*ANGA LA WASHENZI II --- 60*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
“This is the time for us to finish the game,” alisema bwana yule mwenye sauti nzito. Wenzake wakaunga mkono hoja. Na hivyo basi wakakubaliana wanaume wale waliopo Afrika, the intellectual instinct, waanze kutekeleza kazi ya kufutia mbali mamlaka ya China ukanda wa Afrika ya mashariki na kati.
ENDELEA
Sasa mambo yalikuwa yameanza kupamba moto na vita rasmi ilikuwa imetangazwa, ambapo mataifa makubwa ya kibepari yameazimia kumwangusha tembo huyu mkubwa wa mlengo wa pili kabla hajazidi kutapanya na kuharibu shamba lao.
Kwa namna Uchina ilivyokuwa inakuja juu, si kitu cha kuwaza kuwa hofu kuu inatokota kwenye mioyo ya mabepari. Hii ni alama ya kushindwa. Alama ya kuzidiwa maarifa. Kitu ambacho kamwe hawako radhi kukiafiki.
Basi kikao baada ya muda kikafungwa na mabwana wale wakatawanyika. Ila bwana mmoja, si yule bosi wa Rob, alipokuwa kwenye gari aliongea na simu yake kwa muda mfupi akitoa maagizo. Anataka kambi ya wachina imalizwe haraka iwezekanavyo.
Bwana huyu alikuwa anatimiza tu kile walichokubaliana. Na hao aliokuwa anaongea nao hawakuwa wengine bali the intellectual instinct, kundi haramu la mauaji na mienendo ya kimafia, sasa likiwa limeshaweka makazi yake nchini.
**
Baada ya siku mbili … Dar, Uwanja wa ndege.
Ni majira ya mchana. Lee akiwa anakokota kibegi chake kidogo anaongea na simu akiwa ameweka sura ya kazi. Macho yake yamezibwa na miwani ya jua, na mtindo wake wa nywele ameubadili kidogo. Alikuwa amezilaza, na kwa wingi wake zikawa zinakaribia kugota mabegani mwake.
Punde alipotoka ndani uwanja wa ndege, yaani kuikuta barabara, akatia simu yake mfukoni na kuangaza kushoto kwake. Akaliona gari fulani likiwa laja. Range rover sport nyeusi. Ikasimama mbele yake, akakwea.
Gari likatimka kwa mwendo wa wastani uliokuwa unachanganyia kwenda kasi.
“Vipi, mmemwambia yeyote yule?” akauliza Lee.
“Hapana, hakuna anayejua,” akajibu jamaa aliyekaa kando na dereva.
“Safi sana,” Lee akapongeza na kuuliza, “Sheng anaendeleaje?”
“Yuko kama jana tu. Sioni kama kuna mabadiliko,” akaendelea kujibu yule jamaa aliyeketi karibu na dereva. Wakati akiteta akikunja kunja shingo yake kutazama nyuma alipokuwa ameketi Lee.
“Mpaka sasa hamjajua nani anayehusika na utekwaji wake?”
“Hatujajua. Wala sababu za wale wenzetu kujaribu kumuua.”
Lee akanyamaza. Kitu pekee alichokuwa amewaambia hawa watu ni ujio wake na ufanywe kuwa siri. Hakuna la ziada. Hivyo watu hawa hawajui kama Lee alinasa habari zozote toka kwa dada poa Glady.
“Si huko naelekea, tushike barabara ya kushoto,” Lee alielekeza.
“Kwani hatuendi makaoni?” dereva akauliza.
“Tunaenda,” Lee akajibu, “ila baada ya kutoka kwanza huku.”
**
Ngo! Ngo! Ngo! Ngo!
Glady alifunua shuka akaangaza kwa jicho moja. Bado alikuwa yu kitandani majira haya ya mchana na si ajabu kwani amelala asubuhi ya saa nne. Chumbani alikuwa na mwenzake ambaye alikuwa amelala vibaya kiasi cha kuacha maungo yake wazi.
Mwanamke huyo alikuwa ananuka pombe na hata miguuni bado alikuwa ana viatu vyake vya visigino virefu. Na hapo kitandani kulikuwa na chupa tupu ya Vodka.
“We Esther! Esther!” Glady aliita akimsukumasukuma mwenzake. “Wewe si nilikuambia ukalale kwako? Nani kakuruhusu ulale hapa?” Glady aliuliza. Ila alikuwa anaongea na mfu. Huyo Esther alikuwa hasikii hata tone. Mdomo wake unukao kileo, ulikuwa wazi akikoroma kama amekabwa.
“Wewe!” Glady akaendelea kusumbuka na Esther. “Si naongea na wewe Esther!”
Hodi ikagongwa tena. Sasa akili ya Glady ikakumbuka kuwa ameamka kwasababu ya hodi na si Esther. Akasonya. Kichwa kilikuwa kinamgonga kwa mbali na mwili wake ulikuwa umejawa na uchomvu. Alivuta shuka kwanguvu kumpokonya Esther kisha akajifunika na kwenda mlangoni.
Baada ya kuondoa loki zake duni, akakutana uso kwa uso na Lee.
“Kumbe ni wewe?”
“Ndio ni mimi?” Lee akajibu akiegemea ukuta. Alikuwa ameegesha gari lake mbali kidogo na hapa alikuwa mwenyewe.
“Mbona saa hii jua kali?” Glady akauliza na kisha akapiga mhayo.
“Nina maongezi kidogo na wewe,” Lee akajinasibu.
Glady akatikisa kichwa chake akifinyanga lips zake.
“Mchina, nimechoka. Kwanza kama unadhani utanipeleka kule kwenu, sahau kabisa. Kwa niliyoyaona siku ile, yanatosha kabisa!”
