*ANGA LA WASHENZI II --- 67*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
“Let go of me!” Denmark akawaka akiwasukumia wenzake kando, Alipatwa na hasira maradufu. Uso wake ulikuwa mwekundu. Aling’ata meno yake kwanguvu, akasimama na kumtazama Lee akihema kana kwamba mbogo.
Lee akamkaribisha tena kwa kumuita kwa ishara na kusema,
“Camon my lady.”
ENDELEA
Holala! Denmark akanguruma kama simba. Akiwa amekunja uso wake, macho ameyafuma kwa ndita, mdomo ameubinua kama upinde wa mshale, akamsogelea Lee kwa kasi akitengeneza vishindo kana kwamba tembo. Alikuwa amefura haswa. Hakuna alichokuwa anakitaka zaidi ya kummaliza Lee.
Hakika zile dharau zake hakuweza kuzistahimili. Alikuwa amemvua nguo. Alikuwa amemdhalilisha mbele ya wenzake, tena awaongozao.
Basi akatupa ngumi zake kwa fujo. Kwanguvu. Haraka!! Lee akapata kibarua kikubwa cha kujikomboa. Ilikuwa ni kazi kubwa sana kwake kujikiinga dhidi ya mashambulizi haya. Hata kama hakuwa amekubwa, bado mikono yake ilipata maumivu kwani Denmark alikuwa na nguvu mno.
Pale Lee alipokuwa anaona anazidiwa kwa maumivu, basi akawa anasonga nyuma ama kuyeya ‘mazima’ kukwepa kombeo anazotupiwa. Alidumu kwa kama dakika tano, anashambuliwa tu. Anashambuliwa tu! Alishangazwa ni pumzi ya namna gani aliyokuwa nayo Denmark.
Hakuonekana kuchoka wala kupunguza kasi. Kama vile alivyoanza ndivyo alivyokuwa anaenenda. Hakuonekana mtu wa kuchoka muda mfupi ujao, hivyo basi kama Lee hatopata upenyo wa kushambulia, basi muda si mrefu atashindwa tena kujilinda. Atazidiwa. Na huo ndiyo utakuwa mwisho wake.
Akainjika mkono wake wa kuume kukinga ngumi ya Denmark, akainjika na wa kushoto, akarudi nyuma. Akainjika mguu wake kumzuia Denmark kurusha teke. Akainjika tena mkono wake kuume kukinga shambulizi. Akainamisha kichwa, akakipeleka kulia, akakirudisha kushoto kukwepa ngumi.
Alafu akasonga tena kando!
Denmark, kama mtu aliyetambua kuwa Lee anaanza kuzidiwa, akamsongea upesi na kuendelea kumtupia mambo mazito mazito. Mateke, viwiko, ngumi, na hata magoti. Na kweli taratibu mbinu yake ikaanza kuzaa matunda. Sasa Lee akawa akikwepa hii na ile, ijayo inamkomba.
Bahati si kwake, alipochelewa kidogo tu kujikinga, akakumbana na ngumi ya haja ya bwana Denmark iliyofukua taya zake na kumnyanyua juu kama unyoya! Na kabla hajagusa chini, Denmark akapanua mguu wake wa kulia kwenda juu, kisha akamsigina tumbo na kumgotesha sakafuni. Lee akapiga kelele kali!
Aaaaaaggh!! akajikunja kugugumia maumivu makali ya tumbo. Akakunja sura yake akisaga meno.
“Get up bitch!” Denmark akafoka akikodoa macho. Kinywa kilitema mate kana kwamba manyunyu ya mvua ya masika.
“I said get uupp!!”
Akamfuata Lee kwa upesi. Akamzaba mateke mawili ya tumbo. Miranda akashindwa kuvumilia kumwona Lee anashambuliwa kiasi kile. Akapaza sauti, “Stoop!” akisonga kumfuata Denmark, ila kabla hajafika, akastaajabu teke likimsomba kichwa, akajikuta hewani, sekunde, akadondokea chini kama mkungu!
Akapiga yowe la maumivu.
Basi hapa akawa kana kwamba amemtonesha Lee kidonda. Mwanaume huyo akanyanyuka akisema, “Is that the best you have?”
