*ANGA LA WASHENZI II -- 50*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Bwana huyo akazivaa na kufanana vilevile na wahudumu, kisha akatoka ndani kuendea mlango wa chumba namba 75.
Alipofika hapo akabisha hodi.
“mhudumuu!" Akapaza na sauti.
ENDELEA
Baada ya muda kidogo mlango ukafunguka, akachungulia mwanamke mmoja mweupe mwenye nywele mtindo wa afro.
“Samahani, nimekuja kuchukua mataulo," alisema bwana huyu aliyekuja hapa kwa kujidai mhudumu.
Yule dada akatazama ndani kisha akarudisha uso wake kwa huyo mhudumu na kumwambia,
“mataulo si mmeshachukua? Au mwayabadilisha mara ngapi kwa siku?"
Huyu bwana akatabasamu alafu akaomba radhi na kusema, “kama yameshachukuliwa hamna shida, kuna tatizo lingine lolote?"
Dada yule akatikisa kichwa kisha akafunga mlango na mhudumu yule akaenda zake. Alirejea kule alipowaacha wenzake na kuwaambia yale aliyoyakuta huko.
“ina maana hawatakuwapo?" Akauliza yule mwanaume aliyejinasibu kwa jina la Lorenzo Kagula.
“hapana!" Akasema mwanaume mwingine. “tusikate tamaa kiuwepesi hivyo! Kwani kufungua mlango mtu mwingine kunazuia mlengwa watu kuwepo ndani?"
Basi wakakubaliana kwamba inabidi wafanye vivyo hivyo alimradi misheni yao ikamilike. Inabidi tu wavute muda na kisha baadae, majira ya usiku, wakakague vyumba vyote viwili ambavyo wamepewa taarifa kuwa vinawahifadhi watu wao.
Basi Lorenzo akampigia simu mkuu na kumpa mrejesho wa kinachoendelea. Na kwasababu za kuvutia muda, wakaagiza vinywaji vikali kupooza makoo yao.
Wakanywa na kujilaza.
Baadae wakati giza likiwa limeingia, ni majira ya saa mbili usiku, bwana Lorenzo akashtuka na kutazama saa yake ya mkononi.
Kichwa kilikuwa kinamgonga kwa mbali. Wenzake wote walikuwa wote walikuwa wamejilaza hoi. Akataka kuwaamsha ila akasita. Muda wa misheni bado haukuwa umefika.
Basi kurejea usingizini, akapiga tena kinywaji, chupa nzima yeye mwenyewe. Hapo akalala kama mfu wa kale. Hata mwivi angeweza kumnyanyua na kuiba godoro kisha akamrudisha na asisikie lolote lile!
Masaa yakaenda. Ilipohitimu majira ya saa sita kasoro usiku, mmoja wao, yule aliyeigiza mhudumu, akaamka. Akawakurupua wenzake na wote wakaamka isipokuwa Lorenzo.
Walijitahidi sana kumwamsha ila wapi. Hata kama angeamka asingeweza kufanya kitu kwa hali aliyomo. Basi ikabidi wale wengine wapange kufanya tukio pasipo yeye maana isingewezekana misheni hiyo kutokufanyika siku hiyo.
Na hapo tayari Lorenzo, ambaye yupo hoi hajiwezi, alikuwa ameshamwambia bwana Sheng kuwa misheni hiyo ipo chini ya uwezo wao, haina haja ya yeye kusumbuka.
Basi mabwana hawa wakaweka kila kitu sawa. Walikuwa na bunduki mbili zilizojaa risasi. Wakavalia na nguo nyeusi za kazi isipokuwa mmoja ambaye alitumwa akatazame usalama kwanza.
Bwana huyo akatoka na kwenda, baada ya dakika kadhaa akarejea na kuwaambia kila kitu kipo sawa. Basi akavalia sare za wahudumu na kisha wakaenda huko chumbani wanapohisi watu wao wapo.
Yule bwana aliyevalia sare akagonga hodi na kusema, “mhudumuu!" Kisha akangoja.
Kimya.
Akagonga tena na kupaza sauti ya kujitambulisha kuwa mhudumu, ila napo ikawa kimya. Akawatazama wenzake. Ni kama vile waliwasiliana kwa macho, bwana ‘mhudumu' akarudia tena kugonga.
Napo bado kimya. Ila kwa ndani taa ilikuwa inawaka na hili ndilo liliwapa imani kuwa kuna watu ndani.
Wakatazamana.
Mmoja wao aliyekuwepo nyuma, akachomoa kitu mfukoni kisha akachokonoa kitasa. Sauti ikasikika tas-tas! Na alipobinya kitasa, mlango ukaitika kwa kufunguka.
Hawakuingia kwanza, wakangoja kuskiza. Kama sekunde tano hivi, kisha yule bwana mhudumu akazama ndani.
Na mara wenzake punde wakazama ndani.
Wakatazama huku na kule. Hakukuwa na mtu. Wakapekua chumba kizima, kila kona, hakukuwa na kitu!
Basi wasipoteze muda, wakatoka na kwenda kile chumba kingine, cha pili yake. Huko hawakupoteza muda kama ilivyokuwa kwenye hiki cha kwanza, wakachokonoa kitasa na kuzama ndani.
Kulikuwa ni kiza. Waliwasha taa na kuangaza. Hamna kitu! Wakasaka kila kona, hakukuwa na kitu! Hapa wakatazamana kwa butwaa.
