Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI II -- 63*


*Simulizi za series*



ILIPOISHIA


Basi wakashuka na kusogelea hilo eneo. Ajabu wakakuta kuna kikopo kidogo cheupe chenye mfuniko mwekundu. Mmoja akakiokota na kuifunua. Ndani akakuta ‘chip’ yao na karatasi nyeupe yenye ujumbe uliosomeka,


“Welcome to the sky of the damned.” Kumaanisha karibu kwenye anga la washenzi.


ENDELEA


Wakaghafirika sana kukumbwa na kadhia hiyo. Aibu iliyoje hiyo? Waliona wamevulia nguo mbele ya umati. Waliona wamedhalilishwa haswa. Wanashindwaje na watu duni kama hawa? Na tena kwa wakati huo wakiwa wamempoteza mpambanaji mmoja vitani?


Basi wakarejea ndani ya gari lao na wasiende popote bali wakae na kujadili cha kufanya kwa maana sasa hawakuwa na namna mbadala, chip ilikuwa imetolewa mwilini mwa Sheng na hata lile gari lao, ambalo kama lingechukuliwa basi wangelifuatilia, nalo limetelekezwa.


Lakini japo walikuwa ndani ya gari kujadili nini kifuate, ajabu wakajikuta ukimya umewatawala. Vinywa vilikuwa vizito na pengine vichwa navyo viligoma kufikiri kwa muda. Wakakaa hapo kwa muda wa kama dakika kumi hivi, kukiwa kimya. Kitu pekee kilichojuza kuwa kuna watu ni sauti za pumzi.


“Let’s go home,” akapendekeza Wales. “It’s not safe out here.”


Basi gari likawashwa, wakatimka. Wakatembea barabarani kwa mwendo wa kama nusu saa, na wakiwa wamekwama kwenye mataa, kwa nyuma, dereva akaona gari la polisi. Akalitazama kwa umakini kwa kupitia side mirror, punde wakaruhusiwa kwenda. Wakaenda.


Na lile gari la polisi huku nyuma likawa linawafuata. Gari hili lilikuwa la modeli kama zile za corola, lakini lenyewe ubavuni lilikuwa lina rangi nyeusi na maandishi makubwa meupe, POLISI, na kwenye paa kulikuwa na taa ziang’azo, nyekundu na bluu.


Hapa bwana Denmark, dereva, akapata shaka juu ya gari hilo. Akafikiri kuliweka gari lao kando wapate kuteta na polisi ila akaona chaguzi hilo halitakuwa jema. Mazingra hayakuwa mazuri kwa wao kufanya tukio eneo hilo endapo wakikosana na hao wanausalama, basi akaendelea kutembea, na kwa tahadhari akaongeza mwendokasi wa gari.


Alipofika mahali alipoona ni ‘salama’ kwao, basi akaegesha gari kando na kungoja. Punde nalo gari la polisi likafika na kuegesha pembeni pia. Akashuka mwanaume mmoja aliyebebelea bunduki mkononi, na kidogo akashuka mwingine. Huyu yeye alikuwa amevalia sare za polisi.


Yule mwenye nguo za kiraia, akaamuru,


“Shuka chini na weka mikono juu!”


Akisema hayo alikuwa amejiweka mbali kidogo na usafiri huo. Na mikono yake imekaa tenge kujihami. Basi kidogo, Denmark akashuka. Ajabu tayari mwili wake ulikuwa umevalia suti nyeusi na si zile nguo ambazo walifanya nazo tukio.


“Is there any problem, officer?” akauliza.


“Yes, there is!” akajibu yule polisi aliyevalia nguo za kiraia. Bila shaka alikuwa ni mpelelezi.


“Raise up your hands!” akaamuru. Bwana Denmark akatii amri.


“Are you alone in that car?”


“Uuuuhm, no! I am with friends.”


“Tell them to get out! Hands up!”


