Uislamu uliingia kilimanjaro ukiletwa na wafanya biashara …ambao kwenye uhusiano wao na machifu hasa wa Marangu na Machame aliwaruhusu baadhi ya raia wake wakasilimishwa kuwa waislamu …..
Na Jamii ya wasomali na wa comoro waliokuwa wakileta biashara waliweka makazi yao moshi mjini na kuoleana na wageni ..
KUNA waislamu ambao walikuja kutoka Zanzibar wakiambata na wamisionari wao wakiwa wapagazi na waonyesha njia …kuna ambao waliamua kulowea …na pia kuna jamii ya mwanzo ya watu wa kilimanjaro nao walifika Zanzibar kama wapagazi wa wamisionari pale walipokua wanarudi zanzibar kupanda meli kwenda likizo ulaya ….familia za wachagga huko zanzibar kama kina Kissasi na wengine
Phil...
Soma hapo chini Uislam ulivyoingia Uchaggani.
Makala ndefu lakini ina mengi ya faida:
RAJABU IBRAHIM KIRAMA SEHEMU YA KWANZA
Rajabu Ibrahim Kirama aliyezaliwa na kupewa jina la Kirama Muro toka amefariki mwaka wa 1962 watoto wake wamekuwa wakimsomea khitma yaani wakimfanyia hawli kila mwaka.
Katika kipindi hiki ambacho sasa imetimia miaka 58 wahudhuriaji wa hafla hii wameongezeka katika familia.
Hivi sasa hawli hii inahudhuriwa pamoja na wanae, wajukuu na vilembwe wake kwa waume na shughuli hii inawajumuisha mbali na wanafamilia, shughuli hii inahudhuriwa na Waislam kutoka sehemu tofauti za Uchaggani na Arusha.
Halikadhalika khitma hii inahudhuriwa na nduguze ambao wao walibakia katika Ukristo baadhi yao wakitokea Old Moshi na sehemu nyingine za Kilimanjaro.
Baba yake Mzee Rajabu, Muro Mboyo alitafuta hifadhi na kuishi Old Moshi kwa Chief Rindi Mandara miaka mingi mwishoni mwaka miaka ya 1800.
Shughuli hii imekuwa kalenda muhimu katika kijiji cha Nkuu Machame.
Kisomo cha kumrehemu Mzee Rajabu na wenzake waja wema kinafanyika kila mwaka katika msikiti ambao Waislam wameupa jina ‘’Msikiti wa Mzee Rajabu.’’
Katika hawli ya mwaka wa 2019 uliposomwa wasifu wa Mzee Rajabu wajukuu zake waliguswa na historia yake kiasi wakajiuliza kwa nini historia hii isihifadhiwe katika maandishi ili isipotee?
Historia ya Mzee Rajabu yote ilikuwa mikononi kwa mwanae Salim Rajabu ambae baada ya kifo cha baba yake mwaka wa 1962 yeye alikusanya nyaraka zote za baba yake akazitia ndani ya gunia na kuzihifadhi juu ya dari la nyumba yake.
Nyaraka hizi sasa zina umri wa miaka 90 na zilikuwa hapo darini bila kufunguliwa kwa muda wa miaka inayokaribia 60.
Nimebahatika kuwa mtafiti wa kwanza kuzipitia nyaraka hizi na hivi ndivyo nikajikuta nimehusika katika kutafiti maisha ya Mzee Rajabu na mwishowe kuandika kitabu cha maisha yake na jinsi alivyosimama kuuingiza Uislam Uchaggani mahali ambapo Uislam haukuwapo kabisa.
Maisha ya Mzee Rajabu na historia yake ya kuuingiza Uislam Uchaggani ni kilele katika historia ndefu ya ukoo wake wa Nkya.
Historia ya ukoo huu inakwenda nyuma kiasi cha miaka 200 na zaidi na imehifadhiwa kwenye vichwa kama simulizi ikipokelewa kutoka kizazi kimoja hadi kingine hadi kufikia miaka ya 1800.
Historia ya kipindi hiki cha Wamishionari walipoanza kuingia Tanganyika na kufika Uchaggani kulifuatiwa na Tanganyika kuwa koloni la Wajerumani.
Historia hii ya ukoloni imeandikwa na wenyewe Wajerumani kwa yale ambayo wao waliona ndiyo muhimu kwao.
