Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI II --- 73*


*Simulizi za series*



ILIPOISHIA


Basi kwa wakati huo huo, wakina Denmark wakatumia mlango mdogo wa dharura uliokuwapo upande wa rubani, wakachoropoka toka kwenye ndege baada ya kupambana na pepo kali mno. Sasa wakawaacha wakina Jona wakipambana kwenye ndege inayoenda kuanguka.


ENDELEA


Hakukuwa na cha kufanya kunusuru ndege hii, hilo lilikuwa bayana. Ndege ilishapoteza mwelekeo na si tu hivyo, ilikuwa inaelekea kuanguka vibaya sana hivyo kubeba roho za wote wale waliokuwa ndani yake.


Si Jona, Miranda wala Lee waliokuwa na la kufanya hapa. Upepo ulikuwa unaingia mwingi sana kwenye ndege, na muda si mrefu bawa la kulia likapata moto na kukatika, likaacha tundu kubwa kwenye ndege ambalo nalo likazidi kuzamisha upepo uso na kifani.


Hata jitihada za kuchoropoka toka kwenye ndege haikuwa inawezekana. Upepo uliokuwa unaingia ndani ya ndege ulikuwa mkali sana. Uliwabamizisha na kuwang’ang’anizia watu kwenye kuta za ndege. Hata kuhema ilikuwa ni kazi kubwa. Kama ndege hii ingeendelea kufanya hivi kwa muda, basi watu wangekufa kabla haijagota chini.



Kama baada ya dakika kumi na moja tangu ndege ianze kwenda mrama, Miranda akaanza kupoteza fahamu. Macho yake yalipanda juu na kifua chake kikihaha kuhema. Alikuwa anapitia wakati mgumu sana, na zaidi alikuwa ni mwenye ugonjwa wa kuhofia vimo virefu.


Jona alimtazama mwanamke huyo akiwa hana la kufanya. Alichokuwa amekifanya Jona ni kujificha nyuma ya kiti ngangari cha ndege ambacho kilimziba na upepo mkali. Hali haikuwa njema hata kidogo.


Alitazama kushoto na kulia kwake akiwaza namna ya kumkomboa Miranda. Hakutaka kukubali kuwa hamna jinsi. Alifikiri kutambaa aking’ang’ania viti mpaka atakapomfikia Miranda. Ila alipoanza tu kufanya hivyo, akajikuta anatupwa na upepo punde tu baada ya kutoka kwenye mgongo wa ‘siti’.


Alibamiziwa ukutani na upepo ukawa unamsulubu ipasavyo. Alishindwa kuhema kabisa, upepo ulikuwa mwingi mno kiasi kwamba hakuweza kutoa hewa nje bali kuingia tu.


Akiwa anatazama kwa mbali kama mtu aishiaye na uhai wake, macho yanatoa machozi, mdomo ameukaza, masikio hayafanyi kazi, akaona ndege ikiwa inakaribia kufika chini. Na kheri ndege hiyo ikiwa inaelekea baharini!


Sekunde mbili tu, ndege ikakita juu ya uso wa bahari kwanguvu kana kwamba nyangumi mkubwa wa bluu. Ikazama, na taratibu mno ikaanza kusonga kwenda chini kabisa.


Ndege hii wakati yachapa maji ya bahari, ilisababisha mfarakano mkubwa, vioo vilipasuka, viti vilingoka na kadhalika. Lee na Jona walikuwa ni wahanga wa hili, walichanjwa na vioo na hata kukitwa na vitu mbalimbali.


Lakini hapa ndipo palikuwa mahali pa kuokoa roho zao. Ni kheri hata ndege hii ilikomea baharini maana kama ingeliangukia mahali pengine basi ilikuwa ni uhakika kuwa asingenusurika yeyote yule.


Jona aliogelea kumfuata Miranda ambaye alikuwa ameishiwa na nguvu na aelekea kufa. Si kwamba mwanamke huyo hakuwa anajua kuogelea, lah! Bali hakuwa na nguvu kabisa. Mwili wake ulikuwa umeteseka sana angani hivyo hakuwa na nguvu ya kupambana na mawimbi ya bahari.