Denmark akawatazama wenzake na kuwapa ishara ya kichwa. Wote walikuwa wamesikia amri ile, basi wakatoka wakiwa wameweka mikono juu. Na wote walikuwa tayari wamevalia suti zao kama yule mwenzao, Denmark.


“Who are you? And where are you coming from?” Afisa polisi akauliza. Denmark akawatazama wenzake kisha akapaza sauti, “We are just tourists. We are from beach.”


“Beach at this time? … may I see your documents?”


“Aahm, sure you may, but they are not here with us. They are where we live in, would you mind taking you there to see?”


Yule afisa akatazamana na mwenzake kwa macho ya mashaka. Alafu akaurudisha uso wake kwa wale wazungu, akawaamuru wageukie na kushika gari kwa ajili ya ‘search’, wakatii. Basi wale polisi wakajongea na kuanza kuwapekua wakipapasapapasa mifuko na maungo yao.


Walipomaliza, wakawakata wanaume hao wasonge kando na gari nalo lipekuliwe. Wakatii. Polisi wakaangaza ndani ya gari na kurusha macho huku na kule. Hakuna walichopata.


“We are sorry. You can just move on with your journey,” akasema bwana polisi akimpatia mkono Denmark.


“Never mind, it’s just normal,” Denmark akasema kwa tabasamu. Yule polisi na mwenzake wakajongea kufuata gari lao, na hawa wakina Denmark wakazama garini waende.


“ … sio wenyewe, sio wenyewe over …” polisi yule mkaguzi akateta na radio call. Lakini hapa ndipo akagundua kuna kitu hakipo sawa. Mkono wake wa kuume uliobebelea radio call ulikuwa na damu! Kutazama vema, ni kweli na si macho yake.


Hapa moja kwa moja akajua damu hiyo alikuwa ameitoa mkononi mwa Denmark. Basi akashuka upesi, lakini kabla hajasema jambo, gari la wakina Denmark likawa limeng’oa nanga na kujiendea. Akarudi garini na kuanza kulifuatilia.


Kwa ishara wakataka gari hilo likae kando. Lakini kwa sasa wakawa wamenoa, gari halikukaa tena kando na badala yake vita ikaibuka!


“Ndio wenyewe! Ndio wenyewe, over! …” polisi aliteta na radio call yake. Macho yakiwa yamemtoka pima kutazama gari walikimbizalo. “… plate number T 457 AAA, New Bagamoyo road! … T 457 AAA New Bagamoyo road, Over!”


Alipomalizia kusema maneno yake hayo akastaajabu kuona gari lile walikimbizalo, likikata kona ya ghafla, likasimama na kurudi nyuma upande wa kushoto. Pap! Wakatazamana na wale polisi. Kilichofuata hapo ikawa ni simulizi ya kusisimua. Risasi zilitupwa haswa, tena ndani ya muda mfupi tu, ila wale polisi hakuna aliyetoka na uhai wake hata mmoja! Wote wakamiminwa damu na kuachwa na matobo matobo kana kwamba karatasi. Kisha wazungu wakapotea!


Na walipofika huko mbele, wakavamia na kukwapua gari lingine kwa usalama. Sasa wakaondoka pasipo mushkeli mpaka kwenye makazi yao.



***


Saa tano usiku …



Ni nje ya nyumba lakini ndani ya uzio. Hapa Lee alikuwa amepigishwa magoti na Sheng akiwa amelazwa chini. Mbele yao kuna watu watatu nao ni Jona, Miranda, Marwa na Kinoo. Mkononi mwa Jona kuna bunduki ndogo na mdomoni mwa bunduki hiyo kuna kiwamba cha kumezea sauti. Na bunduki hiyo tayari ilikuwa ‘imekokiwa’ kwa ajili ya tukio.


Hapa nje ni baridi. Kuna manyunyu ya mvua. Na kwa namna anga lilivyokuwa limefungamana kwa uweusi, kulionyesha kuna dalili ya mvua kubwa kushuka muda wowote ule.


