*ANGA LA WASHENZI (MSIMU WA PILI) -- 10*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
"Sikujua," afande Devi akajitetea. "Nilimkuta hapo nje kwa muda mrefu. Nikamuuliza akasema haja yake. Nikaona si vibaya ku-"
"Usirudie tena!" Massawe akamkatiza. "Sawa?"
"Sawa afande!"
ENDELEA
Baada ya muda kidogo koplo Massawe akaondoka zake na kumwacha afande Devi peke yake. Devi asipoteze muda akaenda kumwona Jona rumande na kumwonya kuhusu watu wanaomtembelea.
"Hawataki upatiwe chakula, Jona. Utakapoona nimewazuia wageni wako jua nimekosa namna ya kuwaruhusu."
Jona akafadhaishwa sana na hili. Kwanini wanamfanyia hivyo? Nini lilikuwa kosa lake ndani ya jeshi? - uweledi wake?
"Usijali," afande Devi akamtoa mashaka. "Nitakuwa nakusaidia kadiri ya uwezo wangu. Nitakapokuwa napata muda ntakuwa nakupenyezea hata kidogo. Lakini kwa siri sana."
"Ahsante sana Devi," Jona akachonga. "Ila nakuomba uachane na hivi vitu. Wewe bado kijana mdogo na ndiyo kwanza umeanza kazi mwaka huu. Hili linaweza kukugharimu."
"Wala usijali, Jona," Devi akamtoa mashaka. "Wewe ni miongoni mwa watu wachache sana walionipokea vema hapa kituoni wakaniheshimu japokuwa ni mdogo kwao kiumri na kicheo. Hustahili haya. Naamini hauna roho hiyo. Mimi nitakusaidia kadiri ya uwezo wangu."
Afande Devi hakukaa sana hapo, akaenda zake kurudi anapotakiwa kuwapo. Alihofia koplo Massawe anaweza akarudi asimkute ikawa taabu.
**
Kamanda mkuu akiwa anaongozana na maaskari wengine wawili, mmoja akiwa amevalia kiraia, wakakomea langoni mwa rumande ya Jona. Kamanda akamtazama Jona kwa jicho la huruma kisha akadaka vyuma vya lango.
Jona alikuwa amekaa mbali ukutani.
Kamanda akatikisa kichwa kwa masikitiko. Kwa ishara, akamtaka mwanaume Jona ajongee karibu naye. Jona akatii. Akamsogelea mkuu wake huyo na kumtazama machoni.
"Jona," Kamanda akaita. "Kwanini umekubali kuteseka kiasi hiki? Fanya yaishe. Niruhusu nikusaidie. Haustahili kabisa kuwapo humu ndani."
Jona akamtazama Kamanda kwa sekunde kadhaa kisha akamjibu akiwa anang'ata meno.
"Anayestahili kuwepo humu ndani ni wewe pamoja na wenzako. Nitakapofanikiwa kutoka humu, basi jua ni wewe ndiye utakayeingia."
Kamanda mkuu akatabasamu.
"Shida yako ipo hapo, Jona. Unashupaza sana shingo. Unajua kisa cha chui na chungu? ... chui alizamia kijijini kwa watu akiwa anatafuta chakula kwa ajili ya wanae. Hakutaka kumla mtu kabisa bali apekue majikoni aone kama atapata chochote kitu.
Huko akafanikiwa kusikia harufu nzuri kabisa ya chakula toka kwenye chungu kidogo. Kuonja ... alah! Kilikuwa kitamu sana. Akaona kinafaa kupelekea watoto wake porini.
Lakini si bahati, chui akazamisha kichwa chake ndani ya chungu hicho hata akashindwa kukitoa. Akahangaika huku na huko kujinasua asifanikiwe mpaka wanakijiji wakamsikia. Wakajaa kumzunguka.
Walitaka sana kumsaidia, lakini silka ya chui iliwaogopesha kufanya hivyo. Je, Kucha zake zingewaacha salama? Walihofia. Na je wakishatoa hiko chungu kichwani, meno yake hayatawararua?"
Kamanda akaweka kituo. Akameza mate na kumwambia Jona.
"Badili hulka yako, uruhusu kusaidiwa. Kushupaza kwako shingo hakutakupelekea popote zaidi ya shimo la tewa."
Jona akasaga meno.
"Kama ungelibadili hulka yako kwanza, nisingelikuwepo humu ndani," akasema kwa kujiamini, kisha akaita, "Kamanda, kwa makusudi ulitengeneza kidonda kwasababu una dawa mkononi Sawa dawa yako yaweza kuponya lakini vipi maumivu niliyoyapata? Na je kovu utakaloniachia?"
Akahitimisha.
"Silambi mkono unaoniadhibu. Tena pasipo na hatia. Si kwamba ni kiburi, la hasha! Bali itanifanya niwe na hatia. Kamanda, acha nitapambana mpaka tone la mwisho."
Kamanda mkuu akabinua mdomo wake kisha akamtazama mmoja wa watu alioongozana nao kuja hapo, yule aliyevalia kiraia. Akamuuliza:
"Mmempa chakula enh?"
"Hapana, mkuu. Hajala," mwanaume huyo akajitetea akitikisa kichwa.
Kamanda akamtazama Jona kisha akarudisha macho yake kwa yule mwanaume aliyemuuliza. Akampatia maagizo.
