*ANGA LA WASHENZI II --- 74*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Jona akashusha pumzi ndefu. Akatazama mwili wa Raisi kwa macho ya huruma, ila kabla hajauachia mwili huo uzame kwenda sakafuni mwa bahari, wakasikia mlio wa risasi! Kutazama wakamwona Miranda akiwa ametoa macho na kuachama kinywa.
ENDELEA
Jambo hilo lilimshtua sana Jona, alidhani Miranda atakuwa ametwangwa risasi. Akamshika akiwa ametoa macho, akamuuliza, “Miranda, nini?”
Ni kama vile walisahau kuwa risasi yaweza kupigwa kwa mara nyingine tena na kuwadhuru. Miranda akamtazama Jona na kumwambia, “Risasi!”
“Imefanyaje? Imekupiga?” Jona akauliza kwa pupa. Miranda akatikisa kichwa akiwa ameachama kinywa. Akasema kuwa risasi imempitia sikioni muda si mrefu ulopita. Na alikuwa anashangaa kwa kudhani aidha amekufa.
Basi Jona akamzamisha, wote wakazama kwa haraka na kusonga ndani ya maji. Walikuwa wamepata nguvu ghafla, lakini pia tumaini kwenye wakati huu mgumu. Japo walikuwa wanashambuliwa kwa risasi, walipata kujua kuwa hapo karibu na wao kutakuwa na sehemu kavu ya ardhi ambayo husimamiwa na hao watu wanaotaka kuwaua.
Na ni kweli walichokuwa wanadhani. Kwa umbali wa hatua kadhaa toka walipo kulikuwa na kisi kikubwa sana, lakini hawakuwa wamekiona kwasababu ya ukungu. Kisiwa hicho pweke kilikuwa kimejawa na misitu iliyofungamana kwa umbijani.
Kwenye fukwe, mchanga mweupe unaovutia na hata pia matumbawe yakushangaza. Lakini papo hapo kulikuwa na wauaji waliokuwa wamebebelea bunduki, nao ni Denmark na mwenzake Wales.
Wanaume hawa wa kizungu walikuwa wametua mbali kabisa na hiki kisiwa baada ya kujirusha toka kwenye ndege. Walijikuta baharini na hivyo basi wakafanya jitihada za makusudi kufika hapa.
Lakini kinyume kabisa na matarajio yao, wanawaona watu waliowaacha kwenye ndege wakiwa hai. Jambo hili si tu kwamba linawashangaza, bali linawakasirisha mno.
Haraka baada ya kubaini hilo, wanafanya jitihada za kuwamaliza kwa kuwatupia risasi lakini nazo bado hazikufua dafu. Na hapa tuongeapo tayari walikuwa wameshawapoteza watu hao wakiwa hawajui wapo upande upi wa maji.
“You should have killed her!” aling’aka Denmark akimweleza Wales juu ya kosa lake la kumbakiza Miranda. Lakini Wales akajitetea kuwa ni sababu ya upepo. Upepo ulikuwa mkali na hivyo mahesabu yake yakaenda kombo.
Basi hawakuwa na la kufanya hapa zaidi ya kutupa macho yao huku na kule kuwatafuta walengwa wao kwa kutumia hadubini yao. Wakafanya swala hilo kwa muda wa takribani dakika tano, hawakufanikiwa kuona kitu. Ni kama vile walikuwa wameshawapoteza watu wao kabisa.
“Now what we do?” akauliza Wales.
“Search them!” akafoka Denmark, kisha akamzaba Wales kibao cha kichwa. “Fool!”
Wales akakwazika na hiko kitu, lakini hakuwa na la kufanya. Akazamisha macho yake kwenye matundu ya hadubini na kuendelea kusaka wapi walipo watu wao, wakati huo Denmark akaenda kujipumzikia chini ya mti akimtazama.
