*ANGA LA WASHENZI II -- 23*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Hili lamaanisha na kuonyesha namna gani serikali yao inavyowajali, na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata afya bora akaijenge nchi kwa kufanya kazi."
Ilikuwa sauti ya mkuu wa mkoa.
ENDELEA
Na kweli fursa ikachangamkiwa ipasavyo. Watu wenye matatizo mbalimbali wakajaa kwenye meli na kutibiwa bure kabisa. Lakini changamoto ikizuka kuwa wagonjwa walikuwa wengi mno hata wengine wakarejea majumbani pasipo kupata huduma wanayoihitaji.
Baadae usiku kwenye televisheni, habari ikaruka na baadhi ya wananchi waliopata huduma wakoipongeza serikali kwa msaada huo toka nje kwa namna ambavyo walipata mapokezi na huduma za kisasa.
Na hapohapo habarini, kiongozi wa meli hiyo akapata kuongea, pamoja pia na kiongozi mkuu wa mkoa. Wakanena namna uhusiano wao unavyoimarika na kwa namna gani wataendelea kusaidiana zaidi.
**
Saa tatu usiku, Hongkong
Siku yake nzima haikuwa na mafanikio, tunaweza tukasema hivyo kwani kitu alichokuwa amekiendea hakuwa amekipata hata kidogo. Bwana Lee akashusha pumzi, kisha akadaka kiuno. Akatazama saa yake, majira yalikuwa yamemtupa mkono.
Akawaza kuondoka sasa. Pengine akirudi kesho anaweza kumkuta huyu meneja ahusikaye na uwanja huu uliopo ghorofa ya tatu, ambapo ndipo Chen Zi alikuwa anafanyia mazoezi enzi za uhai wake.
Na endapo siku hii ikienda bure, itakuwa hasara kubwa sana kwake maana muda unazidi yoyoma. Alijua wazi hatakiwa kupoteza hata sekunde huko Hongkong maana anaweza hitajika na Sheng mara moja akakosekana.
Akanyanyuka, na kuvaa miwani yake meupe isiyo ya macho bali urembo wa kuficha identity yake. Akachomeka mikono yake mfukoni, kisha akatembea kufuata lifti. Akangoja kidogo, mara ikafunguka na mzee mmoja mfupi mnene mwenye nywele nyeusi na kiwaraza kwa mbali, akatoka kwenye lifti akitembea kwa ukakamavu.
Lee akamtazama mzee huyu. Alikuwa mwenyewe. Amevalia shati na koti la kizibao lililofumwa na ngozi. Chini alivalia suruali brown ya kadeti na kumalizia na raba.
Lee akahisi pengine huyu mwanaume ndiye anahusika na uwanja huu. Mavazi yake yaliakisi mtu wa michezo. Basi akaachana na lifti na kumuita huyu Bwana. Hakugeuka, akanyoosha tu mkono wake kumwambia Lee amefunga hilo eneo, na kwa sasa haitaji mteja yeyote.
Lee akamweleza yeye si mteja, yupo hapo maana ana shida fulani, anaomba amsikize. Yule Bwana akasimama na kumtazama kwa shari. Kisha akamuuliza shida gani hiyo?
Lee akatabasamu kwanza. Hakutaka kumhofisha bwana huyu. Alijitahidi kuwa rafiki kadiri alivyoweza. Akasema kwa ustaarabu kuwa alipewa taarifa kwamba Chen Zi alikuwa akifanyia mazoezi hapo. Basi kwa namna gani atapata mtu anayefahamiana na huyo jamaa?
Yule Bwana akadhani pengine Lee ni polisi. Akastaajabu na kumwambia akiwa amekunja uso, ni kwa mara ngapi watakuja hapo kumsumbua na maswali ya mara kwa mara? Amechoka.na hana muda tena. Na basi ndiyo maana ameamua kutokujihusisha tena na mambo ya burudani.
Lee akatabasamu na kumuahidi hiyo itakuwa mara yake ya mwisho kuja hapo. Hatopenda kumbughudhi, ila kama asipojali amsaidie, naye kwa namna fulani atamfurahisha.
Aliposema hayo alikuwa akigusa mfuko wake. Yule Bwana akatabasamu. Akakunjua uso wake na kumtazama Lee kisha akampasha habari muhimu.
Anajua mengi kuhusiana na Chen Zi, ila swala la kifo chake kimekuwa ni utata hata kwake. Lilikuwa la ghafla mno! Kwa mara zote ambazo Chen Zi alikuwa akifanya mazoezi hapo, alikuwa anakatazama hata washirika wake kutumia sigara, ilikuwa ni ajabu kuja kupewa taarifa kuwa amekufa kwa kuzidisha dozi ya madawa!
Bwana yule akatikisa kichwa. Akatazama chini kwa masikitiko. Alikuw amemkumbuka Chen Zi, si tu kama mteja wakw bali kama mwanae kwa namna alivyokuwa mkarimu.
Lakini asipoteze muda zaidi, akamwelekeza Lee kumhusu mpiga gitaa wa Chen Zi. Huyo anaitwa Chong Pyong. Ni kijana mfupi aliyetoboa kila sehemu ya uso wake. Tangu Chen Zi alipokufa, alijiunga kwenye bendi moja maarufu Hongkong na Shanghai. Wamekuwa wakipiga muziki wao kwenye hoteli mbalimbali!
