Godbless Lema tangu arudi ametoa kauli zilizoibua mijadala, hisia nyingi sana na tafsiri za kila aina kutoka katika makundi mbalimbali ya kijamii.
Amezungumza kuhusu uduni wa ajira za bodaboda na VICOBA visivyo na maana yoyote kwenye jamii ambapo yeye anasema hivi vitu ni "urasimishaji wa umaskini' unaofanywa na watawala. Ameongelea pia hadaa za nabii mkuu Geor Davie wa huko Arusha.
Amegusa vijana, wanawake na dini ambayo ni makundi makubwa sana ya mtaji katika siasa za nchi hii. Japo yote aliyoongelea ndio ukweli mtupu lakini chama chake pia bado kina malengo ya kushika dola hivyo bado kinayahitaji sana haya makundi yote.
Tanzania anayoitazama lema ni ile ya kisasa iliyoendelea, yenye maendeleo ya watu na vitu ambayo raia wake wengi wana ishi hadhi ya binadamu wa karne ya 21. Kwa bahati mbaya sana hatujaifikia hiyo Tanzania na hivyo Lema anapaswa kukubaliana na hali halisi ya sasa tu.
Kama yeye na chama chake wanataka kushika madaraka siasa wanazopaswa kufanya ni zile zile za kijanja janja za kuwahadi bodaboda, mama ntilie, wamachinga na makundi ya dini kwamba watawatengenezea mazingira mazuri zaidi ya kufanya kazi zao na kushamiri. Wenye nguvu katika chama kwa "maslahi ya chama na kushika dola" waafikiane naye asiongele mambo ya gigabyte(GB) katika bongo za watu zinazoweza kuhimili Megabyte(MB) tu.