*ANGA LA WASHENZI II -- 41*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Aliposema hayo akapachika simu mezani. Tulipata kutambua hilo kwa sauti, kisha akaketi na kusema kwa lugha ya kichina, acha tuone nani atakayekuwa ndege wa alfajiri.
ENDELEA
Ni nini alimaanisha bwana huyu? Ni nini anadhamiria kufanya na mbona jambo hili hakumshirikisha Shao? Kwanini alifanyia maongezi haya ndani ya kiza?
Pengine unawaza hali ya Jona na wenzake ukasahau kujiuliza maswali hayo.
Basi siku hii ikaenda. Kesho yake majira ya asubuhi tu, Shao akaamkia ndani ya maabara. Akachukua ile kemikali yake aliyoitengeneza jana yake na akaanza kuifanyia taratibu kuigeuza kuwa katika mfumo wa hewa.
Alifanya zoezi hilo kwa muda wa masaa matatu, kumbuka alikuwa yu mwenyewe, na hatimaye alipogeuza kemikali hiyo kuwa hewa, akaijaribisha kwa panya aliowatoa kwenye hifadhi yake, na punde tu panya hao, watatu kwa idadi, walipovuta hewa ya kemikali hiyo wakafa pasipo kuomba maji!
Shao akatabasamu. Kazi ilikuwa kufyonza tu hewa hiyo na kuiswekwa kwenye kontena zake maalum.
Aliazimia kemikali hiyo kutumika usiku wa siku hiyo. Kwa matarajio yote aliamini itamletea matunda anayoyataka.
**
Saa tano asubuhi ...
Gari, defenda kama yalivyozoeleka kuitwa, ya polisi ilitua mbele ya geti na honi ikapigwa mara nne, geti likafunguliwa na gari likazama ndani.
Lilikuwa limebebelea askari wanaume watano kwa nyuma, na wawili upande wa dereva ambao wao walikuwa wamevalia nguo za raia. Gari hili liliposimama tu, askari wale wakashuka upesi.
Watatu miongoni mwao walikuwa wamebebelea bunduki na mmoja ameshikilia redio koo mkono wa kuume.
Kibarazani alikuwa amesimama BC akishangazwa na ujio huu. Alikuwa amevalia gauni la bafuni alilolifungia vema kiunoni. Alidaka kiuno chake akijiuliza maswali kichwani, punde askari wakamfikia na kumweka chini ya ulinzi, na wakamweleza haja yao kuwa ni kufanyia upekuzi eneo hilo lote maana wanahisi litakuwa linahifadhi mtu wanayemtafuta.
BC akashangaa na hata akawaambia kwamba hamna mtu wanayemhitaji humo. Pia hawana haki ya kumweka chini ya ulinzi kama madai yao hayajathibitishwa.
Pia akawasihi wangoje ampigie na kuongea na mwanasheria wake kwanza.
Madai yake yote hayo yakapuuzwa, askari hawakumzingatia hata kidogo. Wakamweka chini ya ulinzi na kumtia pinguni kisha wakaanza kufanya upekuzi hadidi.
Wakapekuwa kila pande ya nyumba na wakagundua kuwa mwanaume huyo alikuwa na baadhi ya kemikali maabarani mwake. Ila hawakufanikiwa kumpata yeyote yule. Hata yule waliyekuwa wanamdhania yumo.
Basi wakambeba BC na pia wakawasilisha kemikali zake zote walizozitoa maabara na kuzipeleka moja kwa moja kwenye ofisi ya mkemia mkuu kwa ajili ya uchunguzi na maelezo zaidi ya kitaalamu.
Bwana yule mzungu akaswekwa rumande.
Na kama haitoshi, kamanda wa mkoa akaitisha 'press conference' kuwaambia waandishi na wananchi nini kimetokea. Lengo kuu hapa lilikuwa ni kufanya jeshi lionekane 'linashughulika', halijashindwa na kila kitu kipo kwenye 'mikono yao.'
Hivyo japo hawakumpata Jona, bado kutangaza kwenye vyombo vya habari ilikuwa ni turufu! Hata bwana Sheng hili jambo lilimpendeza machoni.
Na baadae kwenye majira ya jioni, bwana huyo wa kichina akaenda kuonana na Kamanda mkuu. Akamweleza kuwa bwana huyo wa kizungu waliyemtia kizuizini anajua fika wapi alipo Jona. Wanachotakiwa kufanya ni kumbana mpaka aseme.
