*ANGA LA WASHENZI -- 69*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
"Ndio, Jona hapa, nina shida na wewe haraka iwezekanavyo."
"Nini shida Jona? Mbona upesi hivyo? Ni mambo ya ile picha?"
"Hapana! Ni kuhusu ajali ya mke wa mheshimiwa!"
"Ooh! My God. Jona, I didn't do it. Honestly!" (Ooh! Mungu wangu. Jona, sijalifanya hilo. Ukweli kabisa!)
ENDELEA
Jona akamtaka waonane kesho kwa ajili ya maongezi zaidi. Akakata simu na kuendelea kuwaza. Kuna yeyote zaidi Miranda?
Aliamini hata kama kuna yeyote zaidi ya Miranda basi njia ya kumpata mtu huyo ni kwa kupitia Miranda tu. Atampatia namna ya kupiga hatua hiyo.
Akatulia baada ya muda kidogo, akampigia simu Marwa. Simu ikaita pasipo matokeo. Akagundua Marwa atakuwa yupo kazini kwa muda huo, hivyo ni ngumu kupokea!
Akaachana naye avute subira mpaka majira ya mchana, aotee muda mwanaume huyo atakuwa akipata chakula cha mchana.
Muda ukasonga.
Kwenye majira ya mchana, saa saba na robo, Marwa akawa kantini akipata chakula. Alikuwa ameketi mwenyewe akijitenga kidogo na wenzake. Na kwakuwa Marwa hakuwa amezoeana na yeyote, basi hakuna aliyemuwazia.
Lakini mwanaume huyo alikuwa anamngoja Panky. Alitegemea atakuja kula na hivyo basi waketi pamoja kwa hapo pembeni.
Muda ukasonga kidogo mpaka majira ya saa saba na dakika ishirini na tano, Panky akaonekana akichukua chakula. Akatazama huku na kule pa kukaa, Marwa akanyoosha mkono amwone, Panky akaenda huko.
"Nilikuwa nakungoja muda wote huo."
"Aanh! Kuna kazi kidogo nilikuwa nazimalizia. Yani huko waliponipeleka ni kama mwehu, kazi kazi kila saa simu tu!"
"Wamekupeleka wapi kwani?"
"Uhasibu na mawasiliano."
Vile vile kama Marwa alivyokuwa anawaza. Ni ngumu sana kwa Sheng kuajiri mtu mpya kwani inakuwa ngumu sana kwa mtu huyo kujua na kuufuata utaratibu wa kazi chini yake hivyo hupendelea kutoa mtu huku na kumweka pale, kama haitaathiri.
"Ila huko hamna kiyoyozi," Marwa akatania. Wakacheka. Wakawa kimya kidogo wakitafuna.
"Sasa kuna kazi ya kufanya," Marwa akaingizia. Kabla hajaendelea simu ikaita, alikuwa ni Jona.
"Yah! Ndo nipo naye ... poa, baadae."
Akaweka simu mezani, na kumwambia Panky maagizo toka kwa Jona. Nini anatakiwa kufanya akirejea ofisini kwake.
"Hope tumeelewana!" Marwa akamalizia.
"Usijali, nitalifanyia kazi. Na nadhani hao watu watakuwa wameshaondoka. Taarifa zao zitakuwepo kule kimalipo. Nitatazama."
Wakamalizia kula, wakarejea kazini. Panky akaanza kukagua nyaraka za risiti na taarifa kadhaa kwenye tarakilishi, pesa zilizotoka hivi karibuni.
Akanoti pembeni na kumtumia ujumbe Marwa kwa kuhofu baadae anaweza akakawia kutoka hivyo hatokutana naye. Alipotuma ujumbe huo, akaendelea na kazi yake kama kawaida.
Lakini baada ya muda kidogo, akaja kuitwa.
"Unahitajika ofisini kwa mkuu," alisema mwanaume mmoja akisimama mbele ya Panky.
"Mimi?"
Japo hakujua anaitiwa nini, moyo wake ukaanza kumtwanga. Alipaliwa na hofu. Kuitwa na mkuu halikuwa jambo dogo hata kidogo.
"Ndio, wewe!" Akasema mleta wito.
"Sawa, nakuja," Panky akajibu.
"Nakungoja twende," mleta wito akamsihi.
"Kwani lazima twende wote?"
"Ndio! Nimeambiwa nikupeleke."
Hapa Panky akazidi kupata hofu. Ina maana wanahisi anaweza kukimbia? Akaacha kazi zake na kuongozana na mwanaume huyo mpaka ofisini mwa Sheng. Alipofika, yule aliyemsindikiza akaagizwa angoje nje.
"Panky," Sheng akaita huku akitazama karatasi kadhaa juu ya kashelf kake kadogo ka kioo juu ya meza.
"Naam, mkuu!" Sheng akaitikia. Mikono yake ilikuwa inatetemeka na kujawa jasho.
Sheng akamuuliza juu ya kazi aliyompatia hapo kitambo ya kummaliza Jona. Panky kusikia hivyo akaishiwa nguvu! Sasa akajua mwisho wake umewadia.
Sheng akiongea kwa lafudh yake ya kimandarin, akamwambia Panky kwamba siri yake isingeweza kudumu kwa muda. Alimpatia kazi na kwa kumdharau hakuitenda, akaja kumlaghai.
Na kwa asili ya uongo wake, inaonyesha ana mahusiano na Jona kwani mwanaume huyo alihama mara moja baada ya yeye kuja kusema amemmaliza.
