*ANGA LA WASHENZI II -- 27*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Tatizo ni kwamba, hapo wakakuta walinzi takribani sita! Wote wakiwa wamebebelea bunduki mikononi mwao. Warefu na waliojaza miili kwa misuli minene!
Marwa akatikisa kichwa. "Hatutoweza, Miranda!"
Miranda akaminya mdomo wake na kukuna kichwa.
"Lazima kutakuwa na njia."
ENDELEA
"Njia gani hiyo na pale waliposimama ndipo kuna mlango?" Marwa akauliza. Miranda hakumjibu, akaendelea kutafakari namna ya kuenenda. Namna ya kuzama mule ndani pasipo kuzuiwa na pande zile za baba.
Baada ya dakika mbili, akamuuliza Marwa, "Kule nyuma hamna njia ya kuingilia?"
Marwa akamwambia hakuna, isipokuwa dirisha tu. Miranda akatulia akiendelea kuwaza. Akamtaka Marwa wangoje hapo kwa muda kidogo. Aliamini wale walinzi sita hawatakaa pale kwa muda mrefu.
Basi wakavuta subira kidogo. Kama dakika kumi hivi, mlinzi mmoja akachoropoka na kuacha wenzake watano. Ila hao walioachwa hawkauonyesha dalili ya kuondoka maana walilaza kabisa miili yao, wakipiga soga za hapa na pale.
Sasa ikabidi Miranda atafute namna ya kuwaondoa hapo maana la sivyo watakesha. Wanaweza kujikuta wanakaa hapo mpaka mambo yakagutukiwa!
Akamuuliza Marwa ampatie ramani ya wapi ilipo 'main switch'. Kidogo Marwa akasita. Hakuwa na kumbukumbu nzuri juu ya wapi ilipo 'main switch' kwa hivyo akamtajia mwanamke huyo sehemu tatu, akibashiri mojawapo itakuwa sahihi.
"Unaenda kufanya nini huko?" Marwa akauliza. Miranda hakujibu, asipoteze muda akamtaka Marwa ajifiche kisha yeye aende huko. Akanyata na kusonga. Akatazama usalama. Akaendea njia yake kwa tahadhari na baada ya muda mfupi akawa amefika kwenye eneo moja ambalo aliambiwa na Marwa.
Kutazama, hapakuwa penyewe! Akasonya na kuanza kufuata mahali pa pili alipoelekezwa na Marwa. Kwa upesi ila kwa tahadhari akasonga akielekea huko. Kabla hajafika akawaona wanaume wawili wakikatiza. Akajibanza. Wanaume wakapita.
Akatazama kondo na kondo, kukawa salama. Akashika tena njia na kutembea. Akanyata kama mende ukutani, hakutoa sauti. Kuchungulia, akaona chumba kidogo chenye tahadhari ya umeme. Akashukuru. Hapo ndipo alikuwa anataka.
Akatazama tena kushoto na kulia. Upesi akatembea kwenda kwenye kichumba hicho. Hapo kwa nje kulikuwa na mwanga kwa hivyo hakutakiwa kukaa hapo kwa muda. Akajaribu kufungua kichumba hicho, mlango ulikuwa umefungwa!
Haraka akavuta begi lake mgongoni akachomoa chuma chembamba alichokizamisha nyuma ya mlango alafu haraka akautegua mlango. Basi ukafunguka. Akazama ndani na kutulia humo.
Muda si mrefu, kama sekunde tatu tu kupita tangu Miranda aingie ndani, mlinzi mmoja akatokea akikatiza hapo. Miranda akatulia kimya ndani ya kijichumba. Mlinzi yule kabla hajapita, akasita, aliona mlango ukiwa wazi.
Akasonga na kuutazama. Akaushika na kuusukuma mbele na nyuma. Na asijiulize sana akaurejeshea mlango ule sawa, kisha akaendelea na safari yake ya lindo.
Miranda akashusha pumzi ndefu, kisha akachomoa miwani ya mpira na kuiveka machoni. Sasa akawa anaona mule kizani, japo kwa mwanga wa kijani.
Akafungua kebo ya swichi.
**
"Marwa!" Sauti ikanguruma sikioni kwa kupitia kifaa kidogo Marwa alichokichomeka sikioni.
"Bado wapo hapo?" Sauti ya Miranda ikauliza kifaani.
"Ndio." Akajibu Marwa kwa kunong'oneza. "Bado wapo, wanne sasa!"
"Sawa," sauti ya Miranda ikajibu.
"Unafanya nini huko, Miranda??" Marwa akauliza akishikizia kifaa chake sikioni. Miranda akamwambia, "nakuja!" Kisha akakata mawasiliano. Marwa akahisi umeme utakata muda si mrefu. Akatazama taa akihesabu muda na akiwaza ni nini Miranda anapanga kichwani.
Ikapita dakika kama tatu, Miranda akawa amefika hapo. Akamwambia Marwa, "tulia, muda si mrefu, ntakwambia cha kufanya!"
Basi wakatulia hapo, muda si mrefu taa zikaanza kufinyafinya. Wale walinzi wakatazama na kuanza kuulizana. Taa zikazidi kufinyafinya maradufu. Miranda akamtazama Marwa na kumtaka avae miwani yake ya kiza kisha akamkabidhi pini nyembamba na kumpa maelekezo mafupi ya kueleweka juu ya kitu cha kufanya.
Marwa alipokwisha fanya hivyo tu, taa zote zikazima baada ya mlio mkubwa wa mlipuko. Kukawa kumejawa na kimuhemuhe. Walinzi wale wakatazamana na kisha upesi wakakimbilia kule kwenye mlipuko wakimwacha mlinzi mmoja pale eneoni.