Kamanda akamwambia aondoe shaka, atalisimamia hilo kwa nguvu zake zote. Ila akamsisitizia tena kuwa jambo lao liwe la siri, hata wenzake hawatakiwi kulijua.
Kamanda akamtoa hofu. Na Sheng hakukaa sana, akaenda zake kurudi makaoni.
**
Baadae majira ya usiku ...
Hodi iligonga mara mbili kwenye makazi ya Sheng. Alipopokea hodi hiyo, akazama ndani Bwana Shao aliyekuwa amevalia suti ya traki rangi nyeusi. Akaketi na kumwambia Sheng juu ya habari zile za polisi kumvamia na kumkamata BC.
Akaeleza namna alivyoshangazwa na habari hiyo maana walikuwa katika mpango. Ila akamuuliza bwana Sheng kama amehusika kwa vyovyote na hiyo oparasheni.
Sheng akakataa, na hata akasema aliwaza pengine ni yeye, yaani bwana Shao, ndiye aliyefanya hilo.
Basi baada ya kwenda tofauti kimaudhui, Shao akamuuliza Sheng kuhusu hilo jambo. Ni nini msimamo wao kwenye hili? Watafanya nini sasa?
Sheng akatikisa kichwa kwanza alafu akamwambia Shao kuwa yeye ahusiki na wala hatahusika na chochote kile kwani kila kitu alimkabidhi yeye.
Na hata akamkumbusha kuhusu ile HATI yao ya kifo. Shao akashangazwa. Asiseme kitu, akaaga na kwenda zake!
**
majira ya saa tano asubuhi ...
Mwanaume mzungu aitwaye Henry Marshall alifika kituoni akiwa amebebelea briefcase nyeusi na pia amevalia suti nyeusi iliyomkaa vema mwilini.
Mwanaume huyu alikuwa ni mwenye nywele rangi ya 'brown'. Macho yenye kiini cheusi. Mwili wake ulikuwa mwembamba na wenye nishati ya kutosha. Alikuwa anatembea kwa ukakamavu. Na macho yake ndani ya miwani nyeupe ya macho, yalikuwa yanaangazaangaza huku na kule.
Akajitambulisha kwa jina na pia dhumuni lake kuwapo hapo. Yeye ni mwanasheria wa Bwana Brown Curtis. Amekuja hapo kwa dhumuni la kumtetea mteja wake.
Na bwana huyo akawachachafya askari hao akiwaambia wamekiuka sheria kwa kumsweka ndani mteja wake kwa mashauri yasiyo na uthibitisho na hata pasipo kuongea naye kama mwanasheria.
Japo bwana Henry alijieleza vema kutokana na nafasi yake, wale askari hawakutaka kumwelewa kabisa. Hata kuonana na Brown Curtis hakuruhusiwa. Basi akaenda zake akisema atalipeleka shauri hilo mahakamani.
Na ana uhakika atashinda, na hilo shauri litaigharimu serikali pesa kubwa!
Hakuwa anatania. Alikuwa ni mwanasheria wa hadhi yake toka Uingereza. Tena anayefahamu vema sheria nje na ndani. Aliapa kulifanyia kazi jambo hili kuonyesha thamani ya pesa anayolipwa na mteja wake.
**
Saa nane mchana ...
Simu iliita kwa muda mfupi tu, Kinoo akapokea na kuiweka sikioni. Alikuwa ni Miranda anampigia na tayari alikuwa anajua mwanamke huyo anataka kuongelea nini.
Nalo si jingine bali swala la BC. Akapokea simu na kuteta. Miranda akamtaka waonane haraka iwezekanavyo kupanga namna ya kufanya kwa ajili ya bosi wao.
Ikachukua kama nusu saa tu, wakawa wamekutana na kujiweka ndani ya gari kunena mawili matatu. Basi Miranda akamwambia Kinoo kuwa inabidi aende kumtembelea BC kule kituoni maana yeye wanaweza kumhisi kwa namna moja ama nyingine kuwa anahusika na Jona kwani alishawahi kufika huko mara kadhaa.
Ila Kinoo naye akasita, akaeleza hofu yake. Vipi kama naye akikamatwa? Miranda akamsihi hamna muda wa kuhofu, na hawana machaguzi mengine zaidi ya kutenda.
Na hapo anapoteta naye, tayari ashafikisha habari za Brown Curtis makao makuu, hivyo wanaweza wakatumwa mawakala hivi karibuni.
Basi Kinoo akaridhia, ataenda kuonana na BC kesho asubuhi na mapema. Ila akamuuliza Miranda, vipi kuhusu bwana yule, Jona? Wapi alipo na anaendeleaje?
**