Mwanahabari Huru
JF-Expert Member
- Mar 9, 2015
- 14,242
- 34,917
Aliyewahi kuwa Mkuu wa Majeshi ya Israeli, Generali Joab Zeruiah alikuwa ni mtu ambaye hakujiamini katika nafasi aliyokuwa nayo. Kila wakati alihofu kuwa angeliondolewa katika nafasi ile hivyo alitumia njia za hila ili kulinda nafasi na masilahi yake! Kuna wakati alipohofia kuwa Mkuu wa Majeshi katika utawala wa Mfalme Sauli, Generali Abner Ner angeliweza kuteuliwa kuchukua nafasi yake, hivyo aliamua kumuua (2Samweli 3:22-30).
Pamoja na kuwa kitendo kile kilichukuliwa kama ni cha kulipiza kisasi, lakini ukweli ni kuwa Abner alifanikiwa kuliweka Jeshi kubwa lililokuwa chini ya Sauli mikononi mwa Daudi. Jambo hilo lilimfanya Joab amuogope na kumuonea wivu Abner.
Kwa kuwa hakujiamini, Generali Joab aliishi katika hali ya kujipendekeza mbele ya Mfalme Daudi na alijitahidi kuupeleleza moyo wa Mfalme ili afanye kitakachompendeza Mfalme. Kuna wakati alikuwa akiwaandaa hata wanawake na kuwapanga maneno ya kuongea ili waende kulia mbele ya Mfalme. Mfalme wakati mwingine kwa kufikiri kuwa huenda ilikuwa ni sauti ya Mungu, alitimiza matakwa ya Joab pasipo kujua (2Samweli 14:1-33).
Mwana wa Mfalme, aliyeitwa Absalom Daudi Boaz alipopania kuutwaa ukuu wa nchi mahali pa baba yake alihakikisha anamwaga damu za watu wengi sana. Kwanza alimuua kaka yake aliyeitwa Amnon Daudi Boaz (2Samweli13:23-38).
Ingawa kitendo kile nacho kilionekana kama ilikuwa ni kulipa kisasi, lakini ukweli ni kuwa Amnoni ndiye aliyekuwa mrithi wa kiti cha ufalme kabla ya Absalom. Baada ya kumuua Amnoni, Absalom akawa ndiye mrithi wa kiti cha ufalme. Hata hivyo, alipoona kuwa anacheleweshwa kupata ufalme, aliamua kufanya baadhi ya mambo yaliyompatia sifa na jina zuri mbele ya watu lakini huku akiwa na lengo la kuwachafua wengine akiwemo Mfalme mwenyewe hadi akafanikiwa kumpindua Mfalme (2Samweli 15:1-12).
Katika miaka ya hivi karibuni, kumejitokeza tabia ya watu hasa wanawake kutaka kueleza shida zao mbele za Rais huku wengine wakifika mahali kuomboleza mbele ya kamera na kumfanya Rais atoe majibu au maelekezo hapo hapo! Matukio haya yanaacha maswali mengi sana. Je, ni nani anakuwa nyuma ya watu hao?
Ni makundi ya kisiasa yanayosigana ndani ya mfumo yanayotaka kutumia ziara za Rais ili kumalizana? Je, ni watu fulani walio karibu na Rais wanatafuta njia ya kujipendekeza zaidi? Je, ni mkakati wa Chama ili kuuonyesha umma kuwa Rais anasikiliza kero za watu hadharani? Je, ni mkakati wa baadhi ya wasaidizi wa Rais kwa sababu wanazozijua wao wenyewe ikiwemo njia ya kutaka kumng'oa msaidizi au mtendaji wa Rais katika eneo analotoka mlalamikaji kwa kuuonyesha udhaifu wake hadharani mbele ya Rais na wananchi?
Je, ni mkakati wa baadhi ya wasaidizi wa Rais wanaotumika kutaka kumchafua Rais kwa kumchomeka katika mitego ya kutoa maamuzi ambayo baadaye yataonekana kuwa yalikuwa ni ya jazba?
Leo Mheshimiwa Rais amekataa kumsikiliza 'mama mmoja kutoka Arusha' aliyesafiri hadi Dar es Salaam kuja kumuona. Kwamba wasaidizi wa Rais walishindwa kumwambia Rais akiwa Ikulu habari za mama yule na wakategea hadi katika mkutano wa hadhara nalo ni jambo fikirishi! Kwa vyo vyote vile, nakubaliana na Rais kuwa mama huyo akasikilizwe na Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Jambo hili linanipa nafasi kuwashauri wasaidizi wa Rais wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Mawaziri, Wakurugenzi, wana itifaki na wana usalama wanaoizunguka ofisi ya Rais. Watu hawa au makundi haya wanao wajibu mkubwa mbele za Mungu na mbele ya Watanzania katika kumshauri, kumsaidia, kumuonya, kumuelekeza, na kumlinda Rais.
Hayo mambo wanayoyaruhusu hadharani hayaonyeshi taswira nzuri ya taasisi ya Urais. Mungu aweze kuwasaidia wote wanaohusika akiwemo Mheshimiwa Rais ili waweze kugundua dhamira iliyoko nyuma ya matendo hayo.
Ni jukumu letu kama Makuhani wa Mungu kuingaliza, kuionya, na kuishauri jamii pamoja na viongozi wao katika zama ambazo Mungu anatuweka tutumike (Ezekieli 33:1-20).
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Mkuu Emmaus Bandekile Mwamakula - Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian ya Uamsho Duniani