*ANGA LA WASHENZI II -- 39*
*Simulizi za series.*
ILIPOISHIA
Lee akatoa hadubini na kupekua eneo hilo kila pande. Alikuwa umbali wa kama kilomita mbili na nusu. Aliporidhika na alichokipata kwa hadubini, akairejesha begini alafu akavalia barakoa.
Mwanaume akazama kazini.
ENDELEA
Ni mwendo wa dakika chache kuwasili ndani ya eneo la tukio kwa namna alivyokuwa anatembea. Alitulia kidogo na kuangaza, eneo lilikuwa linalindwa haswa. Akapiga hesabu kama anaweza kufanikiwa kuingia ndani pasipo kuleta taharuki.
Ilikuwa ngumu. Kila mahali palitapaka walinzi na taa nazo zilikuwa zinaharabu mahesabu. Ilikuwa ngumu kujibanza ukiwapo ndani.
Basi akawa mvumilivu kidogo, akatazama wale walinzi wanaozunguka kwa nje na kutambua mienendo yao. Akasogelea mti uliokuwapo karibu, akakwea kwa haraka alafu akapekua tena mazingira.
Akavuta subra. Kisha kidogo akatoa kakifaa kwenye mkoba wake, kakitu kama kafilimbi rangi nyeusi, akakiweka mdomoni na kukipuliza kwanguvu. Ndani yake kulikuwa na kakipini kadogo chembamba.
Kaliruka na kumkita mlinzi mmoja shingoni kwa usahihi wa hali ya juu! Yule mlinzi akaguna akikunja sura. Kabla hajanyofoa kapini hako shingoni, akajikuta amedondoka chini na kupoteza fahamu!
Lee akataka kurukia ndani, ila akawahi kusita. Alimwona mlinzi mwingine akija upande ule aliokuwa amelala mwenzake chini. Akafika na kustaajabu. Haraka Akaweka kidole chake sikioni akiminyia kufanya mawasiliano na wenziwe.
Ila kabla hajafungua kinywa, chap! Kipini kikamchoma na yeye shingoni, akadondoka chini baada ya sekunde mbili tu!
Sasa Lee akajitupia ndani, akafikia kwa kujituliza na sarakasi. Kisha upesi akaikusanyia miili ya wale watu ukutani, akaifunika na shuka jeusi alilotoa begini, ikaonekana kama kamlima fulani kadogo.
Alafu haraka akasonga akifuata mlango akichomoa kapini fulani ambacho alifungulia kitasa na kuzama ndani.
Kulikuwa kimya.
Alitulia kwa sekunde kama nne akiwaza namna ya kufanya na pia akiskizia huko nje kama wamebashiri lolote. Zilipokwisha sekunde hizo nne, akajongea taratibu.
Ndani kulikuwa na mwanga lakini ilikuwa ngumu kubashiri kama watu wamelala ama lah maana palikuwa kimya na kwa wakati huohuo taa zikiwa zinawaka kila eneo.
Kazi ikawa kwa Lee kutambua ni wapi alipo mtu anayemlenga. Hapa alihitaji kuwa mwangalifu na msikivu mno. Alipotulia kwa sekunde kama tatu, kazi ikawa nyepesi kuliko alivyodhani.
Alisikia sauti ya mtu bafuni akisafisha koo. Bila shaka akamtambua kama ndiye mlengwa wake. Basi akanyata kufuata bafu. Akatulia hapo kidogo, kama baada ya dakika hivi, mlango wa bafu ukafunguliwa.
Akatoka bwana mmoja wa kichina, ana kiwaraza hafifu na mwili wake umemomonyoka kizee. Basi haraka Lee akamminya bwana huyo na kumweka ndani ya uwezo wake. Hata kelele hakuwa anaweza kupiga!
Ila alipomtazama ... alipomtazama akagundua hakuwa makamu wa raisi! Akastaajabu. Basi akiwa amemminya bwana huyo, akamuuliza yeye ni nani? Na makamu wa raisi yupo wapi?
Bwana yule akiwa amebanwa na hofu kuu, na akiwa amebanww mbavu katika namna ambayo hawezi kuongea kwanguvu, akasema yeye ni msaidizi wa makamu, ila akasema hajui makamu alipo!
Lee akaghafirika maana alijua wazi bwana huyo anaongopa. Ni lazima tu atakuwa anajua mlengwa wake alipo. Akamminya zaidi, ila bwana yule hakuwa tayari kusema!
Lee akamziraisha alafu akamlaza chini, akaenda kukagua vyumbani. Akatazama chumba cha kwanza, humo akakuta wanawake wawili wembamba wakiwa wamelala. Ina maana wanawake hawa walikuwapo hapo kumhudumia msaidizi yule wa makamu au makamu mwenyewe.
Lee akaenda chumba cha pili. Taa ilikuwa inawaka ndani, huenda makamu akawa hajalala, akawaza. Basi cha kufanya akagonga mlanga mara mbili na kuskizia.
