzwa kwake? Napo akajiuliza. Ila hakuwa na hofu sana kwani alikuwa na ushahidi wa kumfanya awe salama.

Simu yake ilikuwa ina sauti za Alphonce alizozirekodi kipindi mwanaume huyo akiwa anaropoka. Kumbe alipokuwa ameweka mkono wake mfukoni alikuwa akifanya kazi hiyo.

Na kama haitoshi, alikuwa ana nyaraka za Eliakimu mkononi.

Akashusha pumzi ndefu. Mara ujumbe ukaingia simuni.

ENDELEA

Akautazama, ulikuwa umetoka kwa Panky. Alikuwa anamhitaji afike kwa Marwa mara moja wapate kujadili kile walichokipata. Pasipo kupoteza muda akalipia maji yake na kisha kwenda zake.

"Samahani sitakuhitaji huku," alimwambia Holombe aliyenyanyuka upesi aongozane naye. Holombe akaketi na kumtazama Jona akiyoyoma.

Ndani ya dakika kadhaa akawa amefika nyumbani kwa Marwa na kuwakuta vijana wake wakiwa wanamngoja mezani.

"Tumefanikiwa," Marwa akamwambia akitabasamu. Jona naye akajikuta anatabasamu pia.

"Nini mmepata?" Akauliza.

"Kuna links mbili ambazo zinaenda kwa majina ya BIRD 002 na BIRD 003. Zimekuwa ni link ambazo zinatumiwa sana kuwasiliana na link ya SPACE BUTTON ambayo bila shaka itakuwa ndiyo BIRD 001. Kwahiyo tunaamini kabisa hizi links ni mojawapo ya wale ndege wa mawasiliano."

Kwa Jona jambo hili likaleta mashiko. Na lilithibitishwa na majina ambayo links hizo zilipewa, BIRD yaani kumaanisha ndege. Na kwenye ile picha ni ndege ndiyo walitumika kama ishara.

"Kwahiyo mpaka sasa hizo links mbili kutimiza tano ndizo zimekuwa kitendawili. Hatujajua zipo wapi na zitakuwa zinafanya kazi gani," Panky akaeleza.

"Hamna shida," Jona akawatoa hofu. "Naamini kwenye hizi tulizonazo zinaweza kutusaidia kung'amua hizo zilizobaki."

Marwa akamueleza wame 'trace' links hizo mbili na wamegundua mojawapo inapatikana Dodoma na nyingine ikiwa Nairobi, Kenya. Na zaidi ya hapo wamefanikiwa kupata jumbe kadhaa zilizokuwa zinatumwa toka upande mmoja kwenda mwingine.

Jona akavutiwa na habari hizo. Akawapongeza kwa kazi kubwa waliyofanya. Lakini kama haitoshi, Marwa akamwambia zaidi. Bado wanaweza kuzama kwenye links hizo hata sasa, na kudukua mawasiliano hayo kwa kutumia 'unknown mode'.

Basi kwa haraka Jona akataka kushuhudia jambo hilo. Marwa akazama kwenye links hizo na kuanza kukagua taarifa wakianza na ile ya Dodoma. Huko wakakuta mambo makubwa yaliyowashangaza mno.

Kuna kambi ndogo ya Sheng ndani ya manispaa ya Dodoma. Na kambi hiyo kazi yake ni kupokea maagizo toka kambi kubwa iliyopo Dar es salaam, kuyatekeleza na pia kutuma taarifa kuja kambi kuu juu ya kinachoendelea bungeni.

Kambi hii ya Dodoma ilikuwa inafahamu kila kitu kinachojadiliwa na kitakachojadiliwa bungeni. Ilikuwa inajua maamuzi yote yanayoafikiwa huko na mipango yote ya serikali.

Lakini haswa katika namna zinavyowagusa Wachina. Haswa namna zinavyowaathiri wao katika nchi na ukanda huu wa Afrika Mashariki na kati.

Kambi hiyo ilikuwa inahusika na mauaji ya wabunge na viongozi wote wa serikali waliokuwa kikwazo kwa matakwa ya Wachina kwa kutoa taarifa za viongozi hao kisha kikosi cha wauaji kinaagizwa toka kambi kubwa.

Kwa ufupi tu,

Sheng hakuwa tu genge hatari. La hasha! Alikuwa pia ni jasusi wa kiuchumi. Alikuwa ni mtu anayehakikisha maslahi na matakwa ya Wachina yanatimia!

Kwenye kila mkataba wanaopata Wachina aidha kwenye ukandarasi, ama shughuli yoyote ya kiuchumi nchini, Sheng alikuwa na kivuli ama mkono wake hapo. Kwa kifupi alikuwa anaisambaza dola ya kichina kusini mwa jangwa la Sahara, akianzia Afrika Mashariki na kati.