Mengi katika historia hii yakiwa ni shughuli za Wamishionari, uvumbuzi, kueneza Injili kwa Wachagga na vita vilivyopiganwa baina ya Wajerumani na Wachagga.
Historia inayowahusu Wachagga wenyewe na watawala waliojulikana kama Mangi, historia hii haikupatwa kuandikwa si na Wajerumani au Wachagga wenyewe.
Lakini hii haina maana kuwa historia hii haikuwapo.
Ilikuwapo historia hii na ukoo wa Nkya wanayo historia ambayo ilihifadhiwa kutoka kizazi hadi kizazi ikihadithiwa ndani yao kizazi kimoja kikirithisha simulizi hii kizazi kingine hadi kuingia kwa karne hii ya 21 na kuandikwa na kuwa kitabu.
Mzee Rajabu hakupata kuwa Mkristo alitokea katika Upagani akaingia Uislam yeye na watoto wake wote.
Baada ya kusilimu mwaka wa 1930 alianza taratibu za kujenga msikiti.
Mzee Rajabu kama alivyokuja kufahamika aliingia Uislam baada ya kukutana na Shariff Muhsin kutoka Mombasa alipokwenda Moshi na kufika Machame kwa shughuli za tabligh.
Wakati huo Mzee Rajabu tayari alikuwa na watoto wanane mkubwa akiwa Salim Rajabu ambae alishirikiananae katika ujenzi wa huu msikiti na shule na kwa kila kila jambo lililohusu Uislam.
Paliponyanyuka nyayo ya Mzee Rajabu Salim mwanae alikanyaga ardhi hiyo.
Pamoja nao walikuwa Waislam wa mwanzo wa kijiji cha Nkuu Machame na vijiji vingine vya jirani kama Lyamungo, Masama, Mudio, Kibosho, Mkoanju na Uswaa.
Msikiti huu sasa unakimbilia umri wa miaka 100 na katika kiwanja cha msikiti huu kuna shule (Muslim School) aliyojenga Rajabu Ibrahim Kirama ambayo hadi leo ipo ingawa sasa iko katika mikono ya serkali.
Salim Rajabu alikuwa mtoto mwema kwa baba yake na kwa Waislam wa Machame akaja kuwa mfanyabiashara mkubwa wa nyama akafahamika kwingi Uchaggani.
Mbali na sifa hii Allah alimjaalia Salim nguvu akiweza peke yake kumwangusha ng’ombe chini kuchinjwa kwa ajili ya biashara yake ya nyama.
Dua kubwa ambayo baba yake aliyokuwa akimuombea ni kuwa Allah ampungizie Salim zile nguvu zisije zikawaumiza binadamu wenzake.
Katika hali kama hii Salim akiwa kijana mdogo akawa nguzo ya baba yake na fedha alizopata katika biashara mkono wake ukawa wazi kwa Waislam na Uislam.
Nilipoanza utafiti nilifahamishwa kuwa historia hii kwa kizazi kilichopo imehifadhiwa na mtoto wa Mzee Rajabu, Bi. Hawa bint Rajabu maarufu kwa jina la Mama Ali, Ali likiwa jina la mwanae.
Msingi wa kitabu hiki ni simulizi ambayo nimeipata kutoka kwa Mama Ali ambae anafikia umri wa miaka 85.
Mama Ali ni mjukuu wa Mangi Ngamini Ndesaruo Mamkinga kwa kikeni kwake.
Mangi Ndeseruo Mamkinga alitawala Machame kutoka mwaka wa 1855 – 1880.
Mama Ali kiumeni ni mjukuu wa Muro Mboyo, baba yake Mzee Rajabu aliyekuwa Jemadari wa Vita wa Mangi Ndeseruo Mamkinga.
Huu ndiyo uhusiano wa Mama Ali katika koo hizi mbili kubwa zilizotawala Machame kabla ya ukoloni.
Mama Ali kwa upande wa kikeni kwake ni ukoo wa Chief Shangali.
Chief Abdiel Shangali aliyeshika utawala wakati wa ukoloni wa Waingereza ni kilembwe cha Mangi Ndeseruo Mamkinga.
Utawala wa Waingereza baada ya kuondoka Wajerumani Chief Abdiel Shangali alichagulikuwa kama Mwafrika wa kwanza Tanganyika kuwa Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria (LEGICO) mwaka wa 1945.
Abdiel Shangali alitawala Machame hadi uchifu ulipofutwa baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka wa 1961.