Akasikia sauti nzito ikimwamuru aingie ndani. Akafungua mlango na kuzama. Kutazama, uso kwa uso na mlengwa wake! Alikuwa mwanaume mwembamba mwenye makadirio ya miaka sitini ya mwishoni ama sabini za mwanzoni.
Usoni alikuwa amevalia miwani ya macho. Nywele zimekuwa kama za kahawia kwa mvi za mbali. Alikuwa amevalia kaushi nyeupe na bukta fupi. Amekalia kakiti kadogo kalichopakana na meza ya saizi yake. Juu ya meza hiyo ndogo kulikuwa kuna karatasi kadhaa nyeupe, na diary yenye kava gumu jeusi.
Basi ile kutazamana, bwana makamu akapatwa na woga sana! Akatazama kando upesi kama mtu atafutaye silaha, ila upesi akatupiwa pini shingoni, akanyeta. Punde akaanza kuona mbilimbili, mara kichwa puh mezani!
Lee akafunga mlango na kumsogelea. Akakusanya kila kitu chake na kisha akatengua shingo kumfanya mfu! Akatoka na kwenda kumkuta yule bwana aliyemziraisha. Naye hakumwacha salama, akamtengua shingo kumfanya mfu!
Sasa akabakia na kazi ya kutoka mule ndani. Pengine inaweza ikawa kazi kubwa kuliko kuingia, akatazama kushoto na kulia, wakapita walinzi wawili. Alipoona mazingira murua, akatoka chap kwenda ukutani.
Ila alipofika na kabla hajatoka, mlinzi mmoja akamwona! Akagutuka. Haraka mlinzi akachomoa bunduki yake ndogo na kuifyatua risasi mara mbili! Ila bahati haikuwa kwake, haikumpata mlengwa!
Lee akachumpa nje na kuanza kukimbia kwa kasi. Wale walinzi nao wakajikusanya na kumkimbiza Lee ambaye alikimbilia huko msituni.
Walitoka hapo kama wanaume kumi. Wote wakiwa wamebebelea silaha. Ila hawakufua dafu msituni humo Lee akafanikiwa kuwapotea na kwenda zake salama salmini.
Alikuwa ameegesha pikipiki kubwa mahali, akaiwasilia na kuitia moto, safari ikashika hatamu. Hakutaka hata kubaki Mongolia kabisa, alikuwa amelenga siku hiyohiyo kutoboa mpaka China.
Kazi aliyotumwa alikwisha itekeleza. Tena kwa ustadi mkubwa.
Haikuwa hata na haja ya kuitangaza kwani jua likipanda kesho yake tayari habari zitakuwa zimeshasambazwa na vyombo vya habari kuwa makamu wa raisi na msaidizi wake wameuawa huko nchini Mongolia na mtu asiyejulikana!
**
Saa tatu asubuhi ...
Shao alikuwa na kikao kifupi na vijakazi wake kumi. Walikuwa katika mpango mkakati wa kufanya jambo, tena kubwa na lenye madhara.
Vijakazi wote walikuwa tuli wakimsikiliza mkuu wao, na yeye Shao akatumia huo mwanya kueleza kinagaubaga jambo la kufanyika. Naam. Hakutaka muda upotezwe, bali uhai wa adui.
Alichotaka ni kuletewa kichwa tu. Haijalishi risasi ngapi zitatumika ila jambo litekelezeke, yupo tayari kugharamia kila risasi kugharamia kila risasi itakayopotea kwenye uwanja wa vita.
Basi na wasipoteze muda, kikao kikafungwa na wakaahidiana kukutana tena hapo majira ya saa sita usiku.
**
Saa tatu usiku ...
Gari aina ya Subaru iliyobebelea wanaume watano ilisimama na kuzimwa kabisa. Wanaume hao wakateta kidogo kisha wakatoka wote garini isipokuwa dereva.
Wote hawa walikuwa wamevalia mavazi meusi na kofia za soksi kichwani. Na hata kwa kuwatazama upesi ungeligundua walikuwa wamefichilia silaha za moto.
Wanaume hawa wakatokomea dereva akiwatazama mpaka wanaishilia. Walikunja kona kama mbili kufika mahali walipokuwa wanaelekea.
Wakaruka ukuta, na kuzama ndani.
Kulikuwa ni makazi ya Miranda!
Kimya.
Wakagawana pande. Wakachomoa na silaha zao kuziweka vema viganjani kwa ajili ya kazi. Wawili wakaendea kibanda cha mlinzi, kutazama hamna mtu.
Kwa ukimya wa hali ya juu, wakasonga kuufuata mlango. Na wale wa nyuma na wao wakasonga mlango wa ziada. Wakatulia hapo.
Ndani taa zilikuwa zimewashwa. Na sauti moja ya kike ilikuwa inasikika kwa mbali kuashiria kuna mtu humo.
Basi wale wavamizi, wakahesabu mpaka tatu, wakazama ndani kwa kuvunja mlango kwa mateke yao mazito.
Wakaangaza huku na kule. Hamna kitu! Ila bado ile sauti ya kike ilikuwa inasikika.
**