Akamtajia baadhi ya hizo hoteli. Lee akamshukuru kwa kumpatia kiasi fulani cha pesa kisha akaenda zake.
Basi akashika njia ya kuelekea kituo cha mabasi maana muda bado ulikuwa unaruhusu upatikanaji wake, pia hii itamsaidia kutunza fedha zaidi, kichwani akipanga kutumia taksi wakati wa kurudi tu.
Baada ya muda mfupi, akawa amefika kwenye moja ya hoteli aliyoambiwa na yule Bwana. Bahati akakuta tangazo likinadi uwepo wa ile bendi aliyoambiwa kuwa ndaniye ndo' yupo Chong Pyong.
Ikamlazimu alipie kiingilio kikubwa sana kuingia humo maana ilikuwa hoteli ya 'watu wazito'. Akatafuta mahali pa kukaa, na kisha macho yake yakaangaza mbele kwa wale watumbuizaji.
Hakuchukua muda mrefu, akamwona mlengwa wake kwani kwa kadiri muziki ulivyokuwa unapigwa, Chong Pyong alikuwa anaonekana kwa wepesi maana alijiri mbele kila muda akionyesha umahiri wake kwenye upigaji wa gitaa.
Sasa Lee akaanza kupanga namna ya kumchomoa bwana huyo apate kuteta naye. Ila siku hiyo ikajiri kama bahati, hakungoja sana, mara muziki ukazima na wale watumbuizaji wakaingia kwenye mtindo wa utofauti kidogo.
Sasa alisimama mwimbaji nyuma ya kidaka sauti, akaanza kuimba kwa mtindo wa 'akapela' - sauti kavu pasi na vyombo. Bila shaka walikuwa wamelenga wasikilizaji wapate ladha halisi ya sauti tamu toka kwa mwimbaji, lakini pia kuwapa mapumziko wale wengine wapate kuvuta pumzi baada ya kutumbuiza kwa muda.
Hapo sasa, Lee akamwona Chong Pyong akielekea nyuma ya ukumbi. Akanyanyuka akitazama usalama. Walikuwa wamesimama walinzi kadhaa konani wakiwa wamevalia suti nyeusi na masikio yao yakizibwa na vifaa vya mawasiliano.
Lee akahesabu idadi yao, sita. Na basi akatambua kuwa walinzi hao watakuwa wanamtazama mienendo yake. Na hakuwa amekosea. Walirusha macho kumtazama, na hatimaye wakamtilia shaka. Haikuruhusiwa mtu kueleka kule nyuma ya ukumbi kama wewe si mhusika.
Wale walinzi wakawasiliana, kisha mmoja akanyanyua mguu wake mzito kumfuata Lee kule aelekeapo.
Lee akaongeza mwendo. Na yule mlinzi naye akaongeza mwendo, na akazidi kumtilia Lee shaka. Akapaza sauti kidogo akimtaka Lee asimame hapo hapo alipo. Alijitahidi sauti yake isiwatie hofu wateja wengine waliokuwa wametulia, aidha wakila ama kuburudishwa na sauti tamu ya mtumbuizaji.
Ila Lee akakaidi. Akaendelea kutembea. Na baada ya muda kidogo, akazama nyuma ya jukwaa. Sekunde tano nyuma, na yule Bwana mlinzi naye akakazamia humo.
Akaangaza, ila hakumwona Lee! Kwa umbali wa hatua ishirini walikuwapo baadhi ya wale wahusika wa bendi, kwa idadi watu watano, wawili walikuwa wanatazama baadhi ya vifaa, wawili walikuwa wakiteta na mmoja anakunywa maji.
Mlinzi huyu akapata shaka zaidi juu ya Lee. Akapaza sauti kuwauliza wale wasanii kama wamemwona mtu mgeni humo, wote wakasema hawajui!
Mlinzi akatazama kushoto kwake, kulikuwa kuna korido ndogo inayoelekea stoo, na 'emergency exit door'. Akawaza pengine Lee atakuwa ameenda huko. Ila kabla hajanyanyua mguu, mara king'ora kikaanza kuita kwanguvu!
Kilikuwa ni king'ora kinachoashiria moto kuzuka ndani ya hoteli, mara sauti za watu wakipiga mayowe zikaanza kusikika huku na kule, na watu wakaanza kukimbia kama wehu kila mmoja akitaka kunusuru roho yake.
Hata yule mlinzi akaachana na kumtafuta Lee, akaenda kule kwenye hall kubwa kuhakikisha usalama.
Ila kiuhalisia hakukuwa na moto. Ni kwamba Lee aliwasha 'lighter' karibu na 'sensor', hivyo ikapeleka taarifa ya moto ambao kumbe aliuzima na kutia lighter mfukoni.
Hapa kwenye vurumai ya watu, sasa akageuka kuwa chui aliye mawindoni, jicho lake lilimwagukia Chong Pyong lisimwache. Na baada ya muda mfupi akawa amemtia mkononi. Akamzimisha na kutoka naye kwa kupitia emergency door.
**