HIMARS
JF-Expert Member
- Jan 23, 2012
- 70,791
- 98,334
Bonge la Elimu.Sawa kabisa kwamba asili ya UDA na KAMATA ni DMT. Lakini si sawa kwamba mwaka1967 ndipo zilizaliwa hizo kampuni tanzu mbili. Hilo lilitokea baadaye. Nitaeleza kidogo ninachokumbuka kuhusu DMT.
Baada ya DMT kutaifishwa, kampuni iliendelea kufanya biashara na jina hilo hilo la DMT na biashara yao ilikuwa mjini Dar tu. Vijana wafahamishwe pia kuwa kulikuwa na mabasi ya DMT ya gorofa kama ya London. Hiyo ndiyo asili ya wimbo wenye maneno "Heri ufe kwa kugongwa na basi la gorofa la kwenda Ilala. Usikiombee kifo cha mpenzi cha kugongwa na gari la 'tela' la kwenda Zambia".
Baada ya miaka kadhaa ya DMT kufanya biashara ya kusafirisha wakazi wa Dar kama shirika la Umma, wakaanzisha safari za kwenda mikoani wakiwa bado wakiitwa DMT. Walikuwa wakienda Morogoro, Tabora, Mwanza, Bukoba, Arusha, Musoma, n.k. Wakati kila basi la DMT la kwenda mikoani likiwa na madereva watatu (hata ya kwenda Morogoro) wakipokezana, Tanganyika Bus walikuwa wanatumia dereva mmoja tu kutoka Mwanza kuja Dar. Vivyo hivyo mabasi ya Teeteeko ya kutoka Dar kwenda nyanda za Kusini au Hood Bus kutoka Morogoro kwenda Dar au Iringa. Achilia mbali mabasi ya Wachaga ya kutoka Dar kwenda Moshi/Arusha. Wakati ratiba ya DMT ilikuwa watumie saa 23 kwa safari ya Dar-Tabora, Tanganyika Bus walikuwa wakitumia saa 24 kwa safari ya Dar-Mwanza. Ratiba za mabasi ya DMT ya kwenda mikoani zilikuwa hazifuatwi. Zama hizo mabasi yalikuwa yanaruhusiwa kusafiri usiku. Lakini ilikuwa kila basi la DMT likifika Singida 'linaharibika' na inabidi kulala hapo. Asubuhi basi wala halijashughulikiwa abiria mnaambiwa limepona mnaendelea na safari. Inasemekana madereva walikuwa na wasichana wao hapo ambao lazima wasimame kuwasalimia. Hayo ni baadhi ya matatizo yaliyofanya DMT ya Umma isifanye vizuri kibiashara.
Nauli ya Dar-Tabora ilikuwa Sh.49 ambapo kwa safari za jijini nauli ilikuwa ikibadilika kufuatana na wapi unakwenda, kima cha chini kikiwa Senti 25. Posta-Kurasini nauli ilikuwa Senti 55; Kariakoo-Ubungo Senti 60; Kariakoo-Chuo Kikuu Senti 65; Posta-Pugu Sekondari Senti 90. Baadaye wakaanzisha safari ndefu zaidi kama Kariakoo-Kibaha kwa Sh. 2.50 na wakawa wanaenda hadi TANITA, Kwa Mfipa, Kongowe, Kisarawe, nk.
DMT za mjini zilikuwa zikifanya kazi saa 24, ingawa kadiri usiku unavyokomaa, idadi ya mabasi inapungua. Kwa mfano kuanzia saa sita usiku linabakia basi moja tu la kuzunguka kutoka Temeke kwenda Chuo Kikuu kupitia Morogoro Road na linaendelea mpaka Mwenge na kurudi mjini kupitia Bagamoyo Road na Morocco.
Kufuatana na uhaba wa mabasi ya DMT, mabasi ya binafsi yakaanza kufanya kazi kwa kificho wakitoza Senti 50 bila kujali unapokwenda. Hivyo yakawa yakiitwa Thumuni-Thumuni. Trafiki walikuwa wakiyapiga vita na ndiyo maana walikuwa wakitoza kima kikubwa zaidi ili akishikwa ajione kwamba angalau ameshikwa kwa kuchuma kiasi kinachoeleweka.
Ni dhahiri mabasi ya mjini yalikuwa yakiingiza pato kubwa zaidi ya yale ya kwenda mikoani. Miaka ya sabini katikati ndipo biashara ikagawanywa: usafirishaji wa abiria jijini Dar ukaundiwa kampuni tanzu ya UDA na usafirishaji wa abiria kwenda mikoani ukaundiwa kampuni ya KAMATA, kila kampuni ikijitegemea. Mara baada ya UDA kuundwa, wakaleta mabasi ya Icarus yenye 'tela' ambayo yalikuwa yakichukua abiria karibu ya mia. Kituo kikiwa kimejaa abiria, Icarus ikija inazoa wote. Kampuni ya UDA walikuwa na bendi ya mziki, wakajiita Icarus Kumbakumba. Badiliko jingine waliloleta UDA mara baada ya kuundwa upya ni kuanzisha tikiti za msimu. Unanunua tikiti ya Sh.60 ukaitumia kwa mwezi mzima kwa njia moja k.m. Kariakoo-Ubungo. Ukiwa kwenye njia yako, hata usafiri mara 50 kwa siku hutozwi zaidi. Utatozwa unapoingia njia nyingine tu. Mbali na hiyo, unaweza kununua tikiti ya msimu ya Sh 85 kwenda popote UDA inapokwenda kwa mwezi mzima.
Mwishoni mwa miaka ya sabini nauli zilikuwa zimepanda karibu ya mara tatu ya zilivyokuwa mwanzoni. Mabasi ya binafsi nayo yakaongeza kima kufikia Sh.5 po pote uendapo, ambayo ndiyo ilikuwa thamani ya Dola ya Marekani siku hizo. Hiyo ndiyo asili ya jina la Daladala. Nauli hiyo ilikuwa kubwa sana lakini watu walikuwa wakiyapanda tu kwa ajili ya uhaba wa UDA. Trafiki walipambana sana nayo mpaka Waziri Mkuu, Sokoine, alipoingilia kati na kuyahalalisha.
Hicho ndicho kifupi cha historia ya UDA ninachokumbuka.
Ila inaonesha zamani palikuwa na mfumo mzuri mno