Na kwakuwa kulikuwa ni kiza na vishindo vya watu vilikuwa vinasikika huku na kule, basi Miranda na Marwa wakasonga eneo la maabara pasipo kugutukiwa upesi. Wakamfikia yule mlinzi, Marwa akakimbilia mlangoni wakati Miranda akimkabili yule bwana mlinzi.
Hakupoteza naye muda, mitupo yake mitatu ikamlaza mwanaume chali. Anavuja damu. Na pasipo kupoteza muda, akamburuza mwanaume huyo mpaka mlangoni. Marwa alikuwa tayari ameshaufungua mlango. Wakamzamisha ndani kisha wakafunga mlango.
Haraka Miranda akamweleza fomula ya kemia wanayohitaji kuitazama maabarani humo. Na basi upesi wakaanza kusaka fomula hiyo huku na kule. Maabara ilikuwa imeshona kwa kujaa vitu lukuki hivyo kazi haikuwa nyepesi kutazama huku na kule kutafuta kitu kimoja.
Wakachoma dakika mbili ... tatu ... nne ... tano ... mpaka kumi na tano, hakuna kitu walipata. Mpaka wakaanza kusikia sauti za walinzi wakisongamana huko nje.
Huko nje walikuwa wamefika walinzi watatu wakiwa wamebebelea kurunzi kubwa mikononi kupambana na kiza. Walinzi hao wakasimama hapo mbele, mmoja akapanda kibaraza na kutupa miale ya kurunzi ndani ya dirisha la maabara. Akalipeleka kushoto na kulia. Hakuona kitu.
Miranda na Marwa walikuwa wamejihifadhi chini ya meza wakiwa wamefunikwa na mizigo kadhaa. Wakangoja hapo, kurunzi likapita. Walipoona salama, wakanyanyuka na kuendelea na msako wao walioufanya kimya kimya.
Ikapita dakika tano, Miranda akaona kitu ndani ya chupa ndogo aina ya 'test tube'. Kutazama vema, akaona kuna seti hapo za chupa hizo zikiwa na vimiminika rangi ya 'pinki' iliyopauka.
Uzuri alikuwa ni mtu mwenye ujuzi na mambo ya kemikali. Si tu kuwa alisomea mambo hayo darasani akiwa na diploma, bali pia aliyafanyia kazi kwa muda mrefu akiwa na bwana BC.
Akanong'ona, "Marwa, nahisi ndiyo hizi." Marwa akatazama na kuuliza, "mbona haina badge?"
"Ndio, ila hii ndiyo rangi yake," Miranda akasema kwa uhakika kisha akageuza begi lake na kutoa vizibo vidogo vya mpira, akaziba midomo ya test tube kisha akatia seti hiyo begini na kuweka begi mgongoni.
"Tuondoke," Miranda akamsihi Marwa.
"Tunapitia wapi?"
Miranda akasimama kidogo na kuangaza nje. Wasingeweza kupitia pale mlangoni. Basi akamwambia Marwa watumie dirisha maana ndiyo njia pekee iliyobakia.
Kabla Mara hajatia neno, mara Miranda akatambaa kama mende kufuata dirisha la kusini, mbali kabisana mlango. Alipofika hapo, akajaribu kufungua dirisha hilo. Akagundua lipo 'sild', basi akafungua begi lake kwa mkono hata asitazame. Akapapasapapasa na kutoka na chuma fulani kilichojichanua kama mbawa za 'helikopta'.
Akakinasisha pale dirishani, kisha akaanza kunyongorota mashine ndogo iliyo nyuma ya mbawa hizo. Basi hicho kifaa kikanguruma kidogo, Miranda akatoa mikono upesi, basi zile mbawa za kifaa hicho zikainama na kukuta kioo. Zikazunguka upesi na kabla hazijamaliza kutengeneza tundu, Miranda akakizima na kukinyofoa.
Akamtazama Marwa na kumpa ishara asogee. Marwa akatii. Ila akamuuliza kuhusu kile kioo. Hakitatoa sauti wakashtukiwa?
Miranda akatikisa kichwa, kisha akampatia kidude kidogo chekundu alichokitoa mfukoni, na kumwambia, "utakibonyeza ikifika tatu. Sawa?"
Marwa akapokea agizo. Moja ... mbili ... tatu! Marwa akabonyeza kitufe hicho na hapohapo ikasikika sauti kubwa ya mlipuko. Sauti hiyo kuja kuzima tayari Miranda alishadondosha dirisha zima, wakatoka!
Sauti za watu zikarindima huku na huko. Watu wakawa wanapishana ama kusimamishana wakijiuliza nini kinatokea humo. Kulizuka hali ya taharuki, na ukizingatia bado mwanga haukuwa umerudi.
Basi Miranda na Marwa wakatumia fursa hiyo kufika kwenye uzio, wakanyaka na kujitupia nje baada ya Miranda kufanya kazi yake ya kukata nyaya za umeme. Miranda alitua chini katika namna ambayo alihakiki hakuna kitu kitakachovunjika begini. Mkono wake wa kushoto ulishikilia begi akitua kwa kishindo.
Ila kabla hawajanyanyuka na kuhepa, Miranda akamtaka Marwa atulie hapohapo tuli, la sivyo wangeharibu chakula mwishoni.
"Shhhhhh!!!" Miranda akampa ishara kisha akakagua eneo zima kwa macho yake mepesi.
***