Jweneng sio timu dhaifu kama mashabiki wengi wa Simba wanavyodhani. Hao jamaa wana kasi sana na pasi fupi fupi za haraka kwa hiyo Simba ijipange kweli kweli sio utani. Kwa namna Simba inavyocheza taratibu na huku ina wachezaji wengi wenye umri mkubwa kwa kweli itawasumbua sana kukabiliana na kasi ya Jwenang.
Ushindi au kushindwa vipo mikononi kwa wachezaji na benchi la ufundi la Simba. Na benchi la ufundi likumbushwe kuwa liache kupanga wachezaji kwa kukariri bali waangalie wachezaji wanajituma na zaidi sana wale wachezaji wanaocheza kitimu zaidi. Wale wachezaji wabinafsi wanaotaka waonekane wao huku timu inaharibikiwa wapigwe tu benchi ili timu isonge mbele.
Tatizo kubwa lingine kwa Simba ninaliliona ni kuwa Simba haina mshambuliaji wa maana wa kumaliza mechi au kubadili matokeo. Jobe na Freddy mpaka sasa hivi bado hawajathibitisha huo uwezo labda kama watabadilika mbele ya safari. Nafikiri viongozi wa Simba walikurupuka kwa kuogopa kelele za mashabiki wao lakini walikuwa hawajajipanga wakaamua kuwaacha Baleke na Phiri na kuleta watu ambao viwango vyao havitofautiani na hao waliwaondoa. Kwa hiyo Simba imekuwa inapata ushindi kwa shida sana.
Mbaya zaidi ile "pressing" aliyokuwa anafanya Baleke pale mbele pamoja na udhaifu wake kukosa magoli ya wazi kwa sasa haipo tena kiasi kiufundi viungo na mabeki kwa sasa inawabidi wafanya kazi ya ziada. Simba ikija kukutana na timu ambayo ina mabeki wanaoanzisha mashamblizi kuanzia nyuma itakuwa katika wakati mgumu sana.
Yote kwa yote Simba anaweza kumfunga Jwenang na kufika robo fainali. Lakini mashaka yangu makubwa ni baada ya kuvuka robo fainali. Viongozi wameawaanisha mashabiki wao kuwa Simba itafika nusu fainali mwaka huu lakini nikiangalia safu ya ushambuliaji ya Simba sioni wakifanya vizuri zaidi ya robo fainali labda itokee tu bahati maana mpira wa miguu saa nyingine huwa una matokeo ya ajabu kabisa.