Iliwezekanaje hili? Au taarifa walizopewa hazikuwa sahihi? Ilibidi wajiulize mara mbilimbili. Wakatoka chumbani mule na kurejea chumbani mwao.
Wakamkuta bado Lorenzo amelala. Hawakuhangaika naye, wakateka simu na kupiga kwa mkuu wao kumweleza yaliyojiri.
“ndio, namba ni hizohizo! ... Hamna mtu mkuu, saa zile mara ya kwanza kulikuwa kuna kabinti flani hivi. Sasa hivi hata naye hayupo maana hata tungempata yeye kwa namna moja angeweza kuwa na majibu ... Ndio, mkuu ... Sawa."
Simu ikakata.
“anasemaje?"
“turudi makaoni!"
“saa hii?"
“ndio."
“na hii mishe vipi?"
“amesema huenda taarifa sio sahihi au watakuwa wameshashtukia. Anampigia mtu aliyempa taarifa kwa maongezi zaidi."
Wapoelezana hayo, wakaanza kujipanga waende zao. Walipotia kila kitu kwenye begi, wakamwamsha Lorenzo. Bado hakuamka.
Walimpigapiga makofi na kumvutavuta lakini bado haikusaidia. Ila wakiwa katika huo mchakato, mmoja wao akaona kama rangi nyekundu shukani.
Kutazama vema, damu! Wakamgeuza Lorenzo aliyekuwa amelala kifudifudi, wakagundua mwanaume huyo alikuwa ameuawa! Tumbo lake lilikuwa limejawa na damu ambayo bado ilikuwa ya moto kabisa!
Kutazama vema zaidi, alikuwa ana jeraha la kisu, matundu matatu tumboni! Wakapata kitendawili. Nani aliyemuua Lorenzo ndani ya muda mfupi ambao walitoka?
Hapa wakajikuta wanaamini kuwa walengwa wao walikuwapo mulemule ndani ya hoteli. Na si tu kuwapo bali pia walikuwa wanawafuatilia kiasi cha kujua kuwa wametoka na wakaenda kummaliza Lorenzo!
Haraka wakatoka nje na kuanza kuangaza huku na huko. Na hapa wakashirikiana na walinzi wa hoteli baada ya kuwapa taarifa, msako ukafanyika kote hotelini.
Na hata baadae wakapitia taarifa za watu wote waliokuwamo humo ndani ya hoteli ili wapate kubaini nani hakuwapo au aliyetoka hivi karibuni.
Wakagundua kuna watu wawili tu waliotoka, nao wote wakiwa ni wanaume, kwa majina Zebedayo na Derick, wakiwa ni wakazi wa chumba namba 200.
Zaidi ya hapo hakuna kingine kilichopatikana.
Mabwana wale wakampigia simu mkuu wao na kumweleza habari hizo ambazo zilimshangaza na kumghafirisha sana.
Ila mchezo huu ulianzia wapi na ulifanyikaje?
Ni hivi, wakati mhudumu yule feki wa kwanza kabisa alipokuja kwenye chumba walichokuwa wanakishuku kuwa kina watu wao, akamkuta mwanamke mgeni hapo, ndipo mambo yalipoanza kuchanganyia.
Kwanza, mhudumu huyu hakuwa na kibango cha jina lake kama ilivyo kwa wahudumu wote hapa hotelini. Pili, japo sare yake ilijitahidi sana kufanana na za wahudumu wa pale, bado zilikuwa na kasoro kidogo kwenye ukoleaji wa rangi.
Na tatu, kuja kuulizia taulo kwa majira yale, tena ikiwa tayari yashabadilishwa asubuhi, kulileta shaka. Basi mwanamke huyo aliyempokea, akafikisha taarifa kwa mtu aliyemwomba afanye hivyo kwani alitegemea kutakuwa kuna ugeni mahali hapo.
Na alipotoa taarifa hiyo tu, mwanamke huyo akaondoka zake maana alishamaliza kazi.
Baada ya hapo, mengine yote yakawa historia. Mwindaji akawindwa kwa ustadi.
**
Saa tano asubuhi ...
Hodi sasa ilikuwa inagongwa kama fujo mno mlangoni. Hata Kinoo aliyekuwa amelala usingizi wa mfu akaamka. Akghafirika akipaza sauti yake nzito kuuliza kwa kufoka.
Hakujibiwa.
Akatazama kando, mkewe hakuwapo. Kichwa nacho kilikuwa kinamuuma sana. Alipata hata tabu kusimama. Alijikongoja mpaka sebuleni akitaka kuelekea mlangoni, ila mezani akaona unga fulani mweupe.
Akaujongea na kuutazama. Akaubinyia kwenye kidole chake na kunusa. Akapata shaka. Kabla hajauendea mlango, akaenda jikoni. Akarudi tena chumbani. Akagundua nguo za mkewe hazikuwapo!
Mwanamke ametoroka? Alijiuliza. Ina maana jana usiku alintilia dawa kwenye kinywaji? Akawehuka. Akili yake ikamtuma moja kwa moja kwenye pesa. Tazama pesa kama zipo!
Akatazama, hola! Patupu!
Akahisi miguu imemwishia nguvu. Akahisi mwili umekuwa wa baridi kama barafu. Akahisi haja zote kwa mpigo!
Bam! Bam! Bam! Mlango ukabamizwa tena na tena.
***