*ANGA LA WASHENZI -- 66*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Alilenga kufanya kazi pasipo kupumzika mpaka majira ya chakula cha mchana amalizie kila kiporo mezani. Lakini hakufanikiwa kwenye hilo. Kwani muda si mrefu akapata taarifa mkewe amefariki kwenye ajali mbaya ya gari iliyotokea maeneo ya Makumbusho.
Akachanganyikiwa!
ENDELEA
Akafanya kwenda hospitali alipoambiwa mkewe amekimbiziwa, huko kweli akathibitisha mwanamke huyo amefariki. Mwili wake uliokuwa umeharibika vibaya ulikuwa umeshalazwa mochwari.
Lakini asiamini, akaenda mpaka kuutazama mwili huo mochwari, labda unaweza ukawa si wa mkewe, wameufananisha! Huenda akawa ni mtu mwingine aliyetumia gari la mkewe. Ndio. Inawezekana. Ama kuna mtu aliyeliiba hilo gari na kukimbia nalo, hatimaye akapata ajali!
Alitengeneza kila picha kichwani akijaribu kumnusuru mkewe. Aligeuza kila taarifa aliyoambiwa ili tu amuokoe mkewe kifikra lakini haikubadilisha ukweli. Alikuwa ndiye yeye. Hakuweza kurudisha mikono ya muda nyuma.
Mwili uliokuwa umelala kwenye jokofu za mochwari haukuwa wa mwingine isipokuwa wa mwanamke aliyemzalia watoto.
Haukuwa unatamanika hata kidogo. Paji la uso lilikuwa limechanika. Amevunjikavunjika. Boka akashindwa kujizuia kutoa machozi.
"Alikuwa na mwenzake ndani ya gari. Yeye amenusurika kifo, lakini yu hoi hajiwezi. Taarifa alizozitoa kabla hajaenda kupoteza fahamu ni kwamba walikuwa wanafuatiliwa kwa muda mrefu kabla ajali hiyo haijatokea.
Kwahiyo kwa namna moja ama nyingine hii haikuwa ajali bali tukio lililopangwa," alisema polisi aliyepewa jukumu la upelelezi, kwa jina inspekta Geof.
"Sasa kama ni hivyo, mnangoja nini kumtia nguvuni huyo mshenzi?!" Boka akafoka kwa hasira. "Au sio kazi yenu hiyo?"
Inspekta akamsihi apunguze jazba, mambo hayapelekwi mrama kiasi hiko. Tukio ni kubwa na linahitaji utulivu mkubwa kumbaini mhusika, la sivyo wataishia kuwabambikia watu kesi.
Lakini akamuahidi kwa dhati jambo hilo halitachukua muda kukaa bayana. Amuamini. Akaendaze.
Akamuacha Boka hospitalini akiwa ameshikilia kichwa kwa mawazo. Ni nani amuue mkewe? Kwasababu gani haswa? Alijiumiza zaidi na hayo maswali asiyokuwa na majibu. Akaishia kuvuja machozi, zaidi akapandwa na hasira maradufu.
**
Kwenye vioo vya simu ... whatsapp App.
'Umehakikisha amekufa?'
Typing...
'Ndio, nimefika hospitali kama mwandishi wa habari. Yupo mochwari.'
Typing...
'Na mazingira ya ajali?'
Typing...
'Hamna mtu anaweza jua. Nimefanya kiustadi.'
Typing...
'Nimepata taarifa hakuwa mwenyewe ndani ya gari'
'Ndio alikuwa na mwanamke mwingine yeye hajafa yupo ICU'
Typing ... ikaacha ... typing tena ...
'Una uhakika huyo mwanamke uliyemwacha hai hakukuona?'
'Tukio lilitokea kwa kasi sana hakuniona'
Typing ...
'Kama huna uhakika ni kheri ukammaliza. Hatuna muda wa kusumbuana na polisi'
Typing ...
'Nakuhakikishia hakuna haja hiyo'
'Ok. Stay low. Njoo tuonane.'
Tap ... Offline ...
Moja wa mtu huyu anayechat alikuwa ndani ya basi la mwendokasi. Akazamisha simu mfukoni. Alikuwa amevalia suruali ya kitambaa rangi ya kijivu na viatu vyeusi ving'aavyo.
**
Muhimbili hospital, Dar.
Mlango ulifunguliwa taratibu akaingia mwanaume ndani ya shati jeupe na suruali nyeusi. Akamtazama Alphonce kitandani, akamwona akiwa amelala.
Huu haukuwa muda wa kutazama wagonjwa. Hakuwa amepewa ruhusa wala kuonana na mtu yeyote yule kabla hajaingia humu ndani.
Alikuwa ni Kericho. Mwanaume mzito mwenye rangi maji ya kunde. Macho yake yalikagua chumba upesi kisha akamsogelea Alphonce na kumbana pumzi kwa mikono yake mipana iliyoshamiri mishipa ya damu.
Alphonce aliyepooza angefanya nini kuukomboa uhai wake? Kericho akatekeleza zoezi lake kwa wepesi sana. Alimuacha Alphonce baada ya kusikia mlio wa kuashiria mapigo ya moyo yamekata.
Hakutoka hata jasho. Alphonce akawa amekufa.