Na kwa kufanya hivyo, Sheng anakuwa chini ya serikali ya China. Analindwa na mkono wa serikali hiyo na kupewa nafasi maalum mbele ya macho yao. Anafadhiliwa kifedha, anasikilizwa na kupewa mazingatio ya juu.

Hakufanya haya kwa bahati mbaya ama kwa sababu za faida ya mbuzi, la hasha, bali kujenga ngome itakayomfanya kuwa salama kiuchumi yeye na koo yake.

Sasa akiingiza ama kutoa mizigo nchini China ama Tanzania, anapewa 'badge' ya serikali. Anatumia nafasi hiyo kunufaika kwa kupitishia magendo yake. Anatumia nafasi hiyo kujijenga na kuwa tajiri mkubwa mno. Kuifanya koo yake kuwa 'dons'.

"Hii ishu ni kubwa," akasema Jona. "Ni mtandao mpana mno ambao una nguvu, yatupasa kuwa waangalifu sana. Lakini kwa wakati huo tukipanga namna ya kuangusha mipango hii kama daudi alivyofanya kwa Goliath."

"Tupo pamoja na wewe katika kila namna," Marwa akamueleza na kumpa moyo.

"Knowledge is power," (Ufahamu ni nguvu,) Jona akaongezea. "Hatuwezi kupigana na mtandao kama huu kwa ngumi. Lazima uwe na taarifa za kutosha kwanza. Ujue unapiga wapi na kwanini.

Sasa basi kutambua base hizi ya Dar, Dodoma na Nairobi, hakutoshi kabisa. Impact yake ni ndogo sana kwani kazi zake ni kusafirisha taarifa haswa haswa huku mtendaji mkuu akiwa kambi kuu ya Dar.

Tunahitaji kujua yale mawimbi matatu. Yale mafiga matatu ya ulinzi. Hayo tukikabiliana nayo na kuyamudu, Sheng atakuwa mdhaifu. Sasa tutafanya vile tunavyotaka."

Lakini pia akatoa agizo la kuyatunza yale yote waliyoyapata kama ushahidi. Ni muhimu mno. Na hata pale watakapotaka kuyafunua mambo hayo hadharani basi watatuma hizo taarifa kwa vyombo husika kwa kutumia 'anonymous profile'.

Isijulikane nani ametuma taarifa hizo, wala wapi zimetokea kwasababu kuu mbili. Mosi, kwa usalama wao wakiwa wanaendelea na kazi zao kama kawaida, na pili wapate fursa ya kutambua hatua zitakazochukuliwa juu ya taarifa zao, kama ni kitu kitakachopokelewa ama kufichwa kwanguvu.


***

Saa tano usiku, maeneo ya Msasani.

Sasha akatazama nyuma yake hatua kadhaa baada ya kuacha geti. Hakukuwa na mtu. Akatembea upesi kulifuata gari aina ya Nissan Murano nyeusi, akafungua mlango na kuzama ndani akiketi siti za mbele kabisa.

Mwanamke huyu alikuwa amevalia dira jekundu, kichwani nywele zikiwa timu.Ndani ya gari kulikuwa kuna wanaume wawili vijana wa Sheng: Nigaa na Mombo, Nigaa akiwa ameukamatia usukani na huku mwenziwe akiwa ameketi viti vya nyuma.

"Vipi umefanikiwa?" Nigaa akauliza.

"Bado naskilizia," Sasha akajibu. "Ila uhakika upo lazima tu ntapata nafasi."

Kukawa kimya.

"Nadhani unajua cha kufanya, Sasha. Na jambo hili liwe siri hata dada yako Sarah asilifahamu hata kidogo. Na ujue kabisa hakuna nafasi ya wewe kushindwa kwenye hili. Ukishindwa, utaenda kumsalimu Bite mapema sana," Nigaa akaeleza. Kukawa kimya.

Hakukuwa na maelezo mengine, Sasha akashuka garini, gari likaondoka.

****
- NINI KIMEMTOKEA SASHA NA AGIZO GANI ANASISITIZIWA?
- NINI JONA NA WENZIWE WATAFANYA NA KWA MUDA GANI WATADUMU KUWA SALAMA?
- HATMA YA MKE WA BOKA MIKONONI MWA DHALIMU MIRANDA?
- ALPHONCE YUPO WAPI?
- MIRIAM ATASALIMIKA DHIDI YA WAWINDAJI ROHO YAKE? KUNA NAMNA ATAKUTANA NA JONA?

SEHEMU IJAYO.
 
Tupo pamoja ila kama vile ujazo imepungua
Sikulaumu, tatizo unaangalia wingi wa matukio na si wingi wa maneno. Ipo hivi, huwa naandika characters elfu kumi kwa kila simulizi. Ujazo haujawah pungua ila nyinyi viumbe mkiona mtunzi siku hiyo anaongelea tukio moja kwa undani zaidi. Mnaona mmepunjwa.
 
Back
Top Bottom