“Mbio za sakafuni huishia ukingoni,” akasema Jona akimtazama Lee. “Kiko wapi sasa? Leo upo mbele yangu ukiwa huna msaada, na huyo punda wako akiwa amejilaza kama mwana kuku aliyenyeshewa na mvua. Kuna lolote la kusema kabla ya risasi zangu mbili kung’oa uhai wenu usio na maana kwangu?”


Lee akatazama kwanza chini, na kisha akamtazama Sheng ambaye hakuwa na uhakika kama kweli yu hai au lah, kisha akasema, “Mbele ya macho yenu naweza nikaonekana si wa maana kwa sasa kama ukitazama hapa na si mbele. Lakini …” akamtazama Jona machoni. “Lijalo ni kubwa kuliko hili unalolimaliza. Linatisha, na limedhamiria kuuteka ulimwengu mzima.


Kama wataka kweli kulimaliza, kuyamaliza yote for the good of this country na ulimwengu kwa ujumla, basi unanihitaji.”


“Ni kitu gani hicho unachokiongelea?” Jona akauliza.


“Umeona kile kilichokuwa kule,” akasema Lee. “Umewaona wale waliotuvamia na kwa namna walivyofanya kuteketeza kambi nzima ndani ya muda usiozidi lisaa limoja. Kama haitoshi, watu hao si tu kwamba watatumaliza sisi na kwenda zao, la! Bali wataanzisha ngome yao hapa.


Na kwa kupitia ngome hiyo basi watateka kanda hii like never before. Mtashuhudia mauaji makubwa na hata vita kuzuka ili wapate vile vilivyomo ndani ya nchi hii kabla ya kuikausha kuwa jangwa.


Sidhani kama unawafahamu vema watu hawa zaidi ya kuwaonea hapa. Wameanza huko Uchina, na sasa wamefikia hapa. Wataufikia ulimwengu mzima na kuuweka kiganjani. Kisha watamgeuza kila mtu kikaragosi kabla ya kuwa maiti. Amini nakwambia.”


Jona akatulia kidogo kisha akauliza, “Kwahiyo wewe utawamaliza watu hao?”


“Siwezi kufanya hilo hata kidogo. Mimi ni kama chawa tu ndani ya msitu huo mkubwa. Ila ninachoweza kukifanya ni kuwatambua, na hata kuonyeshea wapi wanapatikana. Pengine mkiwa mmedhamiria, mkapate kuwamaliza kabla maji hayajawafika shingoni.”


Kabla Jona hajatia neno, Lee akasema akiwa anatazama chini, “Pengine sisi twaelekea kuisha, lakini lijalo linatuhofisha hata sisi.” Akanyanyua uso wake na kuendelea kuteta, “Nakupa maisha yangu kwa hii ahadi. Niruhusu nikusaidie kuwamaliza watu hawa, na punde tutakapokamilisha hilo, utanipatia bunduki hiyo mwenyewe, nami nitajimaliza.”


Jona, akiwa amefinyanga macho yake, akamtazama Sheng. “Siwezi kumwacha huyu hai. Hana sababu yoyote ya mimi kumbakizia pumzi.”


Akamnyooshea bunduki, lakini Miranda akaishika bunduki hiyo na kusema, “Ngoja kwanza …”



***


MIRANDA ANATAKA KUSEMA NINI?


NINI KITAFUATA?
 
Mmh yajayo yanatisha kweli.... mkuu wewe ni mnoma sana ahsante kwa leo...[emoji122][emoji122][emoji122]
 
Shunie njoo,

Hii sio ya kuisha leo wala kesho, maana kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo maadui wanavyozidi kuongezeka huku star wa story yetu akikuza timu yake,

Mbaya zaidi RAFIKI anakua ADUI na ADUI anakuwa RAFIKI

Lete vitu mkuu
Hata me naona inanivuruga unavyotegemea sio vile inavyotokea tivu sante
 
Back
Top Bottom