*ANGA LA WASHENZI II -- 26*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Alipomaliza kusema hayo akaendelea kumtazama Jona kwa muda kidogo. Mlango ukagongwa.
"Twende, Marwa!"
ENDELEA
Marwa akanyanyuka na kwenda kumkuta Miranda huko nje. Wakakwea garini na kutimka.
Baada ya robo saa wakawa wamefika karibu na eneo. Miranda akaliegesha gari lake eneo aliloona ni salama, eneo fulani la baa walilolipia kiasi fulani, kisha wakatembea kwenda mahali husika. Wote migongoni mwao walikuwa wamwmevalia vibegi vidogo vyeusi.
Kwa mwendo wao wa upesi, wakatumia kama dakika kumi tu kuwasili, wakaelekea upande wa kushoto wa jengo na kukwea ukuta baada ya kukata nyaya za umeme, Miranda akisimamia zoezi hilo.
Kama nyani, Miranda aliudaka ukuta na kisha akamvuta Marwa, wakazama ndani na 'kunyuti' kwa muda kidogo kusoma rada.
Eneo lilikuwa linalindwa mara mbili ya hapo mwanzo tangu mzigo mpya ulipoletwa na pia tangu antidote ziibwe mara ya kwanza na Jona na Marwa.
Kwa hivyo walitakiwa kuwa makini sana. Makini zaidi. Na hata Marwa alimkubusha hilo Miranda mbali tu na kumuelekeza ramani ya eneo maana yeye ni mwenyeji.
Wakaficha nyuso zao na vinyago. Na kisha wakaanza songa taratibu kuelekea upande wao wa kulia. Mahali walipo kulikuwa na vijumba vidogo vidogo visivyokuwa na watu. Ndani humo kulikuwa na majengo majengo kadhaa na kila jengo likiwa na kazi yake. Aidha ghala ama sehemu pa kupumzikia watu au ofisi.
Eneo lilikuwa kubwa sana! Na lote lilikuwa limezingirwa na uzio. Na kwa makadirio ya haraka, ndani ya eneo hilo kulikuwapo na watu takribani mia mbili hamsini!
Miongoni mwao wakiwa vijakazi, pamoja na walinzi wanaolinda hapo mchana na jioni. Na kila kijipande cha eneo, kilikuwa na kikosi cha walinzi wake. Na kila kikosi kikiwa na kiongozi wake mkuu.
Eneo kubwa lilikuwa linamulikwa na mwanga mkali wa taa. Mahali pachache pachache palikuwa na kiza. Na huko ndiko ambako Miranda na Marwa walikuwa wanajiegeshea huku maeneo yale yenye mwanga wakiyakwepa ama kuyapita kwa upesi sana.
Mpaka kufikia maabara kulikuwa na umbali wa kama nusu na robo ya kilomita. Na hapo katikati walinzi wakiwa wamejaa. Wanarandaranda. Wamebebelea bunduki nzito.
Basi taratibu. Tazama. Pita. Simama. Tazama tena. Pita. Ngoja. Tazama. Pita. Huo ndiyo ulikuwa mchezo. Wakafanikiwa kupita salama robo kilomita.
Ila wakiwa wanatafuna tena umbali huo, kuna mlinzi akahisi jambo. Alikuwa ni baba la miraba minne. Amevalia kibodi cheusi kinachobana misuli na suruali ya jeans 'dark blue'. Bwana huyu alihisi msogezo wa vitu nyuma ya kibanda kimoja cha mawasiliano.
Akasimamisha masikio yake na kukodoa macho. Akashikilia bunduki yake vema mkononi. Akasonga kueleka huko alipopatilia shaka. Akatazama tazama, hakuona kitu. Ila kugeuza shingo, akastaajabu kumkuta mtu amesimama.
Kunyanyua mkono, akanyakwa, akapokwa silaha. Hajakaa vema, akala teke lililomchana shavu. Mwanamke alikuwa amevalia 'high heels'.
Akashika shavu lake linalomimina damu. Akakodoa kwa hasira. Akanyanyuka na kujipanga. Kutazama vema akamwona ni mwanamke. Akaguna.
Basi akarusha ngumi, Miranda akayeya kisha akanyaka mkono huo na kuuviringita kama anauvunja. Mwanaume akabinua mgongo akiugulia, Miranda akamzawadia teke la kifua na kumcheusha damu bwana huyo aliyepepesuka kana kwamba kakumbwa na dhoruba.
Hajasimama vema, Miranda akazunguka na kutuma mguu wake wa kulia, akakata koo la bwana huyo kwa kisigino cha kiatu chake. Mwanaume akalala chini mauti!
Damu zinamwagika haswa. Miranda na Marwa wakamficha kwenye kachombingo fulani cha hilo jengo kisha wakaendelea na safari yao.
Wakakata tena robo kilomita. Wakiwa wanaenda kwa tahadhari kubwa. Simama. Ngoja. Tazama. Tembea. Simama. Ngoja. Tembea.
Wakafikia mahali ambapo palikuwa kama uwanja. Mahali hapo palikuwa na mwanga mkali. Pia kwa mbali, kule konani ya uwanja, walikuwa wamesimama wanaume watatu wakivuta sigara. Mikononi mwao walikuwa wameshikikia kamba za zilizofunga mbwa shingoni.
Bahati Miranda na Marwa waliwaona wanaume hao kwa kutumia hadubini. Wakiwa wamejilaza chini wakajadili namna ya kufanya. Na ilikuwa lazima wakatize hapo kuendelea na safari yao kutokana na mahali walipoingilia.