“Ndiyo maana nipo hapa,” Lee akateta.
“Ina maana wewe huyajui au?”
“Pengine wewe unayajua zaidi … Sikia, Glady, serious, sina muda sana wa kukaa hapa. Tunaweza tukaongea tafadhali? Sidhani kama itachukua muda mrefu.”
“Ulikuwa wapi siku ile nakutumia message? Hukusikia mlio wa risasi?”
“Sikuwapo hapa, nilikuwa China.”
“Oooh!” Glady akakuna kichwa chake kwa kidole kimoja alafu akapiga tena mhayo. ‘Nimechoka, nataka kupumzika.”
Lee akazamisha mkono wake mfukoni na kutoka na ‘wekundu’ kama sita hivi, akamwonyeshea Glady. Glady akatabasamu.
---
“Alinichukua, ila hakufanya chochote na mimi. Alikuwa bize sana kuongea na simu kupanga mikakati ya mauaji. Ila bahati si yake, wale watu aliowatuma walirejeshwa na akawaua kwa mkono wake mwenyewe,” alieleza Glady akiwa ameketi kwenye ngazi. Lee naye akiwa pembeni yake.
“Ulisikia sababu ya yeye kufanya hivyo?” Lee akauliza. Glady akapandisha mabega yake juu na kusema, “Hapana. Ila nilichosikia ni kwamba usiku ule ungekuwa mkubwa sana kwao. Na hata mimi alin’chukua ili akafurahie siku yake hiyo japo haikuishia kuwa nzuri nadhani.”
“Ahsante,” Lee akasema akisimama. “Nitakuhitaji tena karibuni. Namba yako si ile ile?”
“Umenimiss eenh?” Glady akauliza akimkonyeza Lee.
“Ni kwa kazi. Si kama ufikiriavyo,” Lee akamweleza na kisha akaenda zake.
***
Majira ya saa mbili usiku …
Kulikuwa na ukimya eneo hili. Kwa mbali, kwa mbali sana, maongezi yalikuwa yanasikika kwenye makazi ya bwana yule wa kichina aliyefanya hila ya kummaliza bwana Sheng.
Maongezi haya yalichukua muda mfupi, kama vile dakika mbili tu, na muda mwingi kulikuwa ni kimya. Yaani ukimya ulitawala dakika tano za maongezi haya ambayo kwa jumla na zile mbili zilikuwa saba za makutano.
Baada ya dakika hizo, sauti kubwa ya risasi ikavuma … na tena … na tena! Tatu kwa ujumla. Baada ya hapo, wanaume wawili wakatoka ndani ya makazi hayo wakiwa wamebebelea mwili wa bwana yule wa kichina na kwenda kuufukia, Lee akishuhudia.
Baada ya hilo tukio, akaenda zake hospitali kumwona Sheng aliyekuwa amelala kitandani kwa masiku sasa. Bado hakuwa na nguvu. Na mashine ya oksijeni ilikuwa iimefunika mdomo na pua yake.
Kwa mbali mashine ya kuhesabu mapigo ya moyo ilikuwa inafanya kazi, ikilia.
Lee akamsogelea Sheng na kumtazama kwa huruma. Ndani ya kifua chake akijiuliza ni nini kilijiri. Alikuwa anatamani sana kujua. Kichwani alikuwa ana maswali kadha wa kadha.
Akiwa amekaa hapo, mara Sheng akafungua jicho lake la kushoto kwa mbali. Akanyanyua vidole vyake kupapasa mkono wa Lee. Lee akashtuka kwa faraja kuona hilo. Akadaka mkono wa Sheng na kumtazama usoni akikodoa.
Kuna kitu Sheng alikuwa anataka kuongea. Uso wake ulionekana kuhangaika akitaka kusema jambo.. Basi Lee akamwondoa mask yake ya kumvutisha hewa, na kisha akasogeza sikio lake kwenye mdomo wa Sheng uliokuwa unamamata kwa mbali ukiwa umeegemia kushoto.
Sheng, akiwa anakoroma na akisikika kwa mbali sana, akamwambia Lee maneno kadhaa ya kichina. Na baada ya kusema hivyo, akakaa kimya. Lee akawahi kumrejeshea kinyago chake cha kuhemea. Ila hakufungua tena jicho wala kuchezesha tena vidole vyake wala kiungo chochote.
Lee akapata shaka, akamwita Daktari haraka. Naye alipokuja, akaenda kungoja nje. Kwa takribani kama nusu saa, daktari na nesi wakawa wapo ndani, vitu vikiingizwa na kutolewa. Baada ya hapo, daktari akiwa amenyong’onya akamwita Lee ofisini.
“Hali inakuwa mbaya kila uchwao. Ilikuwa ni ajabu sumu inaendelea kumtafuna mwili pasipo kujali juhudi zote hizo tulizofanya.” Daktari akatengeneneza miwani yake na kutazama baadhi ya karatasi ndani ya faili, kisha akasema kwa sauti ya chini;
“Tumekawia. Na hili linaelekea kugharimu maisha yake. Tumegundua ndani ya dripu kulikuwa na sumu. Hatujui imefikaje, na mbaya zaidi majibu yake yameshaanza kuonekana mwilini. Amepooza upande wake wote wa kulia. Matumaini yake ya kupona ni hafifu hafifu mno.”
Akiwa hapo, bado taarifa hizi zikiwa ngumu kuzimeza, mara akasikia king’ora cha hatari kikilia kwanguvu! Punde akaja mwanaume mmoja hapo akiwa amebebelea silaha mkononi. Akasema, “Tumevamiwa!”
***