*ANGA LA WASHENZI (MSIMU WA PILI) -- 09*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Leo hakuwa na pombe ya kumsaidia kulala. Leo hakuwa na Marwa wa kupiga naye soga. Leo alikuwa mwenyewe. Si akiegemea kochi bali ukuta.
Usiku wa aina yake.
ENDELEA
Saa tisa jioni, Ramada hotel.
Vx nyeusi iliingia na kupaki, ndaniye wakatoka Boka na Miranda walioshikana mikono kuingia ndani ya hoteli. Wakapata chakula na kujikuta wamejilaza kwenye vitanda vyembamba karibu na swimming pool.
Walikuwa hapo kurefresh akili zao baada ya kupitia magumu kadhaa hapo nyuma. Boka akifiwa na mumewe wakati Miranda akiwa kwenye kiti-moto baada ya mauaji hayo.
Lakini hatimaye yote yamepita. Yote yamekuwa kheri sasa. Ulikuwa wakati wa kukaa tena pamoja na kuangazia yajayo, tena katika namna ya pekee kabisa haswa baada ya kuachwa na nafasi sasa ya kujivinjari pasipo woga.
Hakukuwa na mtu wa kuwanyima kumeza mate tena.
"Unapenda sana kuja hapa?" Aliuliza Miranda ndani ya bikini. Umbo lake lilikuwa linaonekana vema na pengine kukushawishi ukamwona Boka hakufanya makosa kabisa kuwa 'zezeta' hapa.
Alikuwa anavutia hasa. Kwa rangi yake, uso mpaka na umbo. Na hata namna alivyokuwa anaongea, alivutia kusikilizwa.
"Pametulia sana hapa kuliko kwengine, haswa nyakati za siku za wiki. Ukija hapa you get a real refreshment," alieleza Boka aliyejivunia kuwa na mwanamke mrembo pembeni yake.
Miranda akadaka glasi juu ya kameza kadogo pembeni ya kitanda, akanyonya mafundo mawili kabla hajalaza kichwa chake na kuuliza:
"So nini plan yako kwa sasa?"
Boka akatabasamu kwa mbali. Akageuza mwili wake na kumtazama Miranda.
"Kukuoa," akajibu kwa ufupi.
"Are you serious?" Miranda akaigiza kustaajabu.
"Why not, nipo serious."
Miranda akanyamaza kidogo akiwaza kichwani. Kwa wanawake wengine hii ilikuwa ni 'a million dollar chance'. Sio tu kwenye swala la kuolewa kama kila mwanamke ambavyo angependa kuwa na mume na familia yake, la hasha, bali kuolewa na mtu mwenye nafasi serikalini.
Mtu mzito mwenye pesa. Haikuwa jambo dogo hata kidogo. Lilikuwa ni jambo la kutetemesha mwili na kuukimbiza moyo upesi haswa ukifikiria zile 'shopping' za Dubai, safari za China na Afrika ya kusini.
Lakini kwa Miranda, hili halikuwahi kuwa lengo. Kuolewa. Achilia mbali kuolewa na Boka. Mwanaume huyu hajawahi kumvutia hata chembe. Hamsisimui. Alikuwa hapo kwa ajili ya kufanikisha malengo yake tu.
Hapa akamkumbuka mke wa Boka.
Japokuwa alikuwa ni adui kwenye 'mishe' zake, lakini kwa njia moja ama nyingine alikuwa anamhitaji. Kumtuliza mumewe asifikirie maswala ya kumuoa.
Sasa mke huyo amefariki. Boka atakuwa mwepesi kutafuta mwanamke mwingine na hata kumuoa.
Sasa nini maana yake hii? Inabidi kazi itendeke haraka iwezekanavyo kabla ya mambo haya ya kuoana. Aliwaza Miranda.
Akanyanyua tena glasi ya juisi na kupeleka mrija mdomoni akiwa amejilaza. Akanywa mafundo mawili mepesi akichambua cha kunena.
"Nadhani unajua cha kufanya, mheshimiwa. It is obvious baba yangu hatokukubalia kama hutomfanyia kazi yake."