"Hakikisha hali kwa siku zote anazokaa humu ndani!"
"Ndio, mkuu!" Akajibu mwanaume huyu kwa ukakamavu.
**
Asubuhi ...
Mlango ulipofunguka, alitoka inspekta Geof akiwa amebebelea notebook yake mkononi. Nyuma yake alikuwapo mwanadada Miranda akimsindikiza.
Wakasimama kibarazani, Inspekta akampatia Miranda mkono wa kheri kisha akamkumbusha hatakiwi kuondoka nje ya mji mpaka pale upelelezi utakapokamilika, na kesho atakuja tena kumwona.
Aliposema hayo, inspekta akaondoka zake Miranda akimtazama mpaka anatoka nje ya geti. Akarudi sebuleni na kuketi akikuna kichwa chake kwa mawazo. Nywele zilikuwa timtim, na mwili wake ndani ya dira angavu ulikuwa unahangaika kuweka kila mkao.
Aliwaza. Hakuona kama una upenyo wa kuchomoka katika kesi hii. Kama upo basi ni kama ule wa tundu la sindano. Mambo yamekuwa magumu zaidi. Kwa dalili za wazi, inspekta alionekana kudhamiria kumtia ndani.
Mawazo yake yakaenda mbali. Akamuwazia Jona. Kwanini kesi hii amepewa mtu mwingine mbali na yeye? Aliamini Jona ni mwerevu kung'amua muuaji na si huyu Geof ambaye macho yake yanakomea juu ya zulia.
Akawaza afanyaje? Mawazo yake yote yakamuelekezea msaada wa pekee ni Jona. Akanyanyua simu na kupiga. Hakuwa anafahamu kuwa Jona yupo nyuma ya vyuma.
Simu ikaita pasipo mafanikio. Akaamua kumpigia Kinoo amshirikishe habari zake kwa mara ya kwanza. Hata akisikia amekamatwa basi asije akastaajabu na aje kumtembelea rumande.
Simu ikaita mara mbili kabla ya kupokelewa. Kulikuwa na makelele kuonyesha Kinoo alikuwa mjini kwenye pilika za magari na watu. Miranda asijali hilo, akatimiza adhma yake ya kumhabarisha Kinoo.
"Sidhani kama kesho akija ataniachia huru. Maswali yake yote nilikuwa nababaika kujibu. Najiona kabisa nikitenga shingo kwa mchinjaji."
"Sasa tunafanyaje?" Kinoo akauliza.
"Tumtafute Jona. Naamini anaweza akanisaidia!"
"Jona? Yule polisi?"
"Ndio! Alikuwa ndiye mpelelezi wa hii kesi, ila wamembadilisha!"
"Miranda, kwani hujasikia habari za Jona?"
"Zipi?
Kinoo akamhabarisha Miranda kwamba Jona amekamatwa anatuhumiwa kumuua RPC hivyo asitegemee kumsikia tena.
Miranda akachanganyikiwa. Tumbo likamvuruga. Alikata simu akaiweka kando na kulaza kichwa chake kwenye kiti.
Jona amekamatwa? Jona amemuua RPC? Maswali haya yakazunguka kichwani. Akajikuta anatikisa kichwa chake kama mwehu.
Hapana.
Hakuamini hata chembe.
Akanyanyuka upesi na kwenda ndani.
**
"Jona, naamini hujaua," Miranda alisema kwa sauti ya chini akimtazama Jona kwa macho ya huruma. "You have been framed. Na ubaya si tu inakuumiza wewe bali hata na sisi. I need you out. Things are not the same."
Macho ya Miranda yalibadilika rangi na kuwa mekundu.
Jona alikuwa amesimama akishikilia nondo kwa mkono wake wa kuume akitazama chini. Sijui alikuwa anawaza nini. Ila ungemtazama ungeona moyo wake unaungua. Kifuani alikuwa ana moto mkali.
Alikuwa anasikia maumivu aliyoyaonyesha kwa kung'ata meno yake.
"Jona, Miranda akaita. "We have to do something. Usikae ukaridhika na hii hali. Najua you are innocent."
"Nitafanya nini Miranda nikiwa humu rumande nimebanwa na vyuma?" Jona akauliza. Macho yake yalikuwa mekundu. "Nimedhamiria kweli kufanya kitu, lakini nafanyaje na nipo humu ndani?"
Kabla Miranda hajasema kitu, afande Devi aliwasili eneoni akiwa amebebelea chakula kwenye mfuko. Akamkabidhi Jona.
Akamtazama machoni.
Akamtazama na Miranda kisha akarudisha macho yake kwa Jona.
"Kula upesi!" Akasema kwa kunong'oneza kisha akaenda zake.
**
"Umempatia?" lilikuwa swali la kwanza kutoka kwa koplo Massawe.
"Ndio, nimempa," akajibu afande Devi. Uso wake alikuwa ameukunja. Macho yake yalionyesha mawazo. Aliketi akafungua daftari kubwa la hapo kaunta akaigiza kulitazama ila kiuhalisia alikuwa mbali sana kimawazo.
Ndani ya muda mfupi, Miranda akafika hapo kaunta akiwa anatembea kwa madaha. Mwanamke huyo aka 'sign out' na kuwaaga.
Massawe akanyanyua simu na kupiga.
"Ndio, ameshakula kile chakula ... sawa, mkuu."
***