Denmark akaguna kwa kebehi. Akapiga hatua mbili kumfuata Lee. Akatupa mashambulizi yake kama ilivyo ada. Ila kwa sasa Lee hakupumbazia kama muda ule. Ndani ya dakika moja akawa ametambua cha kufanya.
Denmark akazama kosani. Lahaula! Lee akamkandika ngumi tatu za haraka mno. Akiwa anaugulia, Lee akapanda kwa hewa. Baba, akafyatuka teke lililoadhibu taya za Denmark. Na kama haitoshi likafuatia teke lingine. Denmark, na uzito wake, akanyanyuka juu kabla ya kumwagikia chini.
Yote hayo yalitokea ndani ya sekunde tatu tu! Sekunde tatu tu!
Denmark akachumpa kwa mikono yake na kusimama. Hasira zimemjaa pomoni. Akaja kwa kasi kumfuata Lee. Naye Lee hakumngoja kwa sasa. Akajikuta chini ndani ya muda mfupi, akafyagia miguu ya Lee kwa miondoko ya mdudu nge! Na kwa namna miguu yake ilivyokuwa inazunguka kama feni baridi, Denmark akajikuta akiadhibiwa vilivyo.
Sasa akalazwa chini na kutulia. Alikuwa amezidiwa.
“Hey, are you fine?” Sweden akamuuliza Denmark.
“Do I look like that?” Denmark akafoka na kuamuru, “Kill him!”
Basi wale wanaume watatu, Ireland, Sweden na Wales wakapoke agizo hilo la kushambulia. Ila kabla hawajafanya hilo, mara wakasikia gari huko nje. Wakatazamana. Punde si punde geti likafunguliwa na wanaume wawili wakazama ndani!
“We have to go!” akapaza Denmark. Basi mara Ireland akachomoa cha kuchomoa kwenye nyonga yake na kukibamiza chini. Muda si mrefu moshi ukatanda. Watu wakapotelea! Moshi ulipokoma, hawakuonekana wapi wameelekea.
***
“Inabidi tuwe makini sana. Uzembe kama huo unaweza kutugharimu maisha!” alifoka Jona. Walikuwa wote wamekaa sebuleni isipokuwa Sheng aliyekuwa amelala ndani. Ni tulivu haswa. Na hata umeme uliokuwa umekatika, sasa ulirejea.
“Nitahakikisha halitokei tena kosa kama hilo,” akajitetea Marwa. “Sijui nilipitiwaje? Tulikuja kutahamaki wakiwa karibu haswa. Hata kukimbia hatukuweza.”
Kukawa kimya kidogo. Jona akamtazama Lee aliyekuwa anatazama chini. Uso wake ulikuwa umejaa majeraha na hata mwili wake ulikuwa na maumivu ya hapa na pale. Alikuwa ametulia tuli kana kwamba maji mtungini.
“Ahsante sana, Lee,” akasema Jona. “Sitasahau ulichokifanya siku ya leo, unastahili pongezi.”
Lee akatikisa kichwa chake pasipo kusema jambo. Kisha akaendelea tena kutulia.
“Sasa nini kinafuata? Inabidi tuwe na mipango ya kuwamaliza hawa watu kabla hawajaleta madhara.”
Hapo Lee akateta jambo. “Tafadhali,” Kila mtu akamtazama na kumpa masikio.
“Inabidi tuwe makini sana. Watu wale si wepesi kama pengine tudhaniavyo. Tuhakikishe mipango hiyo inakuwa ya akili zaidi kuliko nguvu. Endapo tukisema twende battle na wao, tutapoteza, na haswa sasa hivi wakiwa wameshindwa kuonyesha umwamba wao kwa mara ya kwanza.
Lazima watajipanga zaidi ya mara hii.”
“Lakini,” akasema Jona. “Wamejuaje makazi yetu?”
Akauliza akimtazama Marwa. Marwa akamtazama Lee na kusema, “Nadhani Lee anaweza kutupatia majibu.”
“Mimi?” Lee akatahamaki. “Nitapata wapi majibu hayo?”
“Lee,” Marwa akaita. “Ulikuwa wapi wakati Sheng alipokuwa ametekwa?”