"Najua!" Boka akadakia. "Si nimeshamkubalia?"
"Kazi moja!" Miranda akajistaajabisha. "You have to show wewe ni mtu anayeweza kumuamini na kumtegemea. Unajua hawa wazungu ni ngumu sana kumwamini mtu, lakini akishakuamini tu basi."
"Kwahiyo unanishauri nini?"
"Mpe sababu ya kukuamini. Tena si moja, kadhaa."
"Nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu. Ila vinataka muda. Huoni nitakawia kukuoa?"
"Kwanini wahofu kuhusu hilo swala? Wadhani kuna mtu atakuja niiba au?" Miranda aliuliza kwa mishebeduo ya kike. "Mimi ni wako tu. Wala usiwe na papara. Hata kwa muda huo utakaokuwa unafanya mambo yako, mimi nitakuwa pembeni yako. Kuna shida?"
Japo Boka hakujibu, alionekana kuafiki alichoambiwa. Hakuwa na usemi.
"Vipi ile safari ya Afrika kusini?" Miranda akauliza. "Umeischedule lini?"
"I think nitaenda huko wiki ijayo Jumatatu."
Alivyojibu hivyo ni kana kwamba Jumatatu hiyo ilikuwa mbali. Siku hiyo ilikuwa ni Alhamis, kwahiyo Jumatatu ilikuwa ni hatua tatu tu kuifikia. Miranda akatabasamu. Hili halikuwa jibu baya kwake kabisa. Lilimaanisha ajiandae.
Lakini kama haitoshi, Boka akamwambia anataka kumkabidhi biashara ya mkewe aiendeshe. Kampuni ile ya vipodozi na urembo, iliyosambaa Afrika mashariki, iwe chini yake.
Swala hili likawa mtambuka kwa Miranda. Hakutaka kuingia kichwakichwa hapa. Alihofia kilichomkuta Mke wake Boka. Lakini pia kujianika kwa maadui zake.
"Huoni tunapaswa kungoja kwanza kesi ya mkeo iishe?" Akauliza.
Kichwani kwake akiwaza mpaka kesi hiyo ikiisha, Jona atakuwa amemsaidia ku 'clear' maadui zake hawa akawa salama.
Hakujua Jona kwa wakati huo alikuwa rumande. Na kesi imesharudishiwa mikononi mwa inspekta Geof, ambaye hafahamu yale aliyokuwa anayafahamu Jona.
Hata kidogo!
**
Baada ya mahojiano yake ya muda mfupi kulingana na muda aliopewa na daktari, inspekta Geof alisafisha koo lake na kusimama akimtazama mwanamke aliyejilaza kitandani.
Mwanamke huyu alikuwa ni shoga yake marehemu mkewe Boka.
Alikuwa anapata wakati mgumu sana kuongea. Mwili wake ulijawa na majeraha makubwa. Na maumivu aliyokuwa anayapata hayakuwa yanamithilika. Kama si sindano za kupunguza maumivu alizokuwa anadungwa, angekuwa analia muda wote.
Ukimtazama ungemuonea huruma. Na kama ungekuwa na moyo mdogo basi isingekuwa ajabu ukajaza machozi machoni.
Hii likazidi kumfanya inspekta Geof aone kuna haja ya kumtafuta mtu aliyehusika na hili kwa nguvu zote. Awajibishwe kwa mujibu wa kile alichokitenda.
Akashusha pumzi ndefu. Mkono wake wa kuume ulikuwa umeshikilia notebook na kalamu.
"Ahsante sana. Ugua pole. Nitakuja kukuona tena karibuni."
Akatoka ndani ya hospitali na kuonana na daktari, kisha akaenda zake kwenye gari lake na kutulia humo kwa dakika kadhaa. Akapitia yale maelezo aliyopewa.
Yote yakamjengea mantiki kumbe mauaji yale ya mkewe mheshimiwa yalikuwa ni kisa cha kimapenzi. Yalikuwa yamesukumwa na wivu wa mapenzi.
Akatikisa kichwa chake kisha akazungushia duara kwa jina la Miranda kwenye notebook, na kuandika kando: 'the primary target'.