Alisaka lakini hakufanikiwa. Jona na wenzake walikuwa tayari wameshazunguka upande wa nyuma wa kisiwa na kukomboa nafsi zao. Jona akiwa bado amembebelea Raisi wakazama ndani ya misitu kwa usalama zaidi. Wakatulia kuvuta hewa na kupumzika.
Lakini walijuaje kama upande huu kuna kisiwa mbali na ukungu uliokuwa unasumbua macho yao?
Punde walipopata nafasi ya kuongea baada ya kuzama ndani ya maji kuepuka risasi, Lee alimuuliza Miranda ni upande upi wa sikio risasi ilmpuliza. Naye Miranda alipojibu, basi wakapata kutengeneza jografia ya wapi risasi ilipotokea, na basi huko ndiko kwenye ardhi kavu.
Sasa wamefanikiwa japo hawajui wapi adui alipo na nini amepanga. Kama litakuwa ndani ya uwezo wao, basi wahakikishe wanawahi kummaliza adui kwani endapo maadui watawawahi wao, basi itakuwa tabu sana maana wao hawana silaha mikononi mwao.
Basi baada ya muda mfupi kupumzika, Jona akauficha mahali mwili wa Raisi na kuwataka wenzake waanza kuwasaka maadui zao kwa tahadhari. Sasa wakaanza kunyatanyata na kuangaza macho yao huku na kule. Ila bado miili yao ilikuwa mizito, na zaidi walikuwa wamechoka. Kupambana kwenye maji kwa muda mrefu, kuliwapunguzia nguvu kwa kiasi kikubwa na hawakuwa na muda wa kutosha wa kupumzika.
Basi wakaendelea kutembea. Kisiwa hiki ni kikubwa, hapa sasa wakaanza kujua. Walitembea kwa muda mrefu lakini bado hawakuwa wamefikia kikomo. Na basi kwasababu walikuwa wamechoka mno, Lee akapendekeza wapumzike maana hata watakapokutana na maadui hawataweza kufua nao dafu kutokana na kuwa dhaifu.
Wazo hilo lilikuwa jema ila hatarishi, watapumzikia wapi? Vipi wakiwa mapumzikoni wakavamiwa? Iliwalazimu kuwa waangalizi maradufu hapa.
“Pengine tupumzikie juu ya miti,” Miranda akashauri, walipoona ni wazo jema, Jona na Lee wakaanza kukata matawi kuunda viota. Walidumu kwenye hilo zoezi kwa dakika kadhaa, walipomaliza wakavifunga viota hivyo mitini na kupumzika.
Haikuwa rahisi kuonekana. Viota hivyo vilifanana na matawi ya miti. Miti ilikuwa mingi sana hapa, kwa mtu kung’amua kuwa kuna makazi huko juu ya miti basi ni juhudi kubwa zimefanyika.
Na kabla hawajajipumzisha, Jona alihakikisha kuwa eneo hilo lipo vema kiulinzi, mbali na macho ya watu.
Basi isichukue muda, wakapitiwa na usingizi. Ila usingizi wa mashaka. Walikuwa wanafumbua macho yao kila muda kutazama, haswa pale walipohisi huenda kuna shaka.
Zikapita dakika kumi na tano, hatimaye wote sasa wakapitiwa na usingizi. Hawakuweza kudumu kutazamatazama tena. Walikuwa wamechoka mno, miili iliwazidi uwezo wao kumudu.
Basi dakika zikasonga zaidi na zaidi. Kama baada ya nusu saa, kule fukweni, bwana Denmark na Wales wakagundua kulikuwa na nyayo za viatu vya binadamu. Walikuwa wamefika ule upande ambao Jona na wenzake walikuwa wameingilia.
“You see,” akasema Denmark. “Now they are here. They are in the island!”
Wakatupa macho yao ndani ya kisiwa. Kilikuwa ni kikubwa sana. Watu wao watakuwa kwa upande gani? Hicho kilikuwa ni kitendawili kikubwa kuking’amua.