“China,” Lee akajibu.
“Huko nini kikatokea?”
“Mambo mengi tu yalitokea. Siwezi kusimulia yote.”
“Lipi lililokuwa kubwa?”
Lee akafikiri kidogo na kisha akasema, “Nilitawazwa kuwa kiongozi.”
“Na hiyo ndiyo sababu,” Marwa akateta. Lakini bado kila mtu akwa kwenye bumbuwazi. Hawakuwa wameelewa jambo.
“Unamaanisha nini kusema hayo?” Lee akauliza. Uso wake ulihakisi namna ambavyo alikuwa kwenye mkanganyiko.
“Utakuwa una chip mwilini mwako. Kama ile aliyokuwa nayo Sheng. Ujio wenu hapa ndiyo ambao umetuweka sisi bayana. Tumekaa hapa kwa muda, na kama wanaume wale wangekuwa wana namna ya kututambua, basi wangeshalifanya hilo tangu pale Jona aliponusurika kukamatwa nao.
Na kwa upande wa Sheng, chip tulishatoa, sasa nini kinabakia hapo kama kielelezo isipokuwa Lee?”
Basi kuthibitisha hilo, Lee akakaguliwa mwili, na kweli ikagundulikana ana chip mwilini mwake. Akajaribu sana kukumbuka nini kilitokea na ni muda gani aliwekewa chip hiyo. Akili yake ikamweleza kuwa itakuwa muda alivyokuwa yu hoi anaumwa!
Lakini kwanini ilifanyika kwa siri hivyo? Mbona hakushirikishwa? Na je kwa Sheng ilikuwa vivyo hivyo? Maswali haya hakuwa na majibu nayo.
“Sasa tunafanyeje?” akauliza Miranda. “Tuiharibu hiyo chip?”
“Alafu?” Jona akauliza.
“Ili wasiweze kututrace!”
“Hapana,” akasema Jona. “Kwakuwa watu wale itakuwa ngumu kuwatambua mahali walipo endapo wakiacha kutumia ule usafiri, hii chip itakuwa nyenzo nzuri ya kutambua na kuwacontrol.”
“How na ipo mikononi mwetu?” Kinoo akauliza.
“Kama walitumia chip hii kuwaongoza mpaka kuja hapa, basi wataitafuta tena. Tena sasa kwa kulipiza kisasi. Hivyo itakuwa rahisi kuwazamisha mtegoni kwa kuitumia.”
Wazo hilo likaonekana kuwa na hekima ndani yake.
“Na punde tutakapowatia mikononi, basi tutapata getaway nzuri sana ya kuwamaliza pamoja na genge lao!”
***
Saa nne asubuhi …
Sauti ya Denmark akifoka ilisikika chumbani. Baada ya muda mfupi, mlango ukafunguliwa akatoka akiwa na sura nyekundu. Mkononi alikuwa amebebelea simu.
Akaelekea sebuleni na kuketi. Wenzake pia walikuwa huko. Na alipofika, wote wakamtazama kana kwamba wanatarajia jambo kutoka kwake. Ila kukawa kimya kwa muda. Denmark alikuwa amefura. Na kutua fundo lake kifuani akaendea maji ya kunywa na kujijaza mafundo manne makubwa makubwa.
Kisha akahema.
“We have to kill him today. So get prepared.” akasema Denmark. Na asiwe mtu wa kungoja maoni, akaenda zake kurudi chumbani. Wenzake wakabaki wakitazamana.
Ni wazi hali ilionekana si shwari.
***
Majira ya saa kumi na mbili jioni …
“Jona!” Marwa akaja chumbani akiita. Uso wake ulikuwa umepaliwa na hofu. Jona alishtuka toka kitandani na kumtazama. “Vipi?”
“Kuna jambo unatakiwa kuona. Upesi!” Marwa akasisitiza na kisha wakaongozana mpaka sebuleni. Jona akakalia kiti na kutazama tarakilishi. Lakini kabla hajaona kitu, Marwa akasema:
“Wapo karibu na Ikulu. Nadhani ….”
“Watakuwa wameenda kumuua Raisi?” Jona akakatiza kwa tahamaki.
***