**
"Nilikuambia usije," Jona alilalama akiwa amekunja sura. Mikono yake ilikuwa imebana nondo za lupango kwanguvu kana kwamba anataka kuzing'oa.
Alimtazama Marwa kwa macho makali. Lakini Marwa aliyekuwa amebebelea mfuko mweusi wa rambo, amesimama mbele yake, alikuwa akimtazama kwa huruma.
"Lakini nitawezaje kukaa nyumbani kwa amani na wewe upo humu?" Marwa aliuliza.
"Ni hatari, Marwa," Jona akamjibu akilalama. "Unadhani nakutania ninavyokuambia hivyo?"
"Kama ni hatari basi tuwe wote. Siwezi nikakaa nyumbani na sijui huku unaendeleaje. Unataka nije nisikie wamekuua na kukuzika pasipo kukuona? Nitakaaje nyumbani nikila na kunywa huku sijui kama tumbo lako limepata kitu? Chakula kitashuka? Kama ni hatari na kuniua, basi waniue! Nimeshapoteza wazazi wangu, sina cha kupoteza tena. Na wewe upo ndani, ntajificha milele?
Ukifa nitapata nguvu ya kulia na wakati ukiwa hai nilishindwa hata kunyoosha mkono kukusaidia? ... siwezi Jona."
Marwa akafungua mfuko wake. Ndaniye kulikuwa kuna hotpot la wastani na chupa ya maji. Akampatia Jona ale.
Ni kama vile alikuwa anajua mwanaume huyo hakula tangu alipowekwa humo ndani.
"Wamekuruhusu kuja humu?" Jona aliuliza.
"Hapana," Marwa akajibu. "Hawakuniruhusu, nikakaa hapo nje siku nzima mpaka askari fulani akaniita na kuniuliza kama nina shida yoyote. Nilipomweleza nimekuja kukuona wewe, akanisadia. Lakini ameniambia nifanye upesi."
"Askari gani huyo?" Jona akauliza akila. Marwa akampatia maelezo yaliyomfanya Jona kutambua ni Afande Devi.
Baada ya muda mfupi, akampatia Marwa vyombo aende zake upesi.
"Kuwa makini sana," akamsisitizia. Marwa akapokea vyombo na kabla hajaenda, akamkumbushia Jona jambo.
"Nilitafuta kuhusu Elliot Parker."
"Ukapata nini?" Jona akawahi kuuliza kufupisha maongezi.
"Nimetafuta kote lakini sijaona hilo jina kama ni mpelelezi wa aidha FBI, CIA, au INTERPOL."
"Nilijua tu!" Jona akajisemea. "Sasa nenda. Fanya upesi! Kuwa makini sana."
**
"Ni nani yule?" Aliuliza koplo Massawe akimtazama Marwa anaishia. Kaunta alikuwa ameketi afande Devi akiwa anapekua daftari kubwa.
"Ni kijana flani hivi," Afande Devi akajibu akifanya jitihada za kukatisha maongezi hayo kwa kufunguafungua daftari kujifanya yupo 'bize'.
"Kijana gani na alikuja hapa kufanya nini?" Koplo Massawe akasisitizia. Alimtazama afande Devi kwa macho ya mashaka. Na kabla afande Devi hajajibu, akasema:
"Unajua tumekatazwa kumruhusu yoyote kumletea chakula yule jamaa. Kwanini ukamruhusu aende huko na mimi nilimzuia?" Massawe akafoka.
"Sikujua," afande Devi akajitetea. "Nilimkuta hapo nje kwa muda mrefu. Nikamuuliza akasema haja yake. Nikaona si vibaya ku-"
"Usirudie tena!" Massawe akamkatiza. "Sawa?"
"Sawa afande!"
**
- MIRANDA ANARUDIWA TENA NA MKONO WA POLISI USIOMJUA. ATASALIMIKA?
- NINI HATMA YA JONA ANAYEFANYIWA VISA RUMANDE?
- NAYO MIENENDO YA MARWA ITAMBAKIZIA UHAI?
Sent from my SM-J110F using
JamiiForums mobile app