Miranda akatazama tena na hadubini yake. Kushoto na kulia. Kushoto na kulia. Kwa mbali wakaona kuna walinzi wengine wakiishilia kwenda kaskazini ya mahali walipo.
"Sasa tunafanyaje?" Marwa akauliza.
"Tungoje kidogo," Miranda akamjibu macho yake yakiwa ndani ya tundu za hadubini. "Muda si mrefu watamaliza ile sigara wanayoshea. Tutajua watatawanyika ama lah!"
Basi wakangoja kwa muda wa kama dakika tatu, kweli wale wanaume wakawa wamemaliza kile kipisi walichokuwa wanashea. Mlinzi mmoja akabaki hapo wakati wawili wakitawanyika. Mmoja akaelekea kushoto na mwingine kulia.
Sasa wakaona huo ndiyo mwanya wa kusonga hapo mataani wakiingiza kuwa kama walinzi, wakitumai kwa umbali ambao yule mlinzi mmoja alipo, itamuwia vigumu kutambua wao ni wavamizi.
Ila kabla hawajanyanyuka, wakastaajabu sauti nyuma yao, "tulia hivyo hivyo!"
Marwa akaogopa sana. Moyo wake ukaanza kupiga makasia.
"Haya ... taratibu! ... nyanyuka mkiwa mmeanika mikono yenu juu!" Akaamuru mwanaume mlinzi aliyekuwa amewanyooshea mdomo wa bunduki.
Basi wakatii. Wakiwa wananyanyuka, Miranda akaigiza kupaliwa na kikohozi kikali. Mlinzi kutazama, upesi Miranda akakanyaga ukuta kisha akajibidua! Mguu wake wa kushoto ukapiga bunduki, na wa kulia ukachana uso wa bwana mlinzi kama kiwembe! Bwana huyo akapiga yowe kali la kuugulia.
Aaaaghh!!!
Mara Miranda akamwamuru afunge mdomo wake upesi akiwa amemnyooshea bunduki. Kisha akamkita na kitako cha bunduki na kumzimisha. Wakamficha na kundelea na safari.
Ila sauti ile ya mlinzi akigugumia maumivu, haikuwa imeishia kwenye masikio yao. Kuna wengine pia walisikia. Nao walitambua hilo, kwa hivyo walitakiwa kuondoka eneo hilo upesi.
Wakakatiza ubavuni mwa uwanja wakiwa wanatembea kwa haraka. Mlinzi yule aliyekuwa mbali konani akarusha macho yake kuangaza, ila hakutia shaka sana. Zaidi alitazama wale wenzake wawili kama wamepotelea, kisha akachomoa sigara nyingine mfukoni na kuiwasha. Akaitia mdomoni.
Akainyonya kwa nguvu na kutema moshi juu kama kiwanda.
"Sasa, tupite njia hii!" Marwa akamwelekeza Miranda. "Hii ni shortcut. Tutavuka barabara mbili, kisha tutakunja kushoto. Kama hatua hamsini hivi, tutakuwa tumewasili."
Wakafuata hayo maelekezo. Wakashika barabara nyembamba iliyowakatisha chochoro. Wakaibuka kwenye njia pana. Wakatazama huku na huko. Salama. Wakavuka na kudaka chochoro nyingine. Napo wakapita, wakakutana na njia kubwa. Wakatazama huku na huko. Hawakumwona mtu. Ila kabla hawajapiga hatua, wakasikia kishindo cha mtu.
Wakasita. Kidogo akakatiza mwanaume mrefu mwenye mwili uliojengeka. Mkononi mwa mwanaume huyo alikuwa ameshikilia kamba ya mbwa. Kabla ya mwanaumr huyo kupita, mbwa akanusa jambo na mara akasimama!
Akatazamatazama huku na huko akinusanusa. Mara akabweka akiangazia kule kwenye uchochoro! Akawa anavuta kamba akitaka kwenda.
Mwanaume yuple aliyemshikilia akatazama kule uchochoroni. Kulikuwani giza, hakuona vema. Mbwa akawa anamvutia huko kwanguvu sana. Mwishowe, akaamua kuacha kamba, mbwa akakimbilia huko upesi na kuzama kichochoroni.
Mwanaume yule akawa amekaa tenge akiwa ameshikilia bunduki yake. Sekunde kama tano, kimya. Hakusikia sauti ya mbwa. Akapata shaka. Akachomoa bunduki yake pajani na kuishika vema. Akaanza jongea kwenda uchochoroni.
Hatua ya kwanza ... hatua ya pili ... hatua ya tatu ... hatua ya n ... mara akashtuka kumwona mbwa anatoka uchochoroni! Akaruka na kusogea kando. Akamwona mbwa amebebelea mfupa mdomoni. Mara ameulaza chini na kuanza kuulambalamba.
Hajakaa vema, akasikia kishindo cha mtu upande wake wa kushoto. Kugeuka, akashanga tu ghafla yupo gizani. Hata hakujua katendwa nini. Akadondoka chini puh! Kama gunia la mkaa.
"Twende!" Miranda akamsihi Marwa kwa sauti ya chini. Mara mwanaume huyo skachomoka alipokuwa amejificha, wakaendelea na safari. Mpaka wakafanikiwa kufika maabara.
Tatizo ni kwamba, hapo wakakuta walinzi takribani sita! Wote wakiwa wamebebelea bunduki mikononi mwao. Warefu na waliojaza miili kwa misuli minene!
Marwa akatikisa kichwa. "Hatutoweza, Miranda!"
Miranda akaminya mdomo wake na kukuna kichwa.
"Lazima kutakuwa na njia."
***
**