Panky akalia kuomba msamaha. Hakuwa na lingine sasa la kufanya zaidi ya hilo. Akalia abakiziwe uhai wake. Atakuwa mtiifu kwa Sheng na hatorudia tena kufanya kosa.
Lakini kwa Sheng hayo yote yalikuwa makelele. Hakumwelewa Panky hata kidogo. Akafungua droo yake na kuchomoa binduki ndogo, akaitazama ina risasi ngapi.
Nne.
Akaikoki na kumwonyeshea Panky mdomo wa bunduki kwenye paji lake la uso.
"Nina mke na watoto wananitegemea. Pia wazazi huko kijijini. Tafadhali bakiza uhai wangu!" Panky akawaga machozi.
Sheng akabofya kitufe cha bunduki mara nne! Chuma zikatoboa kichwa cha Panky na kumlaza chini akiwa mfu!
Baada ya risasi hizo, yule mwanaume aliyeambiwa angoje nje, akaingia ndani na kubeba mwili wa Panky.
**
"Sasa? Si naweza nikatoka?" Akauliza Miriam. Sasa alikuwa ameboreka zaidi kiafya. Alikuwa anawasiliana na mama aliyempokea ambaye alikuwa mlangoni akitazama huko nje.
Ni majira ya jioni sasa. Jua lilikuwa linaelekea kuzama. Na siku hii Miriam aliona inafaa kwake kutoroka.
Tayari mtoto alishaenda kukagua huko nje mpaka barabarani. Akarejesha taarifa kwamba kupo salama.
"Ndio, njoo," mama akamruhusu, Miriam akatoka mpaka huko nje, akamkumbatia mwenyeji wake kumuaga akimshukuru sana. Na akamuahidi atarudi kuja kumshukuru siku moja.
"Bado hutaki nikusindikize?" Akauliza mama mwenyeji.
"Hapana, hatari niliyokuweka kwa muda wote huo inatosha. Acha hili nipambane mwenyewe."
Miriam akaanza kutembea akitazama chini. Kulikuwa na kaumbali kutoka hapo mpaka kituoni. Alikazana kutembea mkononi akiwa amebebelea kamfuko. Na mwili wake ukiwa umehifadhiwa ndani ya dira chakavu alilopewa na mwenyeji wake.
Akiwa amekaribia kituoni, kuna mtu mmoja akamuita.
"We mwanamke!"
Hakugeuka. Akakazana kutembea. Sauti ikamuita tena, we mwanamke we mwanamke. Ila hakugeuka abadani.
Akahisi anafuatwa. Watu walikuwa wengi kiasi chake hivyo kidogo akawa hana woga. Akatembea kwa kasi mpaka akafika kituoni kungoja basi.
"Napanda hilo linalokuja!" Akajisema kifuani. "Hata kama limejaa vipi."
Akatazama kushoto na kulia kwake, watu wote walikuwa wametulia, lakini akamwona mwanaume aliyemtilia shaka. Mwanaume huyu alikuwa amevalia shati jeusi, mweupe kwa rangi mwenye macho mekundu.
Naye huyu mwanaume akamtazama Miriam, wakakutana macho kwa macho. Moyo wa Miriam ukadunda kwa kasi.
Akatazama barabara. Gari alilokuwa analingojea lilikuwa limekaribia kufika. Akaendelea kuapia moyoni kwamba lazima alipande gari hilo, hata iweje.
Gari likasimama, yalikuwa ni yale mabasi ya zamani sana. Lilikuwa linamwaga moshi mzito mweusi ambao ukiujumlisha na vumbi la barabara, basi kupata mafua ama matatizo ya kifua ilikuwa haiepukiki.
"Arusha town hiyo!" Konda akapaza sauti. Lakini gari lilikuwa limejaa mno. Hakukuwa hata na pa kukanyaga sembuse pa kusimama.
Lakini wanaume wawili wakaliwahi, ikiwemo na Miriam watatu, wakang'ang'ana kulidandia. Wanaume wakafanikiwa, Miriam akaambiwa na konda angoje lijalo, hataweza.
Hakuwa namna akangoja. Akatazama mahali alipomuona mwanaume yule aliyekuwa anamtilia shaka, hakumwona!
Akajiuliza kaenda wapi? Akaangaza macho huku na kule lakini kabla hajamaliza msako wake wa macho, ghafla akasikia sauti ya gari lingine laja.
Akajiweka sawia kung'ang'ana. Sasa gari liliposimama akawa wa kwanza kufika mlangoni, akazama ndani!
Japo alikuwa amebanwa haswa, hakujali. Alichotaka ni kutoka tu eneo hilo. Lakini kuna jambo.
Kuna jambo ambalo hakuwa analifahamu.
Nyuma yake alikuwa amesimama mwanaume yule aliyekuwa anamtilia hofu. Kumbe naye aligombania gari hilo na kuzama humo ndani.
Miriam alikuja kufahamu hilo baadae baada ya kukaribia Arusha town! Lakini ajabu ni kwamba, hakuelewa kuna nini ama nini kilifanyika, akajikuta anapoteza fahamu.
"Ni dada yangu, anaumwa!" Miriam alisikia sauti ya mwanaume ikisema huku yeye akipotelea kwa kudhoofu.
Alihisi kabisa sauti hii itakuwa ni ya mwanaume yule aliyemtilia mashaka, lakini hakuweza hata kupayuka wala kujikomboa.
Pap! Akawa gizani kamili asijue kinachoendelea.
**