Mama Ali kwa ufupi ni mjukuu wa Mangi Ngamini kikeni kwake akiwa mtoto wa Bi. Ngumbe Ngamini na kiumeni kwake ni mtoto wa Rajabu Ibrahim Kirama.
Hii ndiyo silsila ya Mama Ali.
Katika mazungumzo yetu Mama Ali alinieleza mgogoro mkubwa uliotokea kati ya babu yake, Muro Mboyo Jemedari wa Vita na Mangi Ndeseruo Mamkinga.
Mgogoro ulihusu urithi wa nafasi ya Mangi kati ya wanae watatu, babu mzaa mama yake, Ngamini na nduguze Ngulelo na Shangali Ndeseruo.
Mama Ali anasema mgogoro huu ulisababisha Mangi Ndeseruo Mamkinga kutoa amri ya kuuliwa Ngamini ili asirithi kiti cha baba yake.
Mtekelezaji wa amri hii alikuwa babu mzaa baba yake Mkuu wa Vita Muro Mboyo.
Muro Mboyo alikataa kutii amri hii na Ngamini alirithi kiti na alikuja kukiachia baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe na kwenda kwenda uhamishoni Old Moshi kwa Mangi Rindi Mandara.
Historia hii huipati popote labda katika ukoo wa Chief Sangali wenyewe.
Shangali Mamkinga akatawazwa na kuwa Mangi mwaka wa 1890 na mwaka wa 1901 aliacha nafasi hiyo ikashikwa na Ngulelo.
Wajerumani wakawa wamechoshwa na vita hivi vya wenyewe kwa wenyewe wakawakamata Mangi 19 wakawanyonga.
Mama Ali anasema kuwa Wajerumani walimpeleka Ngulelo Kismayu, Somalia uhamishoni ili akanyongewe huko lakini hili halikutekelezwa na huko Somalia akaingia Uislam na jina alilochagua ni Selemani.
Taarifa nyingine zinasema alipelekwa Lamu.
Ngulelo aliporudi uhamishoni akawa ndiye Muislam wa kwanza Machame kutoka ukoo wa Shangali.
Akiwa uhamishoni Muro Mboyo alikutana na kufanya urafiki mkubwa na mmeshionari wa Kijerumani Bruno Gutmann kutoka Leipzig Mission aliyefika Kidea Mission, Old Moshi mwaka wa 1902.
Hapa kuna kisa kizuri sana. Mama Ali hakuweza kunipa jina kamili la Gutmann na akilitamka kwa makosa kama ‘’Kutimani.’’
Nilikwenda Kidea Mission Old Moshi kuendelea na utafiti. Kwa mastaajabu makubwa sana nilionyeshwa kaburi la Bruno Gutmann yule Mjerumani rafiki yake Muro Mboyo, babu yake Mama Ali ambae Mama Ali hakuweza kulitamka vyema.
Hili lingekuwa kaburi la Gutmann kama angekufa Uchaggani lakini alikufa Ujerumani mwaka wa 1966.
Gutmann alifanikiwa kuwatia katika Ukristo wazee wengi mashuhuri Old Moshi isipokuwa Muro Mboyo. Yeye alibakia katika Upagani.
Sijaweza kujua kwa nini Muro Mboyo hakuingia Ukristo wakati kila mtu Uchaggani alikuwa anaupokea.
Lakini kwa kukuza urafiki wao Muro Mboyo alimpa ardhi Bruno Gutmann na Gutmann alijenga kanisa ambalo naamini lipo hadi leo ingawa wahusika pale Kidia hawakuweza kunipa taarifa za kutosha.
Nyaraka za Mzee Rajabu zina historia ya babu zake walioishi karne ya 19 na nyadhifa mbalimbali walizoshika katika uongozi wa utawala wa Machame chini ya Mangi.
Babu yake wa tatu alikuwa Waziri wa Mangi Renguo (1784 – 1837), babu wa pili alikuwa Waziri wa Mangi Mamkinga aliyekuwa Mangi kuanzia mwaka wa 1855 – 1880, na baba yake, Muro Mboyo alikuwa Waziri wa Mangi Ndeseruo Mamkinga.
Picha ya kwanza ni Mangi Ndeseruo Mamkinga na picha ya pili ni Bi. Hawa (Mama Ali) bint Rajabu Ibrahim Kirama na Sheikh Idrissa Rajabu Ibrahim Kirama.