Akatoka ndani ya chumba hicho upesi. Kama alivyoingia, hakuna aliyemuona. Akayeya zake.
"Fagio limevunjika," akasema akibinyia simu sikioni.
"Nilikwambia," sauti ikamjibu toka simuni. "Haya leta nilione."
Kericho akakata simu akiiweka Muhimbili mgongoni mwake. Akajipakia kwenye taksi na moja kwa moja akaelekea Mbweni. Akashukia barabarani na kumkabidhi dereva pesa yake alafu akatembea kwa mwendo wa dakika sita kabla hajazama ndani ya nyumba fulani kubwa ambayo bado haikuwa imemaliziwa kupauliwa.
Humo akakutana na Kamanda akiwa amevalia sare ya traksuti nyeusi.
"Umehakikisha kila kitu kipo sawa?"
"Kila kitu kipo kwa mstari," akasema Kericho akitabasamu. Kamanda naye akatabasamu kujibu.
"Safi sana. Nilikuamini ndo' mana nikakupatia hiyo kazi."
Lakini ikatokea upesi sana, Kericho akaona chepeo na jembe kwa umbali wa hatua kadhaa nyuma ya Kamanda. Kabla hajauliza, akajikuta amedidimiziwa kisu tumboni mara tatu!
Chop! Chop! Chop! Akadondoka chini akimimina damu lukuki.
"Hakuna siri ya watu wawili Kericho," Kamanda akasema akimtazama Kericho akijifia.
Kericho akamnyooshea kidole Kamanda mkono wake mmoja ukiwa tumboni umemezwa na damu. Macho yake yalikuwa mekundu. Akatamani kusema jambo lakini hakuweza. Akamtazama Kamanda mpaka roho yake inaacha mwili.
"Kwaheri afande," Kamanda akamfunika macho kisha akachimba shimo na kuufukia mwili wa Kericho humo.
Akakung'utia jasho pembeni alafu akaendea gari lake na kujipakia, akayeya.
Njiani ...
"Ndio, mheshimiwa," akasema akibinyia simu sikioni kwa mkono wake wa kushoto wakati wa kuume ukishikilia usukani.
"Ndio, nimesikia mheshimiwa pole sana kwakweli ... yah! Ndo nipo njiani nakuja ... usijali, nitakuwa hapo muda si mrefu."
Akakata simu.
Nusu saa baadae akawa ameshafika hospitali, yu ndani ya sare, anateta na Boka juu ya ajali ya mkewe. Akampatia Boka pole za kutosha baada ya kumpa kumbatio na mkono wa kheri.
"Nakuhakikishia, mheshimiwa, lazima atakamatwa!" Kamanda akasema kwa sura ya msisitizo. "Atatafutwa kokote alipo. In fact, nina wapelelezi wazuri sana hawataniangusha."
Boka akashukuru.
"Lakini nashangazwa sana, bora ingekuwa mimi ningesema nina maadui wa kisiasa. Lakini kwa mke wangu, mke wangu, ana makosa gani?" Boka akateta kwa uchungu.
"Huwezi jua, Mheshimiwa. Hata hao maadui wako wewe wanaweza wakatumia njia hiyo," Kamanda akamueleza kisha akamuuliza: "kuna yeyote unayemshuku kwenye hili?"
Boka akafikiria kidogo. Akabinua mdomo wake akitikisa kichwa.
"Sidhani." Akafikiri tena. "Sidhani kwakweli."
"Tuliza kichwa," Kamanda akamsihi. "Najua kwa sasa unafikiri mengi lakini baadae utatengemaa kimawazo. Nijulishe."
"Sawa, nitakubarisha. Ahsante."
Wakaachana. Baadae kwenye vyombo vya habari majira ya usiku, Kamanda akanguruma akiongelea kifo cha mke wake Boka na inspekta Alphonce.
Kwa upande wa mke wa Boka akasema uchunguzi unaendelea huku akisisitiza watu waache kusambaza maneno yasiyothibitishwa huko mitandaoni, waache polisi wafanye kazi yao. Kwa upande wa Alphonce akasema mwanaume huyo amefariki kwasababu za kiafya.
"Shit!" Jona akalaani. Alikuwa anatazama taarifa ya habari akimwangalia mkuu wake wa kazi. Yeye pekee ndo alikuwa anajua mwanaume huyo anaongopa juu ya Alphonce.
Aliamini Kamanda ndiye kamuua mdhalimu huyo. Hakuna mwingine.
Ila hakujali.
'Acha wafu wazikane wenyewe.'
Punde simu yake ikaita. Alikuwa ni Kamanda. Akajiuliza anataka nini? Alipopokea Kamanda akamuuliza kama amesikia ya Boka.
"Ndiyo nimetoka kuona kwenye habari," Jona akajibu.
"Ok," Kamanda akaitikia. "Sasa hiyo kazi nimekupatia uifanye. Nataka huyo muuaji apatikane. Sawa?"
Kimya.
"Sawa?"
"Sawa, mkuu!"
**
- JONA ATAYAVUMBUA YAPI KWENYE AJALI HIYO?
- MTU ALIYEVALIA SURUALI YA KITAMBAA YA KIJIVU NA VIATU VYEUSI NDANI YA MWENDOKASI NI NANI?
- KERICHO NDIYO KAENDA NA KILA YAKE?