Wakafuatilia nyayo zile ambazo zilizama ndani ya msitu, lakini hazikudumu sana zikamezwa na majani. Haikuwa tena rahisi kuona nyayo za watu. Hapa sasa wakalazimika kwenda tu kwa hisia. Kitu pekee kilichokuwa kinawapa imani ni kuwa, walengwa wao hawakuwa na silaha kama wao.
Lakini wakiwa njiani, Denmark aliendelea kumsema Wales kwa uzembe aliokuwa ameufanya. Alikuwa anamtupia lawama na hata kumtusi. Na si tu yeye, hata wale wengine ambao tayari walikuwa wamekufa, akisema kuwa wao ndiyo chanzo cha kasi hiyo kuzorota. Laiti kama wangelikuwa wametilia maanani, basi kwa muda huo wangekuwa wapo Uingereza.
Maneno hayo yakawa yanamkwaza sana Wales. Hakuona hoja ya wao kulaumiana wakati walikuwa wapo pamoja kwenye kazi, na zaidi hakuona haja ya Denmark kumwendesha kiasi hicho ingali wote ni watu wa daraja moja. Denmark ni mkubwa kwasababu tu ya kuteuliwa, lazima awapo kiongozi, ila si kusema ana uwezo kushinda wenziwe.
“I am sick and tired of your bullshit, Den!” Akafoka Wales. “Can I have a moment of peace, please?”
“What did you say?” Denmark akauliza akimsogelea Wales.
“You heard it!” akajibu Wales akimtazama Denmark machoni. Basi Denmark akapandwa na hasira na kumzaba kofi kali Wales mpaka kudondoka chini. Mwanaume huyo uso wake ukawa mwekundu kwa hasira.
Akanyanyuka pasipo kusema jambo. Akajikung’uta, na ghafla akamwelekezea bunduki bwana Denmark na kumwagia risasi tatu. Denmark akiwa ametoa macho kwa kutokuamini, akadondoka chini na kufa macho yakiwa wazi.
“Die you bitch!” akafoka Wales kisha akamkandika teke Denmark aliyekuwa mfu tayari. Alipomaliza hapo akachojoa chombo cha mawasiliano toka kwa Denmark na kutoa taarifa makaoni juu ya eneo walilopo, lakini pia kuwa wamepungukiwa idadi ya watu hivyo wanahitajika watu kadhaa kumsaidia.
Alipokata mawasiliano akamtemea mate Denmark na kwenda zake. Ila milio ile ya risasi iliyomuua Denmark iliwashtua na kuwafanya wakina Jona kuwa tenge.
***
Saa tano asubuhi …
Makomandoo sita walikuwa wameshajipaki kwenye ndege ya kivita tayari kwa ajili ya kusafiri kwenda kumtafuta Raisi huko baharini mwa Atlantiki. Makomandoo hawa walikuwa wametoka kuongea na mkuu wao muda mfupi uliopita wakipewa hamasa ya kutenda kazi yao. Ilikuwa ni lazima warejee na Raisi nyumbani. Hata kama amekufa basi warejee na mwili wake.
Basi pasipo kupoteza muda, ndee ikanyanyuka na kwenda kwa kasi sana. Makomandoo wale wakiwa wametulia ukutani mwa ndege wakiwa wamefungia mikanda yenye nguvu. Walikuwa ni wanaume walioshiba haswa. Miili mirefu iliyojengekea. Vifuani wamevalia vijishati vyeusi vilivyobana vifua vyao, miguu imekabwa na kombati za jeshi na vichwa vikiwa vimemezwa na kofia nyekundu za jeshi.
Walikuwa wamejiandaa kwa lolote lile.
Lakini pia kwa wakati huohuo, kuitikia wito wa Wales, Underground office kule Uingereza ilikuwa imeshatuma watu wake kadhaa kwa ajili ya kwenda kumsaidiza Wales kumaliza kazi. Hivyo lilikuwa ni swala la muda tu kwa tu hawa kukutana na kuonyeshana ubabe.
Kisiwa hiki kilikuwa kinaenda kumezwa na damu.
***