Jona akambeba na kutoka naye ndani ya ndege. Akapiga mbizi kwenda mpaka juu, alipofika akavuta hewa fundo kubwa. Akamsaidiza pia na Miranda kuhema. Mara kidogo Lee naye akachomoza juu, Jona akampatia kazi ya kumtazama Miranda ambaye alikuwa ameanza kupata ‘momentum’.


“Nata kurudi kule chini kutazama wengine!” alisema Jona na basi akavuta pumzi kadhaa za kutosha, akazama chini akiogelea kana kwamba samaki.


Ila kinyume na alivyokuwa ametaraji, ndege ilikuwa imeenda chini zaidi, ilibidi afanye jitihada za ziada kuifikia na kuzama ndani kufanya uokozi. Na kwa muda huo huo afanye jambo hilo kwa wepesi kabla hajakaukiwa na pumzi kifuani.


Basi akazama ndani ya ndege na moja kwa moja akapiga mbizi kufuata chumba alimokuwemo Raisi na wahudumu wake. Akafungua mlango huo kwanguvu. Kutazama ndani, akaona wahudumu wale pamoja na Raisi wakiwa hawana dalili ya uhai. Akamfungua Raisi toka kwenye kitanda chake na kumnyanyua pamoja na mhudumu mmoja, daktari, akaanza kupiga mbizi kwenda nje ya ndege.


Ndege ilikuwa imeshuka chini zaidi ya mara alipoingia hivyo safari ya kupanda juu ilikuwa ni ndefu sana. Na kama haitoshi hakuwa peke yake, alikuwa pamoja na watu wawili mabegani, watu wazima wenye kilo zao.


Akajitahidi sana kupiga mbizi, lakini taratibu pumzi yake ikaanza kufikia kikomo. Bado alikuwa mbali na uso wa bahari. Alijitahidi kuongeza nguvu lakini bado hakuwa anaweza kutoboa kabisa. Hata yeye aliliona hilo, basi akawa hana budi kumwachia mtu mmoja apande na mwingine.


Akamwachia daktari, sasa akabaki na Raisi peke yake. Akaongeza kasi maradufu lakini bado hakuwa na uwezo wa kumaliza hili zoezi. Juu kulikuwa mbali. Mbali haswa. Hata kama angelimwachia Raisi aende mwenyewe bado uwezekano ulikuwa mdogo.


Ila hakukata tamaa. Hakutaka kushindwa kwenye hili kabisa. Aliamua ajitahidi kadiri awezavyo, na pale atakapoishia basi ndiyo uwe mwisho wake.


Akaogelea tena na tena, akasonga kama mita tano tu, nguvu zikaanza kumwishia mwilini. Sasa akajihisi mwisho wake umefika. Hakuwa anasonga mbele tena, alianza kuhisi anarudi nyuma kwenda kwenye sakafu ya bahari ambayo hata ndege yenyewe bado haikuwa imefikia.


Mapigo yake ya moyo yalianza kunyamaza. Mikono yake ilianza kupoteza nguvu kumwachia Raisi. Macho yake yalianza kupoteza uwezo wake akielekea kufa.


Sasa akiwa amekata tamaa na amekubali kuwa anakufa, akahisi mkono wake umeshikwa! Akavutwa kwanguvu kuelekea juu. Na punde, sekunde kadhaa, akajikuta yupo juu. Mkono wake wa kuume bado ulikuwa umemshikilia Raisi. Akahema kwanguvu sana. Kwa muda wa kama dakika tano akawa anahema tu … anahema tu.


Alipokuja kutulia, alimwangazia Raisi ambaye alikuwa amepokelewa na Lee na Miranda. Mwanaume huyo alikuwa amekwishafariki. Haikujalisha walifanya jitihada gani, hakukuwa na muitikio wowote ule toka kwake. Hata mapigo yake ya moyo yalikuwa yameshazizima.


Asingeweza kudumu kwenye maji kwa muda wote ule ukizingatia hali yake iliyomfanya asiwe kwenye fahamu zake. Lakini pia inawezekana mwanaume huyo akawa alifariki hata kabla ya ndege kuzama majini. Yote yawezekana kuwa majibu.


Basi Jona akaona ni kheri wautunze mwili wa mheshimiwa huyo kwani inawezekana kuja kuwa na matumizi kwa hapo baadae. Ni vema hata watakapopata nafasi ya kurudi nchini warudi na mwili huo kama kielelezo kuwa walijaribu, angalau walipambana kumnusuru mkuu wa nchi.


Jua lilikuwa lataka kuchipukia, lakini likazongwa sana na mawingu.



***



Saa mbili asubuhi, Julius Nyerere Airport.



Wanaume wawili, maafisa Usalama waliokuwa wamevalia kaunda, walikuwa wamesimama kandokando na uwanja patuapo na paondokeapo ndege.


Mmoja aliyekuwa mfupi na mweusi kuliko mwenzake, alikuwa ametia mkono wake wa kushoto mfukoni na wa kulia ukiwa umeshikilia simu yake kwa maongezi. Alikuwa anaongea na mkubwa wa kazi aliyekuwepo huko makaoni.


“ … ndege imepaishwa na watu wengine, huenda ni maadui. Marubani wote waliotakiwa kuwapo ndnai ya ndege wamekutwa wamekufa! … ndio, mkuu. Tumejaribu lakini mpaka sasa hamna mafanikio. Ndege haionekani kwenye rada yoyote ile, na kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, mara ya mwisho kupatikana ilikuwa ni juu ya bahari ya Atlantiki, upande wa Kaskazini Mashariki … sawa … sawa, mkuu!”


Alipokata simu hiyo, wanaume hao wakaelekea kwenye ofisi ya mawasiliano ya ndege ipatikanayo kwenye Uwanja huo kwa ajili ya taarifa zaidi.


Baada ya masaa mawili, taarifa ikawa rasmi sasa kuwa Ndege iliyokuwa imembebelea Raisi imepotea. Hakuna inapoonekana. Hata kule India ambapo ndipo ilitakiwa kuwapo kwa muda huo, hawana habari nayo.


Taarifa hizi zikazidi kuweka watu kwenye hali ya taharuki na mshangao. Kwasababu za ndani, ikabidi wakubwa wa vyombo vyote vya Usalama wakutane kwa ajili ya kikao cha dharura. Makamu wa Raisi naye akhudhuria kikao hicho kutazamia nini cha kufanya kutoka na hali hii ya kustaajabisha.



***



Miranda alikohoa akiwa amejikunyata. kwa muda wote huo, bado walikuwa kwenye maji. Mvua ilikuwa inanyesha, hali ya hewa ilikuwa baridi sana. Ukungu ulikuwa umetawala kiasi cha kutoona vema pande zao nne za duni.


“Inabidi tumwache,” akasema Lee akimtazama Jona aliyekuwa amesmshikilia Raisi. “Umechoka sana. Anakutia uzito zaidi.”


Jona akatazama mwili wa Raisi. Ulikuwa ni wa zambarau ukiwa na uweupe kwa mbali wa barafu. Ulikuwa ni wa baridi mno kana kwamba jiwe lililotoka kwenye jokofu. Hata mwili wa Jona ulikuwa wa baridi ila si kwa kiasi hiki.


“Labda tutapata msaada,” akasema Jona. Ila sauti yake ilionyesha kabisa kuwa na upungufu wa matumaini. Walikuwa wamepiga mbizi sana lakini mpaka muda huo hawakuwa wameona kitu chochote isipokuwa maji tu. Watakaa humo kwenye maji mpaka muda gani na huku ni ya baridi chini ama karibu na nyuzi sifuri sentigredi?


“Jona,” Miranda naye akaita. “Hatuna namna. Mwache tupambanie maisha yetu kwa mara ya mwisho au tufe wote.”


Jona akashusha pumzi ndefu. Akatazama mwili wa Raisi kwa macho ya huruma, ila kabla hajauachia mwili huo uzame kwenda sakafuni mwa bahari, wakasikia mlio wa risasi! Kutazama wakamwona Miranda akiwa ametoa macho na kuachama kinywa.




***
 
Aiseee ina maana hawa wahalifu wameanguka pamoja na ndege? Aisee hapa kazi ipo tena kubwa mmno
 
Back
Top Bottom