Hivi umepata kujiuliza unapopita katika mitaa mbalimbali ya mjini Dar au mji mwingine wowote Tanzania, jina la mtaa au eneo husika limetokana na nini?
Kwa mfano, Kijito Nyama limetokana na nini? Au Mlalakuwa, Au Mtoni kwa Aziz Ali n.k, n.k. Labda utadhani imetokea tu ... just ipo ipo, hapana! Baadhi ya majina ya mitaa yana historia ndefu na yenye kukumbukwa hata kwa vizazi vijavyo.
Hapa napenda kuwahabarisha maana ya mtaa au eneo la nje kidogo ya jiji la Dar liitwalo Gongo la Mboto.Jina hili limetokana na nini? Nakumbuka nilipata kusimuliwa na mwalimu wangu mmoja miaka ile pale Tambaza Sekondari nikiwa kidato cha pili.
Alisema palikuwa na mzee mmoja mashuhuri ambaye alipata kuishi katika eneo hilo.Huyu jamaa alikuwa mkulima. Jina lake aliitwa Mboto. Siku moja alijilawa kwenda katika konde lake kwa ajili ya kujipatia riziki.
Wakati ule, maeneo yale yalikuwa na giza la mapori na vichaka kadhaa. Jioni yake asirudi nyumbani. Kesho yake hadi mchana Mboto haonekani.
Mbiu ikapigwa watu wakakusanyika,kilichofuata ni msako mkali wa kumtafuta mzee huyu.Baada ya siku kadhaa wakakuta nyayo za mnyama mkubwa mithili ya Simba na ishara ya purukushani kadhaa.
Walipochunguza zaidi wakafanikiwa kukuta Gongo ambalo alipenda kutembea nalo mzee huyu.Wakahisi kuwa Mboto huenda amekutwa na maafa ya kuliwa na Simba. Walichokiona pale ni Gongo lake,Ndipo hilo eneo hadi leo lajulikana kama Gongo la Mboto.
Tuhabarishane maana ya maneno mengine kama Msasani, Mikocheni,Mto wa Mbu n.k.