*ANGA LA WASHENZI -- 59*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Alphonce akacheka. "Nimeshakueleza, Jona. Na ukiendeleza ukaidi, mkono huu ulioteketeza familia yako, utakuteketeza na wewe pia!"
"Nani alikutuma, Alphonce?" Jona akauliza. Macho yake yalikuwa mekundu kama bendera.
"Sina muda wa kuzoza tena, Jona," Alphonce akamjibu. Kisha akamuamuru:
"Nipe hayo mafaili au niyachukue kwanguvu?"
Jona akayaweka mafaili mezani.
"Haya hapa. Chukua."
ENDELEA
Alphonce akatabasamu kwa dharau.
"Nilikuwa naingoja sana hii nafasi," akasema akivua koti lake la suti. "Leo nitakufunda adabu na kuheshimu wakubwa zako."
"Unaonaje tukitoka nje?" Jona akapendekeza. Alphonce kwa majivuno akaufungua mlango na kutangulia kumbini. Akakunja ngumi na kusimama sawia kwa ajili ya mpambano.
Jona akamtazama mwanaume huyu kwa macho ya kina. Akamkagua kuanzia juu mpaka chini kisha akasema na moyo wake.
Akakunja ngumi, akatanua miguu kupata balansi. Basi haraka Alphonce akamvamia. Akarusha ngumi tano kwa wepesi mno na kwa hasira!
Vuup! - vup! vuup! - vup!
Kinyume na mwili wake ulivyo, alikuwa mwepesi kwenye kufanya maamuzi na kujifyatua. Alikuwa ana haja ya kumpiga Jona kuliko Jona alivyokuwa na haja ya kumpiga yeye.
Alikuwa anatumia nguvu nyingi kushambulia. Lakini mdhaifu kwenye kujikinga, Jona akatambua dhaifu hilo. Lakini hakuwa na haja ya kumuua Alphonce. Hakudhani kama mwanaume huyo anastahili kufa kwa haraka.
Hakustahili kabisa!
Mwanaume huyu alistahili kifo cha taratibu taratibu. Mwanaume huyu alistahili mateso ya kufanya kifo kionekane ni ahueni.
Mwanaume huyu alistahili ahisi angalau robo ya maumivu aliyoyapata mkewe na mtoto wake ndani ya moto mkubwa wa kuteketeza!
"Shit!" Alphonce akalaani. Alikuwa sasa ametimiza idadi za ngumi ishirini pasipo kufanikiwa hata moja! Na wala Jona hakuanza kumshambulia.
Akabadilisha mtindo. Sasa akawa anamshambulia Jona kwa mateke zaidi na ngumi za kushtukiza. Hapa sasa akafanikiwa kumtwanga Jona ngumi moja ya shavu iliyompepesa!
Akatema damu na kujipangusa na mgongo wa kiganja. Akaghafirika mno. Akasahau agano lake juu ya Alphonce, akaanza kumshambulia mithili ya nyuki waliotibuliwa mzingani!
Akapangua ngumi za Alphonce kwa mateke. Na kwa kasi ya radi, kabla Alphonce hajafikisha ngumi juu ya mwili wake, yeye akawa ameshampachika mwanaume huyo mateke matatu!
Alphonce alikuwa mwepesi, ila Jona alikuwa mithili ya umeme. Alikuwa anatambua nyendo za Alphonce kabla hajaamua hata kuzitekeleza.
Alphonce akagugumia maumivu akiwa chini. Kifua kilikuwa kinamuwaka moto. Alimtazama Jona kwa ghadhabu kisha akajikakamua kunyanyuka arudi kwenye pambano.
Akakimbia kumfuata Jona, lakini kabla hajafanya shambulizi lolote, akastaajabu Jona amefyeka miguu yake na yupo hewani kimo cha ndama!
Hajakaa vema, akashindiliwa teke la tumbo lililombamizisha sakafuni na kumcheusha damu lita moja!
Akatulia kwa muda chini. Alikuwa hajielewi kwa maumivu makali aliyoyapata. Kichwa kilikuwa kinamgonga, tumbo lilikuwa linamvuta! Alihisi kiuno pia kimeteguka.
Akamtazama Jona, akamwona mwanaume huyo akiwa amesimama mkono wake wa kushoto upo mfukoni. Akamuuliza;
"Umemaliza?" kisha akacheka akionyesha kinywa chake kilichokuwa chekundu kwa damu. "Wewe mshenzi tu! Mshenzi tu kwangu. Unasikia?"
Jona hakujibu kitu. Alikuwa anamtazama na macho yake mekundu.
"Bado nakumbuka vizuri siku ile," Alphonce akajinasibu. "Mkeo alikuwa anapiga yowe kukuita. Mwanao alikuwa analia kwa namna moto ulivyokuwa unamtafuna!"
Akacheka.
"Ilikuwa ni siku maridadi sana! ... siku maridadi sana. Sitaisahau. Ilikuwa ni siku niliyolipiza kisasi changu cha kwanza dhidi yako. Ilikuwa ni siku niliyokufanya nawe uhisi kile nilichopitia mimi kwa kunipokonya nafasi niliyokuwa nayo jeshini.
Ulinifanya nidharaulike sana. Kila mtu alikuona na kukusifu wewe. Kila mtu alikuona shujaa. Kila mtu akanisahau mimi ni nani. Juhudi zangu zote jeshini zikawa ni bure!"
Akatemea damu pembeni.
"Nilikuchukia sana, na hata sasa pia. Ulinipokonya kile nilichokuwa nacho, lakini ..." akaangua kicheko. "Wewe nimekupokonya zaidi!"
Akacheka tena.
"Bado mimi ni mshindi Jona! Bado mimi ni mshindi!"
Jona akachuruza chozi. Akakunja ngumi yake kwa hasira. Moyo wake ulikuwa unavuja damu. Alimkumbuka mkewe. Alimkumbuka mwanae.
Akasaga meno. Mishipa ya damu ikamsimama kichwani.
"Na hata sasa mimi bado ni mshindi!" Alphonce akaropoka akisimama kwa tabu. Akamjongea Jona apate kurusha tena turufu lake la pambano.
Lakini katika namna ambayo hakuielewa ilitokeaje, akastaajabu kujikuta yupo chini! Kitu pekee alichokuwa anakumbuka, ni kusikia kitu kama upepo ukipita masikioni mwake.
Lakini zaidi hakuweza kuusogeza mwili hata kidole! Ni macho tu ndiyo yalikuwa yanasonga huku na kule.
Hakuuhisi mwili wake kabisa.
"Jona!" Akaita. "Jona! Jona umenifanya nini? Umenifanya nini Jona?"
Jona akamtazama pasipo kusema kitu. Macho yake yote yalikuwa yanatiririsha machozi.
"Nisaidie tafadhali!" Alphonce akaomba. Jona akampa mgongo na kwenda zake ndani. Akachukua mafaili yake na kuondoka akimwacha Alphonce anapiga kelele sakafuni.
**
Saa nne usiku...
Kwa mbali muziki laini ulikuwa unaita. Mazingira yalikuwa yametulia kwahiyo basi ungeweza kusikia vizuri sauti tamu ya kukwaruza ya Michael Bolton akiimba kibao chake matata cha Soul Provider cha mnamo mwaka 1989.
Juu ya kochi, alikuwa ameketi Jona akiwa kifua wazi na kibukta chepesi cha kulalia. Juu ya meza ilikuwa imekaa chupa kubwa ya kinywaji kikali, kando yake kulikuwa kuna yale mafaili aliyoyatoa kwa Eliakimu.
Akanyanyua chupa yake ya kinywaji na kuipeleka mdomoni, akagigida mafundo mawili makubwa. Akiwa amekunja uso, akarejesha chupa hiyo mezani akiisoma jina lake.
_Bacardi 151_
Kwenye lebo yake ya kiasi cha ulevi kilikuwa na alcohol 75.5%! Haikuwa mchezo kabisa!
Jona alikinunua kinywaji hiki maana aliona anakihitaji kwa usiku huo. Huwa anakunywa vinywaji vikali ila siku hiyo alihitaji kikali zaidi na zaidi maana alihisi anaweza akashindwa kulala.
Kila saa alipokuwa anatulia alikuwa anasikia maneno ya kebehi ya Alphonce kuhusu familia yake. Kila aliposikia sauti hiyo, akamkumbuka mkewe. Akamkumbuka mtoto wake kuliko kawaida.
Huwa anawakumbuka, lakini leo hii ilikuwa ni kana kwamba ametoka kushuhudia jengo lake likiwa linateketea. Alphonce alimkumbusha kwa kina. Alikitifua kidonda kilichojenga gamba.
Akashindwa hata kupekua mafaili yale, akabaki anakunywa tu. Baada ya kuongeza mafundo matatu tu ya Bacardi, kichwa kikashindwa kuendeleza kazi, fahamu zikakata, akajimwagia kochini!
Jinamizi lililokuwa linamtesa, leo likarudi